KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 12, 2010

KIEMBA: Simba, Yanga timu ngumu kuzichezea


SWALI: Wewe ni miongoni mwa wachezaji wachache, ambao wamewahi kuzichezea timu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti. Hebu tueleze, umejifunza nini kutokana na kuzichezea timu hizo kongwe nchini?
JIBU: Ukweli ni kwamba klabu hizi mbili hazina tofauti kubwa kiuendeshaji. Pia tabia za wanachama na viongozi wake na mambo mengine ya kiutendaji yanafanana. Lakini nisingependa kuzungumza kiundani sana kuhusu mambo hayo.
Lakini kilicho wazi ni kwamba, mashabiki wengi wa soka nchini wanazipenda klabu hizi na kila mchezaji anakuwa kwenye wakati mgumu anapoichezea moja kati ya timu hizi mbili kwa sababu ushindani wa namba unakuwa mkubwa na unapofanya kosa katika mechi kati ya timu hizi mbili, lawama zake huwa ni kubwa na nzito.
SWALI: Una maoni gani kuhusu kikosi cha Simba msimu huu na nafasi yako kwenye kikosi cha kwanza?
JIBU: Uongozi wa Simba umefanya usajili mzuri msimu huu na kwa malengo mazuri. Nadhani benchi la ufundi liliangalia zaidi kila idara kuhakikisha tatizo lililokuwepo msimu uliopita, linatafutiwa ufumbuzi.
Mbali na hilo, bado kuna vita kali hivi sasa ya kila mchezaji kutaka namba kwenye kikosi cha kwanza. Kila mchezaji amekuwa akijifua kwa nguvu zake zote ili kuhakikisha anakuwa fiti muda wote na pia hakosi nafasi ya kucheza.
Kila mchezaji amekuwa akifanya jitihada kubwa ya kumshawishi Kocha Patrick Phiri ampe namba kwenye kikosi cha kwanza. Changamoto hiyo ndiyo iliyonifanya niongeze muda mwingi wa kufanya mazoezi kwa siku ili niweze kufikia kiwango kitakachokubalika kwa kocha wangu.
Ukichezea Simba au Yanga, mchezaji unapaswa kuwa makini sana na kuonyesha uwezo wako wote uwanjani. Vinginevyo, ukizubaa tu, unapoteza namba na kuishia kwenye benchi.
SWALI: Una maoni gani kuhusu kikosi cha sasa cha Taifa Stars? Wewe binafsi una malengo yoyote ya kutaka kuitwa kwenye timu hiyo siku zijazo?
JIBU: Kikosi cha Taifa Stars kwa sasa ni kizuri na nina hakika kama wataendelea kupewa ushirikiano mkubwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wa soka, kinaweza kufuzu kucheza fainali za kombe la Mataifa ya Afrika.
Lakini jambo la msingi ni kwa Kocha Jan Poulsen na benchi zima la ufundi la timu hiyo, kupewa nafasi ili waweze kutimiza majukumu yao.
Kwa upande wangu, niliwahi kuitwa kwenye kikosi hicho na kocha wa zamani, Mshindo Msolwa mwaka 2006 na kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Rwanda.
Mawazo ya kutaka kurejea tena ndani ya kikosi hicho bado yapo kichwani mwangu kwani enzi hizo wachezaji walikuwa wakiitwa kwenye timu, wanatafuta sababu ili wasijiunge nayo, lakini kwa sasa kila mchezaji anapenda kuichezea Taifa Stars baada ya kujitokeza kwa wafadhili wengi.
SWALI: Kwa nini unasema hivyo?
JIBU: Zamani tulipokuwa tukiitwa kwenye kambi ya Taifa Stars, kila mchezaji alilazimika kwenda na vifaa vyake vya michezo. Kuna wakati hata chakula kwa wachezaji kilikuwa cha tabu, tofauti na sasa, ambapo wachezaji wanapata huduma zote muhimu na za ziada na kuwekwa kwenye hoteli zenye hadhi.
SWALI: Unayaonaje maendeleo ya soka hapa nchini hivi sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma?
JIBU: Maendeleo yanaridhisha kwa sababu ushindani katika michuano ya ligi kuu umeongezeka na karibu kila timu ya ligi kuu, inayo timu ya vijana wa chini ya miaka 20 na kumeanzishwa michuano mbalimbali ya vijana.
Ushauri wangu kwa TFF ni kutafuta wadhamini wengine zaidi kwa ajili ya michuano ya vijana kwa lengo la kuongeza ushindani zaidi. Nasema hivyo kwa sababu ushindani kwa michuano ya vijana hivi sasa umekuwa mkubwa na vijana wengi wanajitokeza kwa lengo la kuonyesha vipaji vyao.
Jambo lingine la muhimu ni kwamba naiomba TFF itafute wadhamini kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa makocha kwa sababu wengi waliopo sasa, walisoma miaka mingi iliyopita hivyo wanashindwa kwenda na wakati. Naamini wakiwa wanapata mafunzo ya mara kwa mara, kiwango kitazidi kuongezeka.
SWALI: Ni jambo gani, ambalo limekuwa likikukera katika uendeshaji wa soka hapa nchini?
JIBU: Binafsi nachukizwa sana na baadhi ya waamuzi wa soka nchini, ambao hushindwa kutimiza majukumu yao uwanjani kwa kuweka pembeni sheria 17 za soka na kuchezesha kwa upendeleo. Pia huwa nakerwa sana na tabia za baadhi ya mashabiki wa soka nchini, kupenda kuwashutumu wachezaji kwamba wamehujumu timu zao bila ya kuwa na ushahidi.
Hili la pili ndilo baya zaidi. Mimi ni muislamu safi, siwezi kuwa tayari kukiuka maagizo ya Mungu kwa kufanya mambo kinyume na dini. Ninachowaomba mashabiki wa soka nchini ni kuwaamini wachezaji wao na kama kuna jambo wanalitilia wasiwasi, ni vyema wafanye kwanza uchunguzi badala ya kutoa tuhuma nzito kwa wachezaji kwa sababu kufanya hivyo ni kuwavunja moyo.
SWALI: Elezea historia ya maisha yako na jinsi ulivyojitosa katika soka badala ya michezo mingine.
JIBU:Mimi ni mtoto wa pili wa mzee Ramadhan Kiemba, kati ya watoto watano, ambao mzee alijaliwa kuzaa. Nimesoma shule ya msingi mkoani Arusha na sekondari katika shule ya Jitegemee ya mjini Dar es Salaam.
Nilianza kucheza soka tangu nikiwa mdogo. Nilichezea timu nyingi, lakini ya kwanza kubwa ni Kagera Sugra ya Bukoba. Nilivutiwa sana na Kagera Sugar kwa sababu kulikuwepo utaratibu mzuri wa kutoa maslahi kwa wachezaji ili waweze kujituma uwanjani. Pia nimechezea timu za Yanga, Miembeni, Moro United na sasa nipo Simba.
SWALI: Unaweze kueleza ni kwa nini umekuwa ukihama kutoka timu moja hadi nyingine?
JIBU: Hakuna kingine zaidi ya kutafuta maslahi mazuri zaidi. Sina hakika na maendeleo ya Kagera Sugar yalivyo hivi sasa, lakini kama bado wanaendelea na mfumo uliokuwepo zamani, nina hakika ni timu inayopaswa kuwa mfano wa kuigwa.

No comments:

Post a Comment