KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 12, 2010

CHEGGE: Wasanii wa kweli wameanza kuonekana, wazushi wametoweka


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Saidi Juma Hassan ‘Chegge Chigunda’ ametamba kuwa, hakuna wimbo uliowahi kuvuma kwa kipindi kirefu kama ‘Mkono mmoja’, aliourekodi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Temba na Wahu kutoka Kenya.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Chegge alisema wimbo huo umekaa kwenye chati za nyimbo bora kwa zaidi ya miezi mitatu nab ado unazidi kukubalika kwa mashabiki wengi.
Chegge, ambaye ni mmoja wa wasanii wanaounda kundi la TMK Wanaume Family alisema, ujumbe uliomo kwenye wimbo huo ni mwepesi na hauchoshi kuusikiliza kutokana na mpangilio wake kuwa mzuri.
“Kwa kweni ni wimbo uliotuweka kwenye chati ya juu na naweza kusema kila mahali unakubalika,”alisema Chegge, ambaye mara nyingi hupenda kurekodi nyimbo zake kwa kushirikiana na Temba.
Msanii huyo aliyesokota nywele zake kwa mtindo wa rasta alisema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika muziki wa kizazi kipya hivi sasa na kwamba wasanii wa kweli wameanza kuonekana na wazushi wameanza kupotea.
"Ukiangalia muziki umekuwa mgumu sana. Hivi sasa kila kukicha kunakuwepo na mabadiliko ya kila aina, huyu yupo yule hayupo, ndio mambo yanavyokuwa, watu wameelewa nani mkweli na nani anafoji,” alitamba msanii huyo mwenye makeke anapokuwa stejini.
"Wasanii wameanza kujichuja wenyewe, msanii wa ukweli anabaki kuwa wa ukweli, ambaye hajui anachokifanya anapotea,” aliongeza.
"Ndio maana utaona wale wanaoweza muziki ndio wamebaki kuwa juu siku zote na ambao hawawezi, wanaonekana hawawezi. Inaonekana wameshindwa ingawa siwezi kujua sababu nyingine zinazowakwamisha,” alisema Chegge.
"Lakini kwa wenye akili, wakiangalia wanaona ni wazi wanaojua wanachokifanya ndio wanapeta, wengine wamechemsha. Huwezi kufoji kipaji, kama huna, huna tu, na kama hujui, hujui tu,"aliongeza msanii huyo.
Chegge alisema kufuatia mafanikio makubwa aliyoyapata katika kibao hicho, ameamua kuandaa wimbo mwingine mpya utakaojulikana kwa jina la ‘Fungeni milango’. Alisema atarekodi wimbo huo kwa kushirikiana tena na Temba. "Tuna utaratibu wetu wa kazi tuliojiwekea, kwamba sasa kwenye kundi ni zamu ya watu fulani kufanyakazi na muda fulani ni zamu ya watu fulani,” alisema.
"Sasa ni zamu yangu na Temba, ndio maana unaona kazi zetu ndiyo nyingi zimepewa nafasi, baada ya muda utasikia wengine na kundi hali kadhalika," aliongeza.
"Mfumo huo ndio tumekuwa tukitumia tangu awali na napenda kusisitiza kuwa, kundi letu bado lipo imara kama kawaida na tutazidi kufanya vizuri kwa vile tuna ushirikiano wa dhati na kila mmoja ana uwezo na kile anachokifanya," alisisitiza.
Chegge, ambaye anaishi maeneo ya Sinza, Dar es Salaam, alisema katika maisha yake, anachukia watu wanaopenda kukwamisha maendeleo yake pamoja na wezi wa kazi za wasanii.
Akizungumzia mipango yake ya baadaye, alisema kuwa ni pamoja na kujenga nyumba ya kuishi na kuoa mke mwenye heshima na adabu wakati wote na asiye na ubaguzi wa aina yoyote.
Kuhusu ratiba yake, Chegge alisema kwa kawaida huwa anapenda kuamka saa nne asubuhi na kwenda kwenye mazoezi ya muziki na kundi lake la TMK na anaporejea nyumbani, hutumia muda mwingi kupumzika na kuandika mashairi ya nyimbo zake.
Mbali na kutamba na kibao cha ‘Mkono mmoja’, Chegge pia amewahi kutamba kwa vibao vyake kama vile ‘Karibu kiumeni’ na ‘Mambo bado’ alichomshirikisha Judith Wambura ‘Lady JayDee’.

No comments:

Post a Comment