KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 23, 2017

TAIFA STARS YATUPWA NJE YA RWANDA MICHUANO YA CHAN



TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars imetolewa katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Rwanda.

Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa mjini Kigali, Taifa Stars ilikuwa ikihitaji ushindi ili iweze kufuzu kucheza fainali za michuano hiyo zitakazofanyika mwakani nchini Kenya.

Rwanda imesonga mbele kwa faida ya bao la ugenini, kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Mwanza.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, Fulgence Novatus, amesema kwamba Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti  ya SBL haikuwa na bahati katika mchezo dhidi ya Amavubi ya Rwanda uliofanyika Uwanja wa Kigali ulioko kata ya Nyamirambo.

“Tumecheza vema, tulitafuta nafasi za kutosha. Tumeshambulia sana na kumiliki mpira. Lakini kila tulipojaribu kufunga, bahati haikuwa kwetu,” amesema Novatus mara baada ya mchezo huo.

Matokeo ya sare tasa ya jana yanawapa nafasi ya kusonga mbele Rwanda baada ya sare ya 1-1 katika mchezo uliofanyika Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mchezo huo ni wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) na sasa Rwanda itacheza na Uganda mwezi ujao.

Pamoja na kushindwa kusonge mbele, Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, imeendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi baada ya kucheza mechi 11 za kimataifa na kushinda mitano; kutoka sare mitano na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa.

No comments:

Post a Comment