KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, July 18, 2017

MALINZI AENDELEA KUSOKA KEKO


NA FURAHA OMARY

VIGOGO watatu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  akiwemo Rais wake Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine, wataendelea kusota mahabusu kwa kuwa upelelezi wa shauri lao haujakamilika.

Malinzi (57) na Mwesigwa (46) ambao wako mahabusu katika gereza la Keko na mhasibu Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga (27), aliyeko gereza la Segerea, walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washitakiwa hao walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, ambapo upande wa jamhuri ulikuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai.

Kwa upande wa washitakiwa, Malinzi na Mwesigwa walikuwa wakiwakilishwa na jopo la mawakili  wapya akiwemo Richard Rweyongeza, Nehemiah Nkoko na Jacquline Rweyongeza. 

Mawakili wengine waliotambulishwa kuwawakilisha Malinzi na Mwesigwa ni James Bwana, Rwegeshora, Kashinje Thabit huku Nsiande akiwakilishwa na wakili Senguji Abraham.

Upande wa jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo waliomba shauri lao liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa huku wakili Abraham akiomba kupatiwa hati ya mashitaka na maelezo ya mlalamikaji kwenye kesi hiyo.

Hata hivyo, Swai alidai wakili huyo atapatiwa hati ya mashitaka lakini hawezi kupewa maelezo ya mlalamikaji kwa kuwa shauri hilo halijaanza kusikilizwa.

Hata hivyo, wakili Abraham aliendelea kusisitiza kupatiwa maelezo hayo kwa madai kuwa yatamsaidia mteja wake kufahamu tuhuma zinazomkabili.

Hakimu Mashauri alikubaliana na hoja za upande wa jamhuri kwamba wakili huyo atapatiwa hati ya mashitaka lakini hawezi kupatiwa maelezo ya mlalamikaji kwa kuwa si wakati wake.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi Julai 31, mwaka huu kwa kutajwa na kusema washitakiwa wataendelea kubaki rumande.

Vigogo hao wa TFF walifikishwa mahakamani  kwa mara ya kwanza Julai 26, mwaka huu na TAKUKURU  wakikabiliwa na mashitaka 28 yakiwemo ya kutakatisha fedha makosa ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika hati hiyo ya mashitaka, Malinzi anakabiliwa na mashitaka 26 yakiwemo ya kughushi risiti mbalimbali zikionesha ameikopesha TFF fedha huku Selestine akiwa na mashitaka manne na Nsiande mashitaka mawili.

Shitaka la kwanza, Malinzi na Selestine wanadaiwa Juni 5, mwaka jana jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya kwa pamoja walighushi nyaraka ambayo  maazimio ya kamati ya utendaji ya tarehe hiyo ikionesha kuwa kamati iliamua kubadilisha mtu wa kutia saini wa akaunti zake za benki kutoka Edgar Leonard Masoud na kuwa Nsiande  Isawafo Mwanga.

Selestine anadaiwa Septemba Mosi, mwaka jana katika benki ya Stanbic Tanzania Limited tawi la  Kinondoni, Dar es Salaam  kwa nia ya udanganyifu aliwasilisha nyaraka ya kughushi ambayo ni maazimio ya kamati yautendaji ya TFF ya kubadilisha jina la mtia saini wa akaunti zake.

Shitaka la tatu hadi la 25 linamkabili  Malinzi ambaye anadaiwa  katika tarehe tofauti kati ya Novemba 6,  2013 hadi Septemba 22, 2016 kwenye shirikisho hilo alikuwa akighushi risiti zikiwa na kiwango tofauti cha Dola za Marekani akionesha amelikopesha shirikisho hilo.

Malinzi anadaiwa Novemba 6, 2013, alighushi risiti kuonesha ameikopesha TFF Dola za Marekani 9300, Desemba 17, 2013 aliikopesha  Dola za Marekani 10,000 na Dola 18,000, Dola 500 na Dola 1,032.

Pia  Malinzi anadaiwa Machi 26, 2014, katika shirikisho hilo alighushi risiti zikionesha amelikopesha  Dola 40,000, Machi 13, 2014 amekopesha Dola 5,000. Dola 40,000, Machi 16, 2014 alilikopesha Dola 10,000, Julai 11, 2014 alilikopesha Dola 3,000, Julai 15, 2014 alilikopesha mkopo wa Dola 14,000.

Malinzi anadaiwa Julai 15, 2014 alighushi risiti kuonesha alilikopesha shirikisho hilo Dola 4,000, Julai 25, 2014 alilikopesha Dola 1,000, Agosti 19, 2014 alilikopesha Dola 5,000, Oktoba 11, 2014 alilikopesha mkopo wa Dola 1,200, Agosti 17, 2015 alilikopesha Dola 5,000, Julai 22, 2015 alilikopesha shirikisho hilo Dola 2,000 na Mei 9, mwaka jana, alilikopesha mkopo wa Dola 7,000.

Mashitaka mengine, Malinzi anadaiwa Juni 16, 2016 alighushi risiti akidai kwamba alilikopesha shirikisho hilo Dola 10,000, Agosti 2, mwaka jana, alilikopesha Dola 1,000, Septemba 19, mwaka jana, alilikopesha Dola 1,000 na Septemba 22, mwaka jana, alilikopesha shirikisho hilo mkopo wa Dola 15,000 wakati akijua si kweli.

Malinzi, Selestine na Nsiande wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 jijini Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la kutakatisha fedha na kujipatia Dola za Marekani 375,418 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kughushi.

Rais huyo wa TFF na Selestine wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, mwaka jana kwenye benki ya Stanbic tawi la Kinondoni, Dar es Salaam  kwa pamoja walijipatia Dola za Marekani 375,418 kutoka kwenye benki hiyo wakati wakijua upatikanaji wa fedha hizo ni  zao la kosa la kughushi.

Nsiande anadaiwa katika kipindi hicho, kwenye ofisi za TFF  aliwasaidia Malinzi na Selestine kujipatia fedha kutoka benki ya Stanbic ambazo ni Dola za Marekani 375,418 huku akijua zimepatikana kwa udanganyifu kwa kosa la kughushi nyaraka ya kuhamisha fedha.

Washitakiwa hao waliposomewa mashitaka yao waliyakana.

No comments:

Post a Comment