KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, July 18, 2017

KAMATI YA NIDHAMU TFF YAMTOA KIFUNGONI HAJI MANARA


Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imefuta adhabu dhidi ya wanafamilia wanne waliofungiwa kushiriki masuala la soka
kwa mwaka mmoja.
 

Wanafamilia hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa, James Mwakwinya; Mwenyekiti wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Blassy Kiondo; Kaimu Katibu wake, Ayoub Nyaulingo pamoja na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.

Haji Manara alitiwa hatiani Aprili 23, mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu na za chuki kwa viongozi wa TFF na kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya
mchezaji Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar ambako alifungiwa kushiriki masuala ya mpira kwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni tisa.

Viongozi wa RUREFA walifungiwa kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. milioni mbili kwa kila mmoja kwa makosa ya kukiuka maagizo ya viongozi wa Kamati
ya Uchaguzi ya TFF iliyotaka wasitishe mchakato wa uchaguzi mkoa kwa kuwa kulikuwa na rufaa iliyokatwa TFF.

Akizungumza na Wanahabari leo Julai 17, 2017 Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Tarimba Abbas, alisema viongozi hao wamesamehewa
adhabu zao kwa kuwa waliomba kupitiwa upya kwa mashauri yao na kamati imeona ni bora kuwaachia huru ili kuendeleza masuala ya soka.

“Wapo wengi waliofungiwa wengine maisha na wengine adhabu fupi, msamaha huu ni kwa wale ambao wameomba tu kupitiwa upya kwa adhabu
zao, pia milango ipo wazi kwa wengine ambao wanataka kupitiwa kwa mashauri yao, lakini si kwa wale waliopanga matokeo uwanjani,” alisema
Tarimba.

Kadhalika, Tarimba aliwaomba viongozi wa TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na Viongozi wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kuepuka
maneno machafu ambayo yanasababisha wao kufungiwa.

“Inaonekana viongozi na Maofisa Habari hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa soka na ndio maana matatizo ya kufungiwa yanajitokeza mara
kwa mara, naamini wakipata semina hiyo itawasaidia kujirekebisha na kupunguza kesi kama hizo,” alisema Tarimba.

No comments:

Post a Comment