KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 14, 2017

MAZOEZI AZAM DOZI MWANZO MWISHO



DOZI mwanzo mwisho! Hivyo ndivyo unavyoweza kuyaelezea mazoezi ya Azam FC ya kujiandaa na msimu ujao, ambapo imeanza kujifua kwa staili ya aina yake kwa wachezaji kupewa dozi mara tatu kwa siku.

Huo ni mwendelezo wa mazoezi ya Azam FC tokea ilipoanza maandalizi ya msimu mpya Mei 28 mwaka huu, ikiwa na kikosi chenye sura mpya za wachezaji wengi vijana wenye vipaji vya hali ya juu na baadhi wakiwa ni wazoefu.

Mazoezi hayo ni maalumu kabisa katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu ujao, ambapo Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amepanga kutengeneza kikosi kikali kitakachoweza kufanya makubwa katika siku za usoni.

Kikosi hicho leo kimeshafanya mazoezi mara mbili, saa 1.00 asubuhi na 3.30 asubuhi na kitamalizia dozi ya mwisho saa 11.00 jioni ndani ya viunga vya Azam Complex, Chamazi.

Cioaba amesema faida kubwa ya kufanya mazoezi makali hivi sasa ni kuwajenga wachezaji kwenye maeneo mbalimbali, kiufundi uwanjani, stamina na ustahimilivu kwenye kupambana.

Baada ya kumaliza programu hiyo ya mazoezi, Azam FC itasafiri Julai 20, mwaka huu kuelekea kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikienda kucheza mechi tatu za kirafiki, ya kwanza ikiwa ya mwaliko dhidi ya Mbeya City, itakayofanyika Julai 22 katika siku watakayokuwa wakisherehekea Mbeya City Day.

Mechi nyingine za kirafiki itacheza na timu mbili zilizopanda daraja. Njombe Mji Julai 24 mwaka huu mjini Njombe na ikimaliza ziara hiyo kwa kukipiga na Lipuli ya Iringa Julai 26 kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Julai 27.

No comments:

Post a Comment