Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kundi C, Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) imeingiza sh. 502,131,000 kutokana na watazamaji 57,203.
Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 76,596,254.24 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 7,809,104.
Asilimia 15 ya uwanja sh. 62,658,846.26, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 83,545,128.35 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 20,886,282.09.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 250,635,385.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 12,531,769.25 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
Mechi iliyopita ya Stars dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) kwenye uwanja huo iliingiza sh. 226,546,000.
'
Monday, June 17, 2013
TAIFA STARS KAMBINI TENA JULAI 4
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameiita tena kambini timu hiyo Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inavunja kambi leo (Juni 17 mwaka huu) baada ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, kundi C Kanda ya Africa dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa jana (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kim amesema wachezaji watakaoitwa kambin ni wote walioko kwenye timu hivi sasa isipokuwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika klabu ya TP Mazembe Englebert.
Wachezaji hao ni Juma Kaseja, Aishi Manula, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.
Mechi hiyo namba 37 dhidi ya Uganda (The Cranes) itachezwa jijini Dar es Salaa kati ya Julai 12 na 14 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika wiki mbili baadaye katika Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.
President Kikwete Tours Sunderland Football Club
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete and Chairman and owner of Sunderland Football Club Mr.Ellis Short pose with some students who study football skills at the club’s Academy of Light in Sunderland yestarday afternoon. The Club in collaboration with Symbion Power Tanzania Limited have agreed to build a state of the art football academy in Dar es Salaam at the request of President Kikwete. President Kikwete is London for a three days working visit.
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete talks to pupils attending some lessons on football skills AND HEALTH at Sunderland’s Association Football Club Academy of Light in Sunderland yestarday afternoon.
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete in conversation with Sunderland’s Association Football Club Chairman and owner Mr.Ellis Short at the Club’s Stadium of Light in Sunderland yestarday afternoon.
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete and his delegation pose with some students who attend football training at Sunderland’s Association Football Club Stadium of Light Academy yestarday afternoon. Others in picture from left are Symbion’s Power Limited CEO Mr.Paul Hinks(left), Ilala member of parliament Hon. Musa Zungu(Second left), Minister for Information,Youth ,Culture and Sports Dr.Fenella Mukangara(fourth left) and Minister for Land and Human Settlement Prof.Anna Tibaijuka(right).
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete unveils Sunderland’s Association Football plaque at the club’s Academy of Light yestarday afternoon when the President and his delegation toured the club. On the left, looking on, is the Club’s Chairman and Owner Ellis Short.(photo by Freddy Maro).
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete talks to pupils attending some lessons on football skills AND HEALTH at Sunderland’s Association Football Club Academy of Light in Sunderland yestarday afternoon.
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete in conversation with Sunderland’s Association Football Club Chairman and owner Mr.Ellis Short at the Club’s Stadium of Light in Sunderland yestarday afternoon.
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete and his delegation pose with some students who attend football training at Sunderland’s Association Football Club Stadium of Light Academy yestarday afternoon. Others in picture from left are Symbion’s Power Limited CEO Mr.Paul Hinks(left), Ilala member of parliament Hon. Musa Zungu(Second left), Minister for Information,Youth ,Culture and Sports Dr.Fenella Mukangara(fourth left) and Minister for Land and Human Settlement Prof.Anna Tibaijuka(right).
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete unveils Sunderland’s Association Football plaque at the club’s Academy of Light yestarday afternoon when the President and his delegation toured the club. On the left, looking on, is the Club’s Chairman and Owner Ellis Short.(photo by Freddy Maro).
LUCY NDIYE MREMBO WA MWANZA
SHINDANO la kumsaka mrembo wa mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2013, kiliteguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Lucy Charles, msomi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kuwabwaga warembo wengine 13 waliojitokeza kuwania taji hilo.
Nyota ya mrembo huyo ilianza kuonekana mapema katika mavazi yote aliyovaa, lakini zaidi aliwapagawisha mashabiki wa urembo waliofurika katika ukumbi wa Yatch club baada ya kujibu swali kwa ustadi lililouliza ni changamoto ipi kubwa walionayo vijana wa leo.
Mshindi wa pili katika shindano hilo alikuwa Judith Josephat na mshindi wa tatu ni Suzan Ikombe.
Washindi hao watauwakilisha mkoa wa Mwanza katika shindano la kanda ya ziwa litakalofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Sunday, June 16, 2013
TAIFA STARS YACHAPWA 4-2 NA IVORY COAST
MATUMAINI ya timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 leo yameyeyuka baada ya kuchapwa mabao 4-2 na Ivory Coast katika mechi ya kundi C iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimeifanya Taifa Stars iporomoke nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tano, ikiwa nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa kuwa na pointi 13, ikifuatiwa na Morocco yenye pointi nane. Gambia inashika mkia kwa kuambulia pointi moja.
Licha ya kufungwa, Taifa Stars ilionyesha kiwango cha juu cha soka na magoli yake yalikuwa ya kifundi zaidi ikilinganishwa na wapinzani wao, ambao mabao yao yalitokana na makosa ya kizembe ya mabeki wa Tanzania.
Mshambuliaji Yaya Toure anayechezea klabu ya Manchester City ya England ndiye aliyeibeba Ivory Coast baada ya kuifungia mabao mawili kati ya manne.
Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya kwanza mfungaji akiwa Amri Kiemba baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mbwana Samatta kufuatia mpira wa kurushwa na Erasto Edward Nyoni kusababisha kizazaa langoni mwa Tembo wa Abidjan.
Ivory Coast ilisawazisha bao hilo dakika ya 15 kupitia kwa Lacina Traore baada ya mabeki wa Stars kuzembea kuokoa na Yaya Toure akafunga la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 23, nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars ilirudi mchezoni na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 35 mfungaji Ulimwengu aliyeunganisha krosi maridadi ya Shomary Kapombe. Hata hivyo, Ivory Coast wakapata penalti rahisi baada ya Gervinho kujiangusha wakati anakabiliana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ . Bao hilo lilifungwa na Yaya Toure dakika ya 43.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen dakika ya 87 kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Vincent Barnabas yaliigharimu Tanzania kwa kufungwa bao la nne na kupotea kabisa mchezoni.
Baada ya kutoka Kazimoto, aliyetekeleza majukumu yake vizuri leo, Ivory Coast wakatawala sehemu ya kiungo na kutengeneza bao la nne lililofungwa na Bonny Wilfred dakika ya 88.
Taifa Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe/Khamis Mcha dk 85, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto/Vincent Barnabas dk 87, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Amri Kiemba.
Ivory Coast: Boubakar Barry, Arthur Boca, Didier Zakora, Solomon Kalou/Sio Giovanni, Gervais Yao, Jean Jarques Gosso Gosso, Alain Aurier, Lacina Traore/Bonny Wilfred, Yaya Toure, Geoffrey Serey na Suleiman Bamba/Nori Koffi Christian.
Friday, June 14, 2013
KAISHANGILIENI TAIFA STARS KESHO-KAVISHE
WADHAMINI wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager wamewaomba watanzania washikane na kuungana pamoja wakati wa mechi dhidi ya Ivory Coast kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwani kuna watanzania ambao tayari wamekata tamaa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema Taifa Stars inatakiwa kuungwa mkono na kushangiliwa kwa nguvu kwani wachezaji wameonesha kuwa wana uwezo.
“Hawa ni wanajeshi wetu…nawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi…tuwape sapoti na tuoneshe uzalendo kwani kwenye mpira lolote linawezekana,” alisema. Kavishe alisema watanzania lazima welewa timu hii bado ni changa na ina wachezaji wapya wenye umri mdogo ambao wameonesha uwezo mkubwa.
“Hata ikitokea tusifuzu kwenda Kombe la Dunia, vijana wameshaonesha dalili nzuri na tuna imani tutafanya vizuri katika mashindano mengine kama AFCON na CHAN,” alisema.
Aliwataka wachezaji kutulia uwanjani na kutobabaishwa na ukubwa wa timu ya Ivory Coast kwani wana uwezo wa kuwafunga na kushangaza dunia nzima Jumapili.
“Hii ni kama fainali kwa Ivory Coast na wao pia wamebabaika na kuitilia maanani kabisa mechi hii kwa sababu tukiwafunga ina maana hawatakuwa na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata,” alisema Kavishe.
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetimiza mwaka mmoja tangu ianze kuidhamini Taifa Stars na wadau mbalimbali wamesifia udhamini huu kwani umeleta mabadiliko makubwa katika timu ya Taifa.
Timu ya Ivory Coast iliwasili nchini Alhamisi usiku na imeweka kambi katika hoteli ya Bahari Beach, Kunduchi tayari kwa mechi itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa JUmapili hii saa tisa kamili.
Kwa mujibu wa TFF maandalizi yote yamekamilika na mechi hii inatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya watanzania watakaojitokeza uwanjani na kupitia runinga pia. Ivory Coast inaongoza katika kundi C ikiwa na pointi 10, Tanzania ya tatu na pointi 6, Morocco ya tatu na pointi 5 na Gambia ni ya nne na pointi 1.
Wakati timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao kesho.
Mkutano huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast inafanya mazoezi yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya Gymkhana.
Timu zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9 kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9 kamili alasiri.
Wakati huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana (Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na Uwanja wa Taifa.
Mauzo yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa sh. 50,000 katika ofisi za TFF.
SIMBA, YANGA RUKSA KWENDA DARFUR, LAKINI CECAFA YAZIPIGA CHINI
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
SERIKALI imeziruhusu klabu za Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Super Falcons ya Zanzibar kwenda Sudan kushiriki michuano ya Klabu Buingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amefanya Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dodoma asubuhi ya leo kusema wameruhusu klabu hizo ziende Sudan baada ya kuhakikishiwa na Serikali ya nchi hiyo kwamba itatoa ulinzi wa kutosha dhidi ya timu za Tanzania.
Makalla amesema wameandikiwa barua na Serikali ya Sudan ikiwahakikishia kwamba timu za Tanzania zitapewa ulinzi mkubwa zisiathirike na machafuko yanayoedelea Sudan.
Kufuatia tamko la Serikali kuziruhusu klabu hizo sasa ziende Sudan, sasa ni juu yao ya klabu hizo kuamua kwenda au kutokwenda.
Lakini Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Mkenya Nicholas Musonye amekwshatishia atazichukulia hatua kali klabu hizo zisipokwenda.
Juzi Serikali kupitia Makalla ilitoa tamko la kuzuia klabu za Tanzania kutokwenda Sudan kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kufuatia tamko hilo, jana Yanga, ambao ni mabingwa watetezi kwa miaka miwili mfululizo, walitangaza kuvunja kambi yao hadi wiki mbili baadaye, wakati Kombe la Kagame linaanza kutimua vumbi Juni 18, mwaka huu.
Yanga wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman ya Somalia na APR ya Rwanda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
TFF YATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa notisi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho utakaofanyika Julai 13 mwaka huu kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda moja ya marekebisho ya Katiba.
Notisi hiyo imetolewa juzi (Juni 12 mwaka huu). Rais ameitisha Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Katiba ya TFF baada ya kupata maagizo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa barua yake ya Aprili 29 mwaka huu.
Ajenda rasmi na taarifa nyingine zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(4) ya Katiba ya TFF.
Wanachama wa TFF ambao ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu wanatakiwa kutuma majina ya wajumbe halali. TFF inapenda kuwakumbusha wanachama wake kutuma majina ya wajumbe halali ili kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo.
Ni vizuri kuhakikisha kuwa jina linalotumwa ni la mjumbe halali wa Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya TFF.
RAMBIRAMBI KIFO CHA ABDALLA MSAMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Pan Africans, Simba na Taifa Stars, Abdallah Msamba kilichotokea juzi usiku (Juni 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Msamba akiwa mchezaji, na baadaye kocha wa timu kadhaa alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Villa Squad, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Msamba, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na klabu ya Villa Squad na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko ya mchezaji huyo yamefanyika leo (Juni 14 mwaka huu) katika makaburi ya Ndugumbi mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo wachezaji wa zamani na viongozi mpira wa miguu nchini. Mungu aiweke roho ya marehemu Msamba mahali pema peponi. Amina
TENGA AMPONGEZA RAIS MPYA WA ZFA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amempongeza Rais mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous Faina aliyechaguliwa katika uchaguzo mdogo uliofanyika hivi karibuni.
Amesema ushindi aliopata Faina unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA walivyo na imani naye katika kuhakikisha maendeleo ya mpira wa miguu visiwani humo.
Rais Tenga amesema ni imani yake kuwa Rais Faina ataendeleza ushirikiano uliopo kati ya TFF na ZFA kwa ajili ya ustawi wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumtakiwa kila kheri katika wadhifa wake huo mpya.
WAAMUZI WATATU WAFUNGIWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefungia miezi mitatu waamuzi watatu walioshindwa kuchezesha mechi namba 32 ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Mpwapwa Stars ya Dodoma na Machava FC ya Kilimanjaro iliyokuwa ichezwe Juni 2 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
TFF kupitia Kamati yake ya Waamuzi iliyokutana katika kikao chake cha Juni 12 mwaka huu kupitia taarifa mbalimbali za waamuzi wa RCL ilibaini makosa yaliyofanywa na baadhi ya waamuzi na kuyatolea uamuzi.
Waamuzi hao waliofungiwa ambao wanatoka mkoani Singida ni Jilili Abdallah, Amani Mwaipaja na Theofil Tegamisho. Wamefungiwa kwa kutoripoti katika kituo walichopangiwa (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma) na kutoa taarifa ya uongo kwa kushirikiana na Kamishna wa mechi hiyo.
Kanuni iliyotumika kuwafungia ni ya 28 kifungu (d) na (g) ya Ligi za TFF, na adhabu hiyo imeanza Juni 13 mwaka huu.
Waamuzi hao pamoja na kamishna badala ya kwenda Uwanja wa Jamhuri, wao walikwenda kwenye Uwanja wa Mgambo ulioko Mpwapwa na kuandika ripoti iliyoonesha kuwa timu ya Machava FC haikufika uwanjani wakati wakijua kuwa mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa katika Uwanja wa Jamhuri
MR. NICE ATOSWA, CHAMELEONE ANG'ARA MAREKANI
NAIROBI, Kenya
KAMPUNI ya Grandpa Records ya Kenya imevunja mkataba wake na mwanamuziki Lucas Nkenda 'Mr. Nice'.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Refigah Slams amelieleza gazeti la Daily Nation la Kenya wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya Mr. Nice kukiuka makubaliano kati yao.
Mr. Nice, ambaye amehamishia makazi yake nchini Kenya, aliingia mkataba na kampuni hiyo miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kusimamia kazi zake.
"Tumeamua kumwondoa Mr. Nice katika udhamini wa Grandpa Records kutokana na kukiuka makubaliano yetu," alisema Slams.
Slams amemwelezea Mr. Nice kuwa ni mtu asiye na ushirikiano na ni mgumu kufanya naye kazi.
Alisema tangu walipoingia naye mkataba, mwanamuziki huyo wa kitanzania amesababisha matatizo mengi katika kampuni yake, ambayo hakuwa tayari kuyataja.
"Kwa kifupi, Mr. Nice alikuwa ameingia mikataba na Sallam Sharaf na Lamar wa Tanzania na hakutueleza wakati anaingia mkataba na Grandpa Records,"alisema.
Mr. Nice alitarajiwa kufanya uzinduzi wa albamu yake mpya ya Chali wa Kibera hivi karibuni chini ya udhamini wa kampuni hiyo.
Katika hatua nyingine, mwanamuziki nyota wa Uganda, Jose Chameleone amezindua albamu yake mpya inayojulikana kwa jina la Badilisha nchini Marekani.
Chameleone alifanya uzinduzi wa albamu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya wiki mbili nchini Marekani.
Mtandao wa Msn uliripoti juzi kuwa, tayari mwanamuziki huyo tajiri wa Kiganda ameshafanya maonyesho katika miji ya Seattle na Los Angeles.
Kwa mujibu wa mtandao huo, Chameleone anatarajiwa kufanya maonyesho mengine katika miji ya Dallas na Texas kabla ya kurejea Uganda mwezi ujao.
SIJAACHWA, NAIFURAHIA NDOA YANGU-INI EDO
LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI mwenye mvuto wa Nigeria, Ini Edo amesema si kweli kwamba ndoa yake na mumewe, Philip Ehigwina imevunjika.
Ini aliueleza mtandao wa Nigeriafilms wiki hii kuwa, hana matatizo yoyote na mumewe na kwamba anaifurahia ndoa yake.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti hivi karibuni kuwa, Ini hana furaha kwa sasa kutokana na ndugu wa mume wake kushinikiza aachwe.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ndugu wa Philip hawafurahii kuona kuwa, mcheza filamu huyo ameshindwa kumzalia mtoto ndugu yao baada ya kuolewa miaka minne iliyopita.
"Mashemeji na wakwe wa Ini Edo wamemweleza Philip amuache kama hawezi kumzalia mtoto," zilieleza taarifa hizo.
Hata hivyo, Ini amekanusha vikali taarifa hizo kwa kusema kuwa, hana matatizo na mumewe wala ndugu zake.
"Sitajali mtakachoandika kama kitabadili ukweli kwamba naifurahia ndoa yangu. Nadhani mnapaswa kuachana na uzushi huu,"alisema In.
"Tangu siku ya kwanza nilipoolewa, mmekuwa mkizusha mambo mengi ya kishetani kwangu. Sielewi ni kwa nini hamtaki kuachana na upuuzi huu. Kamwe haitatokea,"alisisitiza.
NIMERITHI FIGA YA MAMA YANGU-OMOTOLA
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Omotola Jalade amesema hajawahi kufanya operesheni ya aina yoyote kwa ajili ya kuupendezesha mwili wake.
Akihojiwa na gazeti la Encomium la Nigeria wiki hii, Omotola alisema amerithi umbile alilonalo kutoka kwa mama yake mzazi.
Mwanamama huyo mwenye sura na umbile lenye mvuto alisema amekuwa akifanya shughuli mbalimbali ili aweze kubaki kama alivyo.
"Hakuna siri katika mwonekano wangu, huo ndiyo ukweli ulivyo. Ukitazama picha ya mama yangu, anaonekana kama msichana. Hadi anafariki, tulizoea kumwita msichana,"alisema.
"Mama yangu alikuwa na umbile la kisichana hata alipokaribia kufikisha umri wa miaka 50. Alikuwa na umbile la kike hasa. Amenirithisha umbile hilo," aliongeza.
Omotola alisema ni kazi ngumu kulifanya umbile lake libaki kama lilivyo kutokana na mazingira ya kazi yake.
Mcheza filamu huyo aliyeolewa na rubani wa ndege na kuzaa naye watoto wanne, alisema pia kuwa hajawahi kutumia dawa za aina yoyote ili kunenepesha 'hips' zake.
"Hata mimi nimekuwa nikizisikia habari hizo, lakini hakuna kitu kama hicho. Kamwe sijawahi kutumia dawa ama kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kunenepesha hips zangu,"alisema.
"Ni suala tu la kuwa mwangalifu na makini katika mwili wangu, kazi na kila kitu,"alisisitiza mwanamama huyo, ambaye pia ni mwanamuziki.
MTIBWA YAITEGA YANGA
UONGOZI wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro umesema hauna mpango kupokea mchezaji yoyote kutoka Yanga kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, hawako tayari kufanya makubaliano ya aina hiyo na Yanga kwa sababu viongozi wake vigeugeu.
Bayser alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na viongozi wa Yanga kuwageuka msimu uliopita kwa kumuuza kipa Shaaban Kado kwa klabu nyingine bila ridhaa yao.
"Hivi sasa tuko makini sana na Yanga. Msimu uliopita walikuja kwetu na kumtaka Said Bahanuzi, tukawapa kwa masharti kwamba watupatie Shaaban Kado kwa mkopo, lakini wakaja kumuuza bila ya kutupatia taarifa,"alisema.
Kutokana na kufanyiwa kitendo hicho, Bayser alisema hawako tayari kuingia makubaliano yoyote na viongozi wa Yanga kuhusu usajili wa wachezaji wao.
"Kuanzia msimu ujao, hatutamsajili mchezaji yoyote kutoka Yanga kwa mkopo kwa vile viongozi wake vigeugeu na tumekuwa tukishindwa kuwaelewa,"alisisitiza.
Akizungumzia usajili wa kikosi chake, Bayser alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na imekuwa ikifanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka kufanya makosa.
Bayser alisema usajili wao utalenga zaidi kuziba mapengo ya wachezaji waliohama na wale, ambao kiwango chao kimeshuka.
Hadi sasa, Mtibwa Sugar imewapoteza mabeki wake wa kati, Issa Rashid, alisajiliwa na Simba na Rajab Zahir, aliyesajiliwa na Yanga.
Hata hivyo, Bayser amesema hawana taarifa yoyote kuhusu klabu za Simba na Yanga kuwasajili wachezaji hao wawili kwa vile hazijafuata taratibu za kuwahamisha.
KIFO CHA MANGWEA KIWE DIRA KUPAMBANA NA MANYANG'AU
NA STEPHEN BALIGEYA
NIMEFARIJIKA sana, nimefurahishwa sana na nimepata nguvu sana. Watanzania wamenifanya nijisikie hivyo, wamenipa ujasiri wa kugeuza mlima kuwa tambarare. Kweli nawashukuru sana.
Hali hiyo inatokana na kile nilichokiandika wiki iliyopita juu ya kifo cha Albert Mangweha. Kifo ambacho niliuliza kwa nini watu wanamlilia na kumsifu kwa maneno matamu baada ya kufa na wakati walishindwa kufanya hivyo akiwa hai?
Nikauliza tena, kwa nini baadhi ya redio zilishiriki kumuua Mangweha kisanii wakati wa uhai wake kwa kukataa kupiga nyimbo zake lakini baada ya kuaga dunia zikajifanya zilimpenda sana na kusifu uwezo wake kiusanii?
Niliuliza, kama redio hizo zingepiga nyimbo za Mangweha kama zilivyopiga wakati wa msiba wake, msanii huyo angekuwa tajiri kiasi gani kwa kupata matamasha na kuuza kazi zake ambazo zimetangazwa sana baada ya kufa?
Katikati ya dimbwi la kufikiria juu ya kifo hicho, nimepata simu nyingi na ujumbe wa maandishi kiasi cha kutisha. Kumbe Watanzania wana dukuduku lakini watasemea wapi?
Taaluma ya habari ni kazi ya jamii. Unafanya kazi kwa maslahi ya jamii pana na si kulitumikia kundi dogo, ambalo linanenepa kwa damu za walio wengi. Kazi ya taaluma hii ni kuwa msemaji na mtetezi wa jamii.
Leo napenda kutoa somo kwa wasanii, ambao kwa kuchukua kifo cha Mangweha kama darasa, wanatakiwa sasa kuamka.
Kuamka huko kuwe na mtazamo mpana miongoni mwao, kwa kutambua kwamba leo mwenzao amefariki kama ngao ya ukombozi wao. Kifo cha Mangweha kiwe kama sadaka ya ukombozi kwao.
Lazima wafikirie namna wenye mabavu watakavyowatumia baada ya kuaga dunia na namna watu hao watakavyonufaika baada ya kuwekwa kaburini.
Kifo cha Mangweha kimeonyesha usanii na unyang’au wa wenye redio, ambao walimtumia Mangweha kama njia ya kuongeza umaarufu wa vituo vyao, lakini pia kujitafutia maslahi zaidi.
Wale walioshiriki kumuua Mangweha kiusanii kiasi cha kumfanya aishi maisha magumu na ya shida, wakafikia hatua ya kusafiri hadi Afrika Kusini ili kuwapasha namna Mangweha alivyofariki.
Wakadiriki kwa mbinu za kimafia kukanusha hata taarifa ya daktari juu ya mwili wa msanii huyo kukutwa na chembe za dawa za kulevya. Kwa nini walikanusha habari za namna hiyo?
Jibu ni rahisi. Kwa sababu msanii huyo alipata msongo wa mawazo kutokana na kazi zake kutupiliwa mbali na hao, ambao wamejifanya ndugu zake.
Msongo huo wa mawazo ulimfanya msanii huyo kujifariji kwa kutumia dawa za kulevya. Lazima Watanzania watambue kwamba kama mtu anakosa mshauri wa haraka wakati anapata msongo wa mawazo, anaweza kutumia njia yoyote iwe halali au haramu kujifariji.
Mangweha alikuwa mhanga wa tatizo hilo. Akajifariji kwa kile kinachoelezwa dawa za kulevya. Marafiki wake wa karibu wanalieleza hili kwa ufasaha. Ripoti ya uchunguzi inaeleza haya kwa ufasaha.
Wale walioshiriki kumuua kwa msongo wa mawazo wakajitosa kupotosha ukweli huu kwa vile walijua fika kwamba kitendo hicho kitawatia fedheha.
Lakini kwa vile hawana soni katika nyuso zao na mioyo yao, wakajifanya wasemaji wa familia ya Mangweha. Wakawateka baadhi ya ndugu wawe wasemaji kupitia redio zao. Huku kote ni kuzidi kuonyesha uibilisi wao uliokamaa.
Tabia hii ya kishetani haikuishia hapo. Bado wakajifanya watalaamu wa kualika wasanii katika redio zao ili wawe wanaeleza uzuri wa Mangweha, lakini nadiriki kusema kwamba wamefanikiwa kidogo maana Watanzania walio wengi wamenasua usanii huo.
Kifo cha Mangweha kiwe funzo kwa wasanii, ambao wamekuwa wakitumikishwa na watu hao, ambao wanasubiri wafe ili waweze kuwasimulia na kuwaeleza kwa uzuri, ambao hawawezi kuelezwa wakiwa hai.
Wananyimwa matamasha, wananyimwa nyimbo zao kupigwa kwenye redio za manyang’au hao, lakini wanasubiri wasanii, ambao wanatumia nafasi hiyo kama ajira badala ya kuiba wafe ili waeleze uzuri wa marehemu.
Marehemu alikuwa mtu mzuri sana, marehemu alikuwa msanii wa kisasa, marehemu alikuwa na malengo makubwa, marehemu alikuwa mtu wa watu, marehemu alikuwa na singo aliyotaka kuachia na ujinga mwingine mwingi tu juu ya sifa za marehemu.
Leo wasanii wanapeleka nyimbo zao zinakaliwa kama hawatakubali masharti ya kinyonyaji. Msanii anatumiwa kwenye matamasha kwa sh. 100,000 na akidai malipo mazuri, anafungiwa duniani na kuzimu.
Matokeo yake wasanii wamekuwa vijibwa vya watu hao. Wasanii wamekuwa watumwa, wanatumikishwa kwa stahili zote, hata zile ambazo hawazitaki.
Wanavumilia upuuzi wote ambao unaua utu wao, lakini fadhila zao watazipata wakifa, pale watakaposifiwa na kunakishiwa kwa rangi zote. Huu ni ujinga ambao Watanzania wanatakiwa kuupinga.
Wasanii sasa waungane, waache kujiona kwamba kwa vile baadhi yao mambo yanawaendea vizuri, basi hawana haja ya kuungana na wenzao wanaouawa kisanii na magabachori hao.
Umoja wao utakuwa nguzo yao kuu kujikomboa, utengano wao utashuhudia sifa zao baada ya kufa, sifa ambazo zitakuwa mithili za malaika aliyeishia duniani.
Lazima wapiganie sifa hizo wapewe wangali hai, hali itakayowasaidia kuinua vipato vyao, kwa maslahi yao, familia na taifa kwa jumla.
Lazima wajiulize ni wasanii wangapi wamekufa kisanii kwa sababu ya uhuni wa watu hao, ambao bado wanaendeleza mapambano kwa wasanii wenye fikra hai?
Kama mgogoro unaofukuta leo na baadhi ya wasanii ungekuwa unahusu wasanii wadogo, kifo cha wasanii hao kingekuwa karibu lakini kazi bado imekuwa ngumu kwao.
Naandika haya si kwa maslahi ya wasanii na umma wa Watanzania kwa jumla, kwani watoto wenye vipaji wanatoka katika jamii zetu, hawana ajira na wanategemea vipaji vyao kujiajiri.
Taifa haliwezi kuendelea kwa watu wote kufanyakazi ofisini. Kazi ya sanaa itaajiri watu wengi kama kutakuwa na fursa sawa kwa vijana hao kufanya kazi zao na kunufaika na kazi zao.
Kwa msingi huo, wasanii na jamii nzima lazima kuungana kupambana na watu hawa ambao wanadhani wako juu ya sayari nyingine katika kuua vipaji vya vijana na kisha wawatumie katika vifo vyao.
Kwa maoni na ushauri, 0752646838,0713976894.
WASOMAJI WA LIWAZOZITO WALIVYOMLILIA MANGWEA
Much respect kwa makala yako. Media zimekuwa na unafiki baada ya msanii kufariki dunia. 0759928344
Uko sawa kaka, yaani wanakera sana.0774401918.
Ni ukweli usiopingika kipindi cha uhai wa Mangweha nyimbo zake hazikusikika redioni wala kwenye televisheni, ila kila siku ya kifo kuna redio zilishinda zinapiga nyimbo zake. Enzi za uhai wake hatukuweza kusikia wimbo wa Mangweha hata mara moja kwa mwaka. Ni ukweli kuwa wasanii wa Tanzania wananyonywa sana na yakitokea mambo kama haya wanaanza kumsifia ujinga, alikuwa mtu wa watu, alikuwa mpole, jamani tumuogope Mungu, uwezo uliopewa na Mungu kisiwe kigezo cha kuwakandamiza wenzako, chonde chonde. 0752752132 Katoro-Geita.
Ipo siku moja watajuta kwa dhambi waliyomfanyia mangweha. 0774629813
Pole na kazi, nakupongeza kwa kuandika makala ya kifo cha mangweha, tunamlilia mangweha baada ya kufa. Safi sana, unajua kazi.Bukoba. 0754648041.
Ebwana kaka Baligeya, mi naitwa Seif Omary, nipo UDOM mwaka wa kwanza Kiswahili Fasihi, yaani uliyoandika ni ukweli kabisa, lakini ni vyema yasiishie hapa, uendelee kuandika makala kama hizi ili kuwaamsha wasanii mazuzu wasiojitambua.0769867781.
Mambo vipi mkubwa, nimelisoma gazeti la Burudani na kusoma makala yako inayohusu kifo cha mangweha. Kiukweli hata mimi ilikuwa inaniboa kila stesheni kupiga nyimbo zake tena na kutoa wasifu wake. Kama kweli wapo karibu naye, mbona hawakutangaza anakwenda Afrika Kusini wakati alipokuwa hai. Hizi stesheni za redio ni za kinafiki. 0719522328.
Ni kweli ndugu vyombo vya habari baadhi ni wanafiki. Mungu huwa analipa hapa hapa duniani, leo kwa huyu, kesho kwao.0764157865
Bwana Stephen Baligeya, umeongea yaliyokuwa moyoni mwangu (Tunamlilia mangweha baada ya kufa). Ni kweli kabisa kwamba vipo vyombo vya habari vinavyoua masoko ya wasanii na kuwafanya waishi kwa shida. Vyombo hivyo tunavijua mpaka majina. By Mzaile Bokilo, nipo Misungiwi-Mwanza 0757283585.
Kaka nakupa pongezi kwa kutowaonea haya waliomnyonya Mangweha mpaka kabaki mifupa mitupu. Matatizo yote wamesababisha wao. Hili ni fundisho kwa wasanii wa bongo, ningependa wamuunge mkono P Funk.
Tatizo la wasanii wa Tanzania hawana kauli moja.0752805090.
Habari kaka, naitwa Paskacaly Mbasha. Kiukweli mi mwenyewe sikuamini kile kilichosemwa na vyombo vya habari kwamba Mangweha ametoweka duniani. Lakini nimekuja kuamini katika kuaga mwili wake.
Machozi yalinitoka bila mwenyewe kujielewa. Inauma sana brother. Kiukweli umimi ndio unaangamiza au unashusha maendeleo ya wasanii wetu. Kumpaisha mwenzako sidhani kama wewe unaweza ukabaki chini, tumekuwa mbele na kujionyesha tunawajali pale wanapopatwa na mauti, tunawasahau pale wanapokuwa na matatizo. Kama kukusanya michango na kuweka majukwaa inawezekana, inashindikana vipi kufanya hivyo wakiwa hai? Naungana na wewe kuwa ni wanafiki na wazandiki, kuweka majukwaa na kupigwa nyimbo zake utadhani wanasherehekea badala ya kuomboleza. Big up brother.0768839171.
Ebwana kaka unatisha. Nimependa makala yako kuhusu kifo cha Mangweha. Umesema mambo ambayo hata mimi yamenikera kabisa. Big up. Kutoka Mwanza.0769096013
Kaka makala yako imenigusa, lakini ungefanya kudokeza kidogo hizo stesheni za radio ili tuwajue waliojifanya wanampenda Mangweha wakati wa mauti kuliko kutuacha na mafumbo.0766915346.
Naomba hizo stesheni zianikwe ili nyingine ziogope. Haiwezekani msanii afe ndio apate umaarufu. Wengine leo ndio wanamjua Mangweha. Naitwa Joseph Sanga kutoka Igunga Tabora.0768603090.
Nakupongeza sana kwa kulijua hili na kupata ujasiri wa kulizungumzia. Itakuwa fundisho kwa vyombo vya habari.0714136226.
Kaka makala hii ya Mangweha umesema ukweli na mimi sina zaidi ya kuunga mkono juu ya jambo hili. Uko sahihi na kuna wasanii wangelitambua hili mpaka leo hii Mangweha angekua hai.0659380040.
Mbona kwenye makala yako unakandamiza chombo kimoja tu cha habari? Kama kweli wewe umekereka, ungetaja media zote sio kuponda sehemu moja tu. Hata sisi wananchi tuna makosa kwa sababu hatutoi support kwa wasanii wetu, hatupaswi kulaumiana.0653936885.
Salute mkuu Baligeya! Nimesoma makala yako, umewachana ndani na nje hawa wanafiki wanaochukulia msiba wa Mangweha kujipatia sifa za kijinga, hasa hawa wanaojiita masupa staa. Naamini walikuwa hata hawajui safari yake ya Afrika Kusini.0764920545.
Umeandika ambacho mimi pia kimeniuma sana, lakini nilikuwa sina pa kusemea. Nafikiri umewakilisha Watanzania wengi walio werevu wa fikra! Najua itakujengea maadui wengi sana kwa ukurasa huo mmoja tu ambao umeelimisha watu wengi kwa wakati mmoja. ‘Only God knows’. 0752809939.
Ukweli kabisa Mangweha alishasahaulika kwenye gemu la muziki wa kizazi kipya. Sasa kafariki amevuma, amekuwa gumzo kila kona bila faida kwake.0652316053.
Hilo hata mimi nakubaliana nalo maana leo hii Mangweha angekuwa tajiri sana, lakini maskini ya Mungu wako wanaokula vizuri , kulala vizuri kupitia mgongo wake. Wasanii wanatakaiwa wafikirie sana juu ya hili, angalau wamuone hata yule Mama Mangweha. I love you bro RIP Mangweha. Husna wa Arusha.0767189858.
Nashangaa hawana chembe ya aibu. Msanii akirekodi kwa P Funk inakuwa shida. Tazama Jay Mo na Mangweha wamezimwa na ndo wamebadili ngoma kali. Kwa kifo hiki, wabadilike. Kutoka Kiteto.0782501774.
Ni vibaya kumfanyia uovu mtu halafu akifa uwe mstari wa mblele kumzika. Nafsi zao zinawasuta. Watanzania tunasikia hayo na ipo siku yatafika mwisho. Haipendekezi wewe mwenyewe uwe stari wa mbele bila kushirikisha wenzio mwanzo hadi mwisho wakati nyimbo za marehemu Mangweha zinapigwa na stesheni zote na kusikika na rika lolote. Zaidi msanii ni nguzo imara kufikisha ujumbe kwa vijana wote kiurahisi. Tumepoteza askari mshauri. Wasanii wawe na chama chao chenye kuratibu mambo yao.089575789.
Nimemaliza kusoma makala yako kuhusu kifo cha msanii Mangweha bila shaka ujumbe utakuwa umewafikia wahusika. Asante.0717796037.
Hawa makupe ni wajinga na watu wasiofaa hata kidogo. Sielewi kwa nini wakati alipokuwa hai, hawakutaka kupiga nyimbo zake. Walimchukulia Mangweha kama mtu asiyekuwa na maana. Leo hii amekufa, wanampamba sifa kibao na kujiweka kimbelembele. Kinachokera zaidi ni kwamba wanajisifu kwamba walimsaidia alipokuwa hai. Nawachukia sana watu hawa kwa unyonyaji wao kwa wasanii. 0713941101.
Habari ya asubuhi! Nimesoma makala yako ya 'Tunamlilia Mangweha baada ya kufa! Kwa kweli upo sahihi kabisa. Nakutakia mafanikio mema katika kazi yako ya uandishi wa habari. Naitwa Bahati Kiula mkazi wa Mikocheni B, Dar es Salaam.
Yaani makala yako imenigusa na kuniumiza moyo wangu sana na hapa nilipo mazungumzo ni hayo ya Mangweha na hizo redio. Kama ulinikataa nilipokuwa hai, hata nikifa usinikubali. 0717353370
Habari brother. Mimi ni mtanzania, naishi Kilimanjaro. Nimeguswa sana na mada yako kuhusu kifo cha Mangweha. Ushauri wangu naomba hivyo vyombo vya habari, ambavyo vina tabia hiyo, muwaweke hadharani watanzania wote watambue kwani huo ni unyama uliokithiri. Inauma sana kuona vijana wetu wanajituma sana, lakini kuna watu wanawamaliza. Iwapo itadhihirika ni kweli, sheria ichukue mkondo wake wafungwe. 0753616171.
Mambo vipi kaka? Uko poa? Mimi mzima wa afya. Nakupongeza sana kaka kwa kuitoa nakala yako kwenye gazeti la Burudani. Baligeya wewe ni mwandishi wa habari, ambaye una mtazamo wa mbali sana. Hawa watu wanaojiona bora katika mambo ya habari ni wabaya sana.
Wanawaua wasanii na muziki huu kwa jumla. Leo Albert Mangweha anaonekana ana thamani wakati tayari amekuwa marehemu. Kipindi alipokuwa hai walikuwa hawamthamini na nyinbo zake hawazichezi. Mungu atamlipia Mangweha kwa unafiki waliomtendea. Endelea hivyo kaka, kusema maneno yaliyo ya kweli na Mungu atakuongoza na kubariki kazi za mikono yako—RIP ALBERT MANGWEHA-ailaze roho yako mahali pema peponi amina. Mangole.0714057304.
Safi sana kaka Stephen Baligeya kwa makala hii ya Mangweha. Tatizo letu watanzania linabaki palepale, unafiki. Hata wewe unawajua waziwazi wanaowaua wasanii na watakaoua wengine pia kwa kuwachanganya kiakili, lakini kama hautawataja moja kwa moja kuwa ndio chanzo cha yote haya, sote tutabaki pale pale na wao wataendelea kufanya yale yale. Atakufa mwingine na wengine mpaka Tanzania tutakapoamua kuambiana ukweli bila kupepesa.0717340184.
KIEMBA: NIMEFUNGA MJADALA
MSHAMBULIAJI Amri Kiemba amesema kwa sasa ameamua kufunga mjadala kuhusu mustakabali wake kisoka baada ya kutia saini mkataba mpya wa kuichezea Simba kwa miaka miwili.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Kiemba alisema si kweli kwamba alikuwa katika harakati za kurejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga.
"Unajua mimi si muongeaji sana. Wakati magazeti yanaandika mimi nimesaini mkataba na Yanga, nilikuwa nashangaa sana, lakini sikutaka kujibu. Sasa ukweli ni huu, nimeingia mkataba na Simba kwa miaka miwili zaidi,"alisema.
Kiemba alisema kwa sasa anaelekeza nguvu zake katika timu ya Taifa, Taifa Stars, ambayo inajiandaa kumenyana na Ivory Coast katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.
"Naamini mjadala wa Kiemba umekwisha salama, sasa ni zamu ya wengine,"alisema.
Kiemba alimwaga wino Simba juzi mbele ya Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are, maarufu kwa jina la Mzee Kinesi.
Kiungo huyo alimwaga wino Simba siku moja baada ya kurejea kutoka Morocco, ambako alikwenda kuichezea Taifa Stars katika mechi dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.
Kiemba alikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Morocco kutokana na kuifungia Taifa Stars bao la kujifariji kwa shuti kali la umbali wa mita zipatazo 25. Katika mechi hiyo, Taifa Stars ilichapwa mabao 2-1.
Baada ya mchezo huo, mashabiki wa soka wa Morocco walianza kumfuatafuata Kiemba wakiomba kupiga naye picha na walimtambua kwa urahisi kutokana na rasta zake.
LIGI YA MABINGWA YA MIKOA KUANZA KESHO
MECHI za kwanza za hatua ya tatu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao, zinatarajiwa kuchezwa keshokutwa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, mechi za marudiano zinatarajiwa kuchezwa Juni 19 mwaka huu.
Wambura alisema Kamati ya Mashindano ya TFF ilikutana juzi mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kupitia ripoti za michezo iliyopita na kufanya uamuzi mbalimbali, ikiwemo mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars na Machava FC, ambayo haikuchezwa.
Ofisa huyo wa TFF alisema, Machava FC, ambayo ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Moshi kwa mabao 2-0, inaendelea katika hatua ya tatu kwa vile haikuhusika katika kukwamisha mchezo wa marudiano uliopangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Wambura alisema Chama cha Soka cha Dodoma (DOREFA) kiliuhamishia mchezo huo kwenye Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa kinyume na maelekezo ya Kamati ya Mashindano ya TFF.
"Kamati katika kikao chake cha awali iliekeleza kuwa mechi zote za RCL zitachezwa makao makuu ya mikoa, isipokuwa kwa Morogoro ambapo timu ya Techfort FC iliruhusiwa kutumia Uwanja wa CCM Mkamba mjini Ifakara,"alisema.
Wambura alizitaja timu nane zilizofuzu kucheza raundi hiyo kuwa ni Friends Rangers ya Dar es Salaam, Kariakoo ya Lindi, Katavi Warriors ya Katavi, Kimondo SC ya Mbeya, Machava ya Kilimanjaro, Njombe Mji ya Njombe, Polisi Jamii ya Mara na Stand United FC ya Shinyanga.
Wakati timu nyingine zimefuzu kwa kushinda mechi zao za raundi ya pili, Njombe Mji imeingia hatua hiyo kwa kuwa timu yenye uwiano mdogo wa kufungwa (best looser) katika hatua ya pili.
Kwa mujibu wa ratiba, katika mechi za hatua hiyo, Kariakoo itamenyana na Friends Rangers, Machava FC na Stand United FC, Polisi Jamii na Katavi Warriors, Kimondo SC na Njombe Mji. Timu zilizoanza kutajwa ndizo zinazoanzia nyumbani.
Wambura alisema kamati ya mashindano imeagiza kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Mpwapwa Stars na Machava FC, Mwijage Rugakingira wa Tanga, ambaye alikwenda uwanja wa Mgambo badala ya Uwanja wa Jamhuri kinyume na maelekezo ya TFF, aondolewe kwenye orodha ya makamishna.
Aliongeza kuwa, waamuzi wa mechi hiyo ambao nao walikwenda Mpwapwa badala ya Dodoma Mjini, wamepelekwa mbele ya Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kutokana na tukio hilo.
"Kamati ya Mashindano imekumbusha kuwa RCL ni mashindano yanayosimamiwa na TFF, hivyo maelekezo yoyote kuhusiana na mashindano hayo, yatatoka TFF na si mahali pengine popote. Msimamizi wa kituo hana mamlaka ya kubadili uwanja,"alisema.
Wambura alisema hatua ya nne ya RCL itachezwa kati ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 29 na 30 mwaka huu.
AZAM YAMTOSA KASEJA
UONGOZI wa klabu ya Azam umesema hauna mpango wa kumsajili kipa namba moja wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Juma Kaseja.
Meneja Msaidizi wa Azam, Jemedari Saidi alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, kikosi chao kwa sasa kimekamilika katika idara zote.
Jemedari alisema kikosi cha Azam kinao makipa watatu walio kwenye kiwango cha juu kisoka, akiwemo kipa namba moja Mwadini Ally na Aishi Manula.
"Tumekuwa tukisia taarifa kupitia kwenye vyombo vya habari kwamba Azam ina mpango wa kumsajili Kaseja kwa ajili ya msimu ujao, lakini msimamo wetu ni kwamba hatutasajili mchezaji yeyote kutoka klabu za ligi kuu,"alisema.
"Uamuzi uliofikiwa na benchi la ufundi ni kwamba, tutawapandisha vijana wetu kutoka kikosi cha pili na tayari tumeshafanya hivyo. Pia hatuna mpango wa kusajili wachezaji wapya kutoka nje ya nchi,"aliongeza.
Kumekuwa na taarifa zenye utata kuhusu hatma ya Kaseja kwenye kikosi cha Simba baada ya mkataba wake kumalizika mwezi uliopita.
Viongozi wa klabu hiyo kongwe nchini wamekuwa wakivutana kuhusu kipa huyo, baadhi yao wakitaka aongezwe mkataba mpya na wengine wakitaka aachwe.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya mchezaji huyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are alisema jana kuwa, itajulikana hivi karibuni.
"Kwa sasa sina la kusema, lakini wakati utakapofika, kila kitu kitakuwa wazi,"alisema.
Thursday, June 13, 2013
IVORY COAST KUTUA DAR LEO USIKU
SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA) limewateua waamuzi kutoka Algeria kuchezesha mechi kati ya timu ya Taifa, Taifa Stars na Ivory Coast.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kumenyana Jumapili katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 204 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, waamuzi walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo ya kundi C wataongozwa na Charef Mehdi Abid atakayekuwa mwamuzi wa kati.
Aliwataja waamuzi wengine kuwa ni Hamza Hammou na Bouabdallah Omari wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Sofiane Bousseter.
Wambura alisema Abdi na wezake wanatarajiwa kutua nchini kesho saa 12 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri (EgyptAir).
Aliongeza kuwa mtathmini wa waamuzi wa mechi hiyo atakuwa Athanase Nkubito kutoka Rwanda, ambaye naye atatua nchini kesho saa 12 jioni kwa ndege ya RwandAir.
Alisema kamishna wa mechi hiyo ni Bernard Mfubusa kutoka Burundi, ambaye anatarajiwa kuwasili nchini kesho saa 3.35 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.
Kwa mujibu wa Wambura, maofisa wote watakaosimamia mechi hiyo wanatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu kurejea kwao.
Wakati huo huo, msafara wa timu ya Taifa ya Ivory Coast (The Elephants) utakaokuwa na watu 80, wakiwemo wachezaji 27, unatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ndege maalumu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa, kikosi hicho kitawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam saa 2.50 usiku na kitafikia hoteli ya Bahari Beach iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wambura, nahodha wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba ameachwa kwenye msafara huo.
Aliwataja Wachezaji watakaokuwemo kwenye kikosi hicho kuwa ni Abdoul Razak, Akpa Akpro Jean-Daniel Dave Lewis, Angoua Brou Benjamin, Arouna Kone, Aurier Serge Alain Stephane, Bamba Souleman, Barry Boubacar, Boka Etienne Arthur, Bolly Mathis Gazoa Kippersund, Bony Wilfried Guemiand, Cisse Abdoul Karim, Diarrassou Ousmane Viera na Dja Djedje Brice Florentin.
Wengine ni Doumbia Seydou, Gbohouo Guelassiognon Sylvain, Gosso Gosso Jean-Jacques, Kalou Salomon Armand Magloire, N’dri Koffi Christian Romaric, Sangare Badra, Serey Die Gnonzaroua Geoffroy, Sio Giovanni, Tiote Cheik Ismael, Toure Yaya Gnegneri, Traore Lacina, Ya Konan Didier, Yao Kouassi Gervais na Zokora Deguy Alain Didier.
Katika hatua nyingine, kiingilio cha chini katika mechi kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, ambavyo viko 17,045, kiingilio kitakuwa sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa, ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni sh. 15,000 kwa VIP C,sh. 20,000 kwa VIP B na sh. 30,000 kwa VIP A.
DIAMOND, WEMA WAKUTANISHWA KWENYE FILAMU
Waandaaji wavunja benki kuwalipa washiriki
Diamond akiri itakuwa kazi ngumu kuliko muziki
LICHA ya kuvunjika kwa uhusiano wao wa kimapenzi, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' na msanii nyota wa filamu, Wema Sepetu watakutanishwa katika filamu.
Wapenzi hao wawili, ambao wamekuwa wakirudiana na kuachana mara kwa mara, wanatarajiwa kucheza filamu mpya itakayoanza kurekodiwa hivi karibuni.
Akihojiwa katika kipindi cha Take One Action kilichorushwa hewani hivi karibuni na kituo cha televisheni cha Clouds, Diamond alisema amelipwa pesa nyingi kwa ajili ya kucheza filamu hiyo.
Diamond alisema hakuna msanii wa filamu aliyewahi kulipwa kiwango hicho cha pesa na kwamba hata yeye hajawahi kulipwa pesa kama hizo katika kazi yake ya muziki.
Hata hivyo, Diamond hakuwa tayari kutaja kiwango hicho cha pesa kwa madai kuwa, taarifa zaidi zitatolewa na waandaaji wa filamu hiyo hivi karibuni.
"Taarifa kuhusu filamu hiyo inahusu nini, lini tutaanza kufanya 'shooting', washiriki wamelipwa kiasi gani cha pesa na picha zake zitachukuliwa maeneo gani, itatolewa na waandaaji,"alisema
Msanii huyo nguli wa muziki wa kizazi kipya alisema anaamini filamu hiyo itakuwa babu kubwa kutokana na maelezo aliyopewa na waandaaji wake.
"Haitakuwa kama hizi filamu zilizozoeleka,"alisema msanii huyo, ambaye amewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki za Kilimanjaro.
Diamond alisema amewahi kuombwa na watu mbalimbali kucheza filamu zao, lakini amekuwa akiwatolea nje kutokana na kutoridhishwa na maudhui yake na mazingira ya uandaaji wake.
Alisema lengo lake ni kuifanya filamu hiyo atakayoicheza kwa kushirikiana na Wema, iwe katika kiwango cha juu ili aweze kuuza jina lake kimataifa.
Licha ya kukubali kucheza filamu hiyo, Diamond alisema anahisi kutatokea matukio mengi ya ajabu wakati wa kupiga picha za filamu hiyo katika maeneo husika.
"Nina hakika baadhi ya wakati mpenzi wangu atakuwa akija kwenye maeneo ya kupiga picha za filamu hiyo kila atakapopata nafasi, hivyo kutakuwa na vijembe na maneno ya hapa na pale,"alisema.
"Hii kazi nahisi itakuwa ngumu kuliko hata ya muziki, lakini namuomba Mungu anisaidie ili niweze kuimaliza salama,"aliongeza msanii huyo.
Japokuwa hakutaka kuweka wazi kuhusu wasiwasi alionao wa kutokea matukio ya ajabu wakati wa upigaji wa picha za filamu hiyo, kauli yake hiyo inamuhusisha Wema na mpenzi wake wa sasa, Penny.
Diamond ana wasiwasi kuwa, iwapo Penny atakuwa akimtembelea katika maeneo watakayokuwa wakipiga picha za filamu hiyo, huenda akakwaruzana na Wema na kurushiana vijembe.
"Si unajua kila mtu analinda chake. Nina hakika yataripotiwa mambo mengi wakati wa kupiga picha za filamu hiyo,"alisema.
Alipoulizwa ni msanii yupi wa filamu wa kike anayevutiwa naye, Diamond hakusita kumtaja Wema.
"Napenda sana uigizaji wa Wema, si kwa sababu alikuwa mpenzi wangu. Waswahili wanasema palipo na ukweli, hakuna haja ya kuficha mambo. Wema anaigiza vizuri sana,"alisema.
Kwa upande wa wacheza filamu wa kiume, Diamond alimtaja msanii anayemvutia kuwa ni Jacob Steven, maarufu kwa jina la JB.
Diamond amewataka watanzania kujenga tabia ya kuwasamehe wasanii pale wanapoteleza na kufanya matendo mabaya mbele ya jamii. Alisema inasikitisha kuona kuwa, matendo mabaya yanavuma zaidi kuliko mazuri.
"Mimi kama Diamond nimekuwa nikifanya mambo mengi mazuri, lakini hayaonekani. Lakini inapotokea nimefanya kitu kidogo chenye mwonekano mbaya, kinakuzwa sana,"alisema.
Sunday, June 9, 2013
TAIFA STARS YACHAPWA 2-1 NA MOROCCO
Taifa Stars imepoteza mechi ya ugenini baada ya kufungwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya kundi C ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Morocco imechezwa leo (Juni 8 mwaka huu) usiku kwenye uga wa Grand Stade de Marrakech, jijini Marrakech.
Licha ya kufungwa, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumjaribu kipa wa Morocco, Nadir Lamyaghri aliyeokoa shuti la mpira wa adhabu la Aggrey Morris katika sekunde ya 40 tu tangu refa Daniel Frazier Bennett kutoka Afrika Kusini apulize filimbi ya kuanzisha pambano hilo.
Refa alitoa faulo hiyo baada ya mshambuliaji Thomas Ulimwengu kukwatuliwa na Ahmed Kantari baada ya kumtambuka beki mwingine wa Simba hao wa milima ya Atlas.
Stars walicheza pungufu kwa dakika 58 baada ya Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumkwatua ndani ya eneo la hatari Abdelaziz Barrada huku akiwa amebaki yeye na mshambuliaji huyo. Adhabu hiyo iliandamana na penati ambayo Morocco waliitumia kupata bao la kuongoza dakika ya 37 mfungaji akiwa Abderazzak Hamed Allah.
Kabla, Stars wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager walitengeneza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 25 baada ya Ulimwengu kufanikiwa kuwatoka mabeki wawili wa Morocco na kuingia eneo la hatari lakini shuti lake hafifu lilidakwa na kipa Lamyaghri.
Morocco waliongeza bao lingine dakika ya 50 na Youssef El Arabi baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kudhibiti pasi ya mwisho ya wachezaji wa timu hiyo, na mshambuliaji huyo kumfunga kirahisi kipa Juma Kaseja.
Kiungo mshambuliaji Amri Kiemba aliifungia Stars bao maridadi dakika ya 61 kwa mkwaju wa mbali uliomshinda kipa Lamyaghri. Kabla ya kuachia shuti hilo, Kiemba aliwatoka wachezaji wa timu ya Morocco ambayo ndiyo imepeta ushindi wake wa kwanza katika mechi hizo za mchujo za Kombe la Dunia.
Dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho Mbwana Samata angeweza kuisawazishia Stars, lakini licha ya kuwatoka mabeki wawili wa Morocco baada ya kupokea pasi ya John Bocco mpira aliopiga ulitoka nje.
Stars ambayo bado inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita inaondoka hapa kesho (Juni 9 mwaka huu) mchana kwa ndege ya EgyptAir kupitia Cairo, Misri na itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 alifajiri (Juni 10 mwaka huu).
Katika mechi hiyo Stars iliwakilishwa na; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngasa/Nadir Haroub, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha/John Bocco, Amri Kiemba na Mbwana Samata.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Marrakech, Morocco
+212 610120619
TENGA: USHIRIKI KOMBE LA KAGAME MIKONONI MWA SERIKALI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan unategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
Tenga, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF, alisema tayari TFF na Serikali zimeshafanya mazungumzo, na Serikali imepewa taarifa zote muhimu kuhusu mashindano kwa ujumla, malazi ya klabu za Tanzania, uhakika wa usalama, usafiri wa ndani na mambo mengine muhimu hivyo kwa sasa Serikali inatathmini taarifa hizo kabla ya kutoa tamko.
“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.
Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.
“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.
Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupata uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.
“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA.”
Friday, June 7, 2013
M 2 THE P AZURU KABURI LA MANGWEA
Hili ndilo kaburi la msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, marehemu Albert Mangwea aliyezikwa jana nyumbani kwao, Kihonda mkoani Morogoro.
Swahiba mkubwa wa marehemu Mangwea, msanii M 2 THE P akiuaga mwili wa mwenzake kabla ya kuzikwa jana. M 2 THE P alisafiri na Mangwea kwenda Afrika Kusini na alikuwa pamoja na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake.
Swahiba mkubwa wa marehemu Mangwea, msanii M 2 THE P akiuaga mwili wa mwenzake kabla ya kuzikwa jana. M 2 THE P alisafiri na Mangwea kwenda Afrika Kusini na alikuwa pamoja na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake.
Wednesday, June 5, 2013
TUNAMLILIA MANGWEA BAADA YA KUFA!
NA STEPHEN BALIGEYA
KAMA kuna kitu ambacho kimenipa kichefuchefu, kunitia kinyaa na kunijengea dhambi ya chuki juu ya baadhi ya watu wanaojinasibisha wema mbele za uso wa dunia na Watanzania, basi ni kifo cha msanii Albert Mangwea.
Niliwasikiliza kwa umakini na wamenifanya nitakafakari na kunipa fursa ya kuchambua kwa umakini kiasi cha kuandika pia kwa umakini juu ya namna Watanzania walivyomlilia msanii huyo.
Ngwea, ‘Mzee wa mikasi’ kama nilivyopenda kumwita, ametutoka, amechoka kuishi kwa fitina, majungu, unafiki na uzandiki wa hapa duniani. Kwangu mimi naona amefanya uamuzi sahihi na makini wa kuamua kwenda kupumzika katika nyumba ya milele.
Nasema kachoka kuishi kwa unafiki, fitina, majungu na uzandiki kwa sababu, kinachozungumzwa na kufanywa juu yake leo, kama kingekuwa kinafanywa wakati yuko hai, inawezekana Mangwea asingechukua uamuzi wa haraka namna hii.
Si kwamba nasema Mangwea kajiua, hapana. Nasema Mangwea angeondoka kwa furaha zaidi kuliko huzuni aliyoondoka nayo. Ameondoka na huzuni huku manyang’au, wanafiki, wafitini na wazandiki wakibaki wakifaidi furaha yake.
Kwa nini baada ya Mangwea kuaga dunia ndipo kila kituo cha redio kinapiga nyimbo zake kwa wingi na kumsifia kuwa alikuwa akiimba nyimbo bora kabisa? Kwa nini wakati akiwa hai, nyimbo hizo zilikuwa hazisikiki katika baadhi ya vituo vya redio nchini?
Nimetafakari kwa kina jambo hili, ambalo limenitia kichefuchefu na kinyaa kisichomithilika. Kwa sababu wasanii wanategemea nyimbo zao kupigwa mara kwa mara katika vituo vya redio na televisheni ili waweze kujitangaza.
Nyimbo zao zinapigwa bure na vituo hivyo, lakini hawalipwi chochote. Hata katika kupigwa huko, bado nyimbo za baadhi ya wasanii akiwemo Mangwea zilikuwa nadra kupigwa.
Kimsingi, nyimbo za wasanii zinapokuwa zinapigwa kwenye redio na televisheni, husaidia vyombo hivyo vya habari kupata wasikilizaji na watazamaji wengi, ambao ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza biashara zao.
Bila wasikilizaji na watazamaji, hakuna redio wala televisheni inayoweza kuwa na ubavu wa kushawishi watangazaji kufanya nayo kazi. Watatangaza vipi na redio na televisheni isiyokuwa na wasikilizaji wala watazamaji wa matangazo yao?.
Ndiyo maana leo kuna vipindi vya muziki, kila redio na televisheni inaweka mbinu za kuwa na wasanii ili iweze kusikilizwa na kuangaliwa na watu wengi ili wafanyabiashara nao wafurahie kuwapa matangazo.
Lakini wakati redio na televisheni zinapata mabilioni ya fedha kupitia wasanii, wahusika hawaingizi kitu. Kibaya zaidi wanaombwa hata fedha ili nyimbo zao ziweze kupigwa katika redio na televisheni.
Kinachokera zaidi ni kwamba bado kuna makupe wanaotumia fursa walizonazo kwenye redio kuwakandamiza wasanii. Wapo wanaokataa kupiga nyimbo za wasanii wanaokataa kunyonywa.
Msanii akikataa kuingia mikataba ya kunyonywa na makupe hao, adhabu yake ni nyimbo zake kutopigwa redioni wala kwenye televisheni wanazoziongoza. Msanii akigoma kwenda kwenye tamasha la makupe hao kwa kudai maslahi mazuri, tishio lake ni kutopigwa nyimbo zake au kutoalikwa kwenye matamasha mengine.
Mangwea alikuwa mmoja wa waathirika. Waliomfanya aishi maisha ya shida na tabu wakati akiwa msanii mkubwa, ndio hao walioubeba msiba wake na kujifanya walimpenda sana.
Wanamsifu kwa nyimbo na mapambio, wanamtukuza mtu aliyekufa, lakini walishindwa kumtukuza na kumsifu akiwa hai. Makupe hawa, ambao wamekuwa na tabia ya kunyonya wasanii, wamejifanya mama na baba wa Mangwea wakati wa mauti.
Walikataa kupiga nyimbo zake kama njia ya kumtangaza na kumfanya apate fursa nyingi za kimuziki. Walikataa kumwalika kwenye matamasha, ambayo wamekuwa wakiyaandaa kama njia ya kumpatia kipato, leo wanajigamba kuwa kijana huyu alikuwa mpole na hakuwa na ugomvi na watu.
Wanamsifu kwa upole wake, kwani wanajua kuwa upole huo ndio walioutumia kumfanya aishi kinyonge mpaka mauti yanamkuta. Walimfanya mbuzi wa kafara, ambaye nina imani kifo chake kitakuwa chachu katika kuleta mabadiliko katika fikra katika vichwa vya wasanii wengine.
Haiwezekani mtu afe ndipo nyimbo zake zinapigwa siku nzima, lakini wakati akiwa hai, nyimbo hizo hizo, ambazo zinasifiwa, zilikuwa hazisikiki wala kuzungumzwa kama zenye ubora. Ubora huo unakuja baada ya kufa kwake.
Unafiki, ujinga na upuuzi huu, ambao unazidi kuwa kasumba ya makupe kuwasifu waliokufa, unazidi kuwafanya watu waliokufa kwa sababu ya mateso yaliyojengwa na wazandiki hawa kumea.
Hebu fikiria, kama nyimbo hizo za Mangwea zingepigwa kama zinavyopigwa leo, angekuwa tajiri kiasi gani? Sifa anazopewa leo, angepewa miaka ya nyuma, angeshiriki matamasha mangapi, ambayo yangempatia fedha?
Leo kila mtoto anamfahamu Mangwea. Wanamfahamu kwa sababu kafariki dunia, lakini kabla ya hapo, waliomfahamu walikuwa wale waliofuatilia kazi zake tangu zamani. Ghafla Mangwea kawa maarufu kama enzi zake, kwa sababu tu amefariki dunia.
Nimesikiliza baadhi ya watangazaji walioko katika redio zilizoshiriki kuua majina ya wasanii wakimsifu Mangwea kwa namna, ambayo mpaka inakera. Wanajulikana namna walivyomfanya Mangwea awe mtumwa na ajutie kuwa msanii.
Nafsi zao zinajua namna walivyoshiriki kumuua Mangwea kiusanii na pengine hata kiroho, lakini leo wanajifanya ndio wasemaji wa Mangwea, ndugu wa Mangwea na familia ya Mangwea. Wanajaribu kuwaaminisha Watanzania kwamba ni watu wema na makini katika kazi zao.
Kwa jumla watu hawa wanatia kichefuchfeu kwani kama wasanii wetu wangekuwa wanatukuzwa namna hii wanapokuwa hai, wangekuwa matajiri kuliko kuwaua na kisha kujifanya tunawalilia siku ya msiba.
Maoni na ushauri 0752646938.
Rooney ampasua kichwa Wenger
LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England, Wayne Rooney amewaweka roho juu mashabiki wa klabu ya Manchester United baada ya kukiri hadharani kwamba, anaweza kuondoka Old Trafford msimu huu.
Kauli hiyo ya Rooney imemfanya Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger awe tayari kuvunja benki na kuweka rekodi ya kumsajili nyota huyo kwa bei mbaya.
Wenger alisema wiki hii kuwa, hawezi kupoteza nafasi adhimu ya kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye anaonekana kutofurahia uwepo wake Old Trafford.
Rooney (27) aling'ara mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni pamoja na kuifungia bao England ilipomenyana na Brazil na kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja wa Maracana.
Mwezi uliopita, gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti kuwa, Arsenal imepata uhakika mkubwa wa kumsajili Rooney baada ya mchezaji huyo kusema kuwa, anataka kuondoka Old Trafford.
Tayari Wenger ameshaweka wazi kuwa, yuko tayari kuvunja rekodi ya kumsajili nyota huyo wa zamani wa klabu ya Everton.
"Rooney ni mchezaji, ambaye anamvutia kila mtu duniani, nani anayeweza kukataa kumsajili," Wenger alikieleza kituo cha televisheni cha Al Jazeera wiki hii.
Wakati Wenger akihaha kumsajili nyota huyo, Kocha Mkuu mpya wa Manchester United, David Moyes anakabiliwa na kazi nzito ya kumshawishi Rooney abaki Old Trafford.
Moyes alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, angependa kumuona Rooney akiendelea kuitumikia Manchester United chini yake kwa vile ni miongoni mwa wachezaji muhimu.
Rooney amekuwa hana uhakika wa namba Manchester United tangu ilipomsaili Robin van Persie. Mholanzi huyo amekuwa akicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, ambayo Rooney alikuwa akiicheza kabla ya ujio wake.
Mapema 2010, Rooney alitishia kuihama Manchester United kabla ya Sir Ferguson kufanikiwa kumtuliza na kumuongezea mkataba mpya.
Msimu huu, Ferguson alimweka benchi Rooney wakati Manchester United iliporudiana na Real Madrid ya Hispania katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya. Badala yake, Ferguson aliwachezesha Van Persie na Danny Welbeck katika nafasi ya ushambuliaji.
Mbali na kumwania Rooney, Wenger pia amepania kumrejesha kiungo wake wa zamani, Cesc Fabregas, ambaye alihama Emirates msimu uliopita na kujiunga na Barcelona ya Hispania.
Wenger anaamini kuwa, mpango wake wa kumrejesha Fabregas hautakuwa mgumu kutokana na mchezaji huyo kutokuwa na uhakika wa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa wakati Fabregas alipojiunga na Barcelona 2011, Arsenal inaweza kumrejesha mchezaji huyo kwa malipo kidogo ya pauni milioni 20.
"Nafikiri kwa sasa amepoteza uhakika wa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona,"alisema Wenger alipokuwa akimuelezea mchezaji huyo.
Wenger alimwelezea Fabregas kuwa ni mchezaji mwenye utulivu na kiwango cha juu cha soka, hivyo anaumia moyoni kwa kutopata nafasi ya kuichezea timu hiyo.
Hata hivyo, Wenger anaweza kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa Manchester City, Manchester United na Chelsea katika kinyang'anyiro cha kumsajili nyota huyo wa England.
Kuna habari kuwa, klabu hizo tatu nazo zimekuwa zikimuwinda kwa udi na uvumba Fabregas kwa lengo la kuziongezea nguvu katika msimu ujao wa ligi.
Fabregas anatarajiwa kukutana na Kocha Mkuu wa Barcelona, Tito Vilanova wiki hii kwa ajili ya kuzungumzia mustakabali wake.
Marafiki wa karibu wa Fabregas wanaamini kuwa, kiungo huyo anaweza kuamua kubaki Barcelona iwapo atahakikishiwa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
Kwa upande wake, Moyes amemtaja Fabregas kuwa ni mmoja wa wachezaji, ambao amepanga kuwasajili kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi chake.
Moyes, ambaye amerithi mikoba ya kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, anatarajiwa kuanza rasmi kibarua cha kuinoa timu hiyo Juni 16 mwaka huu.
NASEEB ABDUL 'DIAMOND' : NATAKA KUWA MSANII WA KIMATAIFA
MSANII nyota wa muziki wa kizazi nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amesema kiwango chake cha chini cha malipo kwa kila onyesho analofanya nje ya nchi ni dola 10,000 za Marekani (sh. milioni 16).
Akihojiwa katika kipindi cha Take One Action kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds wiki hii, Diamond alisema katika baadhi ya nchi, kiwango chake cha malipo kwa kila onyesho ni kati ya dola 15,000 (sh. milioni 24) na 25,000 (sh. milioni 42)
"Sifanyi shoo nje ya nchi chini ya dola 10,000. Katika nchi kama Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), kiwango changu ni dola 25,000. Wakati mwingine nalipwa hadi dola 30,000,"alisema msanii huyo.
Diamond alisema katika nchi kama vile Comoro, ambako anatarajia kwenda kufanya onyesho mwishoni mwa mwezi huu, malipo yake kwa onyesho ni dola 25,000.
Hata hivyo, Diamond alisema wakati mwingine amekuwa akilipwa pesa nyingi kuliko alivyotarajia na alitoa mfano wa Rwanda, ambako promota aliyemwalika huko alimlipa sh. milioni 180,000.
"Mimi nina msimamo na ninapoalikwa nje ni lazima nifuatane na wacheza shoo wangu. Wapo wasanii wengine wa Tanzania wanaomba waende Ulaya wakafanye shoo bure kwa sababu tu hawajakwenda huko siku nyingi,"alisema.
Diamond alisema lengo kubwa alilonalo kwa sasa ni kuwa msanii wa kimataifa na amefikia uamuzi huo kutokana na funzo kubwa alilolipata wakati wa ziara yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Ili kutimiza azma yake hiyo, Diamond alisema ameanza kuandika mashairi yenye mvuto, kurekodi nyimbo zake kwenye studio za kisasa na pia kutengeneza video zenye ubora wa kiwango cha juu.
"Nimeshaanza pia kujifunza elimu ya biashara na kuboresha lugha ya Kiingereza kwa sababu nimekuwa nikikutana na mapromota wengi wa kimataifa,"alisema.
Diamond alisema anatarajia kuingia mkataba na Kampuni ya Fuse ya Uingereza, ambayo imewahi kufanyakazi na wasanii wengi maarufu wa Afrika Magharibi na Fally Ipupa wa DRC.
"Unajua muziki mzuri pekee hautoshi kukufanya uwe mwanamuziki wa kimataia. Lazima uwe na sura na mtazamo wa kimataifa,"alisema msanii huyo aliyewahi kunyakua tuzo kadhaa za muziki za Kilimanjaro.
Diamond alisema haamini iwapo imani za ushirikina zinaweza kumsaidia msanii kupata mafanikio. Alisema anawafahamu watoto wengi wa waganga wa kienyeji, lakini hakuna hata mmoja aliyepata mafanikio makubwa kimaisha.
Alisema mafanikio katika maisha yanapatikana kutokana na mipango ya Mungu na kuongeza kuwa, aliyeandikiwa kupata, hakuna anayeweza kuzuia riziki yake.
"Sijawahi kwenda kwa mganga wa kienyeji hata siku moja katika maisha yangu. Utaratibu wangu ni kuamka usiku na kufanya ibada, nikimuomba Mungu anisaidie. Namuomba sana Mungu,"alisema.
Diamond alisema katika uendeshaji wake wa kazi za muziki, amekuwa akisaidiwa na watu 12, kila mmoja akiwa na kazi yake. Alisema miongoni mwa watu hao, wamo madansa wanne, mtaalamu wa mavazi, wapiga picha wawili, mlinzi na msaidizi wake wa karibu.
Alisema hawezi kukaa na mtu, ambaye hawezi kumsaidia kimuziki na kuongeza kuwa, wapo ndugu zake, ambao wamekuwa wakipenda kusafiri naye, lakini anawakatalia kwa sababu hawawezi kuwa na manufaa kwake.
Diamond alisema miongoni mwa mambo anayotarajia kuyafanya ili kuhakikisha maisha yake hayatetereki ni pamoja na kuwekeza katika ardhi.
"Mimi ni mwoga wa maisha. Nimepitia katika mazingira magumu. Hata niwe na pesa kiasi gani, siwezi kusahau maisha niliyopitia. Wakati mwingine huwa napenda kwenda hoteli ya Slipway, nakaa baharini na kukumbuka nilikotoka, huwa nalia sana,"alisema.
"Ndio sababu nimeamua kuwekeza katika ardhi. Ninamiliki nyumba nyingi. Si sahihi kuwa na fedha nyingi benki, lakini hazizalishi. Nimeshindwa kufanya biashara kubwa kutokana na kukosa wasimamizi,"aliongeza.
Diamond alisema kamwe hapendi kutumia pesa zake kuwahonga wanawake. Alisema amekuwa akifanya hivyo kwa sababu maalumu na kwa jambo la msingi.
Msanii huyo alisema thamani ya mali alizonazo kwa sasa, ni zaidi ya shilingi bilioni moja na ushehe na kutamba kuwa, tangu 2011, haijawahi kutokea akaunti yake kupungua sh. milioni 100.
Licha ya kutunga nyimbo nyingi, Diamond alisema anavutiwa zaidi na 'Binadamu', 'Ukimuona', 'Nenda kamwambie', 'Nitarejea' na 'Lala salama'.
Alisema wimbo wa 'Ukimuona' aliutuinga maalumu kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani, Wema Sepetu wakati wimbo wa Mawazo aliutunga kwa ajili ya mpenzi wake mwingine wa zamani, Jacqueline Wolper.
Alimtaja mwanamke mwingine aliyewahi kumtungia nyimbo kuwa ni mpenzi wake wa kwanza, anayejulikana kwa jina la Sara. Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Mbagala na Nenda kamwambie.
"Sara ndiye mwanamke wangu wa kwanza. Alinipenda japokuwa sikuwa na kitu. Lakini huko mbele alinieleza wazi kwamba, hawezi kuwa na mwanaume asiyekuwa na maslahi kwake. Nilipatwa na uchungu sana,"alisema.
Diamond alisema anapenda kutunga nyimbo zake kwa kufuata mashairi ya muziki wa taarab, ikiwa ni pamoja na kutumia maneno ya kiswahili yenye mvuto.
Je, ni kwa nini Diamond aligoma kupokea fedha alizotuzwa na Wema wakati wa onyesho lake lililofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City?
"Wakati ule nilikuwa bado nina hasira sana baada ya kugombana na Wema. Alinilaghai kimapenzi. Nilikuwa na hasira sana. Nilijifanya kama simuoni,"alisema.
Hata hivyo, Diamond alikiri kuwa hajawahi kutokea kumpenda mwanamke kama ilivyokuwa kwa Wema. Alisema hata mama yake na rafiki zake wanautambua ukweli huo.
Aliitaja skendo iliyowahi kuripotiwa na vyombo vya habari na kuumiza moyo wake kuwa ni ile iliyomuhusisha mama yake na meneja wake, Papaa Misifa kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.
"Habari hiyo iliniumiza sana. Ni bora mtu acheze na kitu chochote kuhusu mimi,lakini siyo mama yangu. Naweza kufanya lolote,"alisema.
"Ni bora tucheze ulingoni wenyewe kwa wenyewe, usimchezee mama yangu. Baada ya Mungu na yeye siogopi kitu kingine chochote na ninaweza kufanya lolote baya. Sintaogopa kwenda jela iwapo itatokea mtu anamuhusisha mama yangu na mambo mabaya,"aliongeza.
BRANDTS AMCHIMBIA MKWARA NGASA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts amebariki kuondoka kwa mshambuliaji Hamisi Kiiza kutoka Uganda, lakini amemchimbia mkwara mshambuliaji mpya, Mrisho Ngasa.
Brandts amesema hana tatizo kuhusu uamuzi wa Kiiza kuondoka Yanga baada ya kushindwa kuelewana na uongozi kuhusu mkataba mpya kwa vile lengo lake lilikuwa ni kutaka kuongezewa pesa.
Kocha huyo alisema hayo juzi usiku baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam akitokea Ubelgiji alikokwenda kwa mapumziko.
"Acha aende, kama anataka fedha nyingi kuliko wenzake, aendetu. Viongozi watafute mchezaji mwingine,"alisema kocha huyo aliyepokewa na Meneja wa Yanga, Hafidh.
Akimzungumzia Ngasa, kocha huyo alisema ni mchezaji mzuri na anaufahamu vyema uwezo wake, lakini amemtahadharisha kwa kusema kuwa, kupangwa kwake kutazingatia uwezo wake mazoezini.
“Inabidi anihakikishie uwezo wake kuanzia mazoezini ili nimpange, vinginevyo nitakuwa nakaa naye benchi,”alisema.
Brandts alisisitiza kuwa, sera yake ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji mazoezini na hatampanga mtu kwa sababu ya jina lake.
Mbelgiji huyo alisema lengo lake ni kuiona Yanga ikicheza kwa kasi zaidi msimu ujao, lakini alikiri kuwa, tatizo kubwa linalowakabili kwa sasa ni kukosa uwanja mzuri wa mazoezi.
Kocha huyo alieleza kusikitishwa kwake na mahudhurio hafifu ya wachezaji katika mazoezi yaliyoanza wiki iliyopita kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.
Alisema iwapo hali hiyo itaendelea, mashabiki wa Yanga wasitarajie timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 18 mwaka huu nchini Sudan.
“Nimeambiwa wachezaji saba tu wa kikosi cha kwanza ndio wanafika mazoezini, wengine wote ni wa kikosi cha pili. Sasa hii si nzuri, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia sana hili, hadi nitakapokutana na uongozi. Nahitaji nidhamu katika timu ili kutimiza malengo na kuwafurahisha mashabiki wetu,”alisema.
Brandts alisema wakati anaondoka nchini, aliuagiza uongozi kusajili wachezaji wapya wazuri katika kila idara ili kuongeza ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza.
Brandts amesema hana tatizo kuhusu uamuzi wa Kiiza kuondoka Yanga baada ya kushindwa kuelewana na uongozi kuhusu mkataba mpya kwa vile lengo lake lilikuwa ni kutaka kuongezewa pesa.
Kocha huyo alisema hayo juzi usiku baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam akitokea Ubelgiji alikokwenda kwa mapumziko.
"Acha aende, kama anataka fedha nyingi kuliko wenzake, aendetu. Viongozi watafute mchezaji mwingine,"alisema kocha huyo aliyepokewa na Meneja wa Yanga, Hafidh.
Akimzungumzia Ngasa, kocha huyo alisema ni mchezaji mzuri na anaufahamu vyema uwezo wake, lakini amemtahadharisha kwa kusema kuwa, kupangwa kwake kutazingatia uwezo wake mazoezini.
“Inabidi anihakikishie uwezo wake kuanzia mazoezini ili nimpange, vinginevyo nitakuwa nakaa naye benchi,”alisema.
Brandts alisisitiza kuwa, sera yake ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji mazoezini na hatampanga mtu kwa sababu ya jina lake.
Mbelgiji huyo alisema lengo lake ni kuiona Yanga ikicheza kwa kasi zaidi msimu ujao, lakini alikiri kuwa, tatizo kubwa linalowakabili kwa sasa ni kukosa uwanja mzuri wa mazoezi.
Kocha huyo alieleza kusikitishwa kwake na mahudhurio hafifu ya wachezaji katika mazoezi yaliyoanza wiki iliyopita kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.
Alisema iwapo hali hiyo itaendelea, mashabiki wa Yanga wasitarajie timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 18 mwaka huu nchini Sudan.
“Nimeambiwa wachezaji saba tu wa kikosi cha kwanza ndio wanafika mazoezini, wengine wote ni wa kikosi cha pili. Sasa hii si nzuri, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia sana hili, hadi nitakapokutana na uongozi. Nahitaji nidhamu katika timu ili kutimiza malengo na kuwafurahisha mashabiki wetu,”alisema.
Brandts alisema wakati anaondoka nchini, aliuagiza uongozi kusajili wachezaji wapya wazuri katika kila idara ili kuongeza ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza.
Subscribe to:
Posts (Atom)