KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 10, 2017

TFF, WILDAID WASAINI MAKUBALIANO KUPIGA VITA UJANGILI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya kupigania uhai wa maisha ya wanyama wa mbugani ya Wildaid Alhamisi Mei 4, mwaka huu kwa pamoja wamesaini makubaliano ya vita dhidi ya ujangili.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwakilishi wa taasisi hiyo, Lily Massa.

Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema kwamba, “Hii ni sehemu nyingine ya TFF kujihusisha na shughuli za kijamii licha ya kuwa na majukumu ya kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu katika kukuza na kuendesha mashindano.”

Malinzi amesema TFF inaendeleza utamaduni wa shughuli mbalimbali za jamii kwani hata kwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Tenga enzi za utawala wake akiwa kiongozi mkuu wa mpira wa miguu, alifanya hivyo katika kampeni za kupinga maambukizi mapya ya UKIMWI.

“Wengi mtakumbuka kuwa kulikuwa pia na vita vya kupigania afya za watoto na kupigania uhai wao pia kampeni za amani ambazo mpira wa miguu umetumika kuelimisha,” amesema.

Kwa hatua hii ya sasa, Rais Malinzi amesema kwamba TFF, inaingia makubaliano hayo na kuiteua timu ya taifa ya vijana Tanzania maarufu kama Serengeti Boys kusimama kidete kupinga uwindaji haramu wa wanyama mbugani kwa kuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wa Mwakilishi wa WildAid, Lily Massa, alishukuru kuingia kwa makubalino hayo akisema kwamba ndoto zao za kupiga vita uwindaji haramu na ujangili, itafanikiwa.

“Tunashukuru kuingia programu hii na ninaamini Mungu atatusaidia,” amesema Massa ambaye taasisi yake iko karibu kila nchi yenye wanyama wa mbugani.

Katika hatua nyingine, Rais Malinzi aliitakia kila la kheri Serengeti Boys ambayo kwa sasa inajiandaa kuingia Gabon kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14, mwaka huu ambako Serengeti Boys ambayo iko Kundi B itakuwa Libreville - Mji Mkuu wa Gabon. Timu nyingine za Kundi B ni Mali, Niger na Angola.

No comments:

Post a Comment