KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 10, 2017

WANAMUZIKI MSONDO NGOMA WARIDHIA BENDI KUREJESHWA TUCTA


WANAMUZIKI wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma wamesema wameridhia bendi yao kurejeshwa kwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA).

Wamesema uamuzi huo wa TUCTA umeleta ahueni kubwa kwao kwa sababu kwa sasa watakuwa na uhakika wa kupata mishahara kila mwezi, tofauti na sasa, ambapo malipo yao hutegemea viingilio vya mashabiki ukumbini.

Kauli ya wanamuziki hao imekuja siku chache baada ya shirikisho hilo kutangaza rasmi kuirejesha bendi hiyo chini yake kama ilivyokuwa enzi za NUTA, JUWATA na OTTU.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. yahaya Msigwa, alitangaza uamuzi huo wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliyofanyika kitaifa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kutokana na uamuzi huo, wanamuziki wa bendi hiyo ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina la TUCTA Jazz Band, watakuwa wakilipwa mishahara kila mwezi, posho mbalimbali, bima ya afya na kulipiwa michango ya kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema mjini Moshi hivi karibuni kuwa, wameufurahia uamuzi huo kwa sababu umewaondoa katika maisha ya kubahatisha na ya kutegemea viingilio vya mashabiki kujiendesha.

Alisema tayari walishafanya mazungumzo ya awali na uongozi wa TUCTA na kukubaliana mambo kadhaa na kwamba, wanachokikubali kwa sasa ni kutia saini makubaliano hayo.

Kibiriti alisema wanachotaka kuona ni wanamuziki wote wanafaidika kutokana na uamuzi huo, ikiwemo kulipwa mishahara kila mwezi na kuhakikisha kuwa, wanafanyakazi kwa bidii na nidhamu wakiwa chini ya uongozi mpya.

Alisema walicho na uhakika nacho kwa sasa ni kwamba, kila mwanamuziki atakuwa na uhakika wa mshahara, iwe wamefanyakazi au hawajafanya, tofauti na ilivyo sasa, ambapo wamekuwa wakitegemea zaidi kulipana posho kila baada ya onyesho.

"Tumepitia kipindi kigumu sana kwa sababu muziki wa dansi kwa sasa hauna soko kama ilivyokuwa huko nyuma, tumekuwa tukilipana posho kila baada ya maonyesho na wakati mwingine fedha tunazopata ni kidogo.

"Lakini kwa sasa chini ya TUCTA, tuna uhakika wa mishahara kila mwezi. Cha msingi ni kufanyakazi tutakazopangiwa kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu ili kuwaridhisha waajiri wetu,"alisema Kibiriti.

Alipoulizwa iwapo wataongeza wanamuziki wapya kwa lengo la kuiimarisha bendi hiyo, meneja huyo alisema hilo litategemea makubaliano ya mwisho watakayofikia na uongozi wa TUCTA.

Alisema kwa hatua waliyofikia, wanapaswa kuiimarisha zaidi bendi hiyo ili iwe bora na imara zaidi na pia kuongeza mvuto kwa mashabiki.

No comments:

Post a Comment