KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 17, 2017

SPORTPESA WAINGIA MKATABA MNONO NA KLABU YA YANGA


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Yanga  Leo wameingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa  na kuwa klabu ya pili kudhaminiwa baada ya watani zao Simba kuwa wa kwanza kuingia kwenye udhamini huo.
Mkataba huo utakuwa ni wa miaka mitano na utagharimu kitita cha Sh bilioni 5.173 huku mwaka wa kwanza Yanga ikiingiza Sh milioni 950.
Mkataba huo umesainiwa  katika makao makuu ya klabu ya Yanga mbele ya waandishi wa habari ambapo SportPesa wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa SportPesa,Pavel Slavkov pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa,Abbas Tarimba huku Yanga waliongozwa na Makamu mwenyekiti Clement Sanga na Katibu Mkuu Bonifance Charles Mkwasa.
Makubaliano hayo yatahusisha kuwepo kwa nembo ya SportPesa kwenye jezi za klabu kuanzia msimu ujao wa Ligi yaani 2017-18 hadi 2021-22.
Mmoja wa Wakurugenzi wa Yanga, Abbas Tarimba amesema leo kuwa mkataba wa Yanga na ule wa Simba haina tofauti na bingwa msimu ujao atalipwa Sh milioni 100 kutoka SportPesa.
“Kwa yule atakayefanikiwa kuchukua ubingwa wa Afrika, yeye tutatoa Sh milioni 250, hii ni sehemu ya bonus kwenye mkataba,” alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwashukuru SportPesa kuungana nao.
“Tunaamini ni sehemu ya kuleta mabadiliko, wamekuja kuunga nasi, tumewapokea na tunawaahidi ushirikiano. Hii ni kati ya kampuni nimeona kwa mara ya kwanza tumejadili mambo mengi. Mengine yatatokea huko mbele lakini ni mambo ya maendeleo,” alisema.
SportPesa ilianzishwa mwaka 2014 nchini Kenya na kuanzishwa kwake imefanikiwa kukua kimataifa kwa kushirikiana na timu kubwa za England ambapo wana mikataba na Hull City,Everton,Arsenal na Southampton pamoja na Ligi Kuu ya Hispania.

No comments:

Post a Comment