KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 18, 2016

YANGA YAIFUNGA MDOMO MWADUI FC

 

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walizoa pointi zote tatu kutoka kwa Mwadui FC baada ya kuichapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mabao hayo ya Yanga yalipachikwa wavuni na washambuliaji Amisi Tambwe kutoka Burundi na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, moja katika kila kipindi.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne, ikiwa

imeshinda tatu na kutoka sare moja. Yanga kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo nyuma ya Simba.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mbao FC ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kuitandika Ruvu Shooting mabao 4-1 kwenye uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Nayo Ndanda FC ilizinduka toka usingizini baada ya kuichapa Majimaji mabao 2-1 kwenye

Uwanja wa Majimaji, Mtibwa Sugar iliishinda Kagera Sugar mabao 2-0 mjini Songea wakati Mbeya City ilitoka suluhu na ndugu zao wa Prisons mjini Mbeya.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Stand United na JKT Ruvu Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati Jumanne African Lyon wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza.

No comments:

Post a Comment