KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2016

KILIMANJARO QUEENS KUTUA DAR LEO KWA NDEGE KUTOKA MWANZA


Mabingwa wapya wa Kombe la Chalenji la CECAFA, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens, inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo Septemba 22, 2016 saa 7.00 mchana kwa ndege ya FastJet ikitokea Mwanza.

Mara baada ya kutua, itakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Coartyard iliyoko Sea View, Upanga jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata chakula cha mchana ambako watakuwako viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wale wa Serikali akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.

Timu hiyo jana, Septemba 21, 2016 ilitua Kagera ambako imetumia siku ya leo kuwafariji wahanga wa tetemeko la ardhi.

Itakumbukwa kwamba kabla ya kwenda Jinja, Uganda ambako ilivuna ubingwa huo katika fainali zilizofanyika jana kwa kuilaza Kenya katika fainali zilizofanyika Uwanja wa Njeru, Kilimanjaro Queens iliweka kambi mjini Bukoba ambako ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi na kushinda mabao 3-0 Septemba 8, mwaka kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Kilimanjaro Queens inatarudi Kagera kusema: “Ahsante” kwa wenyeji akiwamo Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstafu Salum Kijuu aliyewakabidhi bendera kabla ya safari, lakini pia kuwapa pole Wahanga wa janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Edna Lema  wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake, Amina Karuma.

Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.

Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Wakati huo huo, timu ya taifa ya Vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kesho  inatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam, Tanzania kesho Septemba 22, 2016 kwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya kambi ya siku 10 kabla ya kuivaa Congo-Brazzaville katika mchezo wa pili kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Baada ya Serengeti Boys kushinda mabao 3-2, jijini Dar es Salaam, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itafayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

No comments:

Post a Comment