KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, September 24, 2016

SIMBA YANG'ARA LIGI KUU, AZAM YATEPWETA



WAKONGWE wa soka nchini, Simba leo wamezidi kujitanua kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, baada ya kuitandika Majimaji mabao 4-0.

Wakati Simba ikitoka uwanjani na ushindi huo mnono, mabingwa wa mwaka juzi, Azam walishindwa kutamba ugenini baada ya kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na Ndanda FC, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nangwande Sijaona mjini Lindi.

Ikicheza Uwanja wa Taifa, baada ya kuulalamikia Uwanja wa Uhuru kwamba unaumiza wachezaji, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Washambuliaji walioiwezesha Simba kuibuka na ushindi huo mnono walikuwa Jamal Mnyate, aliyefunga mawili, Shizza Kichuya na Daudit Mavugo.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare moja.

Mavugo aliifungia Simba bao la kuongoza kipindi cha kwanza baada ya kipa Amani Simba wa Majimaji kutema shuti lililopigwa na Ibrahim Ajibi.

Kichuya aliiongezea Simba bao la pili kwa njia ya penalti dakika ya 67 baada ya beki mkongwe wa Majimaji, Lulanga Mapunda kuunawa mpira ndani ya 18.

Mnyate aliiongezea Simba bao la pili dakika ua 74 baada ya kumalizia krosi maridhawa kutoka kwa Mo Ibrahim kabla ya kuongeza la nne dakika ya 81 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Jonas Mkude.

Nao Ndanda waliwaadhiri vigogo Azam kwa kuwapiga mweleka wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na Khamis na Mponda, wakati bao la Azam lilifungwa na Bocco.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, JKT Ruvu imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, Prisons ilitoka suluhu na Mwadui, Mtibwa imelazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mbao FC.

Ligi hiyo inaendelea tena keshi wakati Yanga itakapovaana na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga huku Ruvu Shooting ikivaana na Toto Africans.


(PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA MICHUZI)

No comments:

Post a Comment