KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 30, 2016

SAANYA KUZICHEZESHA SIMBA NA YANGA




SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemteua mwamuzi Martin Saanya kuchezesha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga litakalochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Saanya atachezesha mechi hiyo akisaidiwa na Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha.

Hii ni mara ya tatu kwa Saanya, mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), kuchezesha mechi kati ya timu hizo kongwe nchini, katika miaka ya hivi karibuni.

Mara ya mwisho, Saanya alizichezesha Simba na Yanga msimu wa 2013/2014, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Aidha, Saanya alizichezesha timu hizo msimu wa 2014/2015, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, viingilio katika mchezo huo vinatarajiwa kuwa Sh 7,000, 10,000, 20,000 na 30,000.

Timu zote mbili zilirejea Dar es Salaam jana, Simba ikitokea mkoani Morogoro ilikokwenda kuweka kambi wakati Yanga ilikuwa imejichimbia kisiwani Pemba.

SERENGETI BOYS WAAPA KUFIA UWANJANI J'PILI

Makocha wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys’, Bakari Nyundo Shime na Muharami Mohammed anayewanoa makipa watatu wa timu hii, wamesema kwa pamoja: “Tuko tayari kwa vita.”

Shime maarufu kama Mchawi Mweusi, amezungumza hayo wakati anaendelea kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Jamhuri ya Congo utakaofanyika Jumapili Oktoba 2, kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa jijini Brazzaville.

Katika mazungumzo yake, Shime anasema: “Timu iko vizuri. Tumejiandaa vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha. Kwa hivyo, kila kitu kiko sawa, kama tulivyokusudia. Tupo hapa Congo kwa sasa kumalizia au kukumbushia mambo mawili au matatu hivi...

“Lakini pia tupo hapa Congo kuzoea hali ya hewa. Kwa bahati nzuri si tofuati na ya nyumbani Tanzania,” anasema Shime kwa kujiamini kabisa leo mchana Septemba 29, 2016 huku akijiandaa kwenye mazoezi.

Shime anasema kwamba mfumo atakaoutumia ni wa 4-4-2 katika mchezo huo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana. Fainali hizo zitafanyika jijini Antananarivo, Madagascar mwezi Aprili, mwakani.

Anasema kwamba mfumo huo ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani katika michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.”

Shime aliyekuwa mchezaji zamani kabla ya ndoto zake za kusonga mbele kufutwa kwa majeruhi, anasema kwamba benchi nzima la ufundi linafahamu kuwa mchezo wa Jumapili dhidi ya Congo ni mgumu kwa sababu ya umuhimu wake.

Na akiwaelezea Congo - wapinzani wake, Kocha Shime anasema: “Ni timu ya kawaida kwa maana wanafungika. Kwenye mchezo huu ukiangalia kwa makini sisi ndio tunahitaji zaidi ushindi kuliko Congo. Lakini nataka uwaambie Watanzania kwamba pamoja na hayo, nawaheshimu Congo, najua wako nyumbani lakini mwisho wa siku ni wachezaji 11 kila upande ndio watakaoingia uwanjani.”

Amesema kwamba amekiandaa kikosi chake vema kabisa katika eneo la mbinu, ufundi na saikolojia. “Akili za vijana wangu wooooote ni kuhakikisha tunafanya vema kwenye mchzo wa Jumapili.”

Naye Kocha wa Makipa, Muharami Mohammed au Shilton, alisema: “Silaha zangu ziko tayari kwa vita, makipa wangu wangu wote akiwamo Kelvin Kayego, Ramadhani Kabwili na Brazio wote wako fiti. Ye yote kati yao anaweza kucheza.”

MKWASA ATANGAZA KIKOSI CHA TAIFA STARS KITAKACHOIVAA ETHIOPIA



Kocha Mkuu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa ametaja majina ya nyota 24 watakaounda kikosi ambacho kitasafiri mwishoni mwa wiki ijayo kwenda Addis Ababa, Ethiopia kucheza na wenyeji wetu kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Oktoba 8, mwaka huu.

Mkwasa maarufu kwa jina la Master amesema wachezaji aliowaita wataingia kambini Oktoba 2, 2016 kabla ya kuanza kukiandaa kuanzia Oktoba 3, 2016 ikiwa mara baada ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ya mwishoni mwa wiki hii ambako Mwadui itacheza na Azam huku Mbao ikishindina na JKT Ruvu Oktoba 2, mwaka huu.

Nyota wa Stars walioitwa na Mkwasa ni:

Makipa

Deogratius Munishi – Young Africans

Said Kipao – JKT Ruvu

Aishi Manula – Azam FC

 Mabeki

Shomari Kapombe – Azam FC

Juma Abdul – Young Africans

Vicent Andrew - Young Africans

Mwinyi Haji - Young Africans

Mohamed Hussein – Simba SC

David Mwantika - Azam FC

James Josephat – Tanzania Prisons

 Viungo wa Kati

Himid Mao - Azam FC

Mohammed Ibrahim – Simba SC

Jonas Mkude – Simba SC

Muzamiru Yassin – Simba SC

Viungo wa Pembeni

Shiza Kichuya – Simba SC

Simon Msuva - Young Africans

Juma Mahadhi - Young Africans

Jamal Mnyate – Simba

Hassan Kabunda – Mwadui FC

Washambuliaji
Ibrahim Ajib – Simba SC

John Bocco - Azam FC

Mbwana Samatta - CK Genk ya Ubelgiji

Elius Maguli – Oman

Thomas Ulimwengu – TP Mazembe Congo

 Mchezo huo utakaofanyika jijini Addis Ababa, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF), wameo

Hii ni faida kwa Tanzania kama itashinda mchezo huo kwa maana kina alama za nyongeza kama inatokea unaifunga timu mwenyeji.

Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 132 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Ethiopia yenyewe inashika nafasi ya 126.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Ujerumani, Colombia na Brazil.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 34 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Algeria, Senegal, Tunisia na Ghana.

MO AMWAGA MAMILIONI SIMBA KWA AJILI YA KUIUA YANGA KESHO



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Klabu ya Simba inayo furaha kubwa ya kutangaza kumshukuru mlezi wake bwana Mohammed Dewji kwa kuanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.

Dewji maarufu kama Mo tayari ameshaanza kulipia mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na Sekretarieti ya klabu na atafanya hivyo katika kipindi chote cha mpito kuelekea mabadiliko ya kimuundo ya klabu.

Mbali ya hayo mfanyabiashara huyo mkubwa barani Afrika atalipia kodi za nyasi bandia na gharama nyingine za uendeshaji wa klabu.

Uongozi wa Simba unamshukuru sana MO,ukizingatia klabu kwa sasa haina mdhamini na unaamini uwekezaji huo ni chachu ya kuwarejeshea furaha Wanasimba na hatimaye kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya msimu huu na misimu mingi ijayo.

Mwisho klabu inawaomba washabiki wake wajitokeze kwa wingi siku ya Jmosi ya Oktoba Mosi pale uwanja wa Taifa,kuishangilia timu yao itakapocheza mechi ya ligi dhidi ya Yanga.

Tunaamini mechi hiyo ni mwendelezo wa furaha kwa wanachama na washabiki wetu kote nchini.

Pia tuwaombe sana kukumbuka kununua tiketi kwa mawakala wa Selcom waliopo katika maeneo mbalimbali.
Ikumbukwe tiketi za mechi hii ni za kieletroniki.

Imetolewa na
HAJI S. MANARA
MKUU WA HABARI
SIMBA SC


SIMBA NGUVU MOJA

Thursday, September 29, 2016

SERENGETI BOYZ YAWASILI CONGO BRAZZAVILLE


Makocha wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys, Muharami Mohammed Sultan maarufu kama Shilton (kushoto) anayewanoa makipa, Kocha Mkuu Bakari Nyundo Shime au Mchawi Mweusi na Mshauri wa Maendeleo ya soka la Vijana, Kim Poulsen wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuwasili Hoteli ya Michael’s iliyopo Barabara ya Nelson Mandela jijini Brazzaville, Congo.

Wakishuka kutoka kwenye basi

Wakiingia hotelini

Kutoa kushoto, Kibwana Shomari, Yohana Mkomola na Rashid Ada wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys, wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maya Maya mara baada ya kutua leo wakitokea Kigali nchini Rwanda walikopiga kambi kabla ya kuwavaa vijana wenzao wa Congo, Jumapili ya Oktoba 2, 2016 kwenye dimba la Massamba Sebat, Brazzaville.  Timu hiyo imefikia Hoteli ya Michael’s iliyopo Barabara ya Nelson Mandela jijini hapa. Kikosi hicho kimetua salama salmin kujindaa kuifumua Congo Jumapili.


Kipa Na. 1 wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys, Ramadhani Kabwili akionyesha furaja ya kuwa fiti mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maya Maya, tayari kabisa kuwavaa vijana wenzao wa Congo, Jumapili ya Oktoba 2, 2016 kwenye dimba la Massamba Sebat, Brazzaville.  Timu hiyo imefikia Hoteli ya Michael’s iliyopo Barabara ya Nelson Mandela jijini hapa. Kikosi hicho kimetua salama salmin kujindaa kuifumua Congo Jumapili. (Picha na Alfred Lucas wa TFF).


Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys, wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maya Maya mara baada ya kutua leo wakitokea Kigali nchini Rwanda walikopiga kambi kabla ya kuwavaa vijana wenzao wa Congo, Jumapili ya Oktoba 2, 2016 kwenye dimba la Massamba Sebat, Brazzaville.  Timu hiyo imefikia Hoteli ya Michael’s iliyopo Barabara ya Nelson Mandela jijini hapa. Kikosi hicho kimetua salama salmin kujindaa kuifumua Congo Jumapili. (Picha na Alfred Lucas wa TFF).

MANJI AIPA ZAWADI YANGA SASA KUJENGA UWANJA WA KISASA.


Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa timu ya Yanga pamoja na kituo maalumu cha Kukuza vipaji vya michezo.


 Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Yanga, Mama Fatuma Karume wakati wa uzinduzi wa eneo la Uwanja lenye zaidi ya ekari 700 Geza Ulole lililopewa jina la Kijiji cha Yanga leo Jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Kamati ya utendaji ya Yanga na wawakilishi kutoka kwa wadhamini wa timu hiyo Quality Group
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Mehboob Manji ameipatia klabu yake eneo la zaidi ya ekari 700  lilipo Geza Ulole, Kigamboni, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kisasa.

Akiwa amewakilishwa na wasaidizi wake  wamekabidhi eneo hilo leo mchana katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Maofisa wa chama na Serikali ya Kigamboni.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu, Mama Fatma Karume akiwa ameambatana na  Mjumbe mwingine wa Bodi hiyo, Dk. Jabir Idris Katundu pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu, Samuel Lukumay, Sizya Lyimo na Kaimu katibu mkuu Baraka Deusdedit.

Eneo hilo lililopewa jina la Kijiji cha Yanga, rasmi utafanyika ujenzi wa kijiji cha michezo cha yanga ambapo patakuwa na uwanja wa kisasa wa mazoezi, uwanja wa mechi, hosteli na kituo cha kukuza vipaji kwa vijana pamoja na Hospital na shule.

Sunday, September 25, 2016

YANGA YAPWELEA KWA STAND UNITED


MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga leo wametepweta mbele ya Stand United, baada ya kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Bao pekee na la ushindi la Stand United lilipachikwa wavunu na mshambuliaji Pastory Athanas na hivyo kuiwezesha kutoka uwanjani na pointi zote tatu.

Kutokana na ushindi huo, Stand United, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa uongozi kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, imefikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi sita, ikiwa nyuma ya vinara Simba, wenye pointi 16.

Kwa upande wa Yanga,  imeendelea kubaki na pointi  10 baada ya kucheza mechi sita.

Licha ya kushambuliana kwa zamu muda wote wa dakika 45 za kipindi cha kwanza, Yanga na Stand United zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Athanas aliifungia Stand bao hilo la pekee dakika ya 58  baada ya kuwatoka mabeki Haji Mwinyi na Vincent Bossou kabla ya kufumua shuti katikati yao, lililompita ubavuni kipa Ally Mustapha na mpira kutinga wavuni.

Japokuwa Stand United imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa uongozi, haijapoteza mechi hata moja tangu ligi hiyo ilipoanza msimu huu, ikiwa imeshinda mechi tatu na kutoka sare mechi tatu.

TAIFA STARS KUJIPIMA UBAVU NA ETHIOPIA


TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kucheza na Ethiopia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, utakaopigwa Oktoba 8, mwaka huu, mjini Addis Ababa.

Mchezo huo ulio katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), umeombwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF).

Iwapo Taifa Stars itashinda mechi hiyo, huenda ikapanda nafasi za juu katika ubora wa mchezo huo duniani.

Kwa sasa, Tanzania inashika nafasi ya 132 kwa ubora wa soka duniani wakati Ethiopia inashika nafasi ya 126.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa, anatarajiwa kutangaza kikosi kitakachosafiri kwenda Ethiopia, baada ya kumalizika kwa mechi za ligi kuu zitakazochezwa Oktoba 3, mwaka huu.

Saturday, September 24, 2016

SIMBA YANG'ARA LIGI KUU, AZAM YATEPWETA



WAKONGWE wa soka nchini, Simba leo wamezidi kujitanua kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, baada ya kuitandika Majimaji mabao 4-0.

Wakati Simba ikitoka uwanjani na ushindi huo mnono, mabingwa wa mwaka juzi, Azam walishindwa kutamba ugenini baada ya kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na Ndanda FC, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nangwande Sijaona mjini Lindi.

Ikicheza Uwanja wa Taifa, baada ya kuulalamikia Uwanja wa Uhuru kwamba unaumiza wachezaji, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Washambuliaji walioiwezesha Simba kuibuka na ushindi huo mnono walikuwa Jamal Mnyate, aliyefunga mawili, Shizza Kichuya na Daudit Mavugo.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare moja.

Mavugo aliifungia Simba bao la kuongoza kipindi cha kwanza baada ya kipa Amani Simba wa Majimaji kutema shuti lililopigwa na Ibrahim Ajibi.

Kichuya aliiongezea Simba bao la pili kwa njia ya penalti dakika ya 67 baada ya beki mkongwe wa Majimaji, Lulanga Mapunda kuunawa mpira ndani ya 18.

Mnyate aliiongezea Simba bao la pili dakika ua 74 baada ya kumalizia krosi maridhawa kutoka kwa Mo Ibrahim kabla ya kuongeza la nne dakika ya 81 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Jonas Mkude.

Nao Ndanda waliwaadhiri vigogo Azam kwa kuwapiga mweleka wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na Khamis na Mponda, wakati bao la Azam lilifungwa na Bocco.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, JKT Ruvu imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, Prisons ilitoka suluhu na Mwadui, Mtibwa imelazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mbao FC.

Ligi hiyo inaendelea tena keshi wakati Yanga itakapovaana na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga huku Ruvu Shooting ikivaana na Toto Africans.


(PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA MICHUZI)

Thursday, September 22, 2016

NGASSA, DANNY LWANGA WAMWAGA WINO FANJA FC


HATIMAYE mshambuliaji Mrisho Ngassa ameingia mkataba wa kuichezea klabu ya FC Fanja ya Oman kwa miaka miwili.

Ngassa amejiunga na Fanja wiki chache baada ya kuvunja mkataba wake wa kuichezea klabu ya Free State ya Afrika Kusini.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Yanga, Simba na Azam, anaungana na mshambuliaji wa Simba, Danny Lyanga, ambaye naye amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo.

Ngassa alivunja mkataba wa miaka minne na Free State, August 25, 2016, akiwa ameitumikia mwaka mmoja pekee.

Kwa upande wa Lyanga, ambaye alikuwa hana nafasi ya kucheza Simba kutokana nafasi ya ushambuliaji kuwepo na washambuliaji kama Laudit Mavugo kutoka Burundi, Fredrick Blagnon kutoka Ivory Coast na Ibrahim Ajib, uongozi wa Simba ulimruhusu akafanye majaribio klabu ya Fanja SC.

SERENGETI BOYS YAPAA KWENDA KAMBINI RWANDA


TIMU ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys imeondoka nchini leo asubuhi kwenda Rwanda kuweka kambi ya kujiandaa kurudiana na Congo-Brazzaville.

Serengeti Boys imeondoka nchini saa tatu kamili asubuhi kwa ndege na inatarajiwa kuwasili mjini Kigali, Rwanda saa 4.30 asubuhi.

Timu hiyo inatarajiwa kurudiana na Congo-Brazzavile, wiki ijayo katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika, zinazotarajiwa kufanyika mwakani nchini Madagascar.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita, Serengeti Boys iliichapa Congo-Brazzavile mabao 3-2. Ili ifuzu kucheza fainali hizo, Serengeti Boys inahitaji sare ya aina yoyote.


RAIS MAGUFULI AIGAGILIA KILIMANJARO QUEENS



KILIMANJARO QUEENS KUTUA DAR LEO KWA NDEGE KUTOKA MWANZA


Mabingwa wapya wa Kombe la Chalenji la CECAFA, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens, inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo Septemba 22, 2016 saa 7.00 mchana kwa ndege ya FastJet ikitokea Mwanza.

Mara baada ya kutua, itakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Coartyard iliyoko Sea View, Upanga jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata chakula cha mchana ambako watakuwako viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wale wa Serikali akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.

Timu hiyo jana, Septemba 21, 2016 ilitua Kagera ambako imetumia siku ya leo kuwafariji wahanga wa tetemeko la ardhi.

Itakumbukwa kwamba kabla ya kwenda Jinja, Uganda ambako ilivuna ubingwa huo katika fainali zilizofanyika jana kwa kuilaza Kenya katika fainali zilizofanyika Uwanja wa Njeru, Kilimanjaro Queens iliweka kambi mjini Bukoba ambako ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi na kushinda mabao 3-0 Septemba 8, mwaka kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Kilimanjaro Queens inatarudi Kagera kusema: “Ahsante” kwa wenyeji akiwamo Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstafu Salum Kijuu aliyewakabidhi bendera kabla ya safari, lakini pia kuwapa pole Wahanga wa janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Edna Lema  wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake, Amina Karuma.

Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.

Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Wakati huo huo, timu ya taifa ya Vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kesho  inatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam, Tanzania kesho Septemba 22, 2016 kwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya kambi ya siku 10 kabla ya kuivaa Congo-Brazzaville katika mchezo wa pili kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Baada ya Serengeti Boys kushinda mabao 3-2, jijini Dar es Salaam, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itafayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

BOCCO MCHEZAJI BORA WA MWEZI AGOSTI WA LIGI KUU BARA



Mshambuliaji John Bocco wa Azam FC amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Agosti kwa msimu wa 2016/2017.

Bocco ambaye pia ni nahodha wa Azam FC aliwashinda wachezaji Mzamiru Yasin wa Simba na Said Kipao wa JKT Ruvu. Katika mechi mbili ilizocheza katika mwezi huo, Bocco aliifungia  timu yake mabao matatu likiwemo la kusawazisha dhidi ya African Lyon.

Alifunga mabao mengine mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 wa timu yake dhidi ya Majimaji. Katika mechi hizo mbili, Azam FC ilifanikiwa kupata pointi nne kati ya sita.

Mwezi huo ulikuwa na raundi mbili tu za Ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu. Kwa kushinda tuzo hiyo, Bocco atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

TFF YASITISHA MATUMIZI YA UWANJA WA UHURU



Mechi mbili za raundi ya sita za Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Majimaji, na African Lyon na Kagera Sugar sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Uhuru.

Mabadiliko hayo yametokana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusitisha kwa muda kuutumia Uwanja wa Uhuru katika kipindi hiki ambacho limeanza kufanyia marekebisho sehemu ya uwanja huo ambayo ni ya nyasi bandia (artificial turf).

Hivyo, mechi ya Simba na Majimaji itafanyika Jumamosi, Septemba 24 wakati ile ya African Lyon na Kagera Sugar itachezwa Jumatatu, Septemba 26. Jumapili, Septemba 25 Uwanja Taifa utatumiwa kwa mechi ya timu za Wabunge za Simba na Yanga ili kuchangia waathirika wa janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.

Mechi nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom zitakazochezwa Jumamosi, Septemba 24 ni kati ya JKT Ruvu na Mbeya City (Mabatini), Ndanda na Azam (Nangwanda Sijaona), Tanzania Prisons na Mwadui (Sokoine), Mtibwa Sugar na Mbao (Manungu).

Jumapili kutakuwa na mechi kati ya Stand United na Yanga (Kambarage), na Ruvu Shooting na Toto Africans kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Kutokana na marekebisho yanayofanyika Uwanja wa Uhuru, mechi ya kundi ya A ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Ashanti United na Pamba iliyokuwa ichezwe Ijumaa, Septemba 23 kwenye uwanja huo sasa itafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

DRFA YAWAKUMBUSHA MAJUKUMU,KILIMANJARO QUEENS NA SERENGETI BOYS

Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA kimezipongeza timu za taifa za soka,Kilimanjaro Queens iliyofanikiwa kuunyakua ubingwa wa michuano ya CECAFA wanawake iliyofanyika mjini Jinja nchini Uganda.

Timu hiyo iliyoiwakilisha tanzania bara na ikiwa chini ya kocha mkuu Sebastian na msaidizi wake Edina Lema,ilianza mashindano hayo kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ambapo imeisambaratisha Kenya kwa kuifunga magoli 2-1.

Mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo,amesema kitendo cha Kilimanjaro Queens kutwaa kikombe hicho kinaonesha ni kwa kiasi gani walivyo tayari kwaajili ya mapambano,na endapo nguvu kubwa itatumika katika maandalizi yao wanaweza kulitangaza zaidi taifa lao.

Kasongo amelipongeza pia benchi la ufundi kwa uvumilivu mkubwa waliouonesha tangu walipokabidhiwa kikosi hicho licha ya kuwa muda na matayarisho yao hayakuwa rafiki kiushindani.

Michuano hiyo iliyoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka huu na baraza la vyama vya soka katika ukanda wa afrika mashariki,imeiweka tanzania katika ramani kupitia medani ya mpira wa miguu barani afrika.

Mbali na timu hiyo ya wanawake, Drfa imeimwagia sifa Serengeti Boys inayosaka tiketi ya kutinga katika michuano ya kuwania kombe la mataifa ya afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika mwezi april nchini Madagascar.

Kikosi hicho chini ya kocha Bakari Shime, kimesaliwa na mchezo mmoja wa marudiano dhidi ya Congo Brazzaville kabla ya kutinga katika fainali hizo,ambapo katika mchezo wa kwanza wamefanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-2.

Mwenyekiti Kasongo ameongeza kuwa mafanikio ya vikosi hivyo vya taifa ni ya watanzania wote na kuwaomba wachezaji wasibweteke na hali hiyo na badala yake wazidi kujituma ili kuboresha viwango vyao vya kucheza soka na kulisaidia taifa.

IMETOLEWA NA CHAMA CHA SOKA MKOA WA DAR ES SALAAM,DRFA

Wednesday, September 21, 2016

KILIMANJARP QUEENS YAWEKA REKODI YA KUWA YA KWANZA KUTWAA KOMBE LA CHALENJI KWA WANAWAKE








Haikuwa ubashiri, badala yake ilikuwa ni mipango thabiti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha kwamba inavuna ushindi na kuwa mabingwa wa Kombe la Chalenji la CECAFA kwa wanawake baada ya kuilaza Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Nambole jijini Jinja nchini Uganda.

Mabao ya timu ya taifa Tanzania ya wanawake maarufu kama Kilimanjaro Queens katika mchezo wa leo Septemba 20, 2016 yamefungwa na Mwanahamisi Omari katika kipindi cha kwanza kabla ya Kenya kujitutumua na kupata bao la kufutia machozi kipindi cha pili katika mchezo uliokuwa na ushindani wa aina yake.

Matokeo hayo yatakuwa kupozwa kwa ndugu zao wa Zanzibar Queens ambao walitolewa mapema katika mashindano hayo yaliyoanza Septemba 11, 2016 kabla ya kufikia tamati leo katika fainali hizo zilizovutia mashabiki wa mpira wa miguu nchini Uganda ambako kila upande ulikuwa na watu wanaowasapoti.

Timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini Uganda kesho Jumatano na kwenda moja kwa moja Kagera ambako ilipiga kambi kabla ya kwenda Jinja. Itarudi hapo kusema ahsante kwa wenyeji, lakini pia kuwapa pole ya janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Hilda Masanche wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake.

Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.

Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Tuesday, September 20, 2016

DIAMOND TRUST BANK YADHAMINI LIGI KUU YA VODACOM



Benki ya Diamond Trust (DTB) leo imesaini kuingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kudhamini Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) kwa msimu wa mwaka 2016/2017.

DTB inaungana na mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na wadhamini wengine katika kudhamini ligi hiyo maarufu kama Ligi Kuu ya Vodacom.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya utiaji saini huo iliyofanyika Hoteli ya Serena, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Benki hiyo, Joseph Mabusi amesema:  “Udhamini huu utasaidia zaidi maendeleo ya soka nchini kwa kuziwezesha timu shiriki pamoja na jitihada zingine za TFF. Soka inaunganisha Watanzania wa matabaka mbalimbali ambao ni wateja wetu na si kama benki tungependa kuwa karibu nao zaidi kupitia mchezo huu.”

Mabusi aliongeza kwa kusema:  “Tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya ligi kuu na tunaamini udhamini huu utazidisha ari ya kuwahudumia Watanzania wote.

Benki ya Diamond Trust imekuwa ikiipa kipaumbele michezo mbalimbali ikiwemo soka, ambapo timu rasmi ya soka inayoundwa na Wafanyakazi imefanikiwa kushinda vikombe na mataji mbalimbali ya soka likiwemo taji la ligi ya mabenki nchini inayojulikana kama BRAZUKA KIBENKI mwaka 2015 pamoja na ngao ya hisani ya ligi hiyo mwaka 2016.

Benki pia inadhamini timu ya soka ya Agathon iliyopo Mbagala inayoshiriki ligi soka daraja la tatu. Zaidi ya hayo benki pia inajivunia kuwa moja kati ya wadhamini wa michuano ya CECAFA Kagame Cup mwaka 2015.

Ligi hiyo inajumuisha timu 16 kutoka Tanzania bara zinazocheza kwa mfumo wa mechi za nyumbani na ugenini ambazo ni Young Africans, Simba Sports Club, Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Mbeya City, Majimaji, MbaoFC, African Lyon, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons, Stand United, mwadui FC, Ndanda FC na Toto Africans.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Shirikisho la Soka Tanznaia –TFF wakiongozwa na Rais wao Ndugu Jamal Malinzi, Wafanyakazi wa Benki ya DTB, wawakilishi kutoka Vodacom, wadau mbalimbali wa soka pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Malinzi ameshukuru na kuupongeza udhamini huo uliotolewa na benki hiyo na pia ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kukuza soka nchini. “Kwa heshima ana furaha kubwa nawakaribisha DTB Tanzania kwenye ligi kuu na familia ya TFF kwa ujumla.”

Benki ya Diamond Trust ina matawi 25 nchini, ikiwa na matawi kumi na moja (11) jijini Dar es Salaam (Mtaawa Jamaat, Masaki, Morocco, Magomeni, Mbezi, Mbagala, barabara ya Nyerere, Msimbazi - Kariakoo, barabara ya Nelson Mandela, Upanga katika barabara ya umoja wa mataifa na katika makutano ya barabara ya Mirambo na mtaa wa Samora).

Vile vile ina matawi katika miji ya Arusha (2), Mwanza (2) na katika miji ya Dodoma, Kahama, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Tabora ,Tanga na Zanzibar.

DTB Tanzania ni mshirika wa mtandao wa maendeleo ya kiuchumi wa Aga Khan - Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) ambao ni sehemu ya mtandao wa maendeleowa Aga Khan Development Network).

DTB Kenya ni miongoni mwa wanahisa muhimu wa DTB Tanzania. DTB Tanzania pia ni sehemu ya mtandao wa mabenki ya DTB Group yenye matawi zaidi ya 120 Afrika Mashariki na kati.

WAPENZI WA SOKA KUNUFAIKA NA ‘SOKA BANDO’

Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara , “Vodacom Premier League” imesikia kilio cha mashabiki na wapenzi wa soka nchini na kuamua kuwaletea kifurushi maalumu kinachojulikana kama ‘Soka bando’ ambacho ni mahususi kwa ajili ya mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu unaopendwa duniani kote.

Vodacom Tanzania imebuni kifurushi hiki kwa ajili ya kuwapatia taarifa za soka za hapa nchini na ligi za kimataifa kwa gharama nafuu ya shilingi 500/-Kifurushi cha ‘Soka bando’ kitakuwa kinawapatia mashabiki wa soka muda wa maongezi wa dakika 14 Vodacom kwenda Vodacom na pia dakika 2 vodacom kwenda mitandao mingine, na pia utapata sms 20 kwa saa 24.

Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Nandi Mwiyombella amesema “Kwa gharama nafuu ya shilingi 500/-mashabiki wa soka wanaotumia mtandao wa Vodacom watapata taarifa  mbalimbali za soka za hapa nyumbani na kimataifa kwa kipindi cha siku 7,dakika 14 za muda wa maongezi Vodacom kwenda Vodacom, dakika 2 za muda wa maongezi kwa mitandao  yote na jumbe fupi za maneno (SMS) 20 kwa kipindi cha masaa 24”

Alisema Vodacom Tanzania imeleta kifurushi hiki cha ‘Soka bando’ kipindi hiki ambacho msimu wa ligi ya VPL unaendelea ni furaha kwa Mtandao wa Vodacom kuwawezesha mashabiki kupata taarifa za ligi kwa urahisi kupitia mtandao wake ikiwemo kuwapatia burudani wateja wake na watanzania wote kwa ujumla.

“Kampuni inathamini na kutambua mchango wa mashabiki katika kukuza ligi hii tangu ilipoanza kuidhamini hivyo ndio maana tumewaletea kifurushi hiki ili wapate  burudani na taarifa za soka kwa wakati na kwa gharama nafuu”.Alisema Mwiyombella.

Ili kununua kifurushi hiki anachotakiwa kufanya mteja ni kupiga  namba *149 * 01#, na kuchagua ‘Soka Bando’. Baada ya  hapo mteja atapata ujumbe unaomtaka ajisajili kwa timu ya soka anayoishabikia kwa kutuma jina la timu mfano “Yanga”  “Simba” au “Azam” nk. kwenda namba 15460.Pia mteja anaweza kupata taarifa za soka kupitia tovuti ya  Mspoti.vodacom.co.tz.

Wateja watakaojiunga na huduma hii pia watapata  nafasi ya kufurahia ofa na zawadi mbalimbali kutoka  Vodacom kama vile muda wa bure wa maongezi, sms au  MB za kuperuzi inteneti hususani timu wanazoshabikia zitakapokuwa zimeibuka na ushindi wa mchezo.

Msimu mpya wa Ligi Kuu ya VodacomTanzania  bara unaendelea  katika viwanja mbalimbali nchini.

SERENGETI BOYS KUWEKA TENA KAMBI NJE YA NCHI


Baada ya kuifunga Congo-Brazzaville mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa Serengeti inatarajiwa kuondoka Alhamisi wiki hii kwenda kupiga kambi nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, taratibu zinapangwa kuhakikisha kwamba timu hiyo inakwenda kupiga kambi kwenye nchi tulivu inayolingana hali ya hewa na Congo Brazzaville kadhalika chakula pamoja na mazingira. Tanzania na Congo Brazzavile, zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itakayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

Katika mchezo uliofanyika jana Septemba 18, 2016 timu hiyo ya Tanzania maarufu kwa jina la Serengeti Boys ilipata mabao yake kupitia Yohana Mkomola na Abdi Makamba wakati yale ya Congo yalifungwa na Langa-Lesse Percy na Makouana Beni ambao mashabiki wa soka walikuwa wakiwalalamikia kuwa ni “wakubwa.”

Ili ifuzu kwa fainali zitakazofanyika mwakani huko Antananarivo, Madagascar katika fainali zitakazoanzia Aprili, 2017, Serengeti Boys inatakiwa ibaki na matokeo yake ya sasa na ihakikishe inapata ushindi na kama sare basi wapate bao kufuta faida ya bao la ugenini ambalo Congo Brazzaville walikuwa wanasheherekea  baada ya mchezo.

AFRICAN LYON KUIVAA TOTO AFRICAN LEO DAR


Mzunguko wa tano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) utafungwa kesho Jumanne Septemba 20, 2016 kwa mchezo kati ya African Lyon ya Dar es Salaam na Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

African Lyon inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuilaza Mbao FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Toto African ilitoka kufungwa 1-0 na Tanzania Prisons ya Mbeya.

Raundi ya sita utapigwa Septemba 24, 2016 na Septemba 25, 2016 kwa michezo mitano siku ya Jumamosi na mitatu siku ya Jumapili. Siku ya Jumamosi JKT Ruvu itaikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Simba itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Azam FC itasafiri hadi Mtwara kwenda kucheza na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Mwadui ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.

Siku ya Jumapili, Septemba 25, mwaka huu Ruvu Shooting inatarajiwa kuikaribisha Toto African kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani huku Stand United ikiwa mwenyeji wa Young Africans katika dimba la CCM Kambarage wakati Kagera Sugar itakuwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru ikicheza na African Lyon.

KASEJA AACHA GUMZO IVORY COAST

Ivory Coast imeiondoa Tanzania katika mchezo wa mpira wa miguu wa ufukweni baada ya kushinda kwa mabao 6-4, lakini wamebaki na jina la Kipa Na. 1 wa timu ya Tanzania, Juma Kaseja wakisema: “Angekuwa tangu mwanzo, wangekuwa na wakati mgumu.”

Kaseja alikuwa kikwazo kwa Ivory Coast katika mchezo uliofanyika Jumamosi iliyopita huko jijini Abdijan ambako wenyeji walitamba kwamba wangeshinda mabao mengi, lakini kikwazo kilikuwa Kaseja na wakahoji wenyeji wa Tanzania: “Anacheza timu gani Tanzania, au mmemtoa nje ya nchi?”

“Kaseja alicheza kwa umahiri na kuzuia michomo mingi kutoka kwa washambuliaji wa Ivory Coast, na mabao aliyofungwa yalikuwa ni kwa bahati mbaya,” amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu mara baada ya kurejea kutua jijini Dar es Salaam leo alfajiri.

Tanzania imeondolewa kwa jumla ya mabao 13-7 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani kupoteza kwa mabao 7-3. Michezo hiyo ni ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni ambako fainali zake zitafanyika jijini Lagos, Nigeria Desemba, mwaka huu.

TFF imepanga kuhakikisha kwamba inaboresha soka la ufukweni baada ya kutengeneza uwanja maalumu wa mchezo huo ulioko kando ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

KOCHA SERENGETI BOYS ATAMBA LAZIMA WAITOE CONGO BRAZZAVILE NA KUFUZU KUCHEZA FAINALI ZA AFRIKA


Kocha wa Serengeti Boys Bakari Shime amesema, kuwakosa wachezaji wake wawili kwenye kikosi cha kwanza kumechangia timu yake kuruhusu magoli mawili kwenyeuwanja wa nyumbani dhidi ya Congo Brazzaville wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa timu za vijana (U17) zitakazofanyika Madagascar mwaka 2017.

Shime amemtaja beki wa kati Dickson Job pamoja na kiungo Ally Nyanzi kuwa kukosekana kwao kulikuwa ni pengo ambalo madhara yake ni kuruhusu magoli mawili kwenye uwanja wa nyumbani.

“Mapungufu ya kumkosa beki wetu wa kati Dickson Job na kiungo Ally Nyanzi yameathiri timu yetu lakini katika mchezo wa marudiano watakuwepo uwanjani na timu yetu itakuwa strong zaidi”, alisema Shime mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Serengeti Boys huku timu yake ikishinda kwa magoli 3-2.

Shime alipoulizwa kama timu yake itaweza kufuzu kutokana na kuruhusu magoli mawili nyumbani ambayo yatawapa kazi ngumu kwenye mechi ya marudiano alisema, kama Congo wameweza kufunga hapa basi hata Serengeti inaweza kupata magoli ugenini.

“Hakuna ushindi mdogo kwenye mchezo wa soka, kama wao wameweza kufunga magoli, sisi vilevile tunaweza kufunga magoli ugenini. Timu yangu imekuwa na rekodi ya kufunga magoli kwenye viwanja vyovyote vile, tumeweza kufunga magoli kwenye viwanja vya ugenini na nyumbani.”

“Siogopi, tutaweza kulinda vizuri ugenini na kushinda. Katika mechi nane, tumefungwa magoli mawili ya penati na moja la kawaida, kwahiyo unaweza kuona tuna safu nzuri ya ulinzi kwa kiasi gani.”

“Walionekana kutuzidi nguvu lakini nimeelezea kwamba timu yetu ilikuwa na mapungufu kidogo katika sehemu ya ulinzi kwahiyo timu yangu haikuwa kwenye ubora wa kila wakati.”

“Timu bora inashinda popote pale Serengeti ni timu bora, imeshinda mechi zote za nyumbani na haijafungwa mechi hata moja ugenini. Bado tunanafasi ya kushinda Congo au kutoka sare.”

Monday, September 19, 2016

SERENGETI BOYS YAICHEZESHA MCHAKAMCHAKA CONGO BRAZZAVILLE




TIMU ya soka ya Taifa ya Vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys jana ilijiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za Afrika mwakani, baada ya kuichapa Congo Brazzavile mabao 3-2.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Serengeti Boys ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Mshambuliaji Yohana Oscar ndiye aliyeing'arisha Serengeti Boys baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Alifunga bao la kwanza dakika ya 38 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 41.

Congo Brazzavile ilikianza kipindi  cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 73 lililofungwa kwa njia ya penalti na Langa-Lesse Percy baada ya Mboungou Prestige kuchezewa rafu na beki Israel Patrick ndani ya eneo la hatari.

Dakika ya 81, 'Super Sub' Issa Abdi aliipatia Serengeti goli la tatu baada ya mabeki wa Congo kushindwa kuokoa mpira wa kona iliyopigwa na Asadi Juma kabla ya kumkuta mfungaji.

Bopoumela Chardon aliipatia Congo goli la pili dakika ya 90 baada ya wachezaji wa Serengeti kushindwa kuondoa mpira wa kona uliokua unazagaa langoni.
(PICHA KWA HISANI YA MICHUZI BLOGU)

KILIMANJARO QUEENS YATINGA FAINALI KOMBE LA CHALENJI, YAINYUKA UGANDA 4-1

TIMU ya soka ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens jana ilifuzu kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kuibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji, Uganda.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ufundi, Njeru mjini Jinja, Kilimanjaro Queens ilijipatia mabao yote manne katika kipindi cha kwanza.

Kutokana na ushindi huo, Kilimanjaro Queens sasa itavaana na Kenya katika mechi ya fainali itakayopigwa keshokutwa.

Kenya ilitinga hatua hiyo jana baada ya kuishinda Ethiopia mabao 3-2 katika mechi nyingine ya nusu fainali.

Mabao ya Kilimanjaro Queens yalifungwa na Donosia Daniel dakika ya sita, Mwanahamisi Omari 'Gaucho' dakika ya 17, Stumai Abdallah dakika ya 31 na Asha Rashid 'Mwalala'.

Hii ni mara ya kwanza kwa CECAFA kuandaa michuano ya Chalenji kwa wanawake na iwapo Kilimanjaro Queens itatwaa taji hilo, itakuwa imeweka rekodi ya kuwa ya kwanza kulinyakua.

NGASSA AENDA KUJARIBU BAHATI YAKE ARABUNI


KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amewasili katika nchi za Falme ya Kiarabu kwa ajili ya kucheza soka ya kulipwa.

Ngassa aliondoka nchini mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa mwaliko wa klabu ya Fanja ya Oman, ambayo wanasoka wengi wa Tanzania wamewahi kuichezea.

"Ninakwenda Oman kufanya mazungumzo na Fanja,"alisema Ngassa wakati akijiandaa kwenda nchini humo.

Uamuzi wa Ngassa kwenda Oman umekuja wiki chache baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Free State ya Afrika Kusini.

Sunday, September 18, 2016

KUZIONA SERENGETI BOYS, CONGO BRAZZAVILLE LEO DEZO



Na Lorietha Laurence-WHUSM.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo  Mhe.Nape Moses Nnauye ameahidi kutoa shilingi  laki tano kwa kila goli litakalofungwa na timu ya Serengeti Boys  katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 utakaofanyika kesho katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Congo-Brazzaville.

Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mhe.Nape amesema milango ipo wazi kwa wadau wengine wa michezo kujitolea katika kuiwezesha timu  na hivyo kufanya vizuri katika  mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda ili kufuzu kwa fainali hizo.

“Hii timu ni yetu sote hivyo inahitajika tuimiliki, tuepe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville” alisema Mhe. Nape.

Aidha aliongeza kuwa kesho asubuhi atakutana na wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla ya kuanza kwa mechi na kuwataka watanzania  kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa motisha wachezaji kwa kuwashangilia  na kuwatia moyo.

Mbali na hayo Waziri Nape alitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za kieletroniki zilizozinduliwa hivi karibuni kwa kueleza kuwa kadi hizo bado hazijaanza kutumika rasmi ili zitaanza kutumiwa katika mchezo baina ya Wabunge wa Simba na Yanga pamoja na Bongo Fleva.

Timu ya Serengeti Boys inaundwa na vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo wa kesho watahitaji ushindi na baadaye kufanya mechi ya marudiano mnamo Oktoba 2 mwaka huu nchini Congo-Brazzaville.

NI KUFA NA KUPONA KWA KILIMANJARO QUEENS LEO, INACHEZA NUSU FAINALI DHIDI YA UGANDA



TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ya wanawake, Kilimanjaro Queens leo inashuka kwenye Uwanja wa Ufundi, Njeru mjini Jinja, Uganda kumenyana na wenyeji, Korongo Jike katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
Kocha wa Kilimanjaro Queens, Sebastian Nkoma amesema kwamba hakutaka vijana wake kutumia nguvu nyingi katika mchezo wa mwisho wa Kundi B, ili kuzitunza kwa ajili ya Nusu Fainali.
“Nilijua tutacheza na ama Kenya au Uganda katika Nusu Fainali, zote ni timu ngumu, kwa hiyo tukacheza kwa maarifa sana mechi yetu na Ethiopia, ili tusijichoshe sana na kukwepa pia wachezaji kupata maumivu. Tumefanikiwa na sasa tunaelekeza nguvu zetu katika Nusu Fainali,”alisema Nkoma. 
Tanzania imeongoza Kundi B baada ya kushinda kura ya sarafu juzi kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia hivyo kufungana nayo kwa pointi na wasatani wa mabao kileleni, wakati Uganda imeshika nafasi ya pili Kundi A nyuma ya Kenya.
Kwa matokeo hayo, mbali na Kilimanjaro Queens kumenyana na wenyeji Uganda – Nusu Fainali ya itazikutanisha Kenya na Ethiopia.
Kilimanjaro Queens ilianza vizuri michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.
Fainali ya CECAFA Challenge ya kwanza ya wanawake inatarajiwa kufanyika Septemba 20, ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.

YANGA YAIFUNGA MDOMO MWADUI FC

 

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana walizoa pointi zote tatu kutoka kwa Mwadui FC baada ya kuichapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mabao hayo ya Yanga yalipachikwa wavuni na washambuliaji Amisi Tambwe kutoka Burundi na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe, moja katika kila kipindi.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne, ikiwa

imeshinda tatu na kutoka sare moja. Yanga kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo nyuma ya Simba.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mbao FC ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kuitandika Ruvu Shooting mabao 4-1 kwenye uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Nayo Ndanda FC ilizinduka toka usingizini baada ya kuichapa Majimaji mabao 2-1 kwenye

Uwanja wa Majimaji, Mtibwa Sugar iliishinda Kagera Sugar mabao 2-0 mjini Songea wakati Mbeya City ilitoka suluhu na ndugu zao wa Prisons mjini Mbeya.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Stand United na JKT Ruvu Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati Jumanne African Lyon wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza.

SIMBA YAIKALISHA KITAKO AZAM



BAO lililofungwa na mshambuliaji Shiza Kichuya jana liliiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kichuya alifunga bao hilo dakika ya 67 kwa shuti kali akiwa katikati ya mabeki wawili wa Azam, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Saidi Ndemla.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa imetwaa uongozi wa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na wataji wao Yanga wenye pointi 10, sawa na Azam, lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Ushindi huo ulimpa faraja kubwa Kocha Joseph Omog wa Simba, ambaye katika msimu uliopita alikuwa kocha wa Azam kabla ya mkataba wake kuvunjwa.

Tuesday, September 13, 2016

SIMBA, AZAM SASA KUCHEZA UWANJA WA UHURU JUMAMOSI



Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Azam FC na Simba ya Dar es Salaam, utafanyika Jumamosi Septemba 17, 2016 kama ilivyopangwa awali.

Ila mchezo huo utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam badala ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa sababu za kuipa nafasi timu ya taifa ya vijana ya mpira wa miguu ya Congo Brazzaville ambayo itakuwa nchini kwa ajili ya mchezo wa ushindani dhidi ya wenyeji – Serengeti Boys ambayo ni timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Timu hizo zinakutana kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Mchezo huo utafanyika Septemba 18, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam hivyo kutokana na kanuni za mashindano, siku moja kabla mgeni anapata nafasi ya kufanya mazoezi.

Serengeti Boys ambayo ilipiga kambi Shelisheli kujiandaa na mchezo huo ambako imejipanga vyema kuiondoa Congo Brazzaville katika michezo miwili inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali ukianzia huo wa Septemba 18, 2016 kabla ya kurudiana jijini Brazzaville hapo  Septemba 30 au Oktoba 1 au Oktoba 2, mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa (CEO) Azam FC, Saad Kawemba kwa mujibu wa kanuni ya 6 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kipengele cha 5 na 6, ameridhia mchezo huo kufanyika Uwanja wa Uhuru hapo Septemba 17, 2016 na kufuta upotoshwaji unaofanyika kwenye mitandao ya kijamiii.

Kawemba alizungumza hayo, mara baada ya kupokea Ngao ya Hisani halisi mara baada ya tuzo hiyo kufika jijini Dar es Salaam ikitokea China pamoja na vifaa vingine. Itakumbukwa kwamba awali Agosti 17, 2016 mara baada ya kuishinda Young Africans kwa mikwaju ya penalti, Azam walipewa Ngao ya mfano.