'
Saturday, November 28, 2015
ZANZIBAR YAFUFUA MATUMAINI KOMBE LA CHALENJI
ADDIS ABABA, ETHIOPITA
TIMU ya soka ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), jana ilifufua matumaini ya kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea mjini hapa.
Zanzibar jana iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kenya katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
Katika mchezo huo, timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu na katika dakika 29, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifunga bao lakini mwamuzi alikataa kwa madai alikuwa ameotea.
Zanzibar Heroes walifanya shambulizi la kushitukiza dakika 45 ambapo Suleiman Kassim ‘Selembe’ aliipatia timu yake bao la kwanza baada ya kuachia shuti kali akiwa nje ya 18 na kujaa wavuni moja kwa moja.
Hadi mapumziko ya kipindi cha kwanza Zanzibar Heroes walitoka wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 49 Cannavaro alipata nafasi na kupiga shuti ambalo lilitoka nje.
Dakika ya 56 Zanzibar Heroes walipata bao la pili kupitia kwa Hamisi Mcha baada ya kuonganisha krosi safiiliyochongwa na Selembe na kujaa wavuni moja kwa moja.
Kenya walifanya mabadiliko dakika ya 65 ambapo walimtoa Jacob Keli na nafasi yake ilichukuliwa na Kelvin Kimani wakati Zanzibar walimtoa Awadh Juma na kuingia Anthon Mathew.
Wakitandaza kandanda safi, Zanzibar walipata bao la tatu dakika 73 kupitia kwa Selembe baada ya kuwapiga chenga mabeki na kuachia shuti kali lililojaa wavuni moja kwa moja.
Kenya nusura wapate bao dakika 83 ambapo mshambuliaji wake Michael Olunga aliachia shuti kali lililookolewa na kipa Abdulrahman Mohamed.
Kenya walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Jacob Keli baada ya kuachia shuti kali kutokana na mabeki wa Zanzibar Heroes kujichanganya.
Kutokana na matokeo hayo, Zanzibar Heroes inaweza kwenda katika hatua inayofuata ya robo fainali kwa nafasi ya ‘best looser’, lakini inategemea na matokeo ya mechi za leo.
Katika msimamo wa kundi B, Kenya inaongoza kwa kuwa na pointi nne, sawa na Burundi ambapo zimepishana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Uganda ina pointi tatu sawa na Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment