KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, November 13, 2015

RAIS MAGUFULI KUZISHUHUDIA TAIFA STARS NA ALGERIA KESHO


RAIS Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, ambao timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ itavaana na Algeria.

Taifa Stars na Algeria zitapepetana kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Sadiki, alisema Rais Dk. Magufuli, ataongoza Watanzania kuishangilia Taifa Stars katika mchezo huo.

“Tunategemea Rais wetu Dk. John Magufuli atakuwa mstari wa mbele kuwaongoza Watanzania Uwanja wa Taifa kuishangilia Taifa Stars. Ulinzi utaimarishwa,”alisema Sadiki.

Sadiki, ambaye ni mlezi wa Kamati ya Saidia Taifa Stars alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika.

Alisema kamati hiyo imefanya kazi nzuri kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kuiwezesha Taifa Stars kushinda mchezo huo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Tanzania ina kila sababu ya kushinda kwa kuwa imepata maandalizi ya kutosha na ina kocha makini Charles Mkwasa, ambaye ni rafiki wa wachezaji wote.

Alisema hivi karibuni Watanzania walikosa imani na Taifa Stars, baada ya kufanya vibaya, lakini tangu Mkwasa apewe jukumu hilo hamasa imerejea.

Pia Sadiki, amewataka washambuliaji wa kimataifa wanaocheza soka ya kulipwa  timu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, kuipa ushindi Taifa Stars.

Alisema nguvu kubwa waliotumia kuipa ubingwa wa Afrika klabu yao ya TP Mazembe Englebert ya Congo waitumie kuifunga Algeria.

“Kuna timu moja ya Ulaya siwezi kuitaja jina, wachezaji wa hiyo timu wakiwa kwenye klabu yao wanajituma mno, lakini wanapochezea timu ya taifa wamekuwa wakionesha uwezo wa chini hali inayosababisha kuzomewa

“Nawasihi Samata na Ulimwengu wasifike huko, tunataka juhudi zao kwenye timu ya Taifa zionekane na sisi tunawaamini,”alisema Sadiki.

Alisema anaamini wachezaji wa Taifa Stars watajituma na kuweka uzalendo wa taifa lao mbele kuichapa Algeria.

Taifa Stars itacheza na Algeria, baada ya kuitupa nje Malawi kwa jumla ya mabao 2-1 ikiwa chini ya Mkwasa.

Mkwasa, ameingoza timu hiyo katika michezo mitatu ya kimataifa ilipotoka sare ya bao 1-1 na Uganda katika mchezo wa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Aliiongoza Taifa Stars kutoka sare ya bao 1-1 na Nigeria katika mchezo wa kufuzu Fainali za Afrika kabla ya kuvaana na Malawi.

No comments:

Post a Comment