KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 15, 2015

TAIFA STARS YAPOKONYWA TONGE MDOMONI NA ALGERIA, ZATOKA SARE YA MABAO 2-2


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilipokonywa tonge mdomoni na Algeria baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Stars itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa mbele kwa mabao 1-0 hadi wakati wa mapumziko na kuwazidi Waalgeria kwa kila hali uwanjani.

Mbali na kuongoza kipindi hicho, Stars pia ilipata nafasi nzuri zaidi ya tano za kufunga mabao, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake, Elias Maguri, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Farid Mussa.

Maguri alianza kuwainua vitini mashabiki wa Taifa Stars dakika ya 42 alipofunga bao la kwanza kwa kuunganisha kwa kichwa krosi kutoka kwa Mwinyi Haji, aliyepanda na mpira pembeni ya uwanja.

Bao la pili la Stars lilifungwa na Samatta dakika ya 54 baada ya kuunganisha wavuni pande maridhawa kutoka kwa Mudathir Yahya.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Charles Boniface kipindi cha pili, kwa kuwapumzisha Mudathir na Maguri na kuwaingiza Saidi Ndemla na Mrisho Ngasa, yalionekana kupunguza kasi ya timu hiyo na kutoa mwanya kwa Algeria kutawala.

Mabao yote ya Algeria yalifungwa na mshambuliaji wake, Slimani Islam dakika ya 71 na 74.

No comments:

Post a Comment