KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 15, 2015

MAKAMU WA RAIS AWAFARIJI WACHEZAJI WA TAIFA STARS

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, akimfariji nahodha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' baada ya timu hiyo kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Algeria, katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, akimfariji mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu. Kulia ni Mbwana Samatta akibubujikwa na machozi.
SAMIA akimfariji Samatta, baada ya Taifa Stars kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Algeria.
SAMIA akinyoosha mkono kushangilia wakati Taifa Stars ilipopata bao la kuongoza dhidi ya Algeria. Kulia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
SAMIA akiteta jambo na Malinzi wakati wa mchezo huo.
VIKOSI vya Taifa Stars na Algeria kabla ya kuanza kwa mchezo wao jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wachezaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars, wasikatishwe na tamaa na matokeo ya sare waliyoyapata jana dhidi ya Algeria.

Katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilitoka sare ya mabao 2-2 na Algeria.

Akizungumza na wachezaji hao baada ya mchezo huo, Samia aliwataka wachezaji hao kuongeza juhudi na kujituma zaidi ili waweze kushinda mechi ya marudiano.

"Japokuwa mmetoka sare na wapinzani wenu, lakini tumewaona mlivyocheza na kujituma. Msivunjike moyo, hayo ni matokeo ya kawaida katika mchezo. Ongezeni juhudi na kujituma, mna uwezo wa kushinda ugenini,"alisema.

Makamu wa Rais amewataka wachezaji wa Taifa Stars kumuweka mbele Mungu kwa kila jambo kwa vile kwa uwezo wake, wanaweza kushinda mechi ya marudiano.

Taifa Stars na Algeria zinatarajiwa kurudiana keshokutwa mjini Algiers. Ili isonge mbele, Taifa Stars italazimika kushinda mchezo huo au kupata sare ya zaidi ya mabao matatu.

Kikosi cha Taifa Stars kilitarajiwa kuondoka nchini jana usiku kwa ndege ya Fastjet kwenda Algiers kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo.

Samia aliwaeleza wachezaji wa Taifa Stars kuwa, dua za Watanzania zitaelekezwa kwao hivyo wasiwe na hofu ya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment