KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, November 28, 2015

KILI STARS YATOKA SARE YA 1-1 NA WENYEJI ETHIOPIA



Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
TANZANIA Bara imefuzu kwa kishindo Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kufuatia kumaliza mechi za makundi bila kupoteza mchezo.
Bara imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji Ethiopia katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi A leo Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa. Dakika 45 za kwanza zilimalizika bila ya timu hizo kufungana na kipindi cha pili, Kilimanjaro Stars ilianza kupata bao kupitia ka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simon Msuva.
Msuva alifunga bao hilo la pili kwake katika mashindano ya mwaka huu kwa kichwa dakika ya 51 akimalizia krosi maridadi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, Wahabeshi walifanikiwa kupata bao la kusawazisha baada ya beki Salum Mbonde kujifunga katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Mohamed Naser dakika ya 90 na ushei.
Stars sasa inamaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Rwanda iliyomaliza na pointi sita, Ethiopia pointi nne, wakati Somalia inaondoka mikono mitupu.
Mchezo wa kwanza leo, bao la dakika ya 70 la Frank Kalanda limeipa Uganda ushindi wa 1-0 dhidi ya Burundi.
Uganda imemaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Kenya pointi nne ambazo zote zinafuzu moja kwa moja Robo Fainali. 
Sasa Tanzania Bara itamenyana tena na Ethiopia katika Robo Fainali Jumatatu, wakati Uganda itacheza na Malawi katika mchezo wa kwanza keshokutwa.
Jumanne Sudan Kusini itacheza tena na Sudan, wakati Rwanda itamenyana na Kenya.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salum Mbonde, Kevin Yondan, Himid Mao, Said Ndemla, Jonas Mkude, John Bocco, Elias Maguri na Simon Msuva.
Ethiopia; Abel Mamo, Seyoum Tesfaye, Najib Sani, Anteneh Tesfaye, Yared Bayeh, Aschalew Tamene, Panom Gathuoch, Beneyam Tesfaye, Behaylu Girma, Yissack Bereket na Mohamed Naser.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment