KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 25, 2015

KILIMANJARO STARS YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA CHALENJI, ZANZIBAR YAPIGWA 4-0


TANZANIA Bara imejihakikishia kwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Rwanda katika mchezo wa Kundi A jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia.
Ushindi huo, unaifanya Tanzania Bara iongoze Kundi A kwa kufikisha pointi sita na mabao sita, huku ikiwa imefungwa bao moja na sasa itamaliza na wenyeji Ethiopia ikiwa ‘haina presha’.
Kilimanjaro Stars leo ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa kiungo wa Simba SC, Said Ndemla kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 22 baada ya Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kuchezewa rafu na mchezaji mwenzake wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza.
Winga wa Yanga SC, Simon Msuva na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – akaifungia Stars inayofundishwa Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ bao la pili dakika ya 78.
Rwanda ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia kwa Jacques Tuyisenge dakika ya 85. Sasa Amavubi iliyoifunga Ethiopia 1-0 katika mchezo wa kwanza, itamaliza na Somalia waliofungwa 4-0 na Kili Stars.     
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Salum Mbonde, Himid Mao/Jonas Mkude, Simon Msuva, Said Ndemla, John Bocco, Elias Maguri na Deus Kaseke.
Wakati huo huo, Uganda imezinduka katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Zanzibar jioni ya leo mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Huo unakuwa mchezo wa pili mfululizo kwa Zanzibar Heroes kufungwa, baada ya awali kugungwa 1-0 na Burundi na sasa inajiweka katika mazingira magumu kwenda Robo Fainali.
Mabao ya Uganda katika mchezo huo wa Kundi B yamefungwa na Farouk Miya dakika ya 10 na 18, Erisa Ssekisambu dakika ya 48 na Ceasar Okhuti dakika ya 79.
Zanzibar ilipoteza wachezaji wawili kwa kadi nyekundu katika mchezo huo, kwanza kipa wake Mwadini Ally dakika ya 13 na baadaye kiungo Mudathir Yahya dakika ya 74, wote wa Azam FC ya Dar es Salaam. Zanzibar itamaliza na Kenya wakati Uganda itamaliza na Burundi.

No comments:

Post a Comment