KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, November 30, 2015

KILI STARS YATOLEWA KOMBE LA CHALENJI, YAFUNGWA KWA MATUTA NA WENYEJI ETHIOPIA


Na Mwandishi Wetu, ADDIS ABABA
TANZANIA Bara imetolewa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na wenyeji Ethiopia, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Katika mchezo huo wa Robo Fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Tanzania Bara walikuwa wa kwanza kupata kupata bao liliofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyemalizia krosi ya Deus Kaseke dakika ya 25.
Ethiopia walisawazisha kwa penalti ya utata iliyofungwa na Nahodha wake, Panom Gathouch baada ya Mohammed Naser kujiangusha wakati akidhibitiwa na Shomary Kapombe dakika ya 57.
Stars walionekana kutaka kupagawa baada ya wapinzani wao kusawazisha bao na kuanza kuwaletea ubabe marefa, lakini baadaye wakatulia na kuendelea kucheza mpira.
Hata hivyo, bado bahati haikuwa yao, kwani baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1, walitolewa kwa matuta.
Beki Shomary Kapombe na kiungo Jonas Mkude walikwenda kupoteza penalti zao, wakati waliofunga kwa upande wa Kilimanjaro Stars ni kiungo Himid Mao, mshambuliaji Bocco na beki Hassan Kessy.
Waliofunga penalti za Ethiopia ni Panon Gathouch, Mohammed Naser, Ashalew Tamene na Behaylu Girima. 
Katika Robo Fainali ya Kwanza, Uganda imeifunga 2-0 Malawi mabao ya Farouk Miya na Ceasar Okhuti na sasa itakutana na Ethiopia katika Nusu Fainali, wakati Kili Stars inarejea nyumbani Dar es Salaam.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Said Mohamed, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco, Said Ndemla na Deus Kaseke.
Ethiopia; Abel Mamo, Yared Bayeh, Aschalew Tamane, Anteneh Tesfaye, Aschalew Girma, Eliyas Mamo, Zekariyas Tuji, Gothuoch Panom, Beneyam Belay, Mohammed Naser na Bereket Yisshak.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment