KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 1, 2015

SIMBA YAUNGURUMA, YANGA YAREJEA KILELENI


MIAMBA ya soka nchini Simba jana ilitoa onyo kali kwa timu zinazoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Majimaji ya Songea mabao 6-1.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande mmoja, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji Ibrahim Hajib aliweka rekodi ya pili ya kufunga mabao matatu katika mechi moja.

Iliwachukua Simba dakika moja kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Ajib baada ya kufanyika kwa shambulizi la kushtukiza kwenye lango la Majimaji.

Ajib aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 11 alipounganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein kuoka pembeni ya uwanja.

Hamisi Kiiza aliiongezea Simba bao la tatu dakika ya 37 baada ya kuuwahi mpira ndani ya eneo la hatari na kufumua shuti lililotinga wavuni.

Dakika nne baadaye, Ajibu aliifungia Simba bao la nne na kukamilisha orodha yake ya mabao matatu kwa mechi ya jana. Alifunga bao hilo baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Beki Hussein, maarufu kwa jina la Tshabalala, aliiongezea Simba bao la tano dakika ya 78 baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Awadh Juma.

Kiiza alihitimisha karamu ya mabao kwa Simba baada ya kuifungia bao la sita dakika ya 80, kufuatia pige nikupige kwenye lango la Majimaji.

Bao la kujifariji la Majimaji lilifungwa na Ditram Nchimbi dakika ya 88 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mrisho Saidi.

Wakati huo huo, Yanga jana ilirejea kileleni mwa ligi kuu baada ya kuicharaza Kagera Sugar mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kurejea kwenye uongozi wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi moja kati yake na Azam, inayoshuka dimbani leo mjini Mwanza kumenyana na Toto African.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Donaldo Ngoma kipindi cha kwanza kabla ya Daudi Kaseke kuongeza la pili katika kipindi cha pili.

No comments:

Post a Comment