MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars, Mbwana Samatta, amesema anatarajia kuihama klabu yake ya TP Mazembe Englebert ya Congo kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
Samatta, anaondoka TP Mazembe akiwa ameipa ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika na kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo Afrika.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Samatta alisema amechukua uamuzi huo, baada ya kupewa ushauri na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, akimtaka kucheza soka Ulaya.
Samatta, alisema amekuwa akizungumza na Rais huyo mstaafu mara kwa mara na anapowatembelea katika TP Mazembe, aliwasisitizia yeye na Thomas Ulimwengu wasiishie kucheza soka Afrika.
“Ushauri na wosia wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete naufanyia kazi haraka, siku sio nyingi mtafahamu wapi nitakwenda, ndoto zangu ni kucheza soka Ulaya,”alisema Samatta.
Pia nyota huyo amewataka wachezaji chipukizi wa Tanzania kuongeza kasi ili kuchukua nafasi zao TP Mazembe.
“Naamini TP Mazembe itataka tena wachezaji kutoka Tanzania, baada ya sisi kuondoka, huu ni wakati wa wachezaji chipukizi kuchukua nafasi,”alisema Samatta.
Mchezaji huyo aliwasili Dar es Salaam jana asubuhi na Ulimwengu na walijiunga na Taifa Stars kujiandaa na mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Algeria.
Taifa Stars na Algeria zitavaana Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment