'
Wednesday, November 18, 2015
TAIFA STARS YAPIGWA 7-0 NA ALGERIA UGENINI
Na Mahmoud Zubeiry, BLIDA
TANZANIA imetolewa katika mbio za kugombania tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi, baada ya kufungwa mabao 7-0 usiku huu na wenyeji Algeria katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida.
Matokeo hayo, yanaifanya Taifa Stars itolewe kwa jumla ya mabao 9-2, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 na Mbweha hao wa Jangwani katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi mjini Dar es Salaam.
Katika mchezo wa leo usiku wa saa moja kwa majira ya huku sawa na saa tatu kwa majira ya Afrika ya Mashariki , Algeria walipata bao lao la kwanza mapema tu sekunde ya 43 dakika ya kwanza, mfungaji Yacine Brahimi, aliyemalizia krosi ya Mesloub Walid aliyempita beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali, baada ya Himid Mao kupokonywa mpira
Algeria walipata bao la pili dakika ya 23 kupitia kwa Ghoulam Faouzi aliyepiga shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa zaidi ya 20, baada ya kiungo Mudathir Yahya kumchezea rafu Mesloub Walid na kuonyeshwa kadi ya njano.
Mshambuliaji Elias Maguri aliifungia Taifa Stars bao dakika ya 27 kwa shuti la mbali nje ya boki, lakini pamoja na refa Alioum Alioum kuelekea kukubali, akaghairi baada ya ushauri wa msaidizi wake namba mbili, Noupue Nguegoue.
Mudathir Yahya alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 40 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 40 kwa kumkwatua Yacine Brahimi
Na Mahrez Ryad akaifungia Algeria bao la tatu dakika ya 41 kwa shuti kali, akimalizia krosi ya Islam Slimani.
Kipindi cha pili, kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko akiwatoa kipa Ally Mustafa Barthez na winga Farid Mussa na kuwiangiza kipa Aishi Manula na kiungo Salum Telela.
Mabadiliko hayo hayakuwa na msaada wowote kwa Taifa Stars, kwani Algeria ilinufaika zaidi kipindi cha pili kwa kupata mabao manne zaidi.
Islam Slimani alifunga bao la nne dakika ya 48 kwa penalti baada ya Mahrez kugongana na beki wa Taifa Stars, Kevin Yondan.
Ghezzal Faouzi akafunga bao la tano dakika ya 58 kwa penalti baada ya Slimani kugongana na Aishi Manula kwenye boksi wakigombea mpira.
Nahodha wa Mbweha wa Jangwani, Carl Medjani akafunga bao la sita kwa kichwa akimalizia kona ya Mahrez.
Ghezzal Rachid aliyetokea benchi akafunga bao la saba dakika ya 74 akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa Mahrez.
Taifa Stars ikazinduka baada ya bao hilo na kukaribia kufunga mara mbili, kupitia kwa washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Dakika ya 85 Ulimwengu alimpa pasi nzuri Samatta baada ya wawili hao kugongeana vizuri, lakini Mbwana akapiga nje.
Na dakika ya 89, Maguri alimpa pasi nzuri Ulimwengu akafanikiwa kumtoka beki Carl Medjani, lakini kipa M’bolhi Rais akaugusa mpira kidogo na kutoka nje, ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kikosi cha Taifa Stars kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Aishi Manula dk46, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Himid Mao, Mudathir Yahya, Elias Maguri, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Farid Mussa/Salum Telela dk46.
Algeria; M’bolhi Rais, Medjani Carl, Mandi Issa, Ghoulam Faouzi, Belkarou Hichem, Bentaleb Nabil/Guedioura Aldane d36, Riyad Mahrez, Yacine Brahimi/Ghezzal Rachis dk66, Slimani Islam, Mesloub Walid/Ryad Boudebouz dk81 na Zeffanie Mehdi.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment