KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 24, 2010

Buriani 'Jenerali' Juma Mkambi

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa klabu ya Yanga na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Mkambi amefariki dunia. Mkambi alifariki dunia Jumapili iliyopitwa na kuzikwa siku iliyofuata kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Mkambi (55), ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Jenerali, alifariki kutokana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Kabla ya mauti kumkumba, Mkambi alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mazishi ya mwanasoka huyo mkongwe yalihudhuriwa na wanamichezo mbalimbali maarufu nchini, wakiwemo wachezaji wa zamani wa klabu za Simba, Yanga na Taifa Stars.
Enzi za uhai wake, Mkambi alikuwa mchezaji mahiri wa idara ya kiungo, akiwa na uwezo wa kuiunganisha vyema idara ya ulinzi na kiungo na wakati huo huo kusaidia mashambulizi.
Marehemu Mkambi alikuwa mmoja wa wachezaji wa Taifa Stars walioshiriki kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria. Katika fainali hizo, Taifa Stars ilifungwa mechi mbili na kuambulia sare mechi moja.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao kwenye kikosi hicho mwaka huo niJuma Pondamali 'Mensah', Ahmed Amasha, Leodegar Tenga, Salim Amir, Jellah Mtagwa, Mohamed Adolf Rishard, Hussein Ngulungu, Thuweni Ally, Mohamed Salim, Omar Hussein, Leopard Tasso Mukebezi na Peter Tino.
Je, ni kwa nini Mkambi alipewa jina la Jenerali wakati hakuwa mwanajeshi?
Kilichotokea ni kwamba, gazeti moja la Kiingereza la Afrika Magharibi liliandika kuhusu michuano hiyo na kuchambua ubora wa timu zilizoshiriki.
Lilipoizungumzia Tanzania, lilisifu viwango vya wachezaji wa Taifa Stars. Katika moja ya sehemu za habari hiyo, gazeti hilo liliandika:"Generally, Juma Mkambi played so well in midfield," likiwa na maana: "Kwa jumla, Juma Mkambi alicheza vizuri sana katika sehemu ya kiungo."
Gazeti hilo liliposomwa hapa nyumbani, baadhi yetu tulidhani ile ‘Generally’ (kwa ujumla) ilimaanisha cheo cha kijeshi cha ‘General’ na kuanza kumwita Mkambi kwa kutanguliza cheo hicho, tukidhani mwandishi alimwita kwa cheo hicho kwenye makala yake.
Jina hilo liliendelea kutumika kwa Mkambi hadi alipostaafu kucheza soka na hadi mauti yalipomkuta, aliendelea kuitwa hivyo. Kiwango chake katika michuano hiyo kilivifanya vyombo vingi vya habari vimsifu na kwa kweli havikukosea.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Mkambi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika serikali iliyopita, Joel Bendera alimwelezea mchezaji huyo kwamba alikuwa msikivu, aliyejituma na chachu ya hamasa kwa wenzake uwanjani.
Bendera alikuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars iliposhiriki fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980, akiwa chini ya Slowmir Work kutoka Poland.
"Tutamkumbuka siku zote kwani alikuwa mmoja wa wachezaji viungo makini na zaidi nasema alikuwa akijituma sana uwanjani na si mtu wa kusukumwa ndani na nje ya uwanja,”alisema Bendera.
"Tulipokuwa Nigeria, alikuwa akichukia sana kupoteza mchezo, lakini ilikuwa haina jinsi, mchezo wa mpira kufungwa ni sehemu ya mchezo. Tumempoteza mtu muhimu na pia mshauri, maanake mpaka kifo chake, alikuwa mtu wa ushauri hasa jinsi gani tunaweza kujikwamua kwenye soka," aliongeza Bendera.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ambaye aliwahi kucheza na Tenga alisema: "Mkambi alitusaidia sana katika kiungo wakati tulipokuwa Lagos. Nasema hivyo kwa sababu hayo ndiyo mashindano yake makubwa ukiacha hizi Chalenji na mechi nyingine za ligi.”
"Alikuwa na nguvu, alikuwa na uwezo wa kumiliki mipira na alikuwa na mashuti makali. Nilifurahi sana wakati tukicheza pamoja kwani alikuwa akitulisha mipira na alikuwa mpiganaji mzuri uwanjani," alisema Tenga.
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kifo cha Mkambi kimemwacha kwenye simanzi kubwa kwa sababu alikuwa rafiki yake wa karibu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema bila kujali itikadi za klabu zao, alishirikiana vyema na marehemu Mkambi kuanzisha timu ya Tanzania Stars, ambayo iliwahi kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la CAF mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kikamilifu katika maombolezo na mazishiri ya marehemu Mkambi ni pamoja na Jamhuri Kihwelo, Mohamed Mwameja, Mwanamtwa Kihwelo, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Idd Selemani, Dua Said na Lawrence Mwalusako.
Wengine ni Shaaban Geva, Mtemi Ramadhani, Charles Boniface Mkwasa, Makumbi Juma, Kitwana Manara, Omar Gumbo, Athumani Iddi ‘Chama’ na makocha Salum Madadi, Sunday Kayuni na Eugen Mwasamaki.
Mkambi, ambaye ameacha mke na watoto kadhaa, aliianza kupata umaarufu kisoka mwishoni mwa miaka ya 1970 wakati akichezea timu ya Nyota ya Mtwara (sasa Bandari Mtwara), aliyoichezea kwa muda kabla ya kujiunga na Yanga mwaka 1982.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochezea Yanga kwa muda mrefu bila kuhamia klabu nyingine hadi alipostaafu soka mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kabla ya kifo chake, marehemu Mkambi alikuwa katika jopo la Kamati ya Ufundi ya Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na ni mmoja wa washauri wa maendeleo ya soka ya vijana TFF.

No comments:

Post a Comment