KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 25, 2010

Yanga yagonga mwamba kwa Lyon

JARIBIO la klabu ya Yanga kumtoa kwa mkopo kipa Ivan Knezevic kwa ajili ya kupata nafasi ya kumuongeza mshambuliaji Davies Mwape, limegonga mwamba, kufuatia timu ya African Lyon kugoma kumsajili kipa huyo.

Mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu ya Vodacom walipanga kumpeleka kwa mkopo kipa huyo African Lyon, lakini timu hiyo imesisitiza haimuhitaji mzungu huyo kutoka Serbia.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi, mmiliki na meneja mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi alisema wanahitaji wachezaji wazawa zaidi.

“Sisi wenyewe tunatafuta wachezaji wa ndani ili wakifanya vizuri tuwauze, sasa kwa nini tumchukue kipa wa Yanga, ambaye ni mzungu?” Alihoji Kangezi.

Alisema hawana mpango na mchezaji yeyote wa kigeni na waliopo kwenye timu hiyo waking’ara, watawauza nje na ‘biashara’ hiyo inaanzia kwa wachezaji Mbwana Samatta na Hamis Thabiti, ambao wanapelekwa Benfica ya Ureno.

Alisema wachezaji hao walitarajiwa kuondoka jana nchini kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo, huku Jona Kajuna na beki Meshack Abel wakipelekwa Marekani kutafutiwa timu.

“Wachezaji wote wanne wanaondoka Jumatano (jana) na watakuwepo katika nchi hizo kufanya majaribio,” alisema Kangezi.

Kangezi pia alikanusha madai kuwa, Simba imemrejesha Meshack kwa maelezo kwamba, mchezaji huyo anakwenda nje kujaribu bahati yake na kamwe hawezi kukubali kurejea Msimbazi, ambako alikuwepo misimu miwili iliyopita kabla ya kuhamishwa Lyon kwa mkopo.

Wednesday, November 24, 2010

Dk. Nchimbi kuongoza michezo



RAIS Jakaya Kikwete amemteua Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa Waziri wa Habari, Vijana na Michezo.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Nchimbi alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika awamu ya kwanza ya serikali ya nne ya Rais Kikwete.

Dk. Nchimbi amechukua nafasi ya George Mkuchika, ambaye katika baraza jipya lililotangazwa jana, amehamishiwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amemteua Dk. Renella Mukangara kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo.

Dk. Renella amechukua nafasi ya Joel Bendera, ambaye alishindwa katika kura za maoni za uteuzi wa mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini.


Caption
VILIMA KWA VILIMA HAVIKUTANI, LAKINI BINADAMU HUKUTANA!
KOCHA wa makipa wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Pondamali (kulia) akisalimiana na wachezaji wenzake wa zamani wa timu hiyo, Athumani Juma 'Chama' (kushoto) na Mohamed Mwameja (katikati) wakati wa mazishi ya mwanasoka wa zamani nchini, Juma Mkambi yaliyofanyika Jumatatu iliyopita kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

TMK Wanaume Family: Hakuna mchezo



KUNDI la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family lipo mbioni kuachia singo ya ‘Hakuna mchezo’, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya albamu yao ya tatu.

Kiongozi wa kundi hilo, Rashid Ziada 'KR' alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wimbo huo unatarajiwa kuanza kuchezwa mwezi ujao katika vituo mbalimbali vya radio nchini.

KR alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha kazi ya kurekodi singo hiyo, ambayo aliielezea kuwa, itakuwa moto wa kuotea mbali.

Alisema kundi lao lilikuwa kimya kwa muda ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wasanii kutoa kazi zao katika mtindo huru (solo artist), ambapo baada ya kupita katika hatua hiyo, wanajiandaa kutayarisha albamu yao.

KR (33) alisema walimpisha Mheshimiwa Temba na Chege Chigunda kutoa nyimbo zao mpya na baada ya kukamilisha, imefika zamu ya kundi hilo kuendelea kupika nyimbo mpya.

TMK hadi sasa imetoa albamu mbili ambazo ni ‘Kazi ipo’ na ‘Ndio zetu'.

Katika hatua nyingine, KR amesema Aprili mwakani atazindua albamu yake nje ya kundi hilo. Amesema albamu hiyo itakuwa na nyimbo 10 na mpaka sasa ameshakamilisha nyimbo saba.

Q-Chilla avunja ukimya




BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abubakar Katwila amesema anatarajia kuibuka na albamu mpya hivi karibuni.

Akihojiwa katika kipindi cha Bongo Planet kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa mwishoni mwa wiki iliyopita, msanii huyo alisema albamu hiyo itajulikana kwa jina la ‘Machoni’.

Abubakar, maarufu kwa jina la Q-Chilla alisema, amerekodi vibao vilivyomo kwenye albamu hiyo kwa kuwatumia watayarishaji tofauti wa muziki kwa lengo la kuvipa ladha tofauti.

Q-Chilla alisema ukimya wake wa muda mrefu ulitokana na mitihani mbalimbali iliyomkuta katika maisha yake, ambayo alikiri kwamba imempa fundisho kubwa.

“Najua watu wamesema mengi, unaweza kunichukulia vyovyote upendavyo, lakini mitihani ipo na kwangu ni changamoto, watu wasubiri vitu tofauti,”alisema.

Msanii huyo aliyewahi kung’ara kwa kibao chake cha ‘Aseme’ amekiri kuwa, ushindani katika muziki wa kizazi kipya hivi sasa umekuwa mkali, lakini hauwezi kufikia enzi zao.

Alisema wakati alipoanza kutamba katika muziki huo, ushindani ulikuwa mkali zaidi na kila wasanii walipopanda wasanii, vita ya kuwapa mashabiki burudani safi ilikuwa kubwa.

“Enzi zile kila nilipopanda stejini na kuimba, watu walikuwa wakilia. Ilikuwa ukipanda stejini na kumuona msanii huyu na yule, vita inakuwa kali,”alisema.

Akizungumzia hali ya muziki huo kwa sasa, Q-Chilla alisema ushindani upo, wasanii wanafanya vizuri na muziki unakua, lakini pia kuna aina fulani ya upendeleo kwa baadhi ya wasanii.

“Hii ndiyo sababu iliyonifanya nitulie na kuandika zaidi kwa sababu sipaswi kujiona nimebaki peke yangu, haipendezi, mtanichoka haraka,”alisema.

“Kukaa kwangu kimya kwa muda mrefu kumewafanya muwe na hamu na mimi, nahitajika,”aliongeza.

Hata hivyo, Q-Chilla alieleza wasiwasi wake kuwa, muziki wa sasa haudumu kwa muda mrefu kwa vile ni mwepesi na hauna ujumbe wa maana kwa jamii.

“Leo hii mimi nikisimama jukwaani na kuimba ‘Aseme’ na atokee msanii wa sasa aimbe wa kwake, bado mimi nitachukua kijiji changu,”alisema.

Kuliacha Kombe la Chalenji liondoke, itakuwa aibu nyingine kwa Tanzania

Kuliacha Kombe la Chalenji liondoke, itakuwa aibu nyingine kwa Tanzania
MICHUANO ya soka ya Kombe la Tusker Chalenji imepangwa kuanza mwishoni mwa wiki hii hadi Desemba 12 mwaka huu mjini Dar es Salaam, ikizishirikisha timu za mataifa tisa kutoka Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Mbali na nchi hizo tisa wanachama wa baraza hilo, michuano hiyo pia itazishiriki nchi zingine tatu, ambazo zimealikwa. Nchi hizo ni Ivory Coast, Malawi na Zambia.
Kwa mujibu wa CECAFA, nchi wanachama wa baraza hilo zitakazoshiriki katika michuano ya mwaka huu, ambayo imepangwa katika makundi matatu tofauti ni wenyeji Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Zanzibar, Ethiopia na Sudan.
CECAFA imesema uamuzi wa kuzialika Ivory Coast, Malawi na Zambia umelenga kuongeza ushindani na pia kukuza soka katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hasa ikizingatiwa kuwa, viwango vya nchi hizo vipo juu ikilinganishwa na nchi nyingi zinazounda baraza hilo.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema, kwa mara ya kwanza, michuano ya mwaka huu itadhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ambayo itatoa zawadi za jumla ya dola za Marekani 60,000 kwa washindi watatu wa kwanza.
Mbali na kutoa zawadi kwa washindi, Musonye alisema SBL pia itazigharamia timu shiriki usafiri wa ndege wa kwenda na kurudi, chakula na malazi kwa muda wote wa mashindano. Kampuni hiyo itatumia dola 450,000 za Marekani kudhamini michuano hiyo.
Uamuzi wa SBL kudhamini michuano hiyo unastahili kupongezwa, hasa ikizingatiwa kuwa, utaongeza hamasa na ushindani kwa timu shiriki, huku kila moja ikipania kushinda ili ipate zawadi tatu za kwanza za pesa.
Lakini ili michuano hiyo iwe na msisimko na ushindani wa kweli, ni vyema CECAFA ihakikishe kuwa, waamuzi walioteuliwa kuchezesha mechi za michuano hiyo wanafuata na kuheshimu sheria zote 17, badala ya kuchezesha kwa upendeleo kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu.
Hii ni kwa sababu imekuwa ikitokea mara kwa mara, baadhi ya waamuzi wanaoteuliwa kuchezesha michuano hiyo, wamekuwa wakizibeba baadhi ya timu kwa lengo la kuzikomoa timu zingine na hivyo kuharibu kabisa maana nzima ya ushindani.
Lakini kikubwa nilichokilenga kwenye safu hii wiki hii ni kutoa changamoto kwa timu za Tanzania Bara na Zanzibar, kuutumia vyema uenyeji wa michuano hiyo kuhakikisha kombe hilo linabaki nyumbani.
Sababu na uwezo wa timu hizo kulibakisha kombe nyumbani zipo. Ni kwa sababu zinaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa na pia zitakiwa zikicheza kwenye uwanja wa nyumbani, mbele ya maelfu ya mashabiki wake.
Kuliruhusu kombe hilo liondoke nyumbani kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ni aibu na fedheha kubwa kwa Taifa na hali hiyo itawavunja nguvu mashabiki wengi wa soka hapa nchini.
Itakuwa ni sawa na ilivyotokea kwa Simba mwaka 1993 wakati ilipofuzu kucheza fainali za Kombe la CAF, ambapo ilifanikiwa kutoka suluhu na Stella Abidjan ya Ivory Coast mjini Abidjan, lakini ikachapwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ilikuwa siku ya simanzi kubwa kwa mashabiki wa Simba na Watanzania kwa jumla.
Ikumbukwe kuwa, kwa mara ya mwisho, Tanzania Bara ilitwaa kombe hilo mwaka 1994 michuano hiyo ilipofanyika nchini Kenya wakati Zanzibar ililitwaa mwaka 1996 michuano hiyo ilipofanyika nchini Uganda.
Tangu wakati huo, Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa zikishiriki kwenye michuano hiyo kama wasindikizaji, na mbaya zaidi wakati mwingine zimekuwa zikitolewa hatua za awali.
Kwa kuzingatia rekodi hizo, wakati umefika kwa wawakilishi wetu hawa kuhakikisha kuwa, kombe hilo linabaki nchini, si tu kwa ajili ya kurejesha imani kwa mashabiki, bali pia kudhihirisha kuwa, kiwango chetu cha soka nchini kipo juu kama nchi zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Lakini ili hayo yote yawezekane, timu hizo mbili zinapaswa kucheza kwa kujituma, ikiwa ni pamoja na wachezaji wake kufuata na kuheshimu mafunzo ya makocha wao badala ya kila mchezaji kucheza kwa kutumia kipaji chake.
Kauli ya Kocha Jan Poulsen wa Tanzania Bara kwamba ataitumia michuano hiyo kutengeneza kikosi imara cha Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 haifai kupewa nafasi kwa sababu watanzania wanataka kuona kombe linabaki nyumbani na si kuitumia michuano hiyo kama mazoezi.
Ni wazi kuwa, iwapo Tanzania Bara na Zanzibar zitashiriki katika michuano hiyo zikiwa na dhamira ya dhati ya kutwaa ubingwa, lengo hilo litatimia kwa vile katika soka, lolote linawezekana. Cha muhimu ni wachezaji kucheza kwa kujituma huku wakiweka mbele utaifa.

Buriani 'Jenerali' Juma Mkambi

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa klabu ya Yanga na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Mkambi amefariki dunia. Mkambi alifariki dunia Jumapili iliyopitwa na kuzikwa siku iliyofuata kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Mkambi (55), ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Jenerali, alifariki kutokana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Kabla ya mauti kumkumba, Mkambi alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mazishi ya mwanasoka huyo mkongwe yalihudhuriwa na wanamichezo mbalimbali maarufu nchini, wakiwemo wachezaji wa zamani wa klabu za Simba, Yanga na Taifa Stars.
Enzi za uhai wake, Mkambi alikuwa mchezaji mahiri wa idara ya kiungo, akiwa na uwezo wa kuiunganisha vyema idara ya ulinzi na kiungo na wakati huo huo kusaidia mashambulizi.
Marehemu Mkambi alikuwa mmoja wa wachezaji wa Taifa Stars walioshiriki kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria. Katika fainali hizo, Taifa Stars ilifungwa mechi mbili na kuambulia sare mechi moja.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao kwenye kikosi hicho mwaka huo niJuma Pondamali 'Mensah', Ahmed Amasha, Leodegar Tenga, Salim Amir, Jellah Mtagwa, Mohamed Adolf Rishard, Hussein Ngulungu, Thuweni Ally, Mohamed Salim, Omar Hussein, Leopard Tasso Mukebezi na Peter Tino.
Je, ni kwa nini Mkambi alipewa jina la Jenerali wakati hakuwa mwanajeshi?
Kilichotokea ni kwamba, gazeti moja la Kiingereza la Afrika Magharibi liliandika kuhusu michuano hiyo na kuchambua ubora wa timu zilizoshiriki.
Lilipoizungumzia Tanzania, lilisifu viwango vya wachezaji wa Taifa Stars. Katika moja ya sehemu za habari hiyo, gazeti hilo liliandika:"Generally, Juma Mkambi played so well in midfield," likiwa na maana: "Kwa jumla, Juma Mkambi alicheza vizuri sana katika sehemu ya kiungo."
Gazeti hilo liliposomwa hapa nyumbani, baadhi yetu tulidhani ile ‘Generally’ (kwa ujumla) ilimaanisha cheo cha kijeshi cha ‘General’ na kuanza kumwita Mkambi kwa kutanguliza cheo hicho, tukidhani mwandishi alimwita kwa cheo hicho kwenye makala yake.
Jina hilo liliendelea kutumika kwa Mkambi hadi alipostaafu kucheza soka na hadi mauti yalipomkuta, aliendelea kuitwa hivyo. Kiwango chake katika michuano hiyo kilivifanya vyombo vingi vya habari vimsifu na kwa kweli havikukosea.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Mkambi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika serikali iliyopita, Joel Bendera alimwelezea mchezaji huyo kwamba alikuwa msikivu, aliyejituma na chachu ya hamasa kwa wenzake uwanjani.
Bendera alikuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars iliposhiriki fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980, akiwa chini ya Slowmir Work kutoka Poland.
"Tutamkumbuka siku zote kwani alikuwa mmoja wa wachezaji viungo makini na zaidi nasema alikuwa akijituma sana uwanjani na si mtu wa kusukumwa ndani na nje ya uwanja,”alisema Bendera.
"Tulipokuwa Nigeria, alikuwa akichukia sana kupoteza mchezo, lakini ilikuwa haina jinsi, mchezo wa mpira kufungwa ni sehemu ya mchezo. Tumempoteza mtu muhimu na pia mshauri, maanake mpaka kifo chake, alikuwa mtu wa ushauri hasa jinsi gani tunaweza kujikwamua kwenye soka," aliongeza Bendera.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ambaye aliwahi kucheza na Tenga alisema: "Mkambi alitusaidia sana katika kiungo wakati tulipokuwa Lagos. Nasema hivyo kwa sababu hayo ndiyo mashindano yake makubwa ukiacha hizi Chalenji na mechi nyingine za ligi.”
"Alikuwa na nguvu, alikuwa na uwezo wa kumiliki mipira na alikuwa na mashuti makali. Nilifurahi sana wakati tukicheza pamoja kwani alikuwa akitulisha mipira na alikuwa mpiganaji mzuri uwanjani," alisema Tenga.
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kifo cha Mkambi kimemwacha kwenye simanzi kubwa kwa sababu alikuwa rafiki yake wa karibu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema bila kujali itikadi za klabu zao, alishirikiana vyema na marehemu Mkambi kuanzisha timu ya Tanzania Stars, ambayo iliwahi kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la CAF mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kikamilifu katika maombolezo na mazishiri ya marehemu Mkambi ni pamoja na Jamhuri Kihwelo, Mohamed Mwameja, Mwanamtwa Kihwelo, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Idd Selemani, Dua Said na Lawrence Mwalusako.
Wengine ni Shaaban Geva, Mtemi Ramadhani, Charles Boniface Mkwasa, Makumbi Juma, Kitwana Manara, Omar Gumbo, Athumani Iddi ‘Chama’ na makocha Salum Madadi, Sunday Kayuni na Eugen Mwasamaki.
Mkambi, ambaye ameacha mke na watoto kadhaa, aliianza kupata umaarufu kisoka mwishoni mwa miaka ya 1970 wakati akichezea timu ya Nyota ya Mtwara (sasa Bandari Mtwara), aliyoichezea kwa muda kabla ya kujiunga na Yanga mwaka 1982.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochezea Yanga kwa muda mrefu bila kuhamia klabu nyingine hadi alipostaafu soka mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kabla ya kifo chake, marehemu Mkambi alikuwa katika jopo la Kamati ya Ufundi ya Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na ni mmoja wa washauri wa maendeleo ya soka ya vijana TFF.

Thursday, November 18, 2010

SENDOFF PARTY YA FURAHA OMARY





MWANDISHI wa habari wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Furaha Omary jana aliagwa rasmi na ndugu, jamaa na rafiki zake katika sherehe ya Sendoff Party iliyofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba mjini Dar es Salaam. Sherehe hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru, Publications Ltd, ambako Furaha anafanyakazi.

Sikinde yazuiwa kufanya maonyesho DDC Kariakoo

Kisa? Ukumbi wakodishwa kwa mmiliki mpya

BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imezuiwa kufanya maonyesho kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo wa mjini Dar es Salaam.
Uamuzi huo umefikiwa na mmiliki mpya wa ukumbi huo, ….ambaye alishinda tenda ya kuuendesha baada ya Shirika la Uchumi na Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) kuamua kuukodisha.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Dar es Salaam juzi, kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ na Katibu, Hamisi Milambo walisema walitimuliwa kwenye ukumbi huo kuanzia wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa Jeff, awali mmiliki huyo aliwaita na kuwaeleza kwamba, atawaruhusu kuendelea na maonyesho yao ya kila Jumapili kwenye ukumbi huo kwa sababu lengo la kila upande ni kufanya biashara.
“Lakini tulishangaa kuona kuwa, baada ya siku moja alituita tena na kutueleza kuwa, hawezi kuturuhusu kufanya maonyesho hayo kama hatutamlipa sh. 200,000 kwa kila onyesho,”alisema.
“Tulishangazwa na uamuzi huo kwa sababu tangu mwanzo, uongozi wa DDC ulituruhusu kufanya maonyesho yetu bure kwenye ukumbi huo licha ya kwamba kwa sasa bendi inajiendesha kwa kujitegemea. Hatuelewi ni makubaliano gani yaliyofikiwa kati ya mmiliki huyo na uongozi wa DDC,”aliongeza.
Kwa upande wake, Milambo alisema wanahisi hiyo ni hujuma iliyoandaliwa na uongozi wa DDC baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati yao, baada ya baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo kufungua kesi ya kupinga kupunguzwa kazini.
“Tulimuomba mmiliki huyo atupunguzie malipo ya ukumbi kwa sababu uwezo wetu kwa sasa ni mdogo kwa sababu tunajiendesha wenyewe. Tulikuwa tayari kumlipa sh. 50,000 kila wiki, lakini aligoma katakata,”alisema.
Milambo alisema kilichowasikitisha zaidi ni kauli za dharau, ambazo zimekuwa zikitolewa na mmiliki huyo, ikiwa ni pamoja na kuwabeza kuwa hawawezi kumfanya lolote na kwamba hawana chao kwenye ukumbi huo.
Kwa mujibu wa Milambo, awali uongozi wa DDC pia ulitaka kuwatimua kufanya mazoezi kwenye ukumbi wa Mlimani kabla ya baadhi ya viongozi wa serikali kuingilia kati na kuuzuia kufanya hivyo.
Milambo na Jeff wameviomba vyombo vya serikali kuingia kati suala hilo ili kuinusuru bendi hiyo kongwe nchini kusambaratika kwa vile kutoweka kwake kutadhoofisha maendelezo ya muziki nchini.
“Bendi pekee kongwe zilizosalia hapa nchini hivi sasa ni Sikinde na Msondo Ngoma. Mojawapo ikitoweka, ni sawa na kusema utambulisho wa muziki wa Tanzania nao utatoweka,”alisema Jeff.
Juhudi za kumtafuta mmiliki mpya wa ukumbi huo pamoja na Meneja Mkuu wa DDC hazikuweza kufanikiwa kwa vile jana ilikuwa siku ya mapumziko kikazi.

Mambo Hadharani

RAPA na mpuliza trumphet wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Roman Mng'ande 'Romario' akiselebuka na mmoja wa wacheza shoo wapya wa bendi hiyo wakati wa onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Max Bar, Ilala, Dar es Salaam.

Wednesday, November 17, 2010

MAMA RAHMA ASAIDIA BONANZA LA YATIMA


RAIS wa Kampuni ya RBP Oil & Industrial Technology Tanzania Ltd, Rahma Al Kharoos akimkabidhi kitita cha sh. milioni nne, Mkurugenzi wa Taasisi ya Popular Sports and Entertainment Tanzania, Osman Kazi kwa ajili ya kuandaa bonanza la watoto yatima, linalotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ufukwe wa Coco Beach mjini Dar es Salaam.

RAGE: Siondoki Simba ng'o


MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema, kamwe hawezi kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 kutoka mjini Dodoma wiki hii, Rage alisema katiba ya Simba haimzuii kushika nyadhifa mbili kwa wakati mmoja.
Rage alisema, kwa mujibu wa katiba ya Simba, mwenyekiti asipokuwepo, makamu wake ndiye anayeshika majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuendesha vikao vya uongozi na mikutano ya wanachama.
“Hivyo hata kama sintakuwepo Dar es Salaam kwa sababu ya shughuli za Bunge, hiyo haisababishi shughuli za klabu kushindwa kuendelea kwa sababu yupo makamu mwenyekiti,”alisema.
Akitoa mfano, Rage alisema wapo baadhi ya wabunge, ambao pia ni viongozi wa taasisi mbalimbali na wamekuwa wakitekeleza majukumu yao yote mawili bila ya kuwepo kwa mwingiliano ama athari yoyote.
Aliwataja baadhi ya wabunge hao kuwa ni pamoja na Kepteni mstaafu John Komba, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya CCM na pia Mkurugenzi Mtendaji wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha TOT Plus.
Hata hivyo, Rage alisema anatarajia kukutana na viongozi wenzake wa kamati ya utendaji ya Simba mwishoni mwa wiki hii ili kujadili suala hilo kabla ya kulitolea uamuzi wa mwisho.
Wakati huo huo, Rage alithibitisha kuwa, wamekata rufani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupinga adhabu iliyotolewa kwa kipa Juma Kaseja.
TFF ilitangaza kumfungia Kaseja kucheza mechi tatu na pia kumtoza faini ya sh. 500,000 kwa tuhuma za kukataa kumpa mkono Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, kati ya Simba na Yanga, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka huu.
Hata hivyo, TFF imekuwa ikijikanganya kuhusu adhabu hiyo baada ya gazeti moja la kila siku kuchapisha picha iliyomwonyesha Kaseja akipeana mkono na Kandoro wakati wa mechi hiyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni alikaririwa akisema kuwa, taarifa hiyo ilitolewa kimakosa kwa vile Kaseja hakugoma kupeana mkono na Kandoro bali wachezaji wa Yanga.

Uongozi Yanga wamtikisa Manji


UONGOZI wa klabu ya Yanga umeeleza kukerwa na kitendo cha mfadhili wao, Yusuf Manji kuwapigisha kura wachezaji wa timu hiyo kuhusu utendaji kazi wa viongozi na Kocha Kostadin Papic.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, kitendo cha Manji kuteta na wachezaji na kuwataka wamueleze utendaji kazi wa viongozi, hakikubaliki kwa vile kimelenga kuwadhalilisha.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari baadhi ya viongozi wameanza kuhoji uhalali wa Manji kuwataka wachezaji wafanye hivyo wakati wenye mamlaka hayo ni wanachama wa klabu hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, viongozi wa klabu hiyo walikutana wiki iliyopita kwa ajili ya kumjadili mfadhili huyo kuhusu kitendo chake hicho, lakini haikuweza kufahamika mara moja uamuzi waliofikia.
“Hatuwezi kuvumilia kumuona Manji akitudhalilisha kiasi hiki na hana uwezo wa kuwahoji wachezaji kuhusu utendaji wetu wa kazi. Yeye siye aliyetuchagua, yeye ni mfadhili tu, wenye jukumu hilo ni wanachama,”alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Kiongozi huyo pia alieleza kushangazwa kwao na kauli ya Manji kuwataka Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Seif Ahmed kutafuta kocha atakayechukua nafasi ya Papic na pia kumrejesha mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyesajiliwa na Azam FC.
“Sisi tunadhani Manji sasa amefika mbali na kuna kitu anachotaka kifanyika ndani ya Yanga. Lakini sisi kama viongozi tunamuomba atuheshimu kwa sababu tumechaguliwa na wanachama kikatiba na ndiyo wenye uwezo wa kuhoji utendaji wetu wa kazi,”alisema.
Kiongozi huyo alisema kitendo cha Manji kuingilia kati jukumu hilo huenda kimelenga kuzusha mgogoro ndani ya klabu hiyo, ambao unaweza kuathiri mwenendo wa timu katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambayo kwa sasa ipo kwenye mapumziko. Manji alikutana na wachezaji wote wa Yanga wiki mbili zilizopita katika ofisi za Kampuni ya Quality Group zilizopo kwenye barabara ya Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Manji aliwataka wachezaji wapige kura kuhusu uwezo wa Kocha Papic, utendaji wa viongozi wa klabu na mchango wa kila mchezaji kwa timu. Awali, utata ulikuwa umeigubika klabu hiyo kuhusu hatma ya Kocha Papic baada ya kuondoka nchini wiki mbili zilizopita na kurejea kwao Serbia kwa mapumziko.
Kocha huyo, ambaye mkataba wake wa kuinoa timu hiyo unatarajiwa kumalizika Aprili mwaka huu, alikuwa ameweka mgomo baridi wa kukinoa kikosi cha timu hiyo kutokana na kuchelewa kusaini mkataba mpya.
Mgomo huo aliufanya kabla ya mchezo kati ya Yanga na Toto African ya Mwanza, uliofanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-0.

CECAFA yapania kupeleka timu Kombe la Dunia 2014


NAIROBI, Kenya
BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limezindua mkakati wa kutaka ipate mwakilishi katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.
Mkakati huo ulizinduliwa mwanzoni mwa wiki hii mjini Nairobi nchini Kenya, yakiwa ni makubaliano ya pamoja kati ya CECAFA na Kampuni ya East African Breweries (EABL).
Katika kutekeleza mkakati huo, EABL imeamua kudhamini michuano ya soka ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.
Kampuni hiyo imepanga kutumia dola 450,000 za Marekani kwa ajili ya kudhamini michuano hiyo, itakayozishirikisha nchi 12, zikiwemo nchi tatu waalikwa za Ivory Coast, Malawi na Zambia.
CECAFA inataka nchi zilizo wanachama wake kutumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 na pia fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika Machi mwakani nchini Sudan.
Nchi wanachama wa CECAFA zinazotarajiwa kushiriki katika michuano hiyo ni Tanzania Bara, Zanzibar, mabingwa watetezi Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan na Somalia.
Akitangaza mkakati huo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema hawatarajii kurudia aibu ya kukosa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
“CECAFA ni kanda pekee ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) yenye mafanikio makubwa na tunapaswa kupata angalau nafasi moja kati ya tano zilizotengwa kwa bara la Afrika katika fainali zijazo za Kombe la Dunia,”alisema.
Musonye alisema baraza lake limepania kuutumia udhamini wa EABL kuyafanya mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji yawe ya aina yake.
“Fedha tutakazozipata kutoka EABL zitapelekwa moja kwa moja kwa timu shiriki ili kuziwezesha zitoe ushindani mkali,” alisema.
Kwa mujibu wa Musonye, fedha hizo zitatumika kuzisafirisha timu kwenda Dar es Salaam, kuzipatia huduma za malazi na chakula pamoja na usafiri wa ndani.
Mshindi wa michuano hiyo atazawadiwa dola 30,000 za Marekani (sh. milioni 35), wa pili dola 20,000 (sh. milioni 25) na wa tatu dola 10,000 (sh.milioni 15)
“Soka katika ukanda wetu kwa sasa inapata sapoti kubwa, mashabiki wetu wana kiu kubwa ya kupata kiwango bora na kutokana na udhamini huu, tutaweza kuandaa mashindano ya kiwango cha juu na hivyo kukuza kiwango cha soka katika ukanda huu,”alisema Musonye.
Katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa EABL, Seni Adetu alimkabidhi Musonye kombe litakaloshindaniwa katika michuano hiyo. Kombe hilo litapitishwa katika nchi sita kabla ya kutua Dar es Salaam.
Adetu alisema udhamini wa mwaka huu wa Kombe la Chalenji ni sehemu ya mipango ya muda mrefu ya EABL kukuza soka katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuhakikisha mojawapo ya nchi hizo inafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.

SPUTANZA yaandaa tuzo ya mwanasoka bora

CHAMA cha Wanasoka wa Zamani nchini (SPUTANZA) kimesema kitaandaa tuzo maalumu kwa ajili ya mchezaji bora wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2010-2011.
Katibu Mkuu wa SPUTANZA, Said George alisema wiki iliyopita mjini Dar es Salaam kuwa, chama chake kimeamua kujitosa kutoa tuzo hiyo kwa lengo la kuipa hadhi zaidi.
Saidi alisema, japokuwa zipo tuzo za wanamichezo bora zinazotolewa kila mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), wameona ni bora waitengenishe tuzo hiyo na za michezo mingine.
"Hatupingi kuwepo kwa tuzo za TASWA, isipokuwa tuzo ya mchezaji bora wa soka ina hadhi yake. Tunaanza kuitoa kwa mara ya kwanza ligi hii itakapomalizika na wachezaji ndio watakaopendekeza mshindi,"alisema.
Katibu Mkuu huyo wa SPUTANZA alisema, kwa kuanzia watatoa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, mshindi wa pili na wa tatu nakuwataka wahisani mbalimbali kujitokeza kudhamini tuzo hizo.
Wakati huo huo, SPUTANZA imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuvunja mara moja kamati ya kusimamia maadili na hadhi ya wachezaji kwa madai kuwa, imeshindwa kufanyakazi iliyokusudiwa,badala yake imeundwa kwa maslahi binafsi.
Saidi alisema kamati hiyo, ambayo inaongozwa na Wakili Alex Mgongolwa, ambaye ni mnazi mkubwa wa Yanga, imekumbwa na mgongano wa kimaslahi kwa watendaji wake kugubikwa na upenzi badala ya kutenda haki.
"Ni wazi kuwa, Yanga haikufuata taratibu wakati ikivunja mkataba na wachezaji wake wanne, na ni muda mrefu sasa sakata hili halijapatiwa ufumbuzi,”alisema Saidi.
“Na sasa ni usajili wa dirisha dogo, fursa ya wao kupata timu ya kuchezea ni finyu kwa vile uongozi wa Yanga haujawalipa madai yao wanayostahili, "aliongeza.
Alisema chama chake kimeiomba TFF kuzuia usajili wa nyongeza wa Yanga kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu hadi suala la wachezaji hao litakapopatiwa ufumbuzi.
Saidi alisema wachezaji hao wanne wa Yanga waliaochwa kwenye usajili wa msimu huu, walifuata taratibu zote katika kudai haki zao, lakini wamekuwa wakipigwa danadana isiyokuwa na mwisho.
Wachezaji, ambao Yanga imevunja mikataba yao bila kuwalipa haki zao ni Steven Malashi, John Njoroge, Wisdom Ndhlovu na Ally Msigwa. Mikataba ya wachezaji hao ilitakiwa kumalizika mwaka 2012.
Marashi anaidai Yanga sh. milioni 37.5, Ndhlovu anadai sh.milioni 82, Msigwa sh. milioni 89.7 na Njoroge sh. milioni 44.

NYOSHI: Hakuna bendi kama FM Academia



RAIS wa bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia, ‘Wazee wa Ngwasuma’, Nyoshi El Saadat, ametamba kuwa, bendi yake ndiyo inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi mikoani kuliko bendi zingine.
Akizungumza na Burudani mjini hapa wiki iliyopita, Nyoshi alisema, bendi nyingi maarufu nchini, zinapata mashabiki wengi zinapofanya maonyesho Jijini Dar es Salaam, lakini hali huwa tofauti zinapokwenda mikoani.
Nyoshi alitoa majigambo hayo wakati bendi hiyo ilipokuwa ikifanya onyesho la uzinduzi wa albamu yake mpya ya ‘Vuta nikuvute’, lililofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa.
Katika onyesho hilo lililohudhuriwa na mashabiki lukuki, bendi hiyo ilifanikiwa kukonga nyoyo zao kutokana na vibao vyao vipya 11 vilivyopigwa kwa mpangilio wa kuvutia.
“FM Academia kila tunapokwenda kwenye mkoa wowote hapa Tanzania, tunaongoza kwa kupata mashabiki wengi. Bendi zingine nyingi zinapata mashabiki zinapokuwa Dar es Salaam, zikitoka kwenda mikoani, hazipati kitu,”alisema Nyoshi.
Aliongeza kuwa, kinachoifanya bendi hiyo kuwa ‘matawi ya juu’ ni kudumu kwa muda mrefu, wasanii wake kufanyakazi kwa umoja, kuwa na nidhamu ndani na nje ya jukwaa na uwajibikaji wa pamoja.
Kwa mujibu wa Nyoshi, albamu hiyo ni bora na akiwa kiongozi, ameshiriki kutunga nyimbo mbili, ‘Jasmini’ na ‘Ushirikiano wa Tanzania na nchi jirani’.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zingine zilizomo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Shida yangu’ na ’Mgeni’, ambazo zimerekodiwa kwenye studio za Metro za mjini Dar es Salaam.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria onyesho hilo walikiri kuwa, bendi ya FM Academia inafahamu vyema kukidhi kiu ya mashabiki wake na wanamuziki wake wana nidhamu ya hali ya juu wanapokuwa stejini.

Kuigiza filamu nyingi ni kujimaliza-Monalisa


MWIGIZAJI filamu maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherly amefichua kuwa, tabia ya kuigiza filamu nyingi kwa muda mfupi imechangia kushuka kwa hadhi ya fani hiyo.
Yvonne, maarufu kwa jina la Monalisa alisema mjini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa, tabia hiyo haiwajengei heshima wasanii wa fani hiyo bali inawamaliza.
"Lazima utafika wakati, wasanii wa aina hiyo watapotea kabisa. Mashabiki watawachoka haraka na hii ni hatari kwa vile itashusha thamani ya filamu zetu. Msanii anapaswa kufanya mambo kwa mpangilio na hii inaleta heshima, si kukurupuka tu,”alisema.
Monalisa, ambaye ni miongoni mwa wasanii waasisi wa fani hiyo hapa nchini alisema, si kazi rahisi kwa mwigizaji filamu kucheza filamu nyingi kwa muda mfupi na zikawa nzuri.
"Unakuta msanii ndani ya mwezi mmoja anaigiza filamu tano, mtu huyo mmoja kila sehemu unamuona anatokea yeye na uhusika unakuta ni uleule, huko ni kujimaliza,"alisema.
"Msanii unakuwa huna kitu kipya, huna ubunifu, ndio maana ukiangalia filamu nyingi za sasa, hazina jipya. Wasanii wanafanya mambo yaleyale kwa sababu mtu anakuwa hana muda wa kupumzika na akili kufikiria kitu kipya,”aliongeza.
"Kila muda anakuwa ‘bize’ na kukazana kuhakikisha anakamilisha kazi alizonazo. Matokeo yake analipua tu na watazamaji hawapati kitu, ambacho wanategemea, ndio maana mwisho wa siku thamani ya mtu inashuka,”alisisitiza.

'Banana hakuwahi kunikataza kujihusisha na muziki'


MSANII nyota wa kike wa muziki wa kizazi kipya nchini, Maunda Zorro amesema kamwe kaka yake, Banana Zorro hakuwahi kumkataza kujihusisha muziki katika maisha yake.
Badala yake, Maunda amesema alichokuwa akikifanya Banana ni kumuusia mara kwa mara kumaliza kwanza masomo yake kabla ya kujitosa kwenye muziki.
Akihojiwa katika kipindi cha Burudani ni Nyumbani cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Maunda alisema Banana alimpa usia huo kwa sababu fani hiyo ilimuathiri kwa kumfanya ashindwe kuyapa kipaumbele masomo yake.
"Ukweli ni kwamba Banana hakuwahi kunikataza mimi nisijihusishe na muziki. Alichokuwa akiniusia ni kuweka mbele masomo kwanza kabla ya kujitosa kwenye muziki,"alisema.
"Alikuwa akiniambia, hakuna kwenda studio wala kurekodi wimbo, nitafanya hivyo baada ya kumaliza masomo,"aliongeza.
"Banana alifanya hivyo kwa sababu alishabaini tatizo la kuchanganya muziki na masomo kwa vile lilimkuta. Alipokuwa akisoma sekondari, muziki ulimuingia sana kwenye damu yake kiasi kwamba alishindwa kuyapa kipaumbele masomo. Hakutaka nami niingie kwenye mkumbo huo,"alisisitiza.
Kwa mujibu wa Maunda, kwa sasa Banana amekuwa mstari wa mbele kumpatia misaada ya aina mbalimbali kimuziki ili aweze kufanikisha ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.

Amini aamua kutoka kivyake


MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Amini kutoka kundi la THT amedokeza kuhusu mbinu anazotumia kimuziki ili kujiweka kwenye matawi ya juu.
Amini, ambaye kwa sasa anatamba kwa kibao chake cha ‘Unikimbie’, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, anazo nguzo kuu tatu, ambazo amekuwa akizitekeleza kwa lengo la kutimiza azma yake hiyo.
Msanii huyo anayechipukia alisema, amekuwa akitekeleza nguzo hizo kila anapokuwa kwenye maandalizi ya kutoa nyimbo mpya, ndiyo sababu zimekuwa zikiwavutia mashabiki wengi wa muziki huo.
"Kabla sijatunga wimbo wowote, ninakuwa makini katika kuhakikisha nimetuliza kichwa changu, kwani ninakuwa nimetenga muda muafaka wa kuifanyakazi hiyo ipasavyo," alisema Amini, ambaye ni miongoni mwa wasanii chipukizi wanaong'ara kwa sasa.
Aliitaja nguzo yake ya kwanza kuwa ni kukiamini kila anachokifikiria na kukifanyiakazi mara moja kwa kuandaa melodi nzuri kwa ajili ya kuwavutia mashabiki wake.
"Pia ninahakikisha nakuwa makini ninapoutengeneza wimbo wangu na baada ya kumaliza, ninarudia mwanzo mpaka mwisho kwa usahihi na baada ya hapo, ninahakikisha vibwagizo vya wimbo wangu vimekaa sawa," alisema Amini.
Aliitaja nguzo yake ya pili kuwa ni namna anavyoweza kuandaa maneno mazuri ya wimbo na kuongeza kuwa, huo ndio msingi bora wa kuzifanya nyimbo zake zikubalike na mashabiki.
Kwa mujibu wa Amini, nguzo yake ya tatu ni kuhakikisha anafuata misingi yote ya uimbaji na kuongeza kuwa, hilo ndilo lililomwezesha kufika alipo sasa.
"Nipo makini katika kufuata misingi ya uimbaji kwani ninajua namna ya kupanda na kushuka ninapotengeneza wimbo na ninahakikisha sitoki nje ya biti," alisisitiza.
Msanii huyo asiyekuwa na makeke alisema, ametoka mbali kimuziki na anazidi kukua taratibu na kujifunza mengi katika fani hiyo na hilo linamsaidia kujijenga vizuri.
Albamu ya pamoja aliyoifanya kwa kushirikiana na msanii Barnabas, ndiyo iliyomwezesha kuwa matawi ya juu na kwa sasa anajiandaa kupakua albamu ya peke yake, ambayo ameshaanza kuiandaa.
"Nilitoka na Barnabas kwa awamu ya kwanza kwa sababu kila mmoja alifahamika kwa nafasi yake, lakini hivi sasa nimeshaanza kuandaa albamu yangu mwenyewe,”alisema.
“Ninatumia muda mwingi hivi sasa katika kuandaa albamu yangu hii kwa sababu nataka iwe kwenye chati ya juu kimuziki. Nimepanga kuikamilisha albamu hii mwanzoni mwa mwaka 2011," alisema Amini.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zake, zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni pamoja na 'Kumanya', 'Tumetoka mbali', 'Anavuruga', 'Subira', 'Mapenzi ya nani duniani' na 'Unikimbie'.