KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 15, 2015

KOCHA SYLVESTER MARSH AAGWA




RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za ramirambi kwa familia ya Marsh, kufuatia kifo cha kocha wa Taifa ya vijana Sylvester Marsh kilichotokea jana jijini Dar es salaam.

Katika salam zake kwa familia ya marehemu, Mh. Malinzi amesema familia ya mpira wa miguu
nchini TFF imeshtushwa na msiba huo na kusema Shirikisho na Taifa limempoteza mtu muhimu
katika mpira wa miguu nchini.

Mwili wa marehem Marsh utaagwa leo saa 6 kamili mchana, katika kanisa la Hospital ya Taifa
Muhimbili na kutasafirishwa kuelekea Igoma jijini Mwanza kwa mazishi majira ya saa 8 kamili
mchana kwa basi dogo (coaster) la TFF.

Marsh alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Taarifa zinasema Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya
maradhi ya saratani ya koo yaliyokuwa yakimsumbua na ghafla hali yake ikabadilika juzi hadi kufariki
dunia.

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj
Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa,
akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim
Poulsen.

Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba
mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Star na Marsh akaondoka pamoja na Kim
Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.

Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.

Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.

Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.

Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.

Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa
Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.

Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe.

Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.

Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.

Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo.

Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina.


No comments:

Post a Comment