KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 18, 2015

KIGOGO SIMBA KORTINI KWA KUMJERUHI MTOTO WA MANJI


NA FURAHA OMARY

KIGOGO wa Klabu ya Simba, Musleh Al Rawah anayetuhumiwa kumpiga mtoto wa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yussuf Manji, Meheub Manji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu tuhuma hizo.

Musleh ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, anadaiwa kutenda kosa hilo, katika Uwanja wa Taifa, ulioko Chang'ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam, baada ya mechi ya watani Yanga dhidi ya Simba, ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kiongozi huyo wa Simba, alifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi na kusomewa shitaka na Wakili wa Serikali, Genes Tesha akishirikiana na Mwendesha Mashitaka, Jackson Chidunda.

Genes alimsomea Muslen shitaka la kumjeruhi na kumdhuru mwili mtoto wa Manji. Alidai Machi 8, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, ulioko Chang'ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam, mshitakiwa alimpiga teke Meheub na kumpiga usoni na sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha mazito.

Mshitakiwa alikana shitaka, ambapo Wakili Tesha alidai upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi juu ya dhamana kwa mshitakiwa kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika.

Kwa upande wa Wakili wa mshitakiwa huyo, Dk. Damas Ndumbaro, aliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wake kwani ataweza kufika pindi atakapohitajika.

Hakimu Moshi alisema dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa, iwapo atakuwa na mdhamini mmoja kutoka taasisi binafsi inayotambulika au kutoka serikalini na awe na barua ya mwajiri wake.

Alisema barua ya mdhamini ni lazima ikafanyiwe uhakiki na upande wa Jamhuri.

Mshitakiwa huyo aliweza kutimiza masharti hayo na kuachiwa huru kwa dhamana hadi Aprili 20, mwaka huu, kesi itakapotajwa baada ya upande wa Jamhuri kufanya uhakiki wa barua hiyo na kuridhika nayo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, inadaiwa Musleh alimsukuma mtoto huyo wa Manji wakati wakiwa katika lifti wakitoka mpirani.

No comments:

Post a Comment