KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 1, 2015

JK ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA YA KEPTENI KOMBA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Damian Komba, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM na msanii hodari sana wa kizazi chake.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda na Katibu Mkuu wa CCM, MheshimiwaAbdulrahman Kinana, Mheshimiwa Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo, Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.”
“Kwa hakika, sina maneno ya kutosha kuelezea kwa fasaha hasara ambayo taifa letu na chama chetu kimepata kutokana na kifo cha Kepteni Komba. Taifa letu limepoteza hazina kubwa na mtu muhimu. Nimemjua Kepteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi. Alikuwa msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake na katika jambo lolote aliloliamini.,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo na kuongeza:
“Akiwa mwalimu, lakini hasa akiwa Mlinzi wa Taifa katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kepteni Komba alithibitisha sifa zake kama mlinzi wa taifa kwa kipaji chake cha kutunga na kuimba nyingi za kuhamamisha wanajeshi wetu katika ulinzi wa nchi yao. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kisanii kutunga nyimbo za aina zote – ziwe za maombolezo, ziwe za kutoa hamasa, ziwe za makaribisho, ziwe za kampeni za kisiasa na kijamii ama ziwe za kampeni maalum.”
“ Mheshimiwa Komba alikuwa Mbunge hodari sana na wananchi wa Nyasa wamepoteza mtetezi wa uhakika. Mheshimiwa Komba alikuwa mcheshi, aliyependa sana utani na alikuwa na uongozi mkubwa wa kutambua na kulea vipaji vya sanaa na wasanii kama alivyothibitisha katika kuanzisha na kulea Kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT) na kabla ya hapo .”
“Kupitia kwenu Waheshimiwa, naomba mnifikishie salamu zangu za dhati kabisa kwa Wabunge wote ambao wameondokewa na mwenzao na wananchi wa Jimbo la Nyasa na Mkoa wote wa Ruvuma ambao wamepoteza mwakilishi na kiongozi wao. Ndani ya Chama chetu, naomba salamu zangu ziwafikie wanachama wetu wote kwa kupoteza mwanachama mwenzao, ziwafikie viongozi na hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo imepoteza mwakilishi mwenzao na wasanii wote wa Tanzania One Theatre (TOT) ambao Kiongozi wao ameondoka duniani,” amesema Rais na kumalizia:
Naungana na wanafamilia kuomboleza kifo cha rafiki yetu, ndugu yetu na kiongozi mwenzetu. Napenda wanafamilia wajue kuwa natambua uchungu wao katika kipindi hiki na tahayari yao ya  kuondokewa na mhimili wa familia. Niko nao katika maombolezo na katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Kepteni John Damian Komba. Amen.”

No comments:

Post a Comment