'
Monday, March 30, 2015
STARS, MALAWI ZAINGIZA MIL 72/-
Mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika jana jumapili jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kati ya wenyeji timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) umengiza jumla ya tsh 72.839,000 kutokana na idadi ya washabiki 15,762 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo.
Mgawanyo wa mapato kwa mchezo hu ni VAT 18% sh. 11,111,103, gharama za tiketi sh. 3,203,700, gharama za mchezo (15%)sh. 8,778,639, Uwanja (15%) 8,778,639, CAF (10%) sh. 5,852,426 na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF (35%) sh. 35,114,560.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini inatoa shukrani kwa chama cha soka mkoa wa Mwanza (MZFA) kwa ushirikiano wao katika kufanikisha maandalizi ya mchezo huo, waandishi na vyombo vya habari mbalimbali kwa sapoti waliyoitoa kwa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)
Aidha TFF iinawashukru wapenzi, wadau na washabiki wa soka nchini, na hususani wa kanda ya ziwa waliojitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo, kwani waliishangilia Taifa Stars tangu mwanzo wa mchezo mpaka mwisho kwa ustaarabu wa hali juu.
Katika mchezo huo Taifa Star ilitoka sare ya bao 1- 1 dhidi ya The Flames, bao la wageni lilifungwa na Mecium Mhone kabla ya na Mbwana Samatta kuisawazishia Tanzania.
TFF KUMUUNGA MKONO BLATTER UCHAGUZI WA FIFA, TENGA UCHAGUZI WA CAF
Leo Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) akiwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi wamezungumzia uchaguzi wa CAF na FIFA.
Rais Tenga ameishukuru familia ya TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 7 mwaka huu Cairo. Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Pia Rais Tenga amezungumzia msimamo wa bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA anayetetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Uswisi.
Vilevile Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Joseph Sepp Blatter katika uchaguzi wa FIFA.
Katika mkutano huo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa tamko rasmi kuwa kwa niaba ya TFF atampigia kura Joseph Sepp Blatter.
TAIFA STARS YALAZIMISHWA SARE NA MALAWI
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samatta, jana aliinusuru timu ya Taifa, Taifa Stars isiadhiriwe na Malawi.
Mbwana aliinusuru Taifa Stars baada ya kuifungia bao la kusawazisha ilipomenyana na Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Katika mechi hiyo, iliyoko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), timu hizo mbili zilifungana bao 1-1.
Mbwana aliifungia Taifa Stars bao hilo la kusawazisha dakika ya 76, akiwa katikati ya mabeki wa Malawi, baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Mrisho Ngasa.
Malawi ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tatu ya mchezo, lililofungwa na Esau Kanyenda baada ya beki mmoja wa Taifa Stars kupangua vibaya mpira wa kona uliopigwa a Haray Nyirenda.
Wamalawi walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza cha pambano hilo, ambapo wachezaji wa Taifa Stars walishindwa kuipenya ngome ya wapinzani wao.
Taifa Stars: Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Aggrey Morris,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Haroun Chanongo/Mrisho Ngassa, Amri Kiemba/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ , Thomas Ulimwengu/John Bocco na Mbwana Samatta.
Sunday, March 29, 2015
TENGA KUTETA NA WANAHABARI
Rais wa CECAFA na mjumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), Leodgar Tenga kesho Jumatatu Machi 30, 2015 saa 6:30 mchana ataongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF ulioko Uwanja wa Karume.
Waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria mkutano huo bila kukosa.
AZAM, SIMBA, YANGA ZAPIGWA FAINI
Kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kilichoketi jumanne ya tarehe 24, Machi 2015 jijini Dar es salaam, kimepitia taarifa mbalimbali za michezo iliyochezwa na kutoa adhabu kwa wachezaji na vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom.
Katika mechi namba 107 iliyowakutanisha wenyeji Ndanda FC dhidi ya Coastal Unioni, klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi Anold Bugado.
Mechi namba 108 iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, (Stand United dhidi Simba SC), wenyeji timu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(8) kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika ishirini.
Mchezo namba 117 uliozikutanisha Simba SC dhidi ya Yanga SC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, timu ya Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kukataa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Nayo klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(11) baada ya timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, huku mshambualiji wake Dany Mrwanda akipigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(12) kwa kutopeana mikono na wachezaji wa timu hiyo.
Mchezaji Haruna Niyonzima wa Yanga amepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 37(f) kwa kupiga teke meza ya mwamuzi wa akiba baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Suala la mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe kumshika korodani beki wa Simba SC Murshid Juuko limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu.
Kipa wa timu ya Simba SC, Ivo Mapunda amepewa onyo kwa kufunika tangazo la mdhamini wa Ligi Kuu (Vodacom) kwa kutumia taulo lake wakati wa mechi dhidi ya Yanga, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake iwapo atarudia kufanya tukio la aina hiyo.
Nao wachezaji Salum Abubakar wa Azam FC na Richard Maranya wa JKT Ruvu wamepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja na kusimamishwa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) kwa kupigana uwanjani kwenye mechi namba 123 ambapo walitolewa nje kwa kadi nyekundu.
Klabu ya Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) baada ya timu yake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye mchezo namba 130 dhidi ya Young Africans uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi namba 132 iliyozikutanisha Azam na Ndanda SC kwenye uwanja wa Chamazi, klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) baada ya washabiki wake kuwamwagia maji na kuwarushia chupa za maji washabiki wa Azam.
Aidha klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(8) kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi namba 134 dhidi ya timu ya Mbeya City, pia imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye mchezo huo.
Kiongozi wa Stand United, Muhibu Kanu amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kuondolewa kwenye benchi na mwamuzi wa mchezo dhidi ya Mbeya City kutokana na kutumia lugha ya kuhamasisha vurugu kwa timu yake na kupinga uamuzi wa refarii.
Katika mchezo namba 135 uliochezwa jijini Tanga na kuwakutanisha wenyeji Mgambo Shooting dhidi ya Yanga SC, Yanga SC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuvamia uwanja baada ya mechi namba 135 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
STARS, MALAWI DIMBANI LEO
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo inajitupa dimbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kumenyana na tmu ya taifa ya Malawi (The Flames), kuanzia saa
10.30 jioni.
Tiketi za mchezo huo tayari zimeshaanza kuuzwa katika vituo vya uwanja wa Nyamagana na Uwanja wa CCM Kirumba, kwa bei za sh. 5,000 kwa mzunguko, sh. 12,000 kwa jukwaa kuu na sh.20,000 kwa viti vya jukwaa kuu maalumu.
Taifa Stars inashika nafasi ya 100 katika msimamo wa viwango vya FIFA vilivyotolewa mwezi Machi, huku Malawi (The Flames) wakishika wakiwa nafasi ya 91 kwenye viwango hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hoteli ya La Kairo iliyopo Kirumba, Mwanza, Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri , na kilichobakia ni mchezo wenyewe wa leo.
Mayanga alisema vijana wake wote 22 waliopo kambini wapo fiti, wamefanya mazoezi kwa siku tano katika Uwanja wa CCM Kirumba, wapo kwenye ari na morali ya juu na kwamba kikubwa wanachosubiri ni kushuka dimbani kusaka ushindi.
Aidha, Mayanga amewaomba wapenzi wa mpira wa miguu waliopo jijini Mwanza na mikoa ya jirani ya kanda ya ziwa, kujitokeza kwa wingi kesho uwanjani kuja kuwapa sapoti vijana kwa kuwashangilia muda wote wa mchezo.
Tayari waamuzi na kamishina wa mchezo wameshawasili jijini Mwanza. Mwamuzi wa kati atakuw Munyazinza Gervais kutoka Rwanda, akisaidiwa na mshika kibendera wa kwanza Hakizimana Ambroise (Rwanda), mshika kibendera wa pili Niyitegeka Bosco (Rwanda). Mwamuzi wa akiba ni Martin Saanya kutoka Morogoro huku na Kamishina wa mchezo ni Afred Rwiza kutoka Mwanza.
Wachezaji wa Taifa Stars waliopo Mwanza ni Aishi Manula, Mwadini Ali, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Salim Mbonde, Haji Makame, Hassan Isihaka na Abdi Banda.
Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Haroun Chanongo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Frank Domayo, Said Ndemla, John Bocco, Juma Luizio, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta.
Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) iliwasili Mwanza juzi saa sita mchana, ikiwa na kikosi chake kamili kwa ajili ya mchezo dhidi ya Taifa Stars.
Malawi imewasili ikiwa na kikosi chake kamili cha wachezaji 18 na kufikia katika hotel ya JB Belimonte, wakiwemo wachezaji saba wanaocheza soka ya kulipwa katika nchi za Afrika Kusini, Congo DR, Msumbuji na Zimbabwe.
Wachezaji wa kimataifa waliowasili ni nahodha Joseph Kamwendo (TP Mazembe -Congo DR), Chimango Kayira (Costal de Soul - Msumbiji), Frank Banda (HBC Songo - Msumbiji), Esau Kanyenda (Polokwane City - Afrika Kusini), Harry Nyirenda (Black Leopards - Afrika Kusini), Limbikani Mzava (Celtic - Afrika Kusini) Gerald Phiri (Caps United - Zimbambwe)
Wegine ni McDonald Harawa (Hoyale FC), Richard Chipuwa (Wanderers), Lucky Malata (Silver), John Lanjesi (Civo), Francis Mulimbika (Wanderers), John Banda (Blue Eagle), Earnest Tambwe (Surestream) , Micium Mhone (Blue Eagle), Chikoti Chiriwa (Red Lions), Peter Wadabwa (Silver) na Amos Khamula(Support Ballaton).
Mkuu wa msafara ni Alexander Waya, Kocha Mkuu, Young Chimodzi, Kocha Msaidizi, Jack Chamangwana, Kocha wa makipa, Pillip Nyasulu, Daktari wa timu, Levison Mwale, Meneja wa timu, Frank Ndawa na Ofisa Habari, James Sangala.
Thursday, March 26, 2015
YANGA MWENDO MDUNDO
TIMU ya soka ya Yanga jana iliendelea kudhihirisha makali yake katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika JKT Ruvu mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya 33 kupitia kwa mshambuliaji Simon Msuva, aliyeunganisha wavuni kwa shuti kali krosi kutoka pembeni ya uwanja.
Zikiwa zimesalia dakika tatu kuwadia muda wa mapumziko, Yanga ilihesabu bao la pili lililofungwa na Danny Mrwanda, aliyeunganisha pasi kutoka kwa Msuva.
JKT Ruvu ilipata bao la kujifariji dakika ya 45 kupitia kwa Samwel Kamuntu baada ya kupokea pasi akiwa ndani ya mita 18. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.
Yanga ilihitimisha karamu ya magoli dakika ya 56 baada ya Msuva kufunga bao la tatu kutokana na krosi maridhawa kutoka kwa Mrisho Ngasa.
Wednesday, March 25, 2015
STARS YAWASILI MWANZA
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imewasili salama jijini Mwanza, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa siku ya Jumapili, Machi 29, 2015 dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames), mechi itakayochezwa kwenye dimba la Uwanja wa CCM Kirumba.
Kikosi cha Stars kimeondoka kikiwa na wachezaji 18, ambao wameripoti kambini jana, huku kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini Qatar, akitarajiwa kuungana na wenzake leo mchana jijini Mwanza.
Wachezaji waliopo kambini jijini Mwanza ni, magolikipa Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC), walinzi ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Aggrey Morris (Azam FC) , Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Haji Mwinyi (KMKM), Hassan Isihaka na Abdi Banda (Simba SC)
Wengine ni Amri Kiemba, Frank Domayo, Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Haroun Chanongo (Stand United), John Bocco (Azam FC), Juma Luizio (Zesco United), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe).
Mchezaji Mcha Khamis wa Azam FC amejiondoa kikosini kutokana na kuwa majeruhi, huku wachezaji wa Young Africans wakitarajiwa kujiunga na kikosi hicho cha timu ya Taifa mara tu baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya JKT Ruvu siku ya jumatano.
MALAWI KUWASILI ALHAMISI
Msafara wa watu 25 wa timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) unatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam kesho (Alhamisi), kabla ya kuunganisha ndege siku ya ijumaa kuelekea jijini Mwanza tayari kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Taifa Stars siku ya Jumapili.
Katika msafara huo utakaokuwa na wachezaji 18 na viongozi 7, kocha mkuu wa The Flames Young Chimodzi amewajumuisha wachezaji nane (8) katika kikosi chake wanaocheza soka la kulipwa katika nchi za Afrika Kusini, Congo DR, Msumbiji na Zimbabwe.
Wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini ni Limbikani Mzava (Celtic), Harry Nyirenda (Black Leopards), Esau Kanyenda (Polokwane City), na Atusaye Nyondo (University of Pretoria).
Wengine ni Nahodha Joseph Kamwendo (Tp Mazembe - Congo DR), Frank Banda (HBC Songo - Msumbuji), Chimango Kayira (Costal De Sol - Msumbuji) na Gerald Phiri (Caps United - Zimbambwe).
BEACH SOCCER WAREJEA
Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer) imerejea nchini juzi mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ikitokea nchini Misri,ambako mwishoni mwa wiki ilipoteza mchezo wake wa marudiano kwa kufungwa 9-4 na wenyeji.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema timu ya soka la ufukweni haikupata matokeo mazuri katika mchezo wake kutokana na ugeni wa michuano hiyo.
Malinzi alisema uzoefu ndio ulikuwa kikwazo kwa timu ya Tanzania, kwani ndio mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo ikiwa ni miezi sita tangu kutambulishwa kwa mchezo huo nchini Tanzania.
Ili kuwa na timu bora ya Taifa na wachezaji wengi wa mchezo huo, TFF imepanga kuutangaza na kuufundisha mpira wa ufukweni katika mikoa mbali mbali nchini , tofauti na sasa ambapo mchezo huo unachezwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Katika mchezo huo, mabao ya Tanzania yalifungwa na Ally Rabbi (3) Kashiru Salum (1). Tanzania imetolewa kuwania kufuzu kwa fainali za Soka la Ufukweni barani Afrika na Misri kwa jumla ya mabao 15-6.
Misri imefanikiwa kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Soka la Ufukweni Visiwa vya Shelisheli, zitakazofanyika mwezi Aprili, mwaka huu, kwa mara ya saba mfululizo tangu kuanzishwa kwa mchezo huo mwaka 2006 nchini humo.
MALINZI AWAPONGEZA TWIGA STARS
Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini –TFF Bw. Jamal Malinzi ametuma salama za pongezi kwa timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (The She-polopolo).
Katika salam zake Rais Malinzi amesema ushindi walioupata Twiga Stars katika mchezo huo wa awali, umetokana na maandalizi mazuri waliyoyapata chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage, benchi lake la ufundi na TFF.
Aidha Rais amewataka Twiga Stars kutobweteka kwa ushindi huo wa awali walioupata, bali wanapaswa kujiandaa vizuri zaidi kwa ajili ya mchezo wa marudiano ili waweze kupata ushindi na kuipeperusha vuzuri bendera ya Taifa ya Tanzania.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika kati ya April 10,11 na 12, 2015, huu jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja kwenye fainali za Afrika kwa Soka la Wanawake (All Africa Games Women) zitakazofanyika Brazzavile, Congo Septemba 3-18 mwaka huu.
Twiga Stars inatarajiwa kuwasili saa 7 kamili usiku (jumanne) jijini Dar es Salaam kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Ethiopia ikitokea nchini Zambia.
Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), watanzania wote wanawapa pongezi Twiga Stars kwa ushindi walioupata wa awali na kuwatakia maandalizi mema ya mchezo wa marudaiano.
Mabao ya Twiga Stars katika mchezo wa jana dhidi ya Zambia (The She-polopolo) yalifungwa na Asha Rashid (2), Shelder Boniface (1) na Sophia Mwasikili (1).
Monday, March 23, 2015
TWIGASTARS YAPATA USHINDI MNONO UGENINI
TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, jana ilijiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za Afrika baada ya kuichapa Zambia mabao 4-2 katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Lusaka.
Kutokana na ushindi huo, Twiga Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote timu hizo zitakaporudiana wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari kutoka Zambia zimeeleza kuwa, katika mechi hiyo, Twiga Stars ilicheza soka ya kiwango cha juu na kuwazidi wapinzani wao katika kila idara.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Rogasiun Kaijage, alisema kwa njia ya simu kutoka Lusaka kuwa, ushindi huo ulitokana na vijana wake kucheza kwa kufuata maelekezo yake.
Kaijage alisema ushindi huo hautawafanya wabweteke, badala yake watacheza mechi ya marudiano kwa lengo la kuibuka na ushindi mwingine mkubwa zaidi.
SIMBA YAFUFUA MATUMAINI
SIMBA jana iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeleta ahueni kubwa kwa mashabiki wa Simba, kufuatia timu hiyo kuchapwa mabao 2-0 na Mgambo Shooting wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mshambuliaji machachari Ibrahim Ajibu aliwainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 60 baada ya kuifungia bao kwa njia ya penalti baada ya Awadh Juma kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari.
Dakika moja baadaye, Awadhi aliiongezea Simba bao la pili baada ya kuwatoka mabeki wa Ruvu Shooting na kufumua shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.
Elias Maguri alihitimisha furaha ya mashabiki wa Simba dakika ya 75 baada ya kuifungia bao la tatu, baada ya kipa Abdalla wa Ruvu Shooting kutema shuti la Saidi Ndemla na mpira kumkuta mfungaji.
Sunday, March 22, 2015
BEACH SOCCER YAWASILI SALAMA MISRI
Timu ya Taifa ya soka la Ufukweni (Beach Soccer) imewasili salama jijini Cairo nchini Misri tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika
zitakazofanyika Visiwa vya Shelisheli.
Msafara wa timu ya soka la Ufukweni ulipokelewa na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania waliopo
nchini Misri, pamoja na viongozi wa chama cha soka nchini Misri (EFA).
Leo jioni kikosi kinatarajia kufanya mazoezi mepesi, kabla ya kesho kufanya mazoezi ya mwisho
katika uwanja utakaofanyika mchezo siku ya jumapili.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF linaitakia kila la kheri timu ya soka la ufukweni katika
mchezo wake wa marudiano siku ya jumapili dhidi ya Misri.
FAINALI SDL JUMATATU
Fainali ya kumsaka Bingwa wa Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajiwa kufanyika siku ya jumapili katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam siku ya jumatatu Machi 23 mwaka huu kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mchezo huo wa fainali utazikutanisha timu za Mbao FC ya Mwanza dhidi ya Kiluvya United FC ya
Pwani, ambapo mshindi wa mchezo ndio atakua Bingwa mpya wa Ligi Daraja la Pili.
Jumla ya timu nne tayari zimeshapanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutoka Ligi Daraja la Pili
(SDL) ambazo ni Kiluvya United ya Pwani, Mji Njombe ya Njombe, Mbao ya Mwanza na Mji Mkuu
(CDA) ya Dodoma.
YANGA HAKUNA KULALA
YANGA imeendelea kujikita kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya jana kuichapa Mgambo Shooting mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Timu hizo mbili zilicheza kwa kasi katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, lakini hadi kilipomalizika, hakuna iliyoweza kupata bao.
Baada ya kosakosa kadhaa, Yanga ilihesabu bao lake la kwanza dakika ya 78 kupitia kwa Simon
Msuva baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mgambo Shooting.
Dakika tano baadaye, Amis Tambwe aliiongezea Yanga bao la pili baada ya kuunganisha wavuni
kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Msuva kutoka pembeni ya uwanja.
Kwa ushindi huo, Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi
18, ikishinda 11 na kupoteza tatu.
Ligi hiyo inaendelea tena leo wakati Simba itakapomenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam wakati Azam itavaana na Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani,
Tanga.
Thursday, March 19, 2015
YANGA KWA RAHA ZAO, SIMBA YALE YALE
YANGA jana iliwapa raha mashabiki wake baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi wa Yanga katika mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, umeiwezesha kufikisha pointi 34 na pia kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar, katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Bukoba.
Iliwachukua Yanga dakika saba kupata bao la kwanza lililofungwa kwa njia ya penalti na Simon Msuva baada ya kuchezewa rafu mbaya ndani ya eneo la hatari. Kipa Andrew Ntila alishindwa kuzuia penalti hiyo.
Amisi Tambwe aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 15 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mrisho Ngasa, aliyekuwa akihaha uwanja mzima kusaka mabao.
Beki wa zamani wa Simba, Salum Kanoni, aliifungia Kagera Sugar bao la kujifariji kwa njia ya penalti dakika ya 40 baada ya Hussein Javu kumchezea rafu Atupele Green ndani ya eneo la hatari.
Wakati huo huo, timu kongwe ya Simba jana iliwakera na kuwapa unyonge mashabiki wake baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kutokana na kipigo hicho, Simba imebaki kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29, nyumba ya Yanga na Azam.
Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba ilizidiwa kila idara na wapinzani wao, hasa kipindi cha pili.
Shambulizi la kushtukiza lililofanywa na Mgambo kwenye lango la Simba dakika ya 44, liliiwezesha kupata bao la kwanza lililofungwa na Ali Nassoro kwa shuti kali lililomshinda kipa Ivo Mapunda.
Simba ilipata pigo dakika ya 63 baada ya kipa wake, Ivo Mapunda kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Salim Azizi ndani ya eneo la hatari.
Kufuatia Mapunda kutolewa, Simba ililazimika kumtoa Ramadhani Singano na kumuingiza kipa namba mbili, Manyima Peter.
Mgambo ilipata bao la pili dakika ya 66 lililofungwa na Mwalimu Busungu kwa njia ya penalti.
Wednesday, March 18, 2015
KIGOGO SIMBA KORTINI KWA KUMJERUHI MTOTO WA MANJI
NA FURAHA OMARY
KIGOGO wa Klabu ya Simba, Musleh Al Rawah anayetuhumiwa kumpiga mtoto wa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yussuf Manji, Meheub Manji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu tuhuma hizo.
Musleh ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, anadaiwa kutenda kosa hilo, katika Uwanja wa Taifa, ulioko Chang'ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam, baada ya mechi ya watani Yanga dhidi ya Simba, ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kiongozi huyo wa Simba, alifikishwa mahakamani hapo jana na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi na kusomewa shitaka na Wakili wa Serikali, Genes Tesha akishirikiana na Mwendesha Mashitaka, Jackson Chidunda.
Genes alimsomea Muslen shitaka la kumjeruhi na kumdhuru mwili mtoto wa Manji. Alidai Machi 8, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, ulioko Chang'ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam, mshitakiwa alimpiga teke Meheub na kumpiga usoni na sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha mazito.
Mshitakiwa alikana shitaka, ambapo Wakili Tesha alidai upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi juu ya dhamana kwa mshitakiwa kwa kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika.
Kwa upande wa Wakili wa mshitakiwa huyo, Dk. Damas Ndumbaro, aliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wake kwani ataweza kufika pindi atakapohitajika.
Hakimu Moshi alisema dhamana ipo wazi kwa mshitakiwa, iwapo atakuwa na mdhamini mmoja kutoka taasisi binafsi inayotambulika au kutoka serikalini na awe na barua ya mwajiri wake.
Alisema barua ya mdhamini ni lazima ikafanyiwe uhakiki na upande wa Jamhuri.
Mshitakiwa huyo aliweza kutimiza masharti hayo na kuachiwa huru kwa dhamana hadi Aprili 20, mwaka huu, kesi itakapotajwa baada ya upande wa Jamhuri kufanya uhakiki wa barua hiyo na kuridhika nayo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, inadaiwa Musleh alimsukuma mtoto huyo wa Manji wakati wakiwa katika lifti wakitoka mpirani.
FRANCIS CHEKA ABADILISHIWA ADHABU, APEWA KIFUNGO CHA NJE
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, jana ilimbadilishia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela , bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka, ambapo sasa atatumikia kifungo cha nje.
Sambamba na hilo, Cheka atatakiwa kulipa faini ya sh milioni moja kama ilivyoamuliwa awali na mahakama hiyo.
Aidha, Cheka atatakiwa kutumikia kifungo cha saa nne kwa siku, kwa kufanya shughuli katika taasisi za umma, ikiwemo kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na maeneo ambayo atakuwa akipangiwa.
Kulingana na sheria namba 6 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 inayomtaka mfungwa kufanya kazi saa nne bila malipo katika taasisi za umma, imemwezesha bingwa wa dunia wa uzito wa kati
(WBF) Cheka, kutumikia kifungo cha nje badala ya gerezani kama ilivyokuwa hukumu yake ya awali.
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, Saidi Msuya,alidai mahakamani hapo kuwa kutokana na kutiwa hatiani kwa kosa la kumpiga na kumsababishia maumivu meneja wa baa yake, Bahati Kibanda, sheria hiyo ndio imemwezesha bondia huyo kutumikia kifungo chake nje ambapo atatakiwa kufanya kazi kwenye taasisi za umma.
Februari 2, mwaka huu, Cheka alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya sh. milioni moja, ambapo alidaiwa kutenda kosa hilo kwa kumpiga Bahati, aliyekuwa meneja wa baa inayojulikana kwa jina la Vijana Social Hall.
Kutokana na uadilifu wa Cheka akiwa jela,ustawi wa jamii ulitoa pendekezo la kupunguziwa adhabu baada ya kuridhika na mwenendo wa tabia yake akiwa gerezani.
Kwa mujibu wa sheria ya Magereza namba 34 ya mwaka 1967 kifungu cha 51 kilichofanyiwa marekebisho ya sheria namba 9 mwaka 2002 kinampa uwezo wa mkuu wa gereza kuomba kupunzwa kwa adhabu kwa mfungwa.
Kifungu hicho cha sheria kinamruhushu mkuu wa gereza kuiomba ofisi ya ustawi wa jamii kubadilisha au kukungaza adhabu kwa mfungwa endapo tu itaridhika na tabia ya mfungwa gerezani.
Baada ya ustawi wa jamii kupokea ombi hilo na kuitarifu mahakama, ambayo ilitoa hukumu kwa mfungwa na mfungwa kuanza kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii.
Afisa Huduma ya Jamii, Yusufu Ponera, alisema Cheka ni miongoni wa watu 50 walioombewa na mkuu wa gereza kupunguziwa adhabu baada ya kuonyesha tabia nzuri gerezani.
Kifungo cha Francis Cheka kinatarajiwa kumalizika Februari 1 2017. Katika kipindi hiki, Cheka hatakiwi kufanya uharifu wowote wala kutoka nje ya mkoa bila taarifa.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, bondia huyo baada ya kutoka mahakamani hapo, aliomba kutoongea lolote wala kupigwa picha, jambo lililowashangaza baadhi ya watu waliohudhuria mahakamani hapo.
"Wana Morogoro tukiungana na Watanzania wengine nchini, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote walioshirikia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha Cheka ameachiwa huru, Mungu mkubwa,’’ alisema Rashid Matesa.
Hata hivyo, wadau hao wa michezo mkoa wa Morogoro walimtaka Cheka kuhakikisha anatumikia kifungo hicho cha nje kwa uadilifu hadi afikie tamati ili kutoa imani kwa vyombo vya dola.
YANGA, PLATINUM ZAINGIZA MIL 91, LEO NI SIMBA NA MGAMBO, YANGA NA KAGERASUGAR
Mechi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africas dhidi ya timu ya FC Platinum ya Zimbambwe iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam iliingiza mil 91,660,000 kutokana na watazamaji 14,563 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo.
Mgawanyo wa mapato katika mchezo huo ni, VAT 18% sh. 13,982,033, Gharama ya tiketi sh. 12,380,000, Uwanja 15% sh. 9,794,694.92, Gharama za mchezo 15% sh. 9,794,694.92, TFF 5% sh. 3,264,898.31, CAF 5% sh. 3,264,898.31 na Young Africans 60% sh.39.178,779.66
Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea kesho (jumatano) kwa viwanja vitatu kutimua vumbi, Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Young Aricans watawakaribisha Kagera Sugar mchezo utakaoanza majira ya saa 10 kamili jioni.
Jijini Tanga maafande wa Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Simba SC katika mchezo utakaofanyika uwanja wa Mkwakwani, huku jijini Mbeya wenyeji Mbeya City watawakaribisha timu ya ya Stand United kutoka mkoani Shinyanga kwenye uwanja wa Sokoine.
TWIGA STARS KUWAFUATA ZAMBIA IJUMAA
Msafara wa watu 25 wa timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars), unatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia, Jumapili.
Twiga Stars inaanzia hatua ya pili katika kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wanawake baada ya kuwa katika nafasi za juu kwa viwango barani Afrika na endapo itafanikiwa kuwaondoa Wazambia, itafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo.
Msafara utaongozwa na Blassy Kiondo (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji), Beatrice Mgaya (kiongozi msaidizi), Rogasin Kaijage (kocha mkuu), Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano (Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa).
Wachezaji watakokweda Zambia ni Asha Rashid, Mwajuma Abdallah, Mwanahamis Omar, Donisi Minja, Amina Bilal, Fatuma Bashiri, Esther Chabruma, Shelda Mafuru, Maimuna Kaimu, Najiat Abbas, Stumai Abdalla, Fauma Issa, Thereza Yona, Fatuma Hassan, Fatuma Omary, Sophia Mwasikili, Fatuma Khatibu na Etoe Mlenzi.
BEACH SOCCER KUONDOKA ALHAMISI
Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer) inatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Cairo, Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni utakaofanyika Jumapili.
Tanzania inapaswa kupata ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Misri ili kufuzu kwa fainali za soka la ufukweni barani Afrika zitakazofanyika visiwa vya Shelisheli, kufuatia kupoteza mchezo wake awali uliofanyika Escape 1 jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki.
Msafara wa timu ya Beach Soccer utakaoondoka na Shirika la Ndege la Ethiopia, utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Ahmed Msafiri Mgoyi, Kocha Mkuu John Mwansasu, Kocha Msaidizi Ali Sheikh Alhashby, Meneja Deogratius Baltazar na Daktari wa timu, Dr Leonidas Rugambwa.
Wachezaji ni Rajabu Chana Kipango, Ahmed Rajab Juma, Roland Revocatus Kessy, Samwel Sarungi Opanga, Feisal Mohamed Ussi, Mohamed Makame Silima, Mwalimu Akida Hamad, Juma Sultan Ibrahim, Kashiru Salum Said na Ally Rabby Abdallah.
WAMBURA MCHEZAJI BORA VPL FEBRUARI
Kiungo wa timu ya Coastal Union, Godfrey Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Februari 2015 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Wambura amechaguliwa kuwa mchezaji bora baada ya jopo la makocha linalofanya majumuisho ya wachezaji bora wa kila mchezo, ambapo kiungo huyo ameweza kuwapiku wachezaji Saimon Msuva wa Young Africans, Abasirim Chidiebere wa Stand United na Gideon Benson wa Ndanda FC.
Kwa kuibuka mchezaji bora wa mwezi Februari, Wambura atazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.
Wakati huo huo timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajiwa kuagwa mbele ya waandishi wa habari kesho alhamisi saa tano asubuhi katika ukumbi wa TFF Karume.
SPIKA ANNE MAKINDA AMKUMBUKA MAREHEMU KOMBA
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, jana alitoa taarifa ya Spika kuhusu kifo cha aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM),marehemu Kaptein John Komba, aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu, kutokana na shinikizo la damu.
Makinda alitoa taarifa hiyo bungeni mjini hapa jana kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu.
Katika taarifa yake, Spika alisema huo ulikuwa ni msiba mkubwa na wao kama bunge, wamepoteza mtu ambaye ni mpiganaji na atakumbukwa daima.
“Kwa kweli ni msiba mkubwa. Mnamo Febuari 28, mwaka huu, tulimpoteza mbunge mwenzetu Kapteni Komba na kumzika Machi 3, mwaka huu, nyumbani kwao Lituhi mkoani Ruvuma,”alisema.
Spika Anne alisema, marehemu Komba, alifariki kwa ugonjwa wa shinikizo la damu akiwa katika majukumu yake ya kikazi kama mbunge.
Aidha, alisema kabla ya kukutwa na mauti, Komba alikuwa katika maandalizi ya safari ya kwenda nchini Ethiopia kwa shughuli za kibunge.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wabunge kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka marehemu Komba.
Tuesday, March 17, 2015
AZAM YAITUNGUA NDANDA UNITED 1-0, YAREJEA KILELENI LIGI KUU
Timu ya Azam FC imerejea killeni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni ya leo.
Ushindi huo ambao ni sawa na kisasi baada ya Azam FC kufungwa pia 1-0 na Ndanda katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, unaifanya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ifikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 17.
Mabingwa hao watetezi, sasa wanaizidi Yanga SC kwa pointi mbili, ambayo hata hivyo mchezo mmoja mkononi, Jumatano ikitarajiwa kumenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikiongozwa na kocha Mganda, George ‘Best’ Nsimbe kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufukuzwa kwa Mcameroon, Joseph Marius Omog, Azam FC ilipigana kiume kupata ushindi huo.
Sifa zimuendee Didier Kavumbangu aliyefunga bao lake la 10 dakika ya 24 katika Ligi Kuu msimu huu na la 16 jumla tangu ajiunge na Azam FC akiwa anaichezea katika mechi ya 30 leo.
Kavumbangu, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, alifunga bao hilo kwa guu lake la kulia akimalizia pasi ya mfungaji bora wa misimu miwili iliyopita Ligi Kuu, KIpre Herman Tchetche.
Pamoja na ushindi huo, Azam FC ilipata upinzani mkali kutoka kwa Ndanda FC ambao wamepanda Ligi Kuu msimu.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa, Mudathir Yahya, Himid Mao, Frank Domayo/John Bocco dk57, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Amri Kiemba dk82 na Brian Majwega.
Ndanda FC; Wilbert Mweta, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Hemed Kihoja, Cassian Ponela, Zablon Raymond, Jacob Massawe, Ibrahim Mwaipopo/Iddi Kulachi dk57, Nassor Kapama/Gideon Benson dk72, Masoud Ally na Stahmili Mbonde/Kiggi Makassy dk84.
Sunday, March 15, 2015
YANGA KUDADADEKI! YAWABAMIZA WAZIMBABWE 5-1
YANGA SC imetanguliza mguu mmoja hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ili Yanga isisonge mbele, inabidi ifungwe mabao 4-0 na Platinum katika mchezo wa marudiano wiki ijayo mjini Bulawayo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Djamaladen Aden Abdi, aliyesaidiwa na Hassan Eguech Yacin na Abdallah Mahamoud Iltireh wote wa Djibouti, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Mabao ya Yanga SC yalifungwa na viungo Salum Abdul Telela ‘Master’ dakika ya 32 na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ dakika ya 43, wakati bao la Platinum lilifungwa na Walter Musoma dakika ya 45.
Kipindi cha pili, Yanga waliongeza makali na kufanikiwa kupata mabao matatu zaidi, ambayo yanawafanya waende Bulawayo kwenye mchezo wa marudiano, wakiwa wana kazi ndogo tu.
Mabao hayo yalifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 47 na Mrisho Ngassa mawili dakika ya 55 na 90.
Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Simon Msuva alimsetia krosi nzuri Ngassa kufunga bao la tano.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Salum Telela, Simon Msuva/Kpah Sherman, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe na Said Juma ‘Kizota’.
Platinum FC; Petros Mhari, Raphael Muduviana, Kelvin Moyo, Gift Bello, Thabit Kamusuko, Wellington Kamudyariwa/Simon Shoko, Wisdom Mtasa/Aaron Katege, Brian Muzondiwa, Obrey Ufiwa/Emmanuel Mandiranga, Walter Musoma na Elvis Moyo.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
OKWI AINYONGA MTIBWA SUGAR
BAO la Emmanuel Anord Okwi dakika ya 90 ushei limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba SC sasa inafikisha pointi 29 baada ya mechi 18 na kuendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC pointi 30 za mechi 16 sawa na vinara Yanga SC, wenye pointi 31.
Okwi alifunga bao hilo, wakati tayari baadhi ya wapenzi wa Simba SC wameanza kutoka uwanjani, wakiamni matokeo ni sare. Mganda huyo, alifunga baada ya kupata pasi ya Abdi Banda na kumchambua vizuri kipa aliyefanya kazi nzuri leo, Said Mohamed Kasarama.
Mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Yussuf Sekile wa Ruvuma na Abdallah Rashid wa Pwani, Simba SC ndiyo waliotawala na kutengeneza nafasi nyingi, lakini hawakuwa na bahati ya mapema.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji ya Mtibwa Sugar akisaidiana na Ame Ally, lakini wakaishia kuisumbua tu ngombe ya Simba, iliyoongozwa na beki chipukizi, Hassan Isihaka.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdi Banda, Elias Maguri, Emmanuel Okwi na Simon Sserunkuma/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk46.
Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Said Mkopi, Dacis Luhende, Salim Mbonde, Andrew Chikupe, Shaaban Nditi, Ally Sharrif, Henry Joseph, Ame Ally/Mohammed Mkopi dk66, Muzamil Selemba/Ally Yussuf dk86 na Mussa Hassan Mgosi/Vincent Barnabas dk75.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
MKUTANO MKUU TFF WAMALIZIKA SALAMA NA KWA AMANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) jana limefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka katika ukumbi wa Morogoro hoteli ya mjini Morogoro ambapo mgeni Rasmi alikua ni mkuu wa mkoa wa Morogoro Dr Rajabu Rutengwe.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Dr Rutengwe aliushukuru uongozi wa TFF nchini kwa kuweza kuandaa mkutano mkuu mzuri na wa kisasa ambao pia ulifanyikia katika mkoa wake wa Morogoro.
Akiongea na wajumbe wa mkutano mkuu Dr Rutengwe alisema, TFF ina changamoto ambazo inapaswa kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa mpira wa miguu nchini kwa ujumla, changamoto hizo ni kukosekana kwa wataalamu wa vyakula, wataalamu wa tiba na wataalamu wa saikolojia.
Dr Rutengwe aliomba TFF kwa kushirikiana na serikali inapaswa kuandaa wataalamu wengi wa masuala hayo ili kuweza kuendana na mahitaji ya kuwaanda wanamichezo bora ambao watakua tayari kwa ushindani na sio ushiriki.
Aidha mkuu wa mkoa huyo aliipongeza Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuupa mkoa wa Morogoro uenyeji wa mkutano mkuu ambapo pia umefanyika na malengo kufanikiwa kwa asilimia mia moja, na kusema kwa niaba ya serikali ya mkoa wapo tayari kupokea tena mwaliko wa uenyeji wa mikutano mbalimbali ya TFF.
Mkutano ulijadili Ajenda za kawaida ambazo ni Kufungua Mkutano ni Uhakiki wa Wajumbe, Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya Rais, ripoti kutoka kwa Wanachama, Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.
Zingine ni Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013, Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu, Kupitisha bajeti ya 2015, Marekebisho ya Katiba, Mengineyo na Kufunga Mkutano.
Kwa mara ya kwanza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limepata bendera yake ambayo ilipitishwa na mkutano mkuu na asubuhi ya jumapili Machi 15 mwaka huu, imepandishwa kwa mara ya kwanza Morogoro hoteli.
Aidha wajumbe wa mkutano mkuu pia wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini (FDF), ambapo kutaundwa kamisheni maalum itakayoshugulikia suala hilo.
Lengo la kamisheni hiyo ni kuisaidia TFF kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya soka la watoto, vijana, wanawake nchini na kuviwezesha vyama vya soka vya mikoa (FA), vyama shiriki vya TFF kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya soka la vijana.
Pia mkutano mkuu huo ulitoa azimio la kuitaka serikali itoe msamaha wa kodi kwa vifaa vya michezo hasa vinavyotumika kufundishia watoto michezo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 125 na kati yao wajumbe watano ni wanawake.
Kikao kijacho cha mkutano mkuu kitafanyika kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu.
27 WAITWA TAIFA STARS ITAKAYOIVAA MALAWI
Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars ) Mart Nooj, ametangaza kikosi cha wachezaji 27 watakaoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi utakaofanyika uwanja wa CCM Kirumba jijin Mwanza Machi 29, 2015.
Taifa Stars inayotarajia kucheza na The Flames mwishoni mwa mwezi huu, itaingia kambini machi 22 machi katika hotel ya Tansoma kujiandaa na mchezo huo kabla ya kuelekea jijini Mwanza machi 24 kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo.
Wachezaji walioitwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo ni; Magolikipa, Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC), walinzi ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris (Azam FC), Mwinyi Haji (KMKM), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Oscar Joshua (Yanga), Abdi Banda na Hassan Isihaka (Simba SC).
Viungo ni Frank Domayo, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Mcha Khamis (Azam FC), Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United), washambuliaji Mwinyi Kazimoto (Al Markhiry - Qatar),
Saimon Msuva , Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta (Tp Mazembe - Congo DR), John Bocco (Azam FC), na Juma Luizio (Zesco United - Zambia)
Timu ya Taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili jijini Mwanza machi 27, 2015 ikiwa na kikosi kamili, wakiwemo wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, Msumbuji, Congo DR na Zimbambwe.
Malawi inashika nafasi ya 91 katika viwango vipya vya FIFA Duniani vilivyotolewa mwezi huu, huku Tanzania ikipanda kwa nafasi saba na kushika nafasi ya 100.
KOCHA SYLVESTER MARSH AAGWA
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za ramirambi kwa familia ya Marsh, kufuatia kifo cha kocha wa Taifa ya vijana Sylvester Marsh kilichotokea jana jijini Dar es salaam.
Katika salam zake kwa familia ya marehemu, Mh. Malinzi amesema familia ya mpira wa miguu
nchini TFF imeshtushwa na msiba huo na kusema Shirikisho na Taifa limempoteza mtu muhimu
katika mpira wa miguu nchini.
Mwili wa marehem Marsh utaagwa leo saa 6 kamili mchana, katika kanisa la Hospital ya Taifa
Muhimbili na kutasafirishwa kuelekea Igoma jijini Mwanza kwa mazishi majira ya saa 8 kamili
mchana kwa basi dogo (coaster) la TFF.
Marsh alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Taarifa zinasema Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya
maradhi ya saratani ya koo yaliyokuwa yakimsumbua na ghafla hali yake ikabadilika juzi hadi kufariki
dunia.
Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj
Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa,
akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim
Poulsen.
Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba
mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Star na Marsh akaondoka pamoja na Kim
Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.
Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.
Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.
Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.
Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa
Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.
Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe.
Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.
Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo.
Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina.
Wednesday, March 11, 2015
MAANDALIZI MKUTANO MKUU WA TFF YANAENDELEA VIZURI, AJENDA ZATAJWA
Maandalizi ya mkutano mkuu wa mwaka wa TFF utakaofanyika mjini Morogoro kati ya Machi 14,15 mwaka huu katika Ukumbi wa Morogoro Hotel yanaendelea vizuri.
Agenda za mkutano mkuu ni:
1.Kufungua Mkutano
2. Uhakiki wa Wajumbe
3. Kuthibitisha Ajenda.
4. Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita.
5. Yatokanayo na Mkutano uliopita.
6. Hotuba ya Rais.
7. Ripoti kutoka kwa Wanachama
8. Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.
9. Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013.
10. Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu.
11. Kupitisha bajeti ya 2015
12. Marekebisho ya Katiba
13. Mengineyo
14. Kufunga Mkutano.
TANZANIA KUIVAA MISRI IJUMAA BEACH SOCCER
Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer) inatarajiwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri siku ya ijumaa majira ya saa 10 kamili jioni, mchezo utakofanyika katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini Dar es salaam.
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo, ambapo kwa takribani wiki mbili kipo kambini Bamba Beach wakijifua kwa mchezo huo.
Tanzania ilifuzu hatua ya pili baada ya kuiondoa timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12 -9, na endapo itafanikiwa kuwaota Misri, itafuzu moja kwa moja kucheza Fainali za soka la Ufukweni zitakazofanyika Visiwa vya Shelisheli mwezi April mwaka huu.
Waamuzi wa mchezo huo ni Eid Haitham Eid Hassan (Sudan), mwamuzi msaidzi wa kwanza Abaker Mohamed Bilal (Sudan), mwamuzi msaidizi wa pili Abdalla Hassain Hassaballa, mtunza muda (time-keeper) Boubaker Bessem (Tunisia) wakati kamisaa wa mchezo huo ni Khiba Herbert Mohoanyane kutoka Lesotho.
Nayo timu ya Taifa ya Misri inatarajiwa kuwasili Dar es salaam kesho (jumatano) mchana, ambapo itafikia katika hoteli ya Double Tree by Hilton iliyopo Masaki, huku waamuzi wa mchezo huo wakitarajiwa pia kuwasili kesho na kufikia katika hotel ya Protea Oysterbay.
Aidha siku ya alhamis makocha wa timu zote wataongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume kuanzia majira ya saa 5 kamili asubuhi.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Misri kati ya Machi 20,21 na 22 mwaka huu.
Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), inaitakia kila la kheri na ushindi timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach Soccer) katika huo dhidi ya Misri.
Wakati huo huo michezo miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyokuwa iichezwe kesho (jumatano) kati ya JKT Ruvu dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Taifa, na Mgambo Shooting dhidi ya Azam FC uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga imeahirishwa na sasa mechi hizo zitapangiwa tarehe nyingine.
SIMBA, YANGA ZAINGIZA MIL 436
Mechi no.117 iliyowakutanisha Simba na Yanga katika uwanja wa Taifa, imeingiza jumla ya sh. milioni 436,756,000 kutokana na idadi ya watazamaji 49,758 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo.
Watazamaji 309 walikata tiketi za VIP A, 1,310 VIP B, 1,533 VIP C, Rangi ya Machungwa (Orange) 9,913 huku viti vya rangi ya bluu na kijani wakiingia watazamaji 36,693.
Mgawanyo wa mapato ya mchezo huo ni VAT 18% sh.66,623.796, FDF timu mwenyeji sh. 17,415,300, FDF TFF sh.7,463,700, Gharama za tiketi sh.11,669,600.
Mgao wa Uwanja sh. 50,037,540.51, Gharama za mchezo sh.28,354,606.29, Bodi ya Ligi (TPLB) sh. 26,686,688.27, TFF sh.20,015,016.20, DRFA sh. 11,675,426.12, klabu ya Simba sh. 115,086,343 huku Yanga wakipata sh.81,727.83.
Wakati huo huo Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea kesho siku ya jumanne katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wenyeji timu ya Polisi Morogoro watawakaribisha Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.
Siku ya jumatano JKT Ruvu watawakaribisha Young Africans katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku jijini Tanga Mgambo Shooting wakiwa wenyeji wa timu ya Azam FC.
Aidha mechi ya Kombe la Shirikisho (CC) barani Afrika kati ya Young Africans dhidi ya timu ya FC Platinum ya Zimbabwe, itafanyika siku ya jumapili Machi 15, 2015 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Monday, March 9, 2015
OKWI APELEKA KILIO JANGWANI
BAO lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi dakika ya 51, jana liliiwezesha Simba kuwatambia watani wao wa jadi Yanga, kwa kuwachapa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 25 baada ya kuwazidi mbio mabeki wawili wa Yanga na kumpima kipa Ally Mustafa Barthez, aliyekuwa ametoka langoni.
Ushindi huo umeiwezesha Simba kuendeleza ubabe kwa Yanga katika mechi walizokutana hivi karibuni. Walipokutana mwaka jana katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba iliichapa Yanga mabao 2-0.
Katika mechi hiyo, vijana wa Simba walionyesha soka ya kiwango cha juu hasa dakika za mwisho kutokana na kugongeana pasi nyingi bila wachezaji wa Yanga kugusa mpira.
Washambuliaji Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Amisi Tambwe na Danny Mrwanda walikuwa mwiba katika ngome ya Simba, lakini umaliziaji wao mbovu uliwakosesha mabao.
Yanga ilipata pigo kipindi cha pili baada ya kiungo wake Haruna Niyonzima kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kubutua mpira huku mwamuzi akiwa amepuliza filimbi ya kuotea.
Saturday, March 7, 2015
TAIFA STARS KUIVAA MALAWI
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashuka dimbani jumapili Machi 29 mwaka huu, kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mchezo huo wa kirafiki ambao upo katika kalenda ya FIFA kwa timu za Taifa (Machi 23-31) na utatarajiwa kuanza majira ya saa 10 na nusu jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
NKONGO KUCHEZESHA ZESCO Vs AS KALOUM
Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania mwenye beji ya FIFA, Israel Mjuni Nkongo amechaguliwa kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) kati ya wenyeji Zesco FC ya Zambia dhidi ya AS Kaloum ya Guinea.
Katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili, Nkongo atasaidiwa na washika kibendera John Kanyenye na Josephat Bulali na mwamuzi wa akiba Waziri Sheha wote kutoka Tanzania, huku Kamisaa wa mchezo akiwa Mayixole Elvin Shishana kutoka nchini Afrika Kusini
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 13,14,15 Machi mwaka huu nchini Zambia.
KUZIONA SIMBA, YANGA KESHO SH.7,000
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa siku ya Jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).
Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya, Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Wednesday, March 4, 2015
SAFARI YA MWISHO YA MAREHEMU KOMBA
JENEZA lenye mwili wa marehemu John Komba likiteremshwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana kijijini kwake Lituhi, Mbinga mkoani Ruvuma |
RAIS Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka mchanga kwenye kaburi na marehemu Komba |
Mke wa marehemu Komba, Salome Komba (kushoto) akiweka shada la maua kwenye kaburi la mumewe |
Watoto wa marehemu Komba wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu baba yao |
Watoto wa marehemu Komba wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi la maua |
Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Komba |
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Komba |
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Mchemba na Katibu Mwenezi, Nape Nnauye wakiweka shada la maua kaburini |
Msanii Khadija Kopa akiwa na majonzi baada ya kuweka shada la maua kwenye kaburi la Komba |
Subscribe to:
Posts (Atom)