KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, July 1, 2014

MBEYA CITY YAFUNGA USAJILI 2014/2015



NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA


TIMU ya Mbeya City F.C, imefunga rasmi zoezi la usajili kwa msimu ujao wa ligi Kuu ya Tanzania Bara, maarufu zaidi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

Imeelezwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na klabu hiyo, kuwa na mipango ya kupunguza kikosi, ili kuwa na kikosi kidogo chenye ufanisi.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema hayo ni maazimio ya Kikao cha Bodi ya timu hiyo kilichoketi Juni 19, mwaka huu, na kukubaliana kufunga rasmi zoezi la usajili.

Kimbe alisema Bodi imeazimia kuwa na kikosi kidogo, chenye ufanisi na kwa kuzingatia klabu kwa msimu uliomalizika na msimu ujao kutokuuza wachezaji wake.

“Baadhi ya wachezaji watapandishwa toka katika kikosi cha pili, na wachezaji wawili wapya (hakuwataja majina), waliojiunga na timu kwa ajili ya msimu ujao 2014/2015 wanatosha” alisema Kimbe.

Aliongeza mchakato unaoendelea toka Juni 26, mwaka huu ni kutafuta wachezaji, kwa ajili ya kikosi cha pili (Juniour team) A na A2 na mchakato huo utamalizika Julai 2, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa Mbeya City lengo la klabu hiyo ni kupata wachezaji wenye umri kati ya miaka 17 hadi 21. Aliwataja wachezaji ambao muda wao wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo umefika tamati ni Aziz Sibo, ambaye mkataba wake umekwisha muda wake Mei 31 mwaka huu.

Wengine ni Mohamed Suleiman, ambaye amepangiwa majukumu mengine, Baraka Haule, Francis Castro, Jeremiah Mangasini na Richard Brown. Kimbe aliongeza kuwa wacheza Yusuph Wilson na Geofrey Jackson wametolewa kwa mkopo na hakuweka bayana timu walizopelekwa.

Alisema watumishi ambao mikataba yao imekwisha muda wake, na kwa sababu mbalimbali zinazojulikana kwa pande zote na imeshindikana kuihuisha ni pamoja na aliyekuwa kocha msaidizi, Maka Mwalwisi.   Kimbe alisema Mwalwisi mkataba wake umeisha Juni 30, mwaka huu na wakati aliyekuwa Ofisa Habari wa timu hiyo Fredy Jackson mkataba wake ulikwisha toka Mei 31, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment