KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, July 28, 2014

AZAM YAITOA SIMBA KOMBE LA ROLLINGSTONE



AZAM FC imetinga Nusu Fainali ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kwa nchi za Maziwa Makuu, Rollingston baada ya kuitoa Simba SC, zote za Tanzania kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.


Makocha wakuu wa vikosi vya kwanza vya timu hizo za Dar es Salaam, Mcameroon Joseph Marius Omog wa Azam ya Chamazi na Mcroatia Zdravko Logarusic wa Simba ya Msimbazi wote walikuwepo kushuhudia mchezo huo.

Shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa wao, Hamad Juma aliyepangua penalti mbili za wachezaji wa Simba SC, Dadi Yunus na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wakati penalti ya Haruna Abdallah iliota mbawa.

Waliofunga penalti za Simba SC ni Ibrahim Hajibu na Omary Hussein wakati penalti za Azam zilifungwa na Kassim Kisengo, Reyna Mngungila na Adam Omar.

Kipa wa timu ya taifa ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Peter Manyika alipangua penalti mbili pia za Shirazy Abdallah na Masoud Abdallah, lakini akaangushwa na wachezaji wake waliokosa penalti.

Kipa wa Azam FC, Hamad Juma alichomoka kwa shangwe baada ya kupangua mkwaju wa mwisho wa Tshabalala aliyesajiliwa kwa ajili ya kikosi cha kwanza cha Simba SC kutoka Kagera Sugar msimu huu.

Peter Manyika aliyefanya kazi nzuri ya kuokoa michomo mingi ya hatari ndani ya dakika 90 na akaenda kucheza penalti mbili baadaye aliangua kilio baada ya mchezo huo.

Kwa ujumla mchezo ulikuwa mzuri na timu zote zilishambuliana kwa zamu, huki wachezaji wakionyesha vipaji vya hali ya juu. Kwa kutolewa, Simba SC imeungana na watani wao, Yanga SC ambao jana walitolewa katika hatua ya 16 Bora. Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa kesho.

No comments:

Post a Comment