KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 28, 2014

LULU: KANUMBA ALIKUWA MPENZI WANGU



NA FURAHA OMARY

MSANII nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, amekubali mahakamani
kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba (marehemu), na siku ilipotokea kifo cha msanii huyo walikuwa na ugomvi.

Mcheza filamu huyo alisema hayo jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, na kuongeza kuwa, siku ya tukio alikwenda nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, ambako ulitokea ugomvi wakiwa chumbani kwa marehemu.

Lulu, ambaye anakabiliwa na kesi ya kumuua Kanumba bila kukusudia, alikubali hayo mbele ya Jaji Rose Teemba baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Mbogo, kumsomea maelezo ya shitaka hilo la kuua bila kukusudia.

Katika kesi hiyo, Lulu anadaiwa Aprili 7, 2012, eneo la Sinza Vatican, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, alimuua Kanumba bila kukusudia. Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shitaka hilo.
"Nakubali kwamba tulikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba na siku ya tukio nilimtembelea nyumbani kwake na kuingia chumbani kwake na kulikuwa na ugomvi baina yetu. Nakubali nilijaribu kutoka nje, lakini Kanumba alinivuta ndani na kufunga mlango," alisema Lulu.

Lulu pia alikubali kuwa alitoka chumbani na kwenda kumfahamisha mdogo wake,Seth Bosco, kwamba kaka yake ameanguka na kweli baada ya tukio alikamatwa maeneo ya Bamaga na kufikishwa mahakamani.

Awali, akisoma maelezo hayo, Monica alidai kuwa, Aprili 7,2012, Kanumba alikuwa nyumbani kwake maeneo ya Sinza Vatican na mdogo wake, Seth na ilipofika saa sita usiku, alimwambia Seth ajitayarishe waende kustarehe na wakati wanajiandaa, alifika Lulu na kuingia chumbani kwa Kanumba moja kwa moja.

Monica alidai baada ya dakika chache kupita, mdogo wa Kanumba, Seth alisikia malumbano ambapo Kanumba alikuwa akimlalamikia Lulu kwa nini anasikiliza simu ya bwana wake mbele yake na wakaanza kugombana na alimsikia Lulu akilia.

Wakili huyo alidai Seth alisogolea mlangoni na kumkuta mshitakiwa akijitahidi kutaka kutoka nje, lakini Kanumba alimvuta na kumuingiza ndani na kufunga mlango na baada ya muda Lulu alitoka na kumfahamisha kwamba Kanumba amedondoka.

Alidai Seth alikwenda na kumkuta Kanumba yuko sakafuni na hajitambui, hivyo aliamua kumpigia simu daktari wake binafsi, Parpas Kageia, ambaye alifika na alipomfanyia uchunguzi, aligundua ameshafariki, lakini hakumwambia mdogo wake. Alidai daktari alimwambia mdogo wake wamchukue na kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako waliufanyia mwili uchunguzi na kubaini ameshafariki.

Monica alidai mshitakiwa alikamatwa siku hiyo alfajiri eneo la Bamaga na kwa mujibu wa ripoti ya kitabibu ya daktari, Kanumba alifariki kwa kushindwa kupumua kutokana na msukumo katika ubongo na alikuwa na uvimbe katika ubongo na pia ulipata mtikisiko.

Wakili huyo alidai wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, wataita mashahidi wanne akiwemo mdogo wa Kanumba, Seth na daktari wake binafsi na hawatakuwa na kielelezo.

Kwa upande wa mawakili wa Lulu, Peter Kibatala na Fulgence Massawe, walidai watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili, ambavyo ni panga na ripoti ya uchunguzi ya daktari aliyofanyiwa Lulu.

Jaji Rose aliahirisha shauri hilo hadi kikao kingine kitakachopangwa na mahakama.

No comments:

Post a Comment