KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 7, 2014

TAMBWE AINUSURU SIMBA


KASI ya Simba kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara jana ilipunguzwa baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, sare hiyo imeiwezesha Simba kuchupa nafasi ya tatu ikiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Mbeya City, lakini ipo mbele kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Mtibwa inaendelea kushika nafasi ya tano ikiwa na pointi 22.

Mtibwa ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 10 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' kutokana na uzembe wa kipa Ivo Mapunda.

Simba ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 17 wakati Amri Kiemba alipounganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Issa Rashid, lakini ulitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Mtibwa ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Mtibwa ilicheza vizuri katika kipindi cha kwanza huku viungo wake Jamal Simba, Shabani Kisiga na Juma Luizio wakitawala dimba la kati. Katika kipindi hicho, Simba ilionekana kupoteza mawasiliano japokuwa uwanja uliwasumbua kwa kuwa mpira haukuwa ukitulia.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kubadili staili ya mchezo, ambapo ilicheza pasi ndefu na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Mtibwa na hatimaye kupata bao dakika ya 50 lililofungwa na Hamisi Tambwe.

Mtibwa ilipata pigo dakika ya 69 baada ya kiungo wake, Shaaban Nditi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu na kuifanya timu yake ibaki na wachezaji 10 uwanjani.

No comments:

Post a Comment