KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 16, 2014

TFF YAREJESHA MICHUNO YA KOMBE LA TAIFA




MASHINDANO maalumu ya mikoa ya kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 22 hadi Machi 5 mwaka huu, huku ikiigharimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) takribani Sh. Milioni 360.

Michuano hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30 Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya.

Mashindano ya Kombe la Taifa miaka ya nyuma yalikuwa eneo zuri la kuibua vipaji; Pichani ni nyota wa miaka ya 1980, Abubakar Salum 'Sure Boy' akiichezea Yanga, hapa anamtoka beki wa Simba SC Iddi Selemani 'Meya' katika mechi ya watani mwaka 1989.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.

Malinzi alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo, kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.

Baada ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.

Wachezaji hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.

Malinzi alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mwezi Aprili.

“Tunaamini mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars, hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema Malinzi.

Machi 5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

No comments:

Post a Comment