KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 7, 2014

AZAM YAPANIA KUWEKA REKODI


WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam watawakosa nyota wao wanne katika mechi ya awali dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbuji, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Nyota wa Azam watakaokosekana katika mechi hiyo ni pamoja na mshambuliaji hatari, John Bocco na beki Hajji Nuhu, ambao ni majeruhi. Wengine ni chipukizi Ismail Lugambo na Farid Musa.

Ofisa Habari wa Azam, Jaffari Iddi alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Bocco bado majeruhi wakati Nuhu aliumia goti juzi baada ya kuanguka ghafla wakati wa mazoezi yaliyofanyika Chamazi.

Jaffari alisema Lugambo alivunjika mguu mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Azam na Ashanti wakati Farid amekuwa akisumbuliwa na majeraha mara kwa mara na itabidi afanyiwe vipimo vikubwa.

"Farid itabidi afanyiwe vipimo vya MRY kwenye mgongo ili tujue sababu ya kuumia mara kwa mara na Bocco bado goti lake halijawa sawa. Alipewa mapumziko ya wiki mbili na tayari ameshamaliza wiki moja, hivyo hatacheza mchezo huo," alisema Jaffari.

Pamoja na kuwakosa nyota hao, Jaffari alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Ferroviario na kusisitiza kuwa, wamepania kuweka rekodi ya kufika mbali zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana.

Aliongeza kuwa, wamefurahi kupata ruhusa kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ya kucheza mechi hiyo kwenye uwanja wa Chamazi kwa vile wachezaji wao wameuzoea na watautumia vizuri kupata ushindi.

Msimu uliopita, Azam iliiwakikisha Tanzania katika mashindano hayo baada ya kumaliza ligi kuu ikiwa mshindi wa pili, lakini ilitolewa raundi ya tatu. Iwapo Azam itaitoa Ferroviario,  itamenyana na mshindi kati ya St. Michel ya Shelisheli na ASSM Elgeco Plus ya Madagacar

Wakati huo huo, timu za KMKM na Chuoni za Zanzibar, zinaondoka nchini kwenda Ethiopia na Zimbabwe kwa ajili ya mechi zao za michuano ya klabu za Afrika.

KMKM imepangwa kumenyana na Dedebit ya Ethiopia mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya michuano ya klabu bingwa itakayochezwa mjini Addis Ababa wakati Chuoni itamenyana na How Mine ya Zimbabwe katika mechi ya Kombe la Shirikisho, itakayochezwa mjini Harare.

KMKM ilitarajiwa kuondoka jana jioni kwenda Ethiopia kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia wakati Chuoni inatarajiwa kuondoka leo alfajiri kwenda Zimbabwe kwa ndege ya Shirika la Ndege la Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment