KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 3, 2014

SIMBA WAANZA MKAKATI WA UJENZI WA UWANJA


Na Asha Muhaji, Bunju
VIONGOZI na wanachama wapatao 50 wa Klabu ya Simba jana walitembelea eneo la mradi wa uwanja wao ulioko Bunju ‘B’ jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, wanachama hao walifanya kazi ya kulisafisha eneo hilo kwa kufyeka ikiwa ni hatua za awali za kutaka kuuendeleza, ambalo linakadiriwa kuwa na eka 25.

Lengo la kufanya ziara pamoja na kusafisha eneo hilo ni mkakati wa klabu hiyo, kutaka kuanza rasmi mipango ya uendelezaji wa eneo hilo.

Katibu mpya wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga mwenye skafu akizungumza na wanachama wa klabu hiyo katika eneo la kiwanja cha klabu yao, Bunju B, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana.

Eneo hilo linatarajiwa kujengwa uwanja wa mpira utakaokuwa ukimilikiwa na klabu hiyo, pamoja na majengo mengine muhimu yatakayoendana na sura ya kimichezo.

Katika hatua za awali, klabu hiyo imepanga kufyeka pamoja na kupitisha greda lengo likiwa ni kusafisha eneo hilo tayari kwa ujezi wa uwanja utakaoweza kutumiwa na timu yake kwa ajili ya mazoezi na mechi nyingine za kirafiki.

Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameahidi mpaka kufikia Aprili mwaka huu eneo hilo litakuwa na sura ya kiwanja cha michezo huku jitihada zingine zikiendelea kufanywa na uongozi kwa ajili ya mradi mkubwa wa kituo hicho ambacho hapo baadaye utahusisha hosteli ya wachezaji, mgahawa, gym pamoja na bwawa la kuogelea.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mpango wa awali utahusisha kuzungusha uzio eneo lote pamoja na ujenzi wa uwanja wa kuchezea mpira.

Kamwaga alisisitiza mradi wa ujenzi mkubwa wa eneo hilo bado unafanyiwa kazi na uongozi wa klabu hiyo ili kumpata  mkandarasi atakayesimamia ujenzi huo na mipango itakapokuwa tayari basi itawekwa wazi isipokuwa kwa sasa wanachofanya ni hatua za awali za uendelezaji wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment