KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 28, 2014

WAARABU WANAFUNGIKA-MKWASA



KOCHA Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi chao kina kila sababu ya kushinda mchezo wao wa michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mkwasa alisema baada ya kuishuhudia Al Ahly ikicheza na Sfaxien ya Tunisia mjini Cairo, ana hakika Yanga itashinda mechi hiyo.

Yanga inatarajiwa kuvaana na Al Ahly keshokutwa katika mechi ya awali ya raundi ya pili itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye mjini Cairo.

Boniface alikwenda Misri wiki iliyopita kwa lengo la kuichunguza Al Ahly inavyocheza mechi za nyumbani, mbinu zake za nje ya uwanja na uwezo wa timu nzima.

Kocha huyo aliishuhudia timu hiyo ikiichapa Sfaxien mabao 3-2 katika mechi ya fainali ya kuwania Kombe la Super, ambayo huzikutanisha bingwa wa ligi ya mabingwa wa Afrika na mshindi wa Kombe la Shirikisho.

"Tuna uwezo mkubwa wa kuifunga Al Ahly kwa sababu kikosi chetu kwa sasa ni kizuri na kinaundwa na wachezaji wengi wenye kiwango cha juu,"alisema.

Alizitaja sababu zingine zitakazoiwezesha Al Ahly kushinda mechi hiyo kuwa ni umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa wanachama, mashabiki na viongozi wa Yanga.

Mkwasa alisema kwenda kwake Misri na kuishuhudia Al Ahly ikicheza na Sfaxien, kumemwezesha kubaini kasoro nyingi zilizoko kwenye kikosi hicho cha waarabu na mbinu wanazopaswa kutumia ili kushinda mechi zote mbili.

"Zipo mbinu nyingi tunazoweza kuzitumia kuwashinda, lakini siwezi kuzizungumza, lakini nilichoweza kugundua ni kwamba wanafungika. Tutazitumia kasoro walizonazo kupata ushindi,"alisema.

Mkwasa alisema jambo muhimu kwa wachezaji wa Yanga ni kucheza kwa ari na kujituma na kuondoa hofu inayoweza kujengeka miongoni mwao kutokana na kupambana na mabingwa hao wa Afrika.

No comments:

Post a Comment