KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, February 28, 2014

NYOTA WA HOTELI RWANDA AMZIMIA GENEVIEVE NNAJI





LAGOS, Nigeria

HAKEEM Kae-Kazim ni mcheza filamu wa Nigeria mwenye uraia wa Uingereza, ambaye alijipatia sifa na umaarufu mkubwa mwaka 2004 kwa kuigiza kama Georges Rutaganda katika filamu ya Hotel Rwanda, iliyoshinda tuzo lukuki.

Mnigeria huyo, aliyezaliwa Oktoba Mosi, 1962, amecheza filamu nyingi zilizotengenezwa Hollywood, zikiwemo 24, aliyoigiza kama Kanali Ike Dubaku na tamthilia ya Redemption.

Kwa upande wa filamu za Kinigeria, ameshiriki kucheza chache kama vile Last Flight To Abuja na Half Of A Yellow Sun.

Akihojiwa na mtandao wa naijerules wa Nigeria hivi karibuni, Hakeem alielezea mambo mbalimbali kuhusu kazi yake, maisha ya familia na mengineyo. Yafuatayo ni mahojiano hayo ya ana kwa ana.

SWALI: Unajisikiaje kuishi sehemu kubwa ya maisha yako nje ya Nigeria?

JIBU: Ni jambo zuri, lakini kwangu naona la kawaida. Hakuna kitu maalumu hasa, na kama unavyofahamu mimi ni Mnigeria na ninatumia jina la Kinigeria. Lakini sifikirii iwapo nilikosa chochote kwa sababu hadi miaka miwili iliyopita, nimekuwa na kawaida ya kuja kusherehekea sikukuu ya Krismas hapa Nigeria. Napenda vyakula vya asili, napenda mavazi yetu ya asili.

SWALI: Kwa maana hiyo, huwa unakuja kuitazama familia yako wakati wa Krismas?

JIBU: Ndio, huwa nakuja kumtazama mama kwa sababu nilikuwa na umri wa miaka miwili wakati wazazi wangu waliponichukua mimi na kaka yangu mkubwa kwenda Uingereza na tangu wakati huo, tumekuwa tukiishi huko. Lakini kwa sasa baba yangu ni marehemu na mama yangu amekuwa akisafiri mara kwa mara kati ya Nigeria na Uingereza, lakini kaka yangu mkubwa yuko Uingereza pamoja na familia yake. Mimi natoka Abeokuta hivyo huwa natembelea huko mara kwa mara kwenda kumuona mama yangu.

SWALI: Ulianzaje kazi ya uigizaji?

JIBU: Nilianza kwa kujifunza sanaa za maonyesho na baada ya hapo, nikawa nashiriki kufanya maigizo ya kwenye steji Uingereza. Baadaye nilihamia Afrika Kusini na kucheza filamu nyingi pamoja na matangazo ya biashara katika televisheni ya Afrika Kusini. Baada ya kutoka Afrika Kusini, nilihamia Marekani, ambako naishi sasa, nikiwa naendelea kufanya kile ninachokipenda, uigizaji wa filamu.

SWALI: Umeshiriki kucheza filamu nyingi zilizotamba kama vile Hotel Rwanda na 24, ipi iliyokuletea mafanikio makubwa?

JIBU: Kila moja ni nzuri kutokana na utayarishaji wake. 24 ilikuwa filamu bomba na baadaye Hotel Rwanda, ambayo nilifurahia kushiriki kuicheza. Baadaye nilicheza filamu ya X-Men Origins, Wolverine na Pirates of the Caribbean.

SWALI: Nafikiri haikuwa kazi rahisi. Ni changamoto zipi ulizokumbana nazo ukiwa mwafrika uliyejitosa Hollywood?

JIBU: Ni kweli, mwanzoni haikuwa kazi rahisi kwa sababu kuna wakati niliishiwa na kukosa hata pesa ya chakula. Kupata nafasi ya kucheza filamu pia ilikuwa changamoto kwa sababu hapa Nigeria, unakuwa na uhakika wa kupata muswada wa filamu, lakini haiko hivyo katika nchi kama Uingereza. Kama unapata nafasi ya kucheza filamu leo, huwezi kupata nyingine labda hadi baada ya miezi miwili au mitatu. Lakini yote kwa yote, nimepata uzoefu mzuri.

SWALI: Ulikuja Nigeria siku chache zilizopita na tayari umeshiriki kutengeneza tangazo la Etisalat ukiwa na Genevieve Nnaji. Unajisikiaje kupata nafasi ya kushirikiana naye katika kazi hiyo?

JIBU: Kusema kweli, Genevieve ni msichana mrembo na ni mzuri kwa kila anachokifanya. Hivyo nilipata faraja kufanya naye kazi pamoja.

SWALI: Kama ni mzuri kiasi hicho, unafikiri anaweza kupata nafasi ya kuingia Hollywood?

JIBU: Inategemea na nafasi itakayomjia na namna atakavyojiandaa kuipokea. Kama atapata nafasi nzuri na kucheza filamu yenye kiwango cha kimataifa, anaweza kukipata kile anachokitarajia na kutambulika kimataifa.

SWALI: Ni kitu gani kingine kilichokufanya uje Nigeria?

JIBU: Mbali na tangazo la Etisalat, pia nimekuwa nikifanya kazi kwa kushirikiana na baadhi ya waongozaji filamu wa Nigeria kuhusu jinsi ya kukuza kiwango cha filamu za Nollywood ili kilingane na ladha ya kimataifa. Hivyo najiandaa kufungua shule ya kimataifa ya uigizaji filamu, ambayo watu wetu watapata mafunzo.

SWALI: Unayo mipango yoyote ya kucheza filamu ya Kinigeria hivi karibuni?

JIBU: Hapana

SWALI: Kwa nini miswada yetu ya filamu haikuvutii?

JIBU: Nollywood bado inakua na bado haijafikia kiwango cha kimataifa katika masuala ya uongozaji na utayarishaji. Lakini wapo waongozaji wachache wa filamu Nollywood, ambao wana mtazamo sawa na wa kwangu na nimewahi kufanyanao kazi siku za nyuma.

Nimefanya kazi na Tunde Babalola katika filamu ya Last Flight To Abuja, iliyotengenezwa Uingereza. Ni mtu mwenye mtazamo chanya katika masuala ya filamu. Pia nimecheza filamu ya Half Of A Yellow Sun.

Hivyo kama nitapata watu kama yeye na miswada mizuri, kwa nini nisicheze filamu za Kinigeria. Wakati umefika kwetu kuanza kutengeneza filamu zinazoelezea habari zetu na historia yetu. Hatupaswi kusubiri watu wengine watuelezee habari zetu kwa sababu wataeleza visivyo. Tunao watu mashuhuri kama vile Sango, Nnamdi Azikiwe, Awolowo na wengine. Tunahitajika kutengeneza filamu za kihistoria kuhusu wao.

SWALI: Kwa kawaida, wacheza filamu huwa ni watu wa kuhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Unawezaje kuwa na muda wa kufurahi na familia yako?

JIBU: Ninaye mke mwelewa pamoja na watoto watatu. Anaelewa aina ya kazi ninayoifanya na kunisaidia katika mambo mengi.

SWALI: Huwa halalamiki?

JIBU: Ni kweli huwa analalamika kwa sababu muda mwingi nakuwa safarini. Anatoka Afrika Kusini na huko ndiko nilikokutana naye. Tulifunga ndoa na nilikwenda naye Uingereza.Jambo la kufurahisha ni kwamba, kwa sasa natengeneza filamu nyingi Afrika Kusini na mtoto wangu wa mwisho bado hajafikisha umri wa miaka miwili. Lakini nimekuwa nikimuona na kuzungumza naye kupitia mtandao wa Skype kila ninapokuwa sipo nyumbani.

SWALI: Nina hakika unao mashabiki wengi wa kike. Unawezaje kushirikiana nao?

JIBU: Ni kweli ninao mashabiki wengi wa kike, lakini kuna muda maalumu kwa kila kitu. Ninao muda wa kukutana na rafiki zangu, familia na mashabiki wangu, hivyo siwezi kuacha muda huo uingiliane na mwingine. Siku zote huwa napenda kuwajulisha mashabiki wangu wa kike kwamba, nimeoa, hivyo siwaruhusu wawe karibu na mimi bila sababu.
SWALI: Umewahi kukumbana na tukio lolote la kufedhehesha kutoka kwa shabiki wa kike?
JIBU: Ndio, kuna mmoja tulikutana nilipopanda treni akaniona. Akaanza kupiga kelele na kulitaja jina langu. Alitaka kumfanya kila mtu afahamu kwamba mimi ndiye Hakeem na nimecheza filamu fulani na fulani. Lilikuwa tukio la kufedhehesha sana.

No comments:

Post a Comment