KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 3, 2014

TARIMBA KUONGOZA KAMATI YA NIDHAMU TFF



KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefanya uteuzi wa wajumbe kuunda kamati mbili za awali za haki, na kamati mbili za rufani za vyombo hivyo.

Rais wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria ataongoza Kamati ya Nidhamu. Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Wakili Jerome Msemwa (Makamu Mwenyekiti), Kassim Dau, Nassoro Duduma na Kitwana Manara.
 Kamati ya Rufani ya Nidhamu inaendelea kuongozwa na Profesa Mgongo Fimbo wakati makamu wake ni Wakili Hamidu Mbwezeleni. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Titus Bandawe, Twaha Mtengera na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) mstaafu Boniface Mpaze.

Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria anaongoza Kamati ya Maadili. Wajumbe ni Wakili Ezekiel Maganja, Wakili Victoria Mandari, Kanali mstaafu Enos Mfuru na Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Said Mtanda.

Kamati ya Rufani ya Maadili inaundwa na Jaji mstaafu Stephen Ihema (Mwenyekiti), Wakili Alesia Mbuya (Makamu Mwenyekiti), Lilian Kitomari, Jabir Shekimweri na Chabanga Hassan Dyamwale.

Wakati huo huo: TFF imeagiza kifanyike kikao cha dharura kati ya Sekretarieti ya TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na benki ya CRDB ili kutathimini maendeleo ya matumizi ya tiketi za elektroniki.

Lengo la kikao hicho ni kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa mfumo huo wa tiketi za elektroniki ni kutafuta ufumbuzi pamoja changamoto zake.

Viwanja vinane nchini vimefungwa mfumo huo wa tiketi za elektroniki. Viwanja hivyo ni Uwanja wa Azam uliopo Chamazi, Uwanja wa Kaitaba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Uwanja wa Mkwakwani, na CCM Kirumba.

Katika hatua nyingine, TFF imeiagiza Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ifanyie marejeo (review) uamuzi wake wa kuagiza mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) irudiwe mkoani Tabora.

Maagizo hayo yametolewa na Kamati ya Utendaji iliyokutana jana (Februari 1 mwaka huu) baada ya kupokea vielelezo vipya kuhusiana na mechi hiyo iliyochezwa Novemba 22 mwaka jana mjini Shinyanga.

Mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ilivunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada ya kupigwa na wachezaji wa Kanembwa JKT.

Pia Kamati ya Nidhamu ya TFF inatarajiwa kukutana wiki ijayo kujadili tukio hilo la Shinyanga wakiwemo wachezaji wanane wa Kanembwa JKT waliripotiwa kumpiga mwamuzi wa mechi hiyo.

No comments:

Post a Comment