Makore Mashaga, amechaguliwa tena kuwa katibu mkuu BFT
NA AMINA ATHUMANI, BAGAMOYO
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), uliofanyika juzi kwenye hoteli ya Palm Tree mjini hapa, uligubikwa na vurugu za hapa na pale na kusababisha kushindwa kupatikana kwa rais wake.
Vurugu hizo zilizuka baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Jamal Rwamboh kumwengua Mutta Lwakatare kugombea nafasi ya urais kwa madai kuwa, hakuwa na vigezo.
Lwakatare alikuwa akiwania nafasi hiyo pamoja na mgombea mwingine, Andrew Kuyeiyana, ambaye licha ya kupitishwa, hakuambulia kura hata moja baada ya kupigiwa kura za kumkataa.
Chanzo cha vurugu hizo ni kamati ya uchaguzi kufanya usaili kwa wagombea, nusu saa kabla uchaguzi kufanyika na hivyo kuwakosesha nafasi ya kukata rufani wagombea walioenguliwa.
Baadhi ya wapambe wa Lwakatare, walipinga sababu zilizotolewa na kamati hiyo katika kuliengua jina lake na kuvamia meza kuu. Hata hivyo, Rwamboh alishikilia msimamo wake.
Rwamboh aliamuru wajumbe wa uchaguzi huo kupiga kura za ndio na hapana katika nafasi hiyo baada ya kumpitisha Kuyeiyana kuwa mgombea pekee. Kuyeiyana ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF tawi la Dodoma.
Hata hivyo, katika kura hizo, Kuyeiyana aliambulia patupu baada ya kupigiwa kura nyingi za hapana na hivyo kusababisha nafasi hiyo ikose mshindi.
Katika nafasi ya makamu wa rais, mgombea pekee Wililo Lukelo aliibuka mshindi baada ya kupata kura nyingi wakati nafasi ya katibu mkuu ilichukuliwa tena na Makore Mashaga.
Katika nafasi ya mweka hazina, Ntava Kapanda aliibuka kuwa mshindi wakati waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji ni Salum Viduka, Aisha Voniatis, Zuwena Kipingu, Restuta Bura, Juma Bugingo, Said Omari, Mwinyikheri Said na Athony Mwang'onda.
Baada ya uchaguzi huo kumalizika, Makamu wa Rais wa BFT, Wililo, anayekaimu nafasi ya rais alisema, kamati ya utendaji inatarajiwa kukutana leo kujadili uchaguzi mdogo wa nafasi hiyo.
Baadhi ya wagombea walioshinda, walilalamikia mfumo uliotumika kuendesha uchaguzi huo kwa madai kuwa, haukuwa mzuri kutokana na kuwanyima fursa ya kukata rufani wagombea walioenguliwa kwenye usaili.
"Mimi ni mara ya kwanza kuona usaili unafanyika muda mmoja na uchaguzi. Hakuna katiba ya chama chochote inayosema hivyo kwani usaili hufanyika siku moja kabla ili kutoa nafasi kwa walioenguliwa kukata rufani,"alisema Viduka.
Aliongeza kuwa, wajumbe wa kamati ya uchaguzi kutoka Baraza la Michezo Taifa (BMT), walichangia kuutia doa uchaguzi huo kutokana na kushindwa kufuata katiba ya BFT katika kuusimamia.
Uchaguzi wa BFT ulifanyika kwa ufadhili wa Lwakatare, aliyegharamia malazi na chakula kwa wagombea na wapiga kura wote. Awali, uchaguzi huo ilikuwa ufanyike Oktoba mwaka huu, lakini ilishindikana kutokana na ukosefu wa fedha.
No comments:
Post a Comment