'
Monday, December 2, 2013
KOCHA MZUNGU WA SIMBA AANZA KIBARUA
UONGOZI wa klabu ya Simba, jana ulishindwa kumtambulisha kocha mpya wa timu hiyo, Zdravko Lugarusic kutoka Serbia na kipa Yaw Berko kutoka Ghana.
Simba ilipanga kuwatambulisha Lugarusic na Berko kwa waandishi wa habari leo, baada ya wote wawili kutua nchini juzi tayari kwa kuanza kuitumikia timu hiyo.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, utambulisho huo umefutwa kutokana na sababu za kiusalama.
Kamwaga alisema kutokana na kuwepo kwa makundi mawili ya uongozi yanayopingana ndani ya klabu hiyo, waliona isingekuwa busara kufanya utambulisho huo kwa hofu ya kutokea vurugu.
Badala yake, Kamwaga alisema Lugarusic alitarajiwa kuanza kibarua chake jioni kwenye mazoezi ya timu hiyo, yaliyopangwa kufanyika kwenye uwanja wa Kinesi ulioko Manzese, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamwaga, tayari kocha huyo pamoja na kipa Berko wameshaingia mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miezi sita kila mmoja. Walitia saini mikataba hiyo jana, mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope.
Lugarusic anachukua nafasi ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio', ambao walisimamishwa na kamati ya utendaji wakati Berko anachukua nafasi ya Abel Dhaira kutoka Uganda.
Uhuru ilipofika kwenye uwanja wa Kinesi jioni, ilimshuhudia kocha huyo akianza kazi ya kukinoa kikosi hicho huku Berko naye akifanya mazoezi ya ukipa. Pia walikuwepo wachezaji wengine kadhaa waliosajiliwa na Simba msimu huu.
Mazoezi hayo ya Simba pia yalishuhudiwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Joseph Itang'are, maarufu kwa jina la Kinesi, ambaye alifanya mazungumzo na wachezaji kabla ya kumtambulisha kocha mpya pamoja na Berko. Kiongozi mwingine aliyekuwepo kwenye mazoezi hayo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala.
Uhuru pia ilimshuhudia mchezaji mwingine mpya, Kika Musembi kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye alisema amekuja kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, lakini kutokana na kuzuka kwa mgogoro, ameambiwa asubiri.
Kabla ya kuja Simba, Lugarusic alikuwa akiifundisha Gor Mahia ya Kenya wakati Berko aliachwa na Yanga msimu uliopita kutokana na kutokuelewana na viongozi wa klabu hiyo. Berko alianza kuidakia Yanga mwaka 2010, Liberty Proffessionals ya Ghana.
Berko aliletwa nchini na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia, Kostadin Bozidar Papic, ambaye alimuona mlinda mlango huyo wakati anafundisha Hearts Of Oak ya huko mwaka 2008.
Ujio wa Lugarusic na Berko, huenda ukazua mtafaruku mwingine Simba, kufuatia kuwepo kwa makundi mawili ya uongozi yanayopingana.
Awali, Kamati ya Utendaji ya Simba, ilitangaza kumsimamisha uongozi, Mwenyekiti Ismail Aden Rage na makocha Kibadeni na Julio, lakini mapinduzi hayo yalipingwa na Rage na Baraza la Wadhamini.
Rage alitamka hadharani kwamba, bado anawatambua Kibadeni na Julio kuwa makocha wa timu.
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa dharula wa wanachama ndani ya siku 14 ili kuzungumzia mgogoro huo kwa lengo la kuupatia ufumbuzi.
Lakini Rage amepinga agizo hilo la TFF kwa kusema kuwa, haina mamlaka ya kumtaka aitishe mkutano huo. Alisema kikatiba, mwenyekiti wa klabu ndiye anayepaswa kuitisha mkutano mkuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment