KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 24, 2013

MALINZI AIPANGUA TFF





SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemuajiri Katibu wa zamani wa klabu ya Yanga SC, Celestine Mwesigwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa shirishiko hilo.

Taarifa ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi imesema kwamba, Mwesigwa amekidhi sifa za nafasi hiyo, akiwa na kiwango cha elimu ya Shahaha ya Uhusiano wa Kimataifa na Stashahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, TFF pia imemuajiri katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF- ambaye ana Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia na Shahada ya Uzamili ya uongozi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha ESAMI.

Jamal Malinzi amemuajiri Mwesigwa kuwa Katibu mpya TFF anarithi nafasi ya Angetile Osiah

Malinzi amesema, Iddi Mshangama atakaimu ya nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano ya TFF, iliyokuwa inashikiliwa na Saad Kawemba, wakati Danny Msangi atakaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha na Utawala TFF na Boniphace Wambura Mgoyo ataendelea kuwa Ofisa Habari wa shirikisho.

Malinzi aliyesema ajira zote zitaanza rasmi Januari 1 mwakani, pia ameteua Kamati tatu, ya Uchaguzi, Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF nay a Soka ya Ufukweni.

Kamati ya Uchaguzi itakuwa chini ya Mwenyekiti, Wakili Melchesedek Lutema, Makamu wake Wakili Walter Chipeta na Wajumbe Hamidu Mahmoud Omar, Jeremiah John Wambura na Hassan Daalal.

Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF itakuwa chini ya Mwenyekiti Wakili Julius Lugaziya, Makamu wake Wakili Mwita Mwaisaka na Wajumbe Juma Abeid Khamis, Rashid Dilunga na Masoud Issangu, wakati Kamati ya Soka ya Ufukweni itakuwa chini ya Mwenyekiti Ahmed Mgoyi na Wajumbe Deo Lucas, Juma Mgunda, Boniphace Pawasa, Joseph Kanakamfumu na John Mwansasu

Monday, December 23, 2013

YANGA YAMTUPIA VIRAGO BRANDTS



KLABU ya Yanga imetangaza rasmi kumtimua kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts pamoja na benchi lote la ufundi.

Uamuzi wa Yanga kumtimua kocha huyo umekuja siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1 na watani wao wa jadi Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdalla Ahmed Bin Kleb aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Brandts amepewa notisi ya mwezi mmoja kwa ajili ya kumaliza programu zake.
Bin Kleb alisema baada ya notisi hiyo kumalizika, kocha huyo atakuwa huru kwenda anakotaka.

Kwa mujibu wa Bin Kleb, sababu za kumuondoa kocha huyo ni kushuka kwa kiwango cha timu hiyo katika mechi za hivi karibuni na si kipigo cha Simba pekee.

“Kweli mwanzoni alipandisha kiwango cha timu, kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye,”alisema.

Bin Kleb alisema utaratibu wa kuwaondoa maofisa wengine wa benchi la Ufundi unaendelea na kwamba, tayari mipango imeshaanza kufanyika kwa ajili ya kusaka kocha mpya.

Wakati huo huo, Yanga imethibitisha ushiriki wa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayotarajiwa kufanyika Januari mwakani visiwani Zanzibar.
Mbali na kushiriki katika michuano hiyo, Yanga pia inatarajia kufanya ziara ya mafunzo katika moja ya nchi za Ulaya.

SIMBA, YANGA NANI MTANI JEMBE ZAINGIZA MIL 400/-



MECHI ya Nani Mtani Jembe kati ya Yanga na Simba iliyochezwa juzi (Desemba 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 422,611,000.


Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema kwamba mapato hayo ni kutokana na mashabiki 52,589 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 40,000. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 19,044.

Asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa kutokana na mapato hayo ni sh. 64,466,084.75 wakati gharama za kuchapa tiketi ni sh. 7,488,000.

Mgawo mwingine ilikuwa kama ifuatavyo; kila klabu imepata sh. 117,470,066.61, asilimia 15 ya uwanja ni sh. 52,598,537.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 35,065,691.53 wakati gharama za mchezo zilikuwa sh. 28,052,553.22.

Sunday, December 22, 2013

TFF YAJARIBU TIKETI ZA ELEKTRONIKI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa mechi mbili za majaribio ya matumizi ya tiketi za elektroniki zitakazochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi ya kwanza itakuwa Desemba 26 mwaka huu saa 10 jioni ambapo itazikutanisha timu za Azam na Ruvu Shooting. Mechi nyingine itachezwa Januari Mosi mwakani kwa kuzikutanisha Ashanti United na JKT Ruvu.

TFF tunatoa mwito kwa washabiki kujitokeza katika mechi hizo ambapo mbali ya kushuhudia burudani pia watajionea jinsi mfumo huo wa tiketi za elektroniki unavyofanya kazi.

Kwa kushirikiana na benki ya CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo ya tiketi za elektroniki, TFF imepanga vilevile kuandaa mechi nyingine majaribio mikoani kabla ya mfumo huanza kutumika rasmi Januari 25 mwakani katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

PINGAMIZI DIRISHA DOGO MWISHO DES 23
Desemba 23 mwaka huu ndiyo mwisho wa kipindi cha pingamizi kwa usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Katika VPL, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union ndiyo timu pekee kati ya 14 za ligi hiyo ambazo hazikuwasilisha maombi ya usajili katika dirisha dogo.

Ashanti United ndiyo inayoongoza kwa wachezaji 15 ambao ni Kassim Kilungo, Mohamed Banka, Bright Obinna, Victor Costa, Juma Mpongo, Juma Jabu, Ally Kondo, Shafii Rajab, Mohamed Faki, Abubakar Mtiro, Patrick Mhagama, Ally Kabunda, Hassan Kabuda, Idd Ally na Rahim Abdallah.

Ruvu Shooting; Ally Khan na Jumanne Khamis, Rhino Rangers; David Siame, John Kauzeni, Salum Mamlo, Jingo Seleman, Darlington Enyinna, Rajab Twaha, Godfrey Mobi na Mussa Digubike. Mbeya City; Saad Kipanga. Tanzania Prisons; Dennis Liwanda, Godfrey Pastory, Henry Mwalugala, Jamal Salum na Brayton Mponzi.

Oljoro JKT; Jacob Masawe, Mansour Ali, Juma Mohamed, Amour Mohamed, Mohamed Ali, Mussa Nahoda, Benedict Ngasa, Seleman Makame, Shija Mkina, Ali Omar na Shaweji Yusuf. Simba; Uhuru Selemani, Ivo Mapunda, Ali Badru, Awadh Juma, Donald Mosoti na Yaw Berko. Azam; Mouhamed Kone.

Yanga; Hassan Dilunga, Juma Kaseja na Emmanuel Okwi. Mgambo Shooting; Suleiman Khatib, Bolly Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali. JKT Ruvu; Chacha Marwa, Sino Augustino, Idd Mbaga na Cecil Luambano.

KAMATI YA UTENDAJI TFF DES 23
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jamal Malinzi.

Kikao hicho kitakachofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitapitia ajenda mbalimbali ikiwemo uundwaji wa vyombo vya haki (Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Maadili na Kamati ya Uchaguzi).

MANJI AWAFARIJI WANA-YANGA KIPIGO CHA SIMBA


MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Manji amesema kwamba hawakumsajili Juma Kaseja kwa ajili ya kuifunga Simba SC, bali wamemsajili awasaidie kwenye michuano ya Afrika.

Manji ameyasema hayo leo asubuhi makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, siku moja baada ya Yanga kufungwa 3-1 na Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Kaseja akiwa langoni.
Manji alikuwa akimjibu Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali aliyeushutumu uongozi kusajili Juma Kaseja ni makosa.

“Huyu mzee nadhani umri umemzidi, lakini nataka nimkumbushe, huyo Ivo Mapunda aliondoka Yanga akiwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi sita na uongzi wa wakati huo kwa tuhuma za kufungisha kwenye mechi na Simba SC,”.

“Lakini pia nataka nimuulize, wakati Simba inarudisha mabao yote matatu Kaseja alikuwapo langoni? Nadhani hivi vitu si vizuri, tuache kulaumiana tushikamane kwa mustakabali mzuri wa timu,”alisema Manji.

Manji amesema wanaheshimu uwezo wa Kaseja kwa sababu ndiye kipa aliyedaka mechi nyingi za mashindano ya Afrika kati ya makipa wote nchini, hivyo thamani yake haitashuka kwa kufungwa mabao matatu jana.

Pamoja na hayo, Manji amesema kwamba mechi ya jana haikuwa na uzito wowote kwao ni sawa na bonanza au fete, hivyo kufungwa haijawaumiza.

“Tuliamua kucheza kumfurahisha mdhamini TBL, tumefungwa lakini bado tunaongoza ligi, hatujapoteza pointi hata moja, ile ilikuwa fete tu,”alisema Manji.

Manji amekiri Simba SC walicheza vizuri zaidi jana na walistahili ushindi na anawapongeza kwa hilo, pamoja na wadhamini, TBL kwa kuandaa mechi hiyo.

Manji amesema kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika wataboresha timu na benchi la ufundi na timu itaenda tena kambini Ulaya, hivyo anaamini mwakani makali yao yatafufuka na watatetea ubingwa.

Saturday, December 21, 2013

CHEZEA SIMBA WEWEEEE








SIMBA SC ndiye Mtani Jembe 2013. Hiyo inafuatia Wekundu hao wa Msimbazi kuwafunga watani wao wa jadi, Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yamefungwa na Amisi Tambwe mawili na Awadh Juma moja, wakati la Yanga lilifungwa na Emmanuel Okwi.

Katika mchezo huo, Yanga ilimaliza pungufu baada ya beki wake, Kevin Yondan kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, baada ya kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’

Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yote yalifugwa na Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44.
Tambwe alifunga bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya kiufundi ya Said Hamisi Ndemla na kumtungua kipa Juma Kaseja.

Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Jonas Mkude aliyeinasa pasi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kuelekea kwa Frank Domayo, akampasia Henry Joseph ambaye alimpelekea Ndemla, aliyempa mfungaji.

Tambwe alifunga bao la pili kwa penalti baada ya beki wa Yanga, David Luhende kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyeingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Ndemla.

Kwa ujumla, Simba SC ndiyo waliocheza vizuri kipindi cha kwanza wakionana kwa pasi za uhakika, wakati wapinzani wao walikosa mbinu za kuipenya ngome ya Wekundu wa Msimbazi, iliyoongozwa na Mkenya Donald Mosoti Omwanwa.

Krosi nyingi za Mrisho Ngassa kutoka kulia ama zilidakwa na Ivo Mapunda au zilipitiliza nje.

Kipindi cha pili, Yanga SC walianza kwa mabadiliko, wakiingiza wachezaji watatu kwa mpigo, Emmanuel Okwi, Simon Msuva na Hassan Dilunga kuchukua nafasi za Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na Athumani Iddi ‘Chuji’.

Lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia Yanga SC kwani wapinzani wao Simba walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Awadh Juma.

Bao hilo lilitokana na makosa ya beki Mbuyu Twite kumrudishia mpira mfupi kipa Juma Kaseja, ambaye alijaribu kuuweka sawa, lakini akazidiwa na Awadh aliyeupokonya na kuusukumia nyavuni.

Baada ya bao hilo, Simba walianza kucheza kwa kujiamini zaidi wakipiga pasi za kusisimua na kuwafurahisha mashabiki wao, huku Yanga wakihaha kusaka bao la kufutia machozi.

Alikuwa Okwi aliyeifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 87, akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima.

Baada ya mchezo huo, Yanga walikabidhiwa Medali za Fedha Kombe dogo na hundi milioni 98.9, wakati wapinzani wao walivalishwa Medali za Dhahabu, Kombe kubwa na hundi ya Sh. Milioni 1 kutokana na promosheni ya Nani Mtani Jembe.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende/Oscar Joshua dk79, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Juma Abdul dk53, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Hassan Dilunga dk46, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu/Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete dk69 na Hamisi Kiiza/Emmanuel Okwi dk46.

Simba SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk55, Henry Joseph/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk34/Abdulhalim Humud dk72, Amisi Tambwe/Amri Kiemba dk54, Said Ndemla/Ramadhani Singano ‘Messi’dk27 na Awadh Juma   IMETOLEWA KWENYE BLOGU YA BIN ZUBEIRY

Sunday, December 8, 2013

KALALE PEMA MZEE MANDELA AKA MADIBA


MESSI, RONALDO, RIBERY HAPATOSHI TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA 2013



MADRID, Hispania
 ALIANZA kwa utani, lakini hakuwa na maana
hiyo pale Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya
(UEFA), Michel Platini, aliposema
waliongeza muda wa kupiga kura katika
mchakato wa kumpata mwanasoka bora wa
dunia, ili kumkosha Cristiano Ronaldo.
Baadaye, akadokeza tena kuwa, mchezaji wa
Hispania alistahili hasa kushinda tuzo ya
Ballon d'Or 2010 baada ya fainali za Kombe
la Dunia.
Hata hivyo, akashuka kwa kina kuwa, tuzo ya
kumpata mchezaji bora wa 2012/2013, ngumu
sana kwa sababu zinakutanisha wachezaji
mahiri ndiyo maana tabu kuchagua mshindi
kati yao.
Platini amesema kutokana na ugumu huo,tuzo
za safari hii zimeweka historia.
Wachezaji wanaominyana katika tuzo hiyo ni
Ronaldo wa klabu ya Real Madrid, Lionel
Messi wa Barcelona na Franck Ribery
anayekipiga Bayern Munich.
Messi aliisaidia Barcelona kutwaa ubingwa
wa Hispania 'La Liga' pamoja na kufunga
mabao matamu msimu uliopita, lakini Ronaldo
alikuwa msaada kwa Real Madrid, ingawa
hakupata nishani yoyote, wakati winga
Ribery aling'ara na Bayern Munich kwa
kuisaidia kubeba mataji matatu msimu wa
2012/2013.
Katika hayo, limo kombe la ligi ya mabingwa Ulaya.
Platini, ambaye aliwahi kunyakua tuzo ya
Ballon d'Or mara tatu, amesema hana
wasiwasi na kanuni za FIFA za kumpata
mchezaji mshindi.
Akasema kwa mzaha kuwa, muda wa kupiga kura
uliongezwa ili kumsafishia njia Ronaldo,
baada ya kuzozana hadharani na Rais wa FIFA
Sepp Blatter.
"Inavyoonekana Messi anawapiku Ronaldo na
Ribery," alisema.
"Wawili wa kwanza wanavutia na Ribery naye
ameshinda kila kitu.
"Ni wachezaji watatu walio bora. Kuchagua
mshindi wa Ballon d'Or mwaka huu ni ngumu
sana katika historia ya tuzo hii.
"Uamuzi wa kuongeza muda wa kupiga kura
ulikuwa wa FIFA, ingawa inaonekana chanzo
ni msukumo wa Ureno kufuzu Kombe la Dunia
kwa mabao matatu ya Ronaldo dhidi ya
Sweden,"alisema.
Aliongeza, huku anacheka: "Labda FIFA
imefanya hivi kumfurahisha Ronaldo."
Platini pia alishangaa kufuatia mchezaji wa
Hispania kukosa tuzo licha nchi hiyo kuwa
mabingwa wa dunia 2010, badala yake
Ballon d'Or ikaenda kwa Messi mara ya pili.
"Nashangaa kwa nini mchezaji wa Hispania
hakushinda," aliongeza Mfaransa huyo.
"Nakubali kuwa, mwaka 2010, tuzo ya Ballon
d'Or winner ilistahili kutwaliwa na
Mhispania.
"Andres Iniesta, Xavi na mwingine kwangu
mimi, mmojawapo alistahili kushinda. Messi
amenyakua ni bingwa mahiri. Lakini 2010,
tuzo ingekwenda kwa mchezaji kutoka Hispania."
Wakati hayo yakiendelea, bado kuna vita
kali kati ya Messi na Ronaldo kutokana na
wachezaji hao walivyochuana katika tuzo za
Hispania juzi.
Katika tuzo hizo, Ronaldo ameshinda ya
mchezaji mwenye thamani zaidi katika ligi
ya Hispania, huku Messi akitoka na 'zawadi'
mbili.
Messi amebeba tuzo ya mchezaji bora na
mshambuliaji bora wa ligi ya Hispania.
Angalau tuzo hiyo mpya ilimfurahisha
Ronaldo aliyekusanyika na wachezaji
mbalimbali na kupiga nao picha.
Miongoni mwa wachezaji hao ni mshambuliaji
wa Everton, Gerard Deulofeu, anayecheza kwa
mkopo katika timu ya daraja la pili, ambako
ameibuka mchezaji bora msimu uliopita na
kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois
aliyeshinda tuzo ya kipa bora.Kipa huyo anacheza
kwa mkopo Atletico Madrid.
Kudhihirisha kuwa homa ya tuzo hiyo ni
kubwa, wachezaji mashuhuri wametoa maoni yao
na kila mmoja akimpigia kifua amtakaye!
Ronaldo de Lima jana alisema, anadhani Messi
anastahili kushinda tuzo hiyo na kuwapiku 
Ronaldo na Ribery.
Alisema haoni sababu ya nyota huyo wa
Argentina kutabiriwa kuwa mshindi wa tatu.
"Nafikiri Messi atanyakua tena Ballon d'Or,"
Ronaldo aliliambia gazeti la Marca.
"Messi amecheza mechi nyingi katika miaka
mitano iliyopita ni mchezaji nyota katika
ulimwengu wa soka. Sasa, majeraha yake si
makubwa sana, huenda mapumziko yakampa muda
wa kuchaji makali yake."
Ronaldo aliyewahi kucheza Barcelona na Real
Madrid kwa nyakati tofauti, alishinda tuzo
ya Ballon d'Or mara mbili, baada ya
kung'ara 1997 na 2002.
Kipa wa Real Madrid, Iker Casillas amesema
kwa kizazi cha sasa, hajaona mchezaji bora kuliko wote duniani
zaidi ya Ronaldo.
"Kuna mchezaji aliye mbele ya wenzake wote,
mwenye kiwango cha kushangaza na anayestahili sifa zote, huyu si mwingine
bali ni Cristiano Ronaldo," alisema
Casillas, ambaye ni nahodha wa Real Madrid.
"Sifikiri kama kuna shaka kuhusu hilo na
ameonyesha hivyo kutoka mechi moja hadi
nyingine katika timu ya Madrid ni tumaini
na tunamshukuru, miezi michache ijayo
tutafanikisha malengo yetu mwaka huu.”
Casillas anaamini Ronaldo anaweza
kukiongoza kikosi cha Carlo Ancelotti
kutwaa mataji matatu msimu huu.
Sherehe za kumpata mshindi wa tuzo hiyo
zitafanyika Januari 13 mwakani, ambapo mchakato wa
kupiga kura ulifungwa Novemba 29 baada ya
kuongezwa muda wa wiki mbili.

TFF YATANGAZA NAFASI ZA KAYUNI NA KAWEMBA, IDARA ZAFANYIWA MAREKEBISHO


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza nafasi saba za kazi, ikiwemo ya katibu mkuu na mkurugenzi wa ufundi.
Nafasi zingine zilizotangazwa na TFF ni ya mkurugenzi wa fedha na utawala, mkurugenzi wa sheria na uanachama, mkurugenzi wa mashindano, meneja wa biashara na ofisa habari na mawasiliano.
TFF imetangaza nafasi hizo za kazi, kupitia kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kuwataka watu wenye sifa zinazotakiwa, kuwasilisha maombi yao kabla ya Desemba 15 mwaka huu.
Uamuzi wa TFF kutangaza nafasi hizo, umekuja siku chache baada ya shirikisho hilo kupata uongozi mpya, katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Jamal Malinzi alichaguliwa kuwa rais na Wallace Karia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.
Siku chache baada ya uchaguzi huo, kamati ya utendaji ya TFF iliamua kumpa likizo yenye malipo, aliyekuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah. Mkataba wa Angetile ilikuwa umalizike mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa sasa, nafasi ya katibu mkuu inashikiliwa kwa muda na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura.
Habari kutoka ndani ya TFF zimeeleza kuwa, uongozi mpya umeamua kuzifanyia marekebisho baadhi ya idara kwa lengo la kuongeza ufanisi, ambapo idara ya fedha imeunganishwa na utawala wakati idara ya utawala imeunganishwa na sheria.
Awali, idara ya fedha ilikuwa chini ya Yonaza Seleki na idara ya utawala ilikuwa chini ya Mtemi Ramadhani.
Kwa mujibu wa habari hizo, TFF pia imeamua kuunda idara mpya ya biashara, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama idara ya masoko.
Nafasi ya mkurugenzi wa ufundi kwa sasa inashikiliwa na Sunday Kayuni wakati  mkurugenzi wa mashindano ni Saad Kawemba.

SIMBA NIPENI HAKI YANGU-KIBADENI


KOCHA Mkuu wa zamani wa Simba, Abdalla Kibadeni ameutaka uongozi wa klabu hiyo kumlipa fedha anazodai mara moja.
Kibadeni amesema, anaukubali uamuzi wa kamati ya utendaji ya Simba, kumsimamisha kazi yeye na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio', lakini anaomba alipwe pesa zake.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Kibadeni alisema amepokea barua kutoka uongozi wa Simba kuhusu kusimamishwa kwake kwa madai kwamba, mwenendo wa timu katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu haukuwa mzuri.
"Wanasema uwezo wangu wa kufundisha ni mdogo. Mi sitaki kubishana nao kwenye hilo, isipokuwa watu wenye kujua ndio wanaweza kusema kama hilo ni tatizo.
Narudia kusema, nakubali kuachia ngazi ila nitashukuru wakinipatia haki yangu, ambayo nastahili kupata," alisema kocha huyo, ambaye ameingia mkataba wa kuifundisha Ashanti.
Kibadeni aliamua kuweka mambo hadharani kwa kusema, amekumbana na matatizo mengi wakati akiifundisha Simba, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu walioko nje ya uongozi, kutaka nafasi ya kuingia ndani ya timu.
"Kuna migogoro sana, hata mimi nimechoka hii kazi. Kubwa ilikuwa tuhakikishe kwamba timu inafanya vizuri ili badaye tuje kutafuta ubingwa. Nilikuwa na imani kwamba hata mwaka huu tungeweza kupata ubingwa kwa jinsi timu ilivyokua inakwenda," alisema Kibadeni.
"Tumecheza michezo 13 ya mzunguko wa kwanza, tumeshinda sita, tumetoka sare sita na kupoteza mchezo mmoja. Nafasi tuliyoipata ni ya nne katika michezo 13.
Katika hizo mechi 13, mimi nasema nafasi ya nne sio mahali pabaya kwa sababu timu ilicheza mechi 26 za ligi mwaka jana, ikamaliza nafasi ya nne," aliongeza kocha huyo.
Kamati ya Utendaji ya Simba, iliamua kuwasimamisha kazi Kibadeni na Julio mwishoni mwa mwezi uliopita kwa madai ya kutoridhishwa na ufundishaji wao.
Mbali na makocha hao, kamati hiyo pia ilitangaza kumsimamisha Mwenyekiti, Ismail Aden Rage kwa madai ya kutokuwa na imani na uongozi wake.
Hata hivyo, Rage alipinga uamuzi huo na kudai kuwa, kikao kilichopitisha uamuzi huo, kilikuwa batili kwa vile kikatiba, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kukiitisha. Aliitaja sababu nyingine kuwa ni kamati hiyo kushindwa kumpa nafasi ya kujieleza kuhusu tuhuma dhidi yake.
Kufuatia kuzuka kwa mgogoro huo, kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilimtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa dharula wa wanachama ili kujadili suala hilo na kulipatia ufumbuzi. Rage amegoma kuitisha mkutano huo na kwa sasa yuko nje ya nchi.

KILI STARS YALIPA KISASI KWA UGANDA, YATINGA NUSU FAINALI, ITAVAANA NA KENYA


KIPA Ivo Mapunda leo ameibuka shujaa baada ya kuokoa penalti mbili za Dani Sserunkuma na Khalid Aucho wa Uganda na kuipa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ushindi wa penalti 3-2 baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Manispaa, Mombasa, Kenya.
Mbali na kuokoa penalti hizo mbili, Uganda walipoteza penalti nyingine moja baada ya Godfrey Walusimbi kupiga nje, wakati Hamisi Kiiza Emannuel Okwi ndiyo pekee walioifungia Cranes penalti
Waliofunga penalti za Bara ni Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’na Erasto Nyoni, wakati Mbwana Samatta na Amri Kiemba walikosa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Wish Yabarow wa Somalia, aliyesaidiwa na KInde Mussa wa Ethiopia na Mohamed Idam wa Sudan, hadi mapumziko Stars ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1.
Mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Dani Sserunkuma alitangulia kuifungia Cranes bao dakika ya 16, baada ya kupokea krosi ya Hamisi Kiiza aliyemtoka Erasto Nyoni na kufumua shuti la chini lililompita kipa Ivo Mapunda. 
Dakika mbili baadaye, Mrisho Ngassa aliisawazishia Stars baada ya kuwazidi ujanja na maarifa ya kisoka mabeki wa Uganda, akimalizia mpira uliopigwa na Mbwana Ally Samatta.
Mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya DRC, aliangushwa chini nje kidogo ya eneo la hatari na mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa akaenda kupiga mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja kuipatia Stars bao la pili.
Baada ya bao hilo, Stars waliendelea kuishambulia Uganda kwa kujiamini zaidi, lakini mabeki wa Cranes walisimama imara kutoruhusu mabao zaidi.
Kipindi cha pili, Stars ilipata pigo dakika ya 53 baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kutolewa nje kwa nyekundu kwa kumchezea rafu Sserunkuma.
Uganda ikapata bao la kusawazisha dakika ya 73 kupitia kwa Martin Mpuga, aliyeunganisha kona ya Godfrey Walusimbi.
Kwa matokeo hayo, Stars inarudia kuingia Nusu Faniali kama mwaka jana, wakati Uganda wanaacha taji Mombasa na kurejea nyumbani, Kampala.    
Tanzania Bara; Ivo Mapunda, Michael Aidan, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi 80, Amri Kiemba, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Uganda; Benjamin Ochan, Nico Wadada, Muga Martin, Geoffrey Kizito/Said Kyeyune dk64, Godfrey Walusimbi, Kasaga Richard, Khalis Aucho, Mpande Joesph/Brian Majwega dk46, Daniel Sserunkuma, Hamisi Kiiza na Emmanuel Okwi.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

TANZANITE YAPIGWA 4-1 NA AFRIKA KUSINI



TIMU ya soka ya Taifa ya wanawake ya vijana wa chini ya miaka 20, Tanzanite imejiweka kwenye mazingira magumu ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Afrika Kusini.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Tanzanite ilicheza hovyo tangu mwanzo wa mchezo na kuwakatisha tamaa mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo.
Iliwachukua Afrika Kusini dakika nne kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Amogelang Motay kabla ya Tanzanite kusawazisha dakika ya 13 kupitia kwa Theresa Yohana.
Afrika Kusini iliendeleza kasi ya mchezo na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 17 kupitia kwa Shiwe Nogwanya. Timu hizo zilikwenda mapumziko Afrika Kusini ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Mabao mengine ya Afrika Kusini yalifungwa na Mosili Makhoali, dakika ya 61 na 78.
Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo mjini Johannesburg. Ili isonge mbele, Tanzanite itahitaji ushindi wa mabao 4-0.
Kocha wa Tanzanite, Rogasiun Kaijage alikiri baada ya mchezo huo kuwa, vijana wake walizidiwa kimchezo na Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Fenella Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzanite kuacha kulia, badala yake wawe jasiri na kujiandaa vyema kushinda mechi ya marudiano.
Alisema Tanzanite ilicheza vizuri kutokana na maandalizi iliyoyafanya, lakini wapinzani wao walicheza vizuri zaidi ndio sababu waliibuka na ushindi.

Wednesday, December 4, 2013

KILI STARS YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA CHALENJI


Na Sophia Ashery, Nakuru
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imefuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Chalenji, baada ya kuichapa Burundi bao 1-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Afrah mjini hapa, bao pekee na la ushindi la Kilimanjaro Stars lilifungwa na Mbwana Samata, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Samata alifunga bao hilo dakika ya saba baada ya kuunganisha wavuni kwa kiki kali, mpira wa krosi uliopigwa na Salum Abubakar 'Sure Boy' kutoka pembeni ya uwanja.
Kwa matokeo hayo, Kilimanjaro Stars imemaliza mechi za kundi lake ikiwa na pointi saba na sasa itakutana na timu ngumu ya Uganda katika mechi ya robo fainali.
Kilimanjaro Stars ilianza kubisha hodi kwenye lango la Burundi dakika ya pili wakati Mrisho Ngasa alipoingia na mpira ndani ya mita 18, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Arkazar Athur wa Burundi.
Kilimanjaro Stars ilifanya mashambulizi mengine mawili ya nguvu dakika ya 14 na 23, lakini shuti la Himid Mao lilimbabatiza beki mmoja wa Burundi na mpira kutoka nje wakati shuti la Thomas Ulimwengu liligonga mwamba wa goli kabla ya mpira kuokolewa na kipa Arthur wa Burundi.
Burundi nusura ipate bao dakika ya 27 wakati Ndikumana Yussuf alipopewa pasi na kubaki ana kwa ana na kipa Ivo Mapunda wa Kilimanjaro Stars, lakini shuti lake lilimlenga kipa huyo.
Kilimanjaro Stars ilijibu shambulizi hilo dakika ya 28 baada ya Samata kupewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilimlenga kipa Arthur.
Sure Boy angeweza kuifungia bao Kilimanjaro Stars dakika ya 35 baada ya kupokea krosi maridhawa kutoka kwa Samata, akaingia na mpira ndani ya eneo la hatari la Burundi, lakini shuti lake lilitoka nje ya goli. Timu hizo zilikwenda mapumziko Kilimanjaro Stars ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikihaha kusaka bao. Katika mashambulizi hayo, Amri Kiemba alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao Kilimanjaro Stars dakika ya 58, lakini shuti lake lilipaa juu.
Kilimanjaro Stars ilipata nafasi zingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 76, 80 na 83, lakini mshuti ya Samata na Ulimwengu, aidha yaliishia mikononi mwa kipa Arhur ama kutoka nje ya lango.
Kili Stars: Ivo Mapunda, Erasto Nyoni, Himid Mao, Said Morad, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakari, Mbwana Samata, Mrisho Ngasa, Thomas Ulimwengu na Amri Kiemba/Haruna Chanongo.
Burundi: Arakazar Athur, Hakizimana Issa, Hererimana Rashid, Nsabiyumva Fredrick, Nduwimana Jean, Ndikumana Yussuf,  Duhayinavyi Gael, Nduwarugira Christopher, Habonimana Celestin na Hussein Shabaan

NITAACHA UTUKUTU- BALOTELLI


MILAN, Italia
MSHAMBULIAJI mkorofi wa AC Milan, Mario
Balotelli, amesema atafanya kila awezalo
ili kuhakikisha anadhibiti hasira zake
uwanjani na hana mpango wa kuondoka San
Siro.
Nyota huyo, msimu huu amekumbwa na matukio
ya ugomvi katika mechi mbalimbali, ikiwemo
kutaka kuzichapa na Nicolas Spolli kwa
madai ya kumtolea maneno ya ubaguzi wa
rangi, AC Milan ilipocheza na  Catania.
Hata hivyo, beki huyo alisafishwa na kamati
ya nidhamu kwa madai kwamba, hakutenda kosa kinyume na
ilivyokuwa imeelezwa.
Balotelli alionyesha kuchukizwa na uamuzi
huo kwa kukebehi kupitia mtandao wa
twitter, akiandika: "Hahaha! Bahati mbaya, kuna haki
katika nchi hii."
Baada ya hapo, mshambuliaji huyo wa zamani
wa Manchester City, aliweka wazi kuwa
anataka kubadilika,na kuthibitisha kuwa
habanduki katika timu ya AC Milan.
"Kulinganisha na wakati uliopita, vitu
vingi vimebadilika, nitajaribu kubadili
tabia kabisa. Lakini nitabaki," Balotelli
aliliambia jarida la Buone Notizie.
"Nimeweka akilini mwangu mapokezi mazito
niliyopata kutoka kwa mashabiki wakati
nilipojiunga na timu hii," aliongeza.
Balotelli aliendelea kupongeza weledi wa
makocha waliomfundisha tangu alipoanza soka
hadi sasa, kwa kueleza kuwa, wamechangia
maendeleo yake licha ya kuwa na mbinu
tofauti za ufundishaji.
"Kila mmoja amekuwa na mbinu tofauti.
Roberto Mancini amekuwa kama baba, Jose
Mourinho ni mhamasishaji bora na
Massimiliano Allegri, anapenda mshikamano
katika timu," aliongeza Balotelli.

NATAKA UBINGWA-MOURINHO


LONDON, England
JOSE Mourinho, amewataka wachezaji wa
Chelsea wawe na akili ya kutwaa
ubingwa wa ligi kuu ya England.
Kocha huyo wa Chelsea, alirudi Stamford
Bridge, Juni mwaka huu, baada ya kuiongoza
klabu hiyo kubeba ubingwa wa England mara
mbili alipotua kwa mara ya kwanza.
"Kuna maendeleo mengi yamepatikana,"
alisema kocha huyo Mreno, ambaye sasa
kikosi chake kipo nafasi ya pili nyuma ya
Arsenal.
"Kuna vitu katika kazi si rahisi na
kimojawapo ni cha kujenga presha ya kupigania
ubingwa."
"Tuna baadhi ya wachezaji waliotwaa ubingwa
kabla, lakini hawajaupata kwa muda mrefu na
ikitokea kuutwaa, wanasahau," alisema.
"Tuna wachezaji wengine waliokuwa wanacheza
katika klabu tofauti, lakini si kwa sababu ya
kutaka mataji,"aliongeza.
Alisema utamaduni wa kutaka timu iongoze
katika ligi, ikiwemo kupigana mwanzo hadi
mwisho kwa kutambua kila hatua ni muhimu
kwa sababu inaweza kuleta tofauti, inapaswa
kuwa sehemu ya maisha ya wachezaji wake.
"Ni mchakato. Si kitu unachoweza
kukifanya kwa kubonyeza. Nataka wafikiri kama
ninavyofikiri. Katika kazi yangu, napenda
kumaliza wa kwanza au nafasi ya pili na
nikishindwa nakosa raha," alisisitiza.
Chelsea jana ilicheza na Sunderland, huku
ikiwa imepitwa alama nne na vinara Arsenal.
Hata hivyo, Mourinho ametabiri timu sita
zinaweza kuwa bingwa wa England na
kuonya kuwa, Tottenham na Manchester United
hazitaendelea kufanya vibaya kwa vile zina
muda mwingi wa kurekebisha makosa.
Spurs inapitwa alama 10 na Arsenal, wakati
United imezidiwa pointi tisa na washika
bunduki hao.
"Kwa hatua hii, Spurs na Man United
zinatambua hatua inayofuata ni kupunguza
pengo la pointi kutoka 10 hadi saba (nyuma
ya vinara Arsenal) au kutoka tisa mpaka
sita ndipo zitakuwepo kwenye mbio za
ubingwa,"alisema.
"Pia nafikiri wanajua hatua inayofuata
wakipitwa kutoka pointi 10 hadi 13 au tisa
mpaka 12, mambo yatakuwa magumu,"alisisitiza kocha huyo.
 "Kwa sasa, timu kama Arsenal hazina presha
kwa sababu zikipigwa moja, hakuna
kinachowaathiri. Baadhi zinafahamu
zikianguka, hali itakuwa tete," alisema.

MATAJIRI YANGA WAMFUNGIA SAFARI OKWI



WAJUMBE wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Yanga,
Seif Ahmed 'Magari' na Abdalah Bin Kleb wametua
mjini Nakuru kwa ajili ya kusaka wachezaji.
Seif na Bin Kleb, waliwasili Nakuru jana asubuhi na kusema
kuwa, wamekuja kuwafuatilia wachezaji watatu.
Bin Kleb, aliwataja wachezaji hao kuwa ni Emmanuel Okwi,
Daniel Ssenkuruma wa Uganda na Abdul Razak Fiston wa Burundi.
Alisema walipata taarifa za wachezaji hao kutoka
kwa mmoja wa mawakala, ambaye yupo mjini hapa
kufuatilia wachezaji.
Aliongeza kuwa, ujio wao nchini Kenya umelenga kuwaona kwa
macho wachezaji hao na pia kutathmini uwezo wao kabla ya
kuamua kuwasajili.
Bin Kleb alikiri kuwa, kwa muda mrefu Yanga imekuwa na
shauku ya kutaka kumsajili Okwi, ambaye
anamaliza mkataba na klabu yake ya sasa Februari
mwakani.
Alisema kama wataridhika na viwango vya
wachezaji hao, watakuwa tayari kumwaga mamilioni ya
fedha ili waweze kuwasajili.
"Tunachotaka ni kupata wachezaji wazuri na kila
wakala tuliyemuuliza kuhusu wachezaji hao,
aliwamwagia sifa na sasa tumekuja ili kuhakikisha
viwango vyao," alisema Bin Kleb.
Viongozi hao wa Yanga watapata nafasi ya
kumuona Abdul Razak Fiston wa Burundi wakati
timu yake itakaposhuka dimbani kuumana na
Kilimanjaro Stars katika mchezo uliochezwa jana
kwenye uwanja wa Afraha, Nakuru.
Okwi na Ssenkuruma wataonekana leo wakati timu yao ya Uganda
itakapoikabili Sudan.

YAYA TOURE: ASANTENI


LONDON, England
KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City ya England, Yaya Toure amewashukuru mashabiki kwa kumchagua kuwa mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika ya BBC.

Toure (30), ambaye aliteuliwa kuwania tuzo hiyo kwa miaka minne mfululizo, alitangazwa kuwa mshindi juzi baada ya kuwabwaga wanasoka wenzake wanne waliofuzu kuingia fainali.

Wanasoka wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Pierre-Emerick Aubameyang, Victor Moses, John Mikel Obi na Jonathan Pitroipa.

"Asanteni mashabiki wote duniani, mnaoendelea kuniunga mkono. Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani mashabiki wanakupenda na kuikubali kazi yako,"amesema kiungo huyo.

"Hiki ni kitu fulani maalumu kwa sababu si kura ya kocha, klabu au nahodha wa timu ya taifa. Ni kura za mashabiki,"aliongeza nyota huyo wa zamani, aliyewahi kuchezea klabu ya Barcelona ya Hispania.

"Siku zote, ni jambo linalofurahisha unapokuwa na mashabiki wengi nyuma yako. Nimefurahi kwa sababu tuzo hiyo nimepewa na mashabiki, nawashukuru sana,"anasema.

Toure anasema, alikuwa na kila sababu ya kushinda tuzo hiyo baada ya kuteuliwa kuiwania kwa miaka minne mfululizo.

Anasema kushinda tuzo hiyo kwake ni mafanikio makubwa, hasa ikizingatiwa kuwa, wanasoka alioshindana nao, wapo kwenye kiwango cha juu na wanacheza soka ya kimataifa.

"Nadhani pia kuwa, soka ya Afrika imekuwa ikipiga hatua kubwa kimaendeleo na hii ina maana kubwa kwetu. Nikiwa mwafrika, ninayo furaha kubwa," anasema Toure.

Uteuzi wa wanasoka walioteuliwa kuwania tuzo hiyo, ulifanywa na wataalamu 44 wa soka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Vigezo vilivyozingatiwa katika uteuzi huo ni
akili, ufundi, ushirikiano na wachezaji wengine na nidhamu.

Mshindi wa tuzo hiyo, alipatikana kutokana na kura zilizopigwa na mashabiki kupitia mtandao wa BBC, aidha kwa njia ya simu au ujumbe wa maandishi.

Mashabiki wamempa Toure tuzo hiyo kutokana na kuiletea mafanikio makubwa Ivory Coast mwaka uliopita na pia kuonyesha uwezo mkubwa katika kucheza soka na kufunga mabao.

Mwaka 2013 haukuwa wa mafanikio makubwa kwa Toure kutokana na kutoshinda tuzo yoyote katika klabu ya Manchester City na Ivory Coast, lakini alionyesha kiwango cha juu katika kusakata kabumbu.

Baada ya kukatishwa tamaa kutokana na Manchester City kushindwa kutetea taji lake msimu uliopita, Toure amerejea uwanjani msimu huu kivingine, akiwa ameongeza kitu kipya katika uchezaji wake, kutokana na kuwa mahiri kwa ufungaji wa mabao ya mipira ya adhabu.

Toure alionyesha uwezo huo katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu ya England dhidi ya Newcastle kabla ya kufunga tena bao kwa staili hiyo katika mechi dhidi ya Hull. Ameshafunga mabao manne kwa staili hiyo, kati ya mabao saba aliyoifungia Manchester City.

Kwa mujibu wa rekodi, Toure amefunga mabao 13 hadi sasa kwa klabu yake hiyo pamoja na timu ya taifa ya Ivory Coast, ambayo ni ya kujivunia kwa mchezaji wa kiungo.

Uwezo huo wa Toure pamoja na uongozi wake, umeiwezesha Manchester City kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo hadi sasa.

Toure pia alikuwa msaada kubwa katika kikosi cha Ivory Coast, kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, zitakazofanyika nchini Brazil.

Ushindi huo ulikuwa faraja kubwa kwa Ivory Coast baada ya kuvurunda katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na Nigeria.

Nje ya uwanja, Toure amekuwa akiongoza mapambano ya kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi katika soka, baada ya kukumbwa na hali hiyo wakati wa mechi ya michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow ya Russia.

Wafuatao ni washindi wa tuzo zilizopita za mwanasoka bora wa Afrika wa BBC:
•2012 - Christopher Katongo (Zambia & Henan Construction)
•2011 - Andre 'Dede' Ayew (Marseille & Ghana)
•2010 - Asamoah Gyan (Sunderland & Ghana)
•2009 - Didier Drogba (Chelsea & Ivory Coast)
•2008 - Mohamed Aboutrika (Al Ahly & Egypt)
•2007 - Emmanuel Adebayor (Arsenal & Togo)
•2006 - Michael Essien (Chelsea & Ghana)
•2005 - Mohamed Barakat (Al Ahly & Egypt)
•2004 - Jay Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
•2003 - Jay Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
•2002 - El Hadji Diouf (Liverpool & Senegal)
•2001 - Sammy Kuffour (Bayern Munich & Ghana)
•2000 - Patrick Mboma (Parma & Cameroon)

Monday, December 2, 2013

KASEJA ARIPOTI KAZINI YANGA



KIPA mpya wa klabu ya Yanga, Juma Kaseja ameanza rasmi mazoezi na timu hiyo kwa ajili ya kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na klabu bingwa Afrika.

Kaseja alianza mazoezi hayo jana yaliyofanyika kwenye uwanja wa Bora ulioko Kijitonyama, Dar es Salaam, akisimamiwa na Kocha wa Makipa, Razack Siwa.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Kaseja kufanya mazoezi na Yanga baada ya kushindwa kufanya hivyo wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mkono.

Kipa huyo alisaliwa na Yanga mwezi uliopita, wakati wa usajili wa dirisha dogo, baada ya kuachwa na Simba msimu uliopita kwa madai ya kiwango chake kushuka.

Katika mazoezi ya jana, Kaseja alishirikiana na kipa mwingine wa zamani wa Simba, Ally Mustapha 'Barthez', ambaye tangu msimu uliopita, amekuwa kipa namba moja wa Yanga.

Hata hivyo, Barthez alipoteza namba yake kwenye kikosi cha Yanga baada ya timu hiyo kulazimishwa kutoka sare ya mabao 3-3 na Simba katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.

Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Deogratius Munishi 'Dida', ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha Tanzania Bara, kinachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini Kenya.
 
Kocha Siwa alichukua muda mrefu kuzungumza na Kaseja na Barthez kabla ya kuanza kuwapa mazoezi ya pamoja.

Mazoezi hayo pia yalihudhuriwa na wachezaji wote wa Yanga, isipokuwa nyota wake watano walioko kwenye kikosi cha Tanzania Bara. Nyota hao ni Dida, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Athumani Iddi 'Chuji' na Simon Msuva.

KOCHA MZUNGU WA SIMBA AANZA KIBARUA




UONGOZI wa klabu ya Simba, jana ulishindwa kumtambulisha kocha mpya wa timu hiyo, Zdravko Lugarusic kutoka Serbia na kipa Yaw Berko kutoka Ghana.

Simba ilipanga kuwatambulisha Lugarusic na Berko kwa waandishi wa habari leo, baada ya wote wawili kutua nchini juzi tayari kwa kuanza kuitumikia timu hiyo.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, utambulisho huo umefutwa kutokana na sababu za kiusalama.

Kamwaga alisema kutokana na kuwepo kwa makundi mawili ya uongozi yanayopingana ndani ya klabu hiyo, waliona isingekuwa busara kufanya utambulisho huo kwa hofu ya kutokea vurugu.

Badala yake, Kamwaga alisema Lugarusic alitarajiwa kuanza kibarua chake jioni kwenye mazoezi ya timu hiyo, yaliyopangwa kufanyika kwenye uwanja wa Kinesi ulioko Manzese, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamwaga, tayari kocha huyo pamoja na kipa Berko wameshaingia mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miezi sita kila mmoja. Walitia saini mikataba hiyo jana, mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope.

Lugarusic anachukua nafasi ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio', ambao walisimamishwa na kamati ya utendaji wakati Berko anachukua nafasi ya Abel Dhaira kutoka Uganda.

Uhuru ilipofika kwenye uwanja wa Kinesi jioni, ilimshuhudia kocha huyo akianza kazi ya kukinoa kikosi hicho huku Berko naye akifanya mazoezi ya ukipa. Pia walikuwepo wachezaji wengine kadhaa waliosajiliwa na Simba msimu huu.

Mazoezi hayo ya Simba pia yalishuhudiwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Joseph Itang'are, maarufu kwa jina la Kinesi, ambaye alifanya mazungumzo na wachezaji kabla ya kumtambulisha kocha mpya pamoja na Berko. Kiongozi mwingine aliyekuwepo kwenye mazoezi hayo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala.

Uhuru pia ilimshuhudia mchezaji mwingine mpya, Kika Musembi kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye alisema amekuja kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, lakini kutokana na kuzuka kwa mgogoro, ameambiwa asubiri.

Kabla ya kuja Simba, Lugarusic alikuwa akiifundisha Gor Mahia ya Kenya wakati Berko aliachwa na Yanga msimu uliopita kutokana na kutokuelewana na viongozi wa klabu hiyo. Berko alianza kuidakia Yanga mwaka 2010, Liberty Proffessionals ya Ghana.

Berko aliletwa nchini na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia, Kostadin Bozidar Papic, ambaye alimuona mlinda mlango huyo wakati anafundisha Hearts Of Oak ya huko mwaka 2008.

Ujio wa Lugarusic na Berko, huenda ukazua mtafaruku mwingine Simba, kufuatia kuwepo kwa makundi mawili ya uongozi yanayopingana.

Awali, Kamati ya Utendaji ya Simba, ilitangaza kumsimamisha uongozi, Mwenyekiti Ismail Aden Rage na makocha Kibadeni na Julio, lakini mapinduzi hayo yalipingwa na Rage na Baraza la Wadhamini.

Rage alitamka hadharani kwamba, bado anawatambua Kibadeni na Julio kuwa makocha wa timu.
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa dharula wa wanachama ndani ya siku 14 ili kuzungumzia mgogoro huo kwa lengo la kuupatia ufumbuzi.

Lakini Rage amepinga agizo hilo la TFF kwa kusema kuwa, haina mamlaka ya kumtaka aitishe mkutano huo. Alisema kikatiba, mwenyekiti wa klabu ndiye anayepaswa kuitisha mkutano mkuu.

KUZIONA TANZANITES, AFRIKA KUSINI BUKU



KIINGILIO cha chini katika mechi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia kwa timu za vijana wa chini ya umri wa miaka 20, kati ya Tanzania, Tanzanites na Afrika Kusini ni sh. 1,000.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kiingilio hicho ni kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na orange.

Timu hizo mbili zinatarajiwa kumenyana Desemba 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Pambano hilo limepangwa kuanza saa 10 jioni.

Kwa mujibu wa Wambura, viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A watalipa sh. 10,000.

Tanzanites, chini ya Kocha Rogasian Kaijage, inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na ule wa Taifa, Dar es Salaam, kujiandaa kwa mechi hiyo.

Wambura alisema kambi ya Tanzanites hivi sasa imehamia Msimbazi Hotel kutoka Ruvu mkoani Pwani.

Tanzanites ilivuka raundi ya kwanza baada ya kuibamiza Angola mabao 15-1. Katika mechi ya awali, ilishinda mabao 10-0 mjini Dar es Salaam kabla ya kushinda mechi ya marudiano mabao 5-1 mjini Luanda.

SAMATA, ULIMWENGU WATUA NAIROBI KUONGEZA NGUVU KILI STARS



WACHEZAJI Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu, wamesema watahakikisha timu yao ya
Kilimanjaro Stars inacheza fainali za mwaka huu
za Kombe la Chalenji.

Ulimwengu, alitua mjina hapa juzi wakati Samata
alitua jana, tayari kuungana na Kilimanjaro Stars
katika michuano hiyo.

Samata alisema atafurahi kuona timu yake
ikicheza fainali za mwaka huu baada ya kushindwa
kufanya hivyo kwa miaka miwili mfululizo.

Alisema furaha yake ni kuona Kilimanjaro Stars
inafanya vyema katika michuano hiyo na kufika
hatua hiyo muhimu.

"Tumekosa michezo miwili ya awali katika
michuano hii, lakini mchezo wa mwisho ni lazima
tutumie nguvu zetu tukiungana na wenzetu kwa ajili
ya kuipatia ushindi timu yetu na kutinga hatua ya
robo fainali," alisema Samata.

Naye Ulimwengu alisema, hasira za kukosa ubingwa
wa michuano ya Kombe la Shirikisho wakiwa na timu
yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo, zitaishia katika michuano hii.

Ulimwengu alisema hawatapenda kuona timu yao
ikiishia katika hatua za awali za michuano hiyo na
kuongeza kuwa, wapo tayari kupambana kwa nguvu zao zote.

Samata na Ulimwengu wataungana na kikosi cha
Kilimanjaro Stars katika mchezo wa mwisho wa
kundi B itakapoivaa Burundi. Mchezo huo utafanyika keshokutwa.

Sunday, December 1, 2013

KILIMANJARO STARS YANUSA ROBO FAINALI



Frank Domayo (kushoto) na Ramadhani Singano 'Messi' wakimpongeza Haruna  Chanongo baada ya kuifungia bao pekee Kilimanjaro Stars dhidi ya Somalia jana katika mechi ya michuano ya Kombe la Chalenji, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi. (Picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry).

NA SOPHIA ASHERY, NAIROBI

TANZANIA Bara, jana ilijiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji, baada ya kuichapa Somalia bao 1-0.

Katika mechi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo mjini hapa, Kilimanjaro Stars ilijipatia bao lake la pekee na la ushindi dakika ya 57 kupitia kwa mshambuliaji Haruna Chanongo.

Chanongo alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ramadhani Singano 'Messi'. Wote wawili waliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi za Elias Maguli na Amri Kiemba.

Kwa ushindi huo, Kilimanjaro Stars sasa inazo pointi nne baada ya kucheza mechi mbili na inatarajiwa kutupa karata yake ya mwisho keshokutwa kwa kumenyana na
Burundi.

Pambano hilo lilianza kwa kasi ndogo huku kila timu ikiusoma mchezo wa mwenzake. Kilimanjaro Stars nusura ipate bao dakika ya tisa wakati Elias Maguli kupokea pasi safi kutoka kwa Mrisho Ngasa, lakini shuti lake lilitoka nje.

Somalia ilijibu shambulizi hilo dakika ya 16 wakati Jabir Hassan alipopewa pasi na kubaki ana kwa ana na kipa Ivo Mapunda, lakini shuti lake lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa huyo.

Kiungo Athumani Iddi 'Chuji' alifanyakazi nzuri dakika ya 21 na kumtengenezea chumba safi Ngasa, lakini shuti lake lilitoka nje.

Nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao ilipotezwa na Kili Stars dakika ya 40 wakati Abubakar Salum alipotoa pasi safi ya juu kwa Said Morad, lakini mpira wa kichwa alioupiga, ulikuwa mboga kwa kipa Mohamed Sherrif wa Somalia. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Somalia ilichachamaa dakika ya 71 na kufanya shambulizi kali kwenye lango la Kili Stars,  lakini shuti la Jabril Mohamed lilidakwa na kipa Mapunda.

Kili Stars: Ivo Mapunda, Himidi Mao, Erasto Nyoni, Saidi Moradm Kelvin Yondan, Frank Domayo, Abubakar Salum, Athumani Iddi, Mrisho Ngasa/Farid Mussa, Elias Maguli/ Ramadhani Singano 'Messi', Amri Kiemba/Haruna Chanongo.

Somalia: Mohamed Sherrif, Hassan Ali, Mohamed Shidane, Aden Hussein, Hassan Hussein, Daud Hassan, Sidi Mohamed, Mohamed Abdi, Jabril Hassan, Mohamed Saleh, Sadaq Abdulkadir.

SIMBA SASA VURUGU TUPU, KOCHA MPYA, BERKO KUTAMBULISHWA LEO




KLABU ya Simba leo inatarajiwa kuwatambulisha rasmi kipa wake mpya,
Yaw Berko kutoka Ghana na Kocha, Zdravko Logarusic kutoka Croatia.

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, utambulisho huo utafanyika makao makuu ya klabu hiyo, mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.

Kamwaga alisema, Logarusic, ambaye aliwahi kuifundisha Gor Mahia ya Kenya, ameletwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Abdalla Kibadeni, ambaye amesimamishwa.

Kwa mujibu wa Kamwaga, baada ya utambulisho huo, Logarusic ataanza rasmi kukinoa kikosi cha Simba kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Januari mwakani.

Alisema Berko atatambulishwa akiwa kipa mpya wa Simba, kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu. Usajili wa dirisha dogo unatarajiwa kumalizika Desemba 15 mwaka huu.

Berko, aliwahi kuichezea Yanga misimu miwili iliyopita, lakini aliachwa kwenye usajili wa msimu huu kutokana na kushindwa kuelewana na viongozi wa klabu hiyo.
Kipa huyo ameletwa kuziba pengo la Juma Kaseja, ambaye amejiunga na Yanga.

Hata hivyo, ujio wa Logarusic na Berko huenda ukazua mtafaruku mwingine mkubwa Simba, kufuatia kuwepo kwa makundi mawili ya viongozi yanayopingana ndani ya Simba.

Awali, kamati ya utendaji ya Simba, ilitangaza kumsimamisha Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage na makocha Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo, lakini mapinduzi hayo yalipingwa na Rage pamoja na Baraza la Wadhamini.

Baada ya kupinga mapinduzi hayo, Rage alitamka hadharani kuwa, Kibadeni ataendelea kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemtaka Rage aitishe mkutano mkuu wa dharula wa wanachama ndani ya siku 14 ili kuzungumzia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi.

Lakini Rage amepinga agizo hilo la TFF na kusema kuwa, limekiuka katiba ya Simba na kumvua madaraka ya uenyekiti kwa vile mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu ni mwenyekiti pekee.

EMMANUEL ASHINDA MIL 50/- ZA EBSS



MSHIRIKI Emmanuel Msuya kutoka Mwanza, juzi usiku alitawazwa kuwa mshindi wa shindano la Epiq Bongo Star Search 2013 baada ya kuwabwaga washiriki wenzake watano walioingia fainali.

Katika fainali hiyo, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Escape 1, Dar es Salaam, Emmanuel alitangazwa kuwa mshindi na jaji mkuu wa mashindano hayo, Rita Poulsen.

Washiriki watano waliotinga fainali ya shindano hilo ni Amina Chibaba,Elizabeth Mwakijambile, Emmanuel,Maina Thadei na Melisa John.

Baadaye, washiriki watatu walienguliwa na kubaki Emmanuel na Elizabeth, ambao walitinga fainali.
Kutokana na ushindi huo, Emmanuel alizawadiwa kitita cha sh. milioni 50. Alikabidhiwa fedha hizo na Rita, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark Production, inayoandaa mashindano hayo.

Emmanuel amerithi taji hilo kutoka ka Walter Chilambo, ambaye aliibuka mshindi mwaka jana.

Fainali hiyo, ambayo ilichelewa kuanza, ilipambwa kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali maarufu wa Tanzania, wakiwemo Barnaba, Makomando,Young Killer, Chilambo, Shaa, Kimbunga na Snura.

BFT YASHINDWA KUMPATA RAIS


Makore Mashaga, amechaguliwa tena kuwa katibu mkuu BFT

NA AMINA ATHUMANI, BAGAMOYO

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), uliofanyika juzi kwenye hoteli ya Palm Tree mjini hapa, uligubikwa na vurugu za hapa na pale na kusababisha kushindwa kupatikana kwa rais wake.

Vurugu hizo zilizuka baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Jamal Rwamboh kumwengua Mutta Lwakatare kugombea nafasi ya urais kwa madai kuwa, hakuwa na vigezo.

Lwakatare alikuwa akiwania nafasi hiyo pamoja na mgombea mwingine, Andrew Kuyeiyana, ambaye licha ya kupitishwa, hakuambulia kura hata moja baada ya kupigiwa kura za kumkataa.

Chanzo cha vurugu hizo ni kamati ya  uchaguzi kufanya usaili kwa wagombea, nusu saa kabla uchaguzi kufanyika na hivyo kuwakosesha nafasi ya kukata rufani wagombea walioenguliwa.

Baadhi ya wapambe wa Lwakatare, walipinga sababu zilizotolewa na kamati hiyo katika kuliengua jina lake na kuvamia meza kuu. Hata hivyo, Rwamboh alishikilia msimamo wake.

Rwamboh aliamuru wajumbe wa uchaguzi huo kupiga kura za ndio na hapana katika nafasi hiyo baada ya kumpitisha Kuyeiyana kuwa mgombea pekee. Kuyeiyana ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF tawi la Dodoma.

Hata hivyo, katika kura hizo, Kuyeiyana aliambulia patupu baada ya kupigiwa kura nyingi za hapana na hivyo kusababisha nafasi hiyo ikose mshindi.

Katika nafasi ya makamu wa rais, mgombea pekee Wililo Lukelo aliibuka mshindi baada ya kupata kura nyingi wakati nafasi ya katibu mkuu ilichukuliwa tena na Makore Mashaga.

Katika nafasi ya mweka hazina, Ntava Kapanda aliibuka kuwa mshindi wakati waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji ni Salum Viduka,  Aisha Voniatis, Zuwena Kipingu,  Restuta Bura, Juma Bugingo, Said Omari, Mwinyikheri Said na Athony Mwang'onda.  

Baada ya uchaguzi huo kumalizika, Makamu wa Rais wa BFT, Wililo, anayekaimu nafasi ya rais alisema, kamati ya utendaji inatarajiwa kukutana leo kujadili uchaguzi mdogo wa nafasi hiyo.

Baadhi ya wagombea walioshinda, walilalamikia mfumo uliotumika kuendesha uchaguzi huo kwa madai kuwa, haukuwa mzuri kutokana na kuwanyima fursa ya kukata rufani wagombea walioenguliwa kwenye usaili.

"Mimi ni mara ya kwanza kuona usaili unafanyika muda mmoja na uchaguzi. Hakuna  katiba ya chama chochote inayosema hivyo kwani usaili hufanyika siku moja kabla ili kutoa nafasi kwa walioenguliwa kukata rufani,"alisema Viduka.

Aliongeza kuwa, wajumbe wa kamati ya uchaguzi kutoka Baraza la Michezo Taifa (BMT), walichangia kuutia doa uchaguzi huo kutokana na kushindwa kufuata katiba ya BFT katika kuusimamia.

Uchaguzi wa BFT ulifanyika kwa ufadhili wa Lwakatare, aliyegharamia malazi na chakula kwa wagombea na wapiga kura wote. Awali, uchaguzi huo ilikuwa ufanyike Oktoba mwaka huu, lakini ilishindikana kutokana na ukosefu wa fedha.

BURIANI TABU LEY ROCHEREAU




BRUSSELS, Ubelgiji
MWANAMUZIKI mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Pascal Tabu Ley Rochereau, amefariki katika hospitali moja ya mjini Brussels.

Tabu Ley, alifariki juzi saa mbili usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi. Alianza kuugua ugonjwa huo tangu 2008.

Meneja wa zamani wa mwanamuziki huyo, Mekansi Modero, ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, amethibitisha taarifa za kifo cha Tabu Ley, baada ya kuthibitishiwa na ndugu wa karibu wa mkongwe huyo.

Mwanamuziki Nyboma Mwandido, anayeishi mjini Paris, Ufaransa pia amethibitisha taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo mkongwe.

Tabu Ley alikuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo kwa muda mrefu na alikuwa akitembea kwa kutumia baiskeli maalumu kutokana na kushindwa kutembea kwa miguu.

Kifo cha Tabu Ley kimewapa simanzi kubwa mashabiki wa muziki barani Afrika, kutokana na kuwa mmoja wa watu mahiri, ambaye nyimbo zake zilikuwa na mvuto wa aina yake.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tabu Ley aliamua kuachana na muziki na kujitosa katika masuala ya siasa, baada ya kuteuliwa kuwa waziri katika serikali ya Rais wa zamani wa DRC, Laurent Kabila mwaka 1997

Awali, Tabu Ley alilazimika kuikimbia DRC na kwenda kuishi uhamishoni nchini Ubelgiji kutokana na kutoelewana na rais wa zamani wa nchi hiyo, marehemu Mobutu Sese Seko.

Kabla ya kwenda Ubelgiji, Tabu Ley aliishi kwa muda nchini Ufaransa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo. Baada ya hali kuanza kuwa mbaya, alihamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya kupatiwa matibabu maalumu.

Enza za uhai wake, Tabu Ley alikuwa akichuana vikali na wakati nyota wa DRC wa wakati huo kama vile Joseph Kabasele, Nicolas Kasanda na Rwambo Lwanzo Makiadi 'Franco'.

Alianza kujihusisha na muziki 1959 akiwa mtunzi, mwimbaji na mcheza shoo akiwa katika bendi ya African azz, iliyokuwa ikiongozwa na Kabasele. Mkongwe huyo amerekodi na kuimba nyimbo zaidi ya 2,000 na kutoa albamu 250.

Alizaliwa 1940 katika mji wa Bandundu nchini DRC. Alianza maisha akiitwa Pascal Tabu. Akiwa na umri wa miaka 14, aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao aliurekodi na kundi maarufu la African Jazz, lililokuwa chini ya Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle).

Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza sekondari 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz.

Alikuwa mmoja wa wanamuziki walioimba wimbo Independence Cha Cha, wa Grande Kalle, uliotikisa anga la Afrika miaka ya 1960. Wimbo huo ukawa rasmi wa kusherehekea uhuru wa DRC.

Baada ya miaka minne, alijiengua katika kundi la African Jazz. Akiwa na mpiga gita mahiri, Nicholaus Kassanda, wakaanzisha kundi la African Fiesta, ambalo alidumu nalo hadi 1965.

Wakati DRC ikiwaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali, aliamua kuachana na  Nico na kuanzisha kundi lake la African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash na kurekodi kibao maarufu cha Afrika Mokili Mobimba, ambacho kilivuka mauzo ya nakala milioni moja miaka ya 1970 na kuiingiza bendi hiyo kuwa kati ya bendi zilizopata mafanikio ya juu katika Afrika kwa wakati huo.

Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni miongoni mwa wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.

Mwaka 1970, Tabu Ley alianzisha bendi ya Orchestre Afrisa International. Wakati huo Afrisa na TPOK Jazz, ndizo zilizokuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon na Mose Konzo.

Kutokana na umahiri wake, Tabu Ley aliweza kupata tuzo kutoka serikali za nchi kama Chad, iliyompa heshima ya 'Officer of The National Order' wakati Senegal ilimpa heshima ya 'Knight of Senegal' na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau.

Katikati ya miaka ya 1980, Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika, Mbilia Bel. Baadae Tabu Ley alimuoa Mbilia, wakapata mtoto mmoja.

Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho mwanamama huyo, aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri.

Mwaka 1988, Tabu Ley akagundua kipaji cha mwimbaji mwingine wa kike, Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake. Katika kipindi hicho, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya ile ya rumba ya Afrisa na TP OK Jazz, ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tabu Ley, alihamia Marekani, akawa anaishi Kusini mwa California na kubadili  muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la kimataifa.Akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley na Babeti Soukous.

Mwaka 1996, Tabu Ley, alishiriki katika album ya kundi la Africando, akiimba wimbo wa Paquita, ambao aliurekodi miaka ya 1960, akiwa na African Fiesta.

Tabu Ley alipata cheo cha uwaziri katika utawala wa Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Kabila, 2005, alipewa cheo cha gavana.

Mwaka 2006,  Tabu Ley,  alishirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu, Maika Munah na kurekodi album yake ya mwisho, iliyoitwa Tempelo. Katika albumu hiyo, binti yake, Melodie aliimba nyimbo kadhaa.

Saturday, November 30, 2013

SALAM ZA MALINZI KWA JK

 
SALAMU ZA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA KWENYE HAFLA YA KUPOKEA KOMBE HALISI LA DUNIA TANZANIA
 
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 
Mheshimiwa Dk. Fennela Mukangara- Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
 
Ndugu Dioniz Malinzi- Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
 
Mkuu wa msafara wa FIFA/Coca-Cola
 
Bw Yebeltal Getachew- Meneja Mkazi wa Coca-Cola
 
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
 
Wageni waalikwa
 
Mabibi na mabwana
 
Mheshimiwa Rais, nianze kwa kukushukuru kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe halisi la Dunia.
 
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.
 
Coca-Cola ni washirika wetu wa karibu na wamekuwa wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu
mwaka 2007, mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kuibua vipaji vingi ambapo baadhi yao wameweza kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.
 
Tunawashukuru sana Coca-Cola na tunaahidi  kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kuendeleza soka ya vijana.
 
Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba, 2009 wakati unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa kwa uongozi wa mpira wa Tanzania.
 
Ulitushauri tuimarishe uongozi na utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi klabu, ulitushauri tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha kufundisha timu zetu za mpira na pia ulitushauri tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka wakiwa na umri mdogo.
 
Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu tuliuzingatia na tulifanya jitihada za kuufanyia kazi. Hali ya utulivu katika uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale palipoonyesha dalili za migogoro tulikemea na ikibidi tulichukua hatua madhubuti kutatua migogoro.
 
Tumefanya kozi mbalimbali za kuwaendeleza walimu wetu wa mpira, waamuzi, madaktari na viongozi wetu wa ngazi mbalimbali na matokeo yake yanaonekana katika kuinuka kwa viwango vyao vya ufundishaji na utoaji uamuzi uwanjani.
 
Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza mwaka 2009 maendeleo ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya mpira kwa Taifa letu. Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28, Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa.
 
Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
 
Fainali hizi uhusisha mataifa manane yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha timu mbili zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza fainali za dunia za vijana chini ya umri wa miaka
17.
 
Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine Babayaro na wengine kadhaa.
 
Ili tupate timu nzuri ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019.
 
Katika kuboresha kikosi hiki mwaka 2015 tutafanya mashindano ya kitaifa ya umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa ya umri chini ya miaka 14, 2017 yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na 2018 yatakuwa ya umri chini ya miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha mwisho cha kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.
 
Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020, kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.
 
Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013, Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Afrika umri
chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019.
 
Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kanuni za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika haina budi ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi yake(Letter of support from Government).
 
Wiki ijayo tutawasilisha barua kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono na Serikali katika azma yetu hii, tunaomba Serikali ituunge mkono katika jambo hili.
 
Mheshimiwa Rais nimalizie kwa kukushukuru tena kwa uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wanaotupa katika shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa kutuwezesha kuwa moja ya nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili, Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa karibu.
 
Watanzania wenzangu ninaomba tuje kwa wingi kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuliona Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni kuwa ipo siku Kapteni wa Timu yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania kombe hili.
 
Asante