KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 17, 2010

Tambo,mbwembwe, vituko vyatawala pambano la Simba na Yanga


"Kuloga wameloga wao, mechi tumeshinda sisi," hizo zilikuwa kelele za shangwe kutoka kwa mashabiki wa soka wa Yanga baada ya timu yao kushinda bao 1-0 dhidi ya Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Mamia ya mashabiki wa klabu hiyo walikimbia mchakamchaka katika mitaa ya Kirumba, wakipita huku na kule na wengine walifurika kwenye baa wakinywa pombe na kushangilia kwa mbinde na staili tofauti ili kujipongeza baada ya ushindi huo.
Furaha ya mashabiki hao ilikuwa kubwa kupindukia kutokana na kushinda mechi, ambayo ilikuwa na homa kubwa kwa timu zote kutokana na kila upande kupania kushinda, ambapo kwa sababu hiyo, wanazi wa klabu hizo wa kutoka Dar es Salaam, waliopo Mwanza na mikoa mengine ya Kanda ya Ziwa, kutupiana makonde.
Hali kabla ya mchezo
Yanga waliwasili jijini Mwanza Ijumaa saa 5:30 asubuhi wakiwa na msafara wa watu 45, kati yao wakiwemo wachezaji 20 na wengine walikuwa viongozi na mashabiki wa klabu hiyo.
Kuwasili kwa timu hiyo kulilipua shangwe kwa mashabiki wao waliokuwa wametangulia na waliopo Mwanza, ambao walikwenda kuipokea timu kwa shangwe na kuisindikiza hotelini na baadaye kuingia uwanja wa CCM Kirumba kwa mazoezi ya siku moja kabla ya mechi.
Yanga, ambao walikuwa wageni wa Simba walipofika uwanjani, walizusha kizaazaa baada ya baadhi ya mashabiki wa Simba waliotaka kuingia kushuhudia mazoezi hayo, kukataliwa kufanya hivyo kwa madai kuwa, walikuwa wanataka kuiba mbinu za wapinzani wao.
Mashabiki wa Yanga walikaa milangoni na wengine majukwaani na walisikika wakiapa kuwa, bora afe mtu kuliko wenzao wa Simba kuingia ndani.
“Nyinyi hamuingii hata kwa nini, tutapigana hadi asubuhi, tokeni wauza chipsi na mayai tunawajua sana hapa, mnajidai babu kubwa," walisikika wakisema wanazi wa Jangwani.
Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), ambao walikuwepo nje ya Uwanja wa CCM Kirumba kulinda fedha za tiketi, ambazo zilianza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo,walikaa kimya kutazama tambo hizo, lakini baadaye iliwalazimu kuingilia kati kwa kuwatawanya mashabiki wa Simba baada ya makonde kufumka.
Fujo zilikuwa kubwa na kusababisha wapenzi wengi kukimbia ovyo mitaani baada ya kundi la mashabiki wa Yanga maarufu kama 'Yanga Bomba' kuwasili Mwanza usiku na kwenda moja kwa moja uwanjani, ambako waliwaongezea nguvu wenzao na kufanikiwa kuwashinda manazi wa Simba, ambao baadhi yao waliumizwa.
Jumamosi ilikuwa siku ya mechi yenyewe na homa ilikuwa imepanda maradufu kwa sababu kila baa ilikuwa imefurika mashabiki wa timu hizo waliokuwa wanakunywa pombe na kutambiana hadi baadhi kuonyeshana nguo za ndani.
"Rangi ya kijani na njano haifai kuwa vazi, mimi mwanamke napenda kuvaa nyekundu na nyeupe," alitamba shabiki mmoja mbele ya wenzake wa Yanga wakati wanakula mlo wa mchana, ambapo baadaye alivua jeans na kuonyesha nguo aliyovaa kudhihirisha alichokuwa anakisema.
Walitambiana kwa muda na kisha wakazika tofauti za usimba na uyanga kwa kucheza pamoja nyimbo na ngoma zilizokuwa zinapigwa na mashabiki wa Yanga nje ya Hoteli ya Wendele.
"Wera wera...oya oya mwanangu," alisema Sofia, mwanachama maarufu wa Simba wakati akicheza na kukumbatiana kwa furaha na mashabiki wanawake wa Yanga kuonyesha upendo na kwamba, Simba na Yanga upinzani upo uwanjani, lakini katika mambo mengine wao ni ndugu!
Iliwadia zamu ya uwanjani, ambapo mashabiki wanaokaribia 20,000 walikuwa wamejaaa hadi mechi hiyo ilipoanza. Rangi za kijani, njano, nyekundu na nyeupe za miamvuli, bendera, fulana, trakisuti na mavazi ya aina tofauti zilipamba uwanja huo.
Mashabiki waliimba kwa zamu, Yanga walipokuwa wanacheza, wale wa Simba walijibu mapigo na mara nyingine wote walionekana kuishiwa tambo na kubaki kimya.
Saa 8:50 mchana, wachezaji wa Simba waliingia uwanjani bila ya gari wakitokea upande wa Kaskazini wakiongozwa na kipa Ali Mustafa 'Barthez'. Ilibidi mtu uwe mwepesi kuona 'utundu' wao baada ya kuingia huku wanageuka nyuma na kubadilisha kitendo hicho haraka.
Wote walipita uwanjani na kushangiliwa kwa nguvu kisha waliingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo na mara Yanga nao waliwasili kwa mbwembwe. Timu hiyo ikiongozwa na msafara wa magari matatu, iliwasili uwanjani saa 9:22.
Dakika tano baadaye, mbinje kutoka kwa mashabiki wa Yanga zililipuka baada Kocha Mserbia, Kostadin Papic akiwa amevaa suti ya rangi nyeusi, kuingia uwanjani na kuonyesha skafu ya rangi ya kijani na njano iliyoandikwa Yanga. Uso wa kocha huyo ulikuwa umejaa tabasamu.
Saa 10:20 jioni, mechi ilianza na Simba walionekana kama wangeshinda mchezo huo baada ya kulishambulia lango la Yanga kama nyuki na kukosa mabao kutokana na kipa Yaw Berko kusimama imara langoni.
Emmanuel Okwi na Joseph Owino ni wachezaji, ambao hawataisahau mechi hiyo kutokana na kukosa mabao, ambayo yangeipa Simba uongozi wa ligi kuu na tambo dhidi ya wapinzani wao wa jadi.
Dakika ya pili na tatu, Okwi alionekana kuwa tishio kwa ngome ya Yanga baada ya kuuwahi mpira uliookolewa kwa kifua na beki Shadrack Nsajigwa na kupiga shuti, ambalo Berko alilipangua kwa ufundi na kuwafokea mabeki wake.
Berko alionyesha kuwa ni mchezaji bora wa mechi hiyo baada ya kubaki yeye na Okwi na kumfuata kama nyati aliyejeruhiwa na kuuondoa mkwaju wa Mganda huyo na mashabiki wa Simba kubaki wameshika vichwa wakiwa hawaamini kilichotokea.
Kipa huyo alionyesha kuwa habahatishi kuondoa michomo baada ya kuruka juu na kuudokoa mkwaju wa Patrick Ochan, ambao dhahiri ulikuwa unajaa wavuni. Mpira huo ulizaa kona tasa, ambazo Simba walipata tano na walishindwa kuzitumia.
Nafasi nyeti kuliko zote, ambazo Simba watakaa wazililie daima ni ya Owino, aliyepiga mpira nje wakati kipa Berko ameshaangukia upande mwingine huku zikiwa zimebaki dakika sita mtanange kumalizika.
Kwa ujumla, Simba walicheza vizuri dakika 20 za kwanza na ilifuata zamu ya Yanga kutawala mchezo, lakini tatizo kubwa la timu hiyo lilikuwa katika ushambuliaji kwa sababu Jerry Tegete na Nsa Job walishindwa kuwapenya Juma Nyoso, Owino na Maftah waliokuwa wamesimama imara kumlinda Kaseja asipate madhara.
Kupoteza nafasi za wazi za mwanzo kuliwagharimu Simba kwani kipindi cha pili kilikuwa cha Yanga, waliokuwa wanatafuta bao kwa udi na uvumba na kufanikiwa katika dakika ya 70 baada ya Tegete kupenyezewa pande refu na Ernest Boakye na kuitumia pasi hiyo kwa umakini.
Tegete alikimbia kama mashine na kubaki ana kwa ana na Kaseja, ambapo alifumua kiki iliyojaa wavuni kupitia nyavu za juu ya goli. Kwa mwonekano, Kaseja alidhani mpinzani wake angepiga pembeni.
Goli hilo liliwapa nguvu Yanga na kufanya mashambulizi mawili ya haraka, ambayo hayakuzaa matunda. Nsa Job kuna wakati aliwaweka roho juu mabeki wa Simba na Kaseja alicharuka na kumchezea rafu mbaya kwa kumrukia kichwani.
Alionyeshwa kadi ya njano na Simba walijipanga kuonyesha wanataka kushambulia na kupata bao la kusawazisha, lakini haikuwezekana tena baada ya mabeki wa Yanga kujipanga na kuondoa hatari zote.
Ilikuwa zamu ya butua butua kwa kila timu.Mabeki wa Yanga walipiga mpira mbele kwa nguvu na staili ya chogo chemba ilionekana katika mchezo huo kupitia beki Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye aliondoa shambulizi moja namna hiyo na kushangiliwa. Mchezo ulimalizika kwa Yanga kushinda bao hilo pekee la Tegete anayeonekana ni mwiba kwa Kaseja.
Nderemo za Yanga zimeendelea hadi jana kwa baadhi ya mashabiki wao waliotoka Dar es Salaam kubaki jijini Mwanza na kujipongeza kwa vinywaji, lakini mashabiki wachache wa Simba walionekana kukatiza mitaa ya jiji hilo.
Mashabiki wa Msimbazi wa kutoka Dar es Salaam waliobaki Mwanza walikuwa wanyonge, ingawa baadhi yao walionyesha kukomaa kisoka baada ya kuwapongeza wenzao kwa mafanikio hayo.
Yanga wamefikisha pointi 19 zinazowapa uhakika wa kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu na Simba wamebaki nafasi ya pili baada ya kuwa wamejikusanyia pointi 14 katika mechi saba.
Kauli za makocha.
Patrick Phiri wa Simba alisema amesikitishwa kupoteza mechi hiyo muhimu na kufafanua kuwa, anakwenda kujipanga na wachezaji wake kwa ajili ya michezo mingine.
"Inauma maana tumepata nafasi nyingi, lakini tumeshindwa kuzitumia. Wenzetu Yanga wamepata moja na wameshinda, ndio mchezo ulivyo," alisema Phiri.
Akizungumzia waamuzi, kocha huyo alisema hawakuwa na tatizo bali walijitahidi kuhimili presha ya mchezo huo mkubwa.
Kostadin Papic hakuwa na raha kwani alichukizwa kutimuliwa kwenye benchi na mwamuzi wa pembeni. "Sijui nilikosa nini, mimi ni kocha ninayejua kazi yangu, inakuwaje mshika kibendera anitoe," alilalamika Papic na kusema anajua wajibu wa kazi yake kwani ameifanya miaka 24.
Kilichowasibu Simba
Japokuwa wengi walishindwa kujua kwa nini timu hiyo ya Msimbazi ilifungwa, ukweli ni kwamba walikuwa wamejikaza moyoni, kwani pengo la nyota wake Mussa Hassan 'Mgosi', Nico Nyagawa, Uhuru Selemani na Salum Kanoni, ambao ni majeruhi lilichangia kipigo hicho.
Hakuna kificho kwamba wachezaji hao wamekuwa tegemeo la Simba katika kikosi cha kwanza kwa misimu mingi. Uzoefu wa Kanoni haufanani na Haruna Shamte. Santo na Hilary Echesa ni wazuri, lakini Nyagawa naye bado lulu na mzoefu wa kutosha na siasa za Simba na Yanga. Vivyo hivyo kwa Mgosi na Ochan, aliyechezeshwa sehemu ya ushambuliaji. Mgosi amewiva zaidi ya Mkenya huyo.
Yango nao wana pengo la mshambuliaji wa kusaidiana na Tegete, lakini ipo haja ya kuutazama upya ukuta wao kwa vile Cannavaro na Isaack Boakye hawakuwa wanaelewana sana ikilinganishwa na alivyokuwa anacheza pamoja na Wisdom Ndlovu.
Ushirikina pia ni suala, ambalo lilitawala mchezo huo na ndio kilikuwa chanzo cha wanachama wa timu hizo kusukumiana makonde kabla ya mchezo, lakini kama kweli unafanya kazi, basi umeinufaisha Yanga.
Baadhi ya viongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na wanachama wenye uchungu na Yanga, walilinda uwanja wa Kirumba hadi asubuhi kuhakikisha 'dawa' zao hazichezewi na Simba ambao walionekana dhahiri kuchelewa kuzinduka!
Walijifunika shuka asubuhi wakati wenzao wametawala uwanja nao wakawa wanapambana kutaka kwenda kufanya vitu vyao. Wakiwa wenyeji, walikuwa na nafasi ya kuugeuza hata bahari kama walipenda kufanya hivyo.
Simba walikuwa na zaidi ya wiki moja ya kutembeza ‘ndumba’ uwanjani kwa sababu walifika Mwanza mapema wakitokea mikoa ya Tabora na Shinyanga, lakini walijisahau na kuwa bize katika mazoezi ya soka pekee.
Hiyo ni mara ya nane timu hizo kukumbana katika jiji la Mwanza.Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1974, Yanga iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Nyamagana. Katika mechi za ligi pekee, ilikuwa mara ya nne kukutana. Mashindano mengine waliyokutana ni ya Kombe la Hedex, Tusker na mechi nyingine za kirafiki.

No comments:

Post a Comment