MSHAMBULIAJI Jerry Tegete (kulia) wa Yanga akiwa na baba yake, John Tegete mara baada ya pambano la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba kumalizika juzi mjini Mwanza. Yanga ilishinda bao 1-0.
PAMBANO la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga lililochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, limeingiza sh. milioni 138.
Akitangaza mapato hayo jana, Mkurugenzi wa Fedha wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ahmed Naheka alisema, fedha hizo zilipatikana kutokana na idadi ya mashabiki 25,000 walioingia uwanjani kwa kulipa kiingilio.
Kufuatia kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha, Naheka alisema kila klabu ilipata mgawo wa zaidi ya sh. milioni 33 wakati makato mengine yalikwenda TFF, Chama cha Soka cha Mwanza (MRFA) na uwanja.
Naheka alisema mapato hayo ni kadirio la juu kwenye uwanja huo na yamevunja rekodi ya mapato yaliyopatika mwaka 2007 kati ya timu hizo, ambapo sh. milioni 100 zilipatikana.
Mkurugenzi huyo wa fedha wa TFF alipongeza usimamizi mzuri wa mechi hiyo uliofanywa kwa pamoja na MRFA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ambao alisema ndio uliowezesha kupatikana kwa mapato hayo.
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki, Yanga iliendeleza ubabe wake kwa Simba baada ya kuichapa bao 1-0.
Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Yanga dhidi ya Simba katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Yanga pia iliichapa Simba mabao 3-1 katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani iliyochezwa Agosti mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena keshokutwa wakati Simba itakapomenyana na AFC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba; Mtibwa itavaana na Azam kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro; Polisi itaikaribisha African Lyon mjini Dodoma wakati Ruvu Shooting itacheza na Majimaji mjini Morogoro.
Yanga wanatarajiwa kuteremka tena dimbani Alhamisi kumenyana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment