WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga ikiwa imeshaanza kupanda, viongozi wa klabu hizo wamekuwa katika mikakati kabambe, kila upande ukipania kuibuka na ushindi.
Timu hizo kongwe nchini zinatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Homa ya pambano hilo ilianza kupanda wiki iliyopita baada ya viongozi wa klabu hizo kuwawekea ulinzi mkali wachezaji wao waliokuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichokuwa kikijiandaa kumenyana na Morocco.
Hofu ya viongozi wa klabu hizo ilikuwa huenda upande mwingine ungetinga kwenye kambi hiyo kwa lengo la kuwashawishi wachezaji wao wacheze chini ya kiwango.
Hilo lilijidhihirisha wakati wachezaji wa Yanga walipofika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 kati ya Taifa Stars na Morocco. Katika mechi hiyo, Taifa Stars ilichapwa bao 1-0.
Viongozi wa Yanga waliwawekea wachezaji wa timu hiyo ulinzi mkali wakati walipokuwa wakiingia na kutoka kwenye uwanja huo ili kuhakikisha hawafanyi mazungumzo na mtu yeyote.
Ulinzi huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo, Mohamed Bhinda, Meneja wa timu hiyo, Emmanuel Mpangala na Kocha Mkuu, Kostadin Papic. Kazi ya viongozi hao ilikuwa kuhakikisha wachezaji hao hawapati nafasi ya kuzungumza ama kuonyeshana idhara na mtu yeyote.
Mbali na kuwawekea ulinzi huo wachezaji wao, mzozo mkubwa ulizuka baina ya viongozi wa klabu hizo mbili baada ya mchezo huo, kila upande ukitaka kuwachukua wachezaji wao waliokuwemo kwenye kikosi cha Stars.
Bhinda alitaka kuwachukua Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika na Nurdin Bakari wakati viongozi wa Simba walitaka kuwachukua Juma Kaseja,Mohamed Banka na Haruna Shamte.
Hata hivyo, mzozo huo ulizimwa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao waliwazuia wachezaji hao kuondoka hadi siku iliyofuata baada ya kambi ya Stars kuvunjwa.
Vituko vingine vilivyopamba moto kwa klabu hizo ni kuwepo kwa imani za ushirikina. Tayari klabu hizo mbili zimeshaunda kamati za ‘uchawi’ zinazoongozwa na wazee, kila upande ukipania kutumia imani hizo kuibuka na ushindi.
Wazee wa Yanga walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwa lengo la kupanga mbinu za kuibuka na ushindi dhidi ya mahasimu wao.
Moja ya mikakati iliyoamualiwa na wazee hao wa Yanga ni kuwalisha yamini wachezaji wao, ili iwapo yeyote kati yao ataihujumu, adhurike. Mpango huo umepangwa kufanyika kabla ya timu kwenda Mwanza. Lakini bado haijajulikana iwapo tayari wachezaji hao wameshalishwa yamini.
Uamuzi wa wazee wa Yanga kuwalisha yamini wachezaji wao umekuja baada ya kubainika kuwa, baadhi yao wana uhusiano wa karibu na viongozi wa Simba, hasa wanachama wa kundi la Friends of Simba.
Yanga imeweka kambi Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo. Kambi ya timu hiyo ipo chini ya ulinzi mkali wa baadhi ya wanachama maarufu kwa jina la ‘Makomandoo’.
Tayari baadhi ya wanachama na wafanyabiashara wenye mapenzi mema na Yanga wameahidi kutoa zawadi mbalimbali za fedha kwa wachezaji wao iwapo wataibuka na ushindi dhidi ya Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alijigamba wiki hii kuwa, maandalizi yao kwa ajili ya pambano hilo yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa, hawaoni kitakachowakwamisha kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
“Iwe, isiwe lazima mnyama afe tena safari hii,” alijigamba msemaji huyo wa Yanga.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha alisema wameshabaini njia zote zilizokuwa zikitumiwa na Simba kuwaangamizi na kuziziba barabara.
“Ile janja waliyokuwa wakiitumia Simba kutufunga, tumeshaibaini, sasa kazi ni moja tu, lazima mnyama afe,”alisisitiza.
Kwa upande wa Simba, timu hiyo iliweka kambi mjini Tabora kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo kabla ya kwenda Shinyanga, ambako ilicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Kahama United na kuibuka na ushindi.
Maandalizi ya Simba kwa ajili ya mechi hiyo yamekuwa yakifanyika kimya kimya huku wafadhili mbalimbali wakiwa wamewaahidi wachezaji kitita kikubwa cha fedha iwapo wataibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Wafadhili hao, wakiongozwa na kundi la Friends of Simba wamepania kuiona timu yao ikishinda, baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani, iliyochezwa Agosti mwaka huu.
Hali ndani ya klabu hiyo kwa sasa ipo shwari baada ya awali kuripotiwa kuzuka kwa tofauti kati ya viongozi na kundi la Friends of Simba mara baada ya kumalizika kwa tamasha la ‘Simba Day’.
Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alitamba kuwa, maandalizi yao hadi sasa yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa, ushindi ni lazima katika mechi ya keshokutwa.
“Tulifungwa na Yanga katika mechi ya kuwania ngao ya hisani kwa bahati mbaya, lakini hilo halitatokea tena Mwanza, lazima tutoke uwanjani na pointi zote tatu,”alisema.
No comments:
Post a Comment