Klabu ya simba imetangaza kikosi cha wachezaji ishirini na sita .
JUMA KASEJA
ALLY MUSTAFA.
RAMADHAN SHAMTE .
SALUM KANONI
MUSSA MGOSI.
JUMA JABU.
JUMA NYOSO
AMIR MAFTAH.
JOSEPH OWINO.
MOHAMED BANKA.
KEVIN YONDAN.
DAVID NAFTARI.
ABDULLHIM HUMOOD.
JERRY SANTO .
HILALI ECHESA.
AMIR KIEMBA.
SHIJA MKINA.
NICO NYAGAWA.
RASHID GUMBO.
UHURU SULEIMAN.
SALUM AZIZ.
EMANNUEL OKWI.
PATRICK OCHAN.
MBWANA SAMATA.
MOHAMED KIJUSO.
CHARLES HAULE..
KOCHA MKUU.
PATRICK PHIRI
MAKOCHA WASAIDIZI .
SAID AMRI.
SULEIMAN MATOLA.
'
Wednesday, July 21, 2010
Friday, July 16, 2010
Nafurahia mwili wangu sasa-Janet Jackson
LOS ANGELES, Marekani
MWANAMUZIKI nyota wa zamani wa Marekani, Janet Jackson amesema, kwa sasa anaufuarhia zaidi mwili wake kuliko alivyokuwa miongo mitatu iliyopita.
Janet (44), mwanamuziki ndugu na waliokuwa wakiunda kundi la Jackson Five, alisema hayo kupitia jarida la Essence, toleo la hivi karibuni.
Akiwa na umri wa miaka 11 hadi 13, Janet alikuwa akishiriki kucheza vipindi vya televisheni vya Penny Woods na Good Times miaka ya 1970.
Lakini alidai alikuwa akijihisi vibaya kuhusu kukuwa kwa mwili wake wakati akishiriki kwenye vipindi mbalimbali vya televisheni ya Marekani.
“Wakati nikicheza kipindi cha Good Times, walinitaka nikibane kifua changu,”alisema.
“Nilianza kubadilika kimwili tangu nikiwa mdogo. Hawakunieleza iwapo wangenifanyia hivyo,”aliongeza.
Janet alisema wakati mwingine alikuwa akivalishwa masweta yanayobana kifua chake ili kukifanya kionekane hakina maziwa na kuongeza kuwa, hali hiyo ilikuwa ikimkera.
“Fikiria wewe ni mtoto usiye na hatia na mara unaanza kuwaza kwamba muonekano wako wa asili si mzuri. Hali hii iliniathiri sana,”alisema mwanamuziki huyo.
Janet, ambaye picha yake imetumika kwenye ukurasa wa mbele wa jarida la Essence toleo la hivi karibuni alisema kwa sasa amebadili mwelekeo.
Kwa sasa, mwanamuziki huyo anaandika kitabu kitakachoitwa True You, kinachozungumzia mazoezi ya mwili na vyakula vinavyofaa kuliwa.
“Nilitaka kuandika kitabu hiki kwa sababu nataka watoto wapate kitu cha kusoka na kuelewa kwamba wao ni wazuri kwa jinsi walivyo,”alisema.
“Ilinichukua muda kuwa hivi nilivyo sasa. Lakini napenda maisha yangu. Natamani ningekuwa na msimamo huu tangu nikiwa mdogo. Lakini siku zote kila kitu hutokea kwa sababu maalumu,”aliongeza.
Licha ya kifo cha kaka yake, Michael Jackson mwaka jana, Janet alisema anayafurahia maisha yake.
“Nina bahati. Kwa sasa nipo huru,”alisema mwanamuziki huyo, aliyetengana na mchumba wake wa miaka mingi, Jermeine Dupri mwaka 2009.
“Siwezi tena kuingizwa kwenye mtego wa mkataba ambao siufurahii. Nipo huru na nafurahia hali hii. Naweza kufanya chochote ninachokitaka,”alisema.
Hivi karibuni, Janet alikutwa akivinjari na Wissam Al Mana, mwanaume anayedaiwa kuwa na umri mkubwa kuliko yeye, akiwa amemzidi kwa miaka kumi.
'Cheryl Cole dhoofulhali, nusura apoteze maisha
LONDON, England
HALI ya mwanamuziki Cheryl Cole wa Uingereza bado tata na ilikuwa almanusura apoteze maisha kutokana na kuugua ugonjwa wa malaria.
Rafiki mmoja wa karibu na mwanamuziki huyo, alilieleza gazeti la Daily Mail la Uingereza wiki hii kuwa, hali Cheryl bado haijawa nzuri.
Cheryl (27) alipatwa na ugonjwa huo alipokuja Tanzania kwa mapumziko akiwa na rafiki yake mpya wa kiume, Derek Hough wiki tatu zilizopita
Kwa mujibu wa rafiki huyo, Cheryl amewekewa vifaa maalumu vya kumsaidia kupumua, kuongezwa maji mwilini na kwamba hawezi kuzungumza. Rafiki huyo alisema Cheryl amelazwa kwenye hospitali moja binafsi ya mjini London, alikopelekwa wiki iliyopita kwa ajili ya matibabu.
“Ilikuwa bado kidogo tumpoteze na bado anaendelea kutibiwa. Amedhoofika sana na ugonjwa huu nusura uyaondoe maisha yake,”alisema rafiki huyo.
“Tunamshukuru Mungu kwamba ugonjwa huu uligundulika mapema. Hadi sasa hawezi kuzungumza. Baadhi ya wakati anakuwa kwenye hali mbaya na wakati mwingine anapata nafuu, anachoweza kufanya ni kulia,”aliongeza rafiki huyo.
Rafiki huuo alisema ilikuwa vigumu kutoa taarifa za maendeleo ya hali ya mwanamuziki huyo kwa sababu ilikuwa ikibadilika mara kwa mara. Alisema walishindwa kuwahakikishia mashabiki kuhusu hali yake.
“Ukweli ni kwamba ilikuwa almanusura tumpoteze mtu wa pekee. Hawezi hata kuzungumza wala kuelewa kinachoendelea kwake. Inasikitisha,”alisema.
“Inasikitisha kumuona Cheryl akiwa katika hali hii. Angeweza kupoteza maisha. Bado hajapona, na wala hajakaribia kupona. Bado yupo kwenye hali mbaya,”aliongeza rafiki huyo.
Aliongeza kuwa, tangu alipolazwa kwenye hospitali hiyo siku sita zilizopita, amekuwa akisaidiwa kupumua kwa kutumia mashine maalumu na amekuwa akiwekewa chupa za maji mara kwa mara.
Kwa mujibu wa rafiki huyo, kinga za mwili za mwanamuziki huyo zimepungua na hawezi kupambana na magonjwa makubwa kama vile malaria.
“Hana kumbukumbu ya leo wala jana. Analia muda wote na huwa hataki mama yake awe mbali naye,”alisema rafiki huyo.
Awali, Cheryl alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha London kabla ya kuhamishiwa kwenye hospitali moja binafsi ya mjini humo.
Mbali na wauguzi, watu wengine pekee wanaoruhusiwa kumuona mwanamuziki huyo ni mama yake mzazi, Joan Callaghan na rafiki yake wa karibu, Derek (25), ambaye amehamia kwenye nyumba ya Cheryl.
Baadhi ya marafiki wa mwanamuziki huyo wamekuwa wakimshutumu mumewe wa zamani, Ashley Cole, mchezaji wa klabu ya Chelsea ya England kuwa ndiye aliyemsababishia hali hiyo baada ya kutengana.
Cole, ambaye aliichezea England katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini, yupo mjini California, Marekani alikokwenda kwa mapumziko na hajawahi kwenda hospitali kumjulia hali mwanamuziki huyo.
Mwanasoka huyo alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, kwa sasa Cheryl sio sehemu ya maisha yake na ameamua kumsahau moja kwa moja.
Naomi Campbell kutoa ushahidi kesi ya Taylor
LONDON, Uingereza
MWANAMITINDO nyota duniani, Naomi Campbell anatarajiwa kutoa ushahidi mbele ya mahakama ya kimataifa katika kesi ya uhalifu wa kivita, inayomkabili Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor.
Msemaji wa mwanamitindo huyo, alisema juzi kuwa, Naomi anatarajiwa kutoa ushahidi huo Julai 29 mwaka huu katika mahakama ya The Hague.
Taylor anatuhumiwa kutumia almasi kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea nchini Sierra Leone na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wamemtaka Naomi kutoa ushahidi kuhusu tuhuma kwamba, alipokea madini ya almasi kutoka kwa Taylor mwaka 1997.
“Yeye ni shahidi, ambaye ametakiwa kusaidia kuthibitisha matukio yaliyotokea mwaka 1997. Naomi ameeleza wazi kuwa, yupo tayari kusaidia sheria ichukue mkondo wake,”alisema msemaji wa mwanamitindo huyo.
“Kwa kuondoa wasiwasi wowote, (Naomi) hatuhumiwi kufanya lolote baya na hahusiki na kesi hiyo,”aliongeza.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wanataka kufahamu iwapo Naomi alipokea madini ya almasi kutoka kwa Taylor katika hafla iliyoandaliwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela nchini humo mwaka 1997.
Awali, msemaji wa mahakama hiyo alisema Naomi alikanusha kupokea madini kutoka kwa Taylor na alikataa kuzungumza na waendesha mashtaka.
Akihojiwa katika kipindi cha Oprah Winfrey Show, Naomi hakuwa tayari kuthibitisha ama kukanusha kwamba alipokea madini hayo, badala yake alisema: “Sitaki kuhusishwa katika kesi ya mtu huyu. Amefanya baadhi ya mambo ya kutisha na sitaki kuiingiza familia yangu kwenye hatari.”
Mbali na Naomi, mwigizaji nyota wa filamu wa Marekani, Mia Farrow naye huenda akatoa ushahidi katika kesi hiyo. Mia ndiye anayedaiwa kumweleza Naomi kuhusu zawadi hiyo ya madini.
Taylor ameshakanusha tuhuma za mashtaka 11 aliyoshtakiwa katika kesi hiyo. Kesi hiyo imeshachukua zaidi ya miaka miwili tangu ilipoanza kusikilizwa.
Kiongozi huyo wa zamani wa Liberia, anatuhumiwa kuuza madini ya almasi na kununua silaha kwa ajili ya magaidi wa RUF wa Sierra Leone, ambao waliendesha vita vilivyosababisha kukatwa mikono na miguu kwa raia kadhaa wan chi hiyo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea kati ya mwaka 1991 hadi 2001.
Kaseja aipasua kichwa Simba
KIPA namba moja wa klabu ya Simba, Juma Kaseja amegoma kujiunga na timu hiyo hadi atakapolipwa pesa zilizobaki za usajili wake wa msimu uliopita.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, kipa huyo alilipwa pesa nusu za usajili msimu uliopita na kuahidiwa kuwa, angemaliziwa baadaye.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja kiasi cha fedha alichoahidiwa kulipwa kipa huyo, fedha alizolipwa awali na zilizobaki.
Lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, Kaseja aliahidiwa kulipwa sh. milioni 25 na Simba baada ya kusajiliwa msimu uliopita akitokea Yanga.
Kabla ya kurejea Simba, Kaseja aliichezea Yanga mwaka juzi baada ya kusajiliwa kwa kitita cha sh. milioni 45.
“Kaseja ameapa kwamba hatajiunga na kambi ya Simba hadi atakapomaliziwa pesa zake zilizobaki, ambazo aliahidiwa na uongozi uliopita,” kilisema chanzo cha habari ndani ya klabu hiyo.
Licha ya kutojiunga na kambi ya timu hiyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, Kaseja amekuwa akifanya mazoezi binafsi kwenye gym na viwanja mbalimbali vya soka.
Mbali na Kaseja, uchunguzi zaidi umebaini kuwa beki Kelvin Yondani naye hajaripoti kwenye kambi ya timu hiyo kutokana na kutomaliziwa baadhi ya pesa anazoidai klabu hiyo.
Wachezaji wengine wanaowaumiza vichwa viongozi wa Simba kutokana na kushindwa kuripoti kambini ni Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Patrick Ochan, ambaye amesajiliwa msimu huu.
Simba ilianza kambi wiki iliyopita kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 21 mwaka huu.
Alipoulizwa kuhusu kutoripoti kwa wachezaji hao, Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi hauna taarifa zozote.
Ndimbo alisema uongozi umeshaanza kufanya mawasiliano na wachezaji hao ili kujua matatizo yao kabla ya kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Hata hivyo, Ndimbo alisema baadhi ya wachezaji wa kigeni wameshawasili nchini na kuanza mazoezi na wenzao. Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Hilary Echessa na Jerry Santo kutoka Kenya.
Ndimbo alisema mazoezi ya timu hiyo yanafanyika chini ya Kocha Msaidizi, Amri Said kabla ya kurejea kwa Kocha Mkuu, Patrick Phiri, aliyeko Zambia kwa mapumziko. Alisema Phiri anatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa wiki hii.
Igangula atangaza vita dhidi ya makomandoo
MGOMBEA uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga, Mbaraka Igangula amesema, iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, hatatoa nafasi kwa wanachama maarufu kwa jina la ‘makomandoo’ kukaa milangoni wakati wa mechi za ligi.
Akizungumza na wanachama wa Yanga wa matawi ya Magomeni, Manzese na Tandale mjini Dar es Salaam juzi, Igangula alisema kazi ya kusimamia mapato ya mechi za ligi itafanywa na wanachama wa matawi. “Napenda kuliweka wazi hili kwamba, iwapo nitachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Yanga, ‘makomandoo’ hawatakuwa na nafasi katika kudhibiti mapato. Kazi hii itafanywa kwa zamu na wanachama wa matawi yote ya Yanga ya Dar es Salaam na watalipwa siku hiyo hiyo,”alisema.
Igangula alisema pia kuwa, asingependa kuiona Yanga ikiwa na viongozi wasiokuwa na kazi na ambao wamekuwa wakiitegemea klabu hiyo kuendesha maisha yao.
Alisema viongozi wa aina hiyo hawapaswi kupewa nafasi kwa sababu badala ya kuiendeleza klabu, watafanya kila njia ili kuitumia kupata fedha za kujikimu.
Mgombea huyo amewaonya pia wanachama wa Yanga wasichague viongozi, ambao wamekuwa wakiwanyonya wachezaji wa timu hiyo kwa kuwaomba pesa ama kuwakata sehemu fulani ya pesa katika malipo yao.
“Wapo baadhi ya viongozi, ambao wamekuwa wakiwaomba wachezaji ‘teni pasenti’ katika malipo yao ya usajili, mishahara na posho mbalimbali. Hawa nao hawatakuwa na nafasi Yanga,”alisema.
Igangula alisema, klabu hiyo inapaswa kuwa na uongozi imara utakaozingatia katiba, kanuni, sera na misingi ya demokrasia katika kuendesha shughuli zake.
Alisema iwapo hayo yatafanyika, itakuwa rahisi kwa wanachama wa Yanga kuwa na umoja, uwazi, usawa, uhuru na kuwepo kwa uwajibikaji katika kuendeleza michezo.
Aliitaja mikakati yake mingine kuwa ni kuhakikisha Yanga inakuwa imara kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ili kuendesha shughuli zake kiufanisi na kutoa huduma kwa wanachama na wachezaji wake.
Alisema Yanga ni klabu kubwa na yenye mahitaji mengi makubwa, hivyo inapaswa kuongozwa na viongozi bora wenye sifa katika kuleta maendeleo ya soka na utawala.
“Kiongozi wa Yanga anapaswa kuwa na kazi ya kuaminika, inayompa kipato cha maisha yake, ili asiitegemee Yanga kumuendeshea maisha yake.
“Pia anapaswa kuwa mwaminifu na mwenye rekodi safi ya kuaminiwa, hasa katika masuala ya fedha, awe na uwezo wa kuongoza, aliyeiva kiungozi na mwenye uwezo wa kubuni miradi yenye kuipa fedha Yanga,”alisema Igangula na kusisitiza kuwa anazo sifa hizo na nyinginezo hivyo anastahili kuiongoza Yanga.
Igangula aliwaahidi wanachama wa matawi hayo kuwa, iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, atarejesha michezo ya wanawake, darts, snuka, ngumi na pia kuimarisha timu za vijana wa umri mbalimbali.
Mgombea huyo alijigamba pia kuwa, chini ya uongozi wake, atahakikisha Yanga inarejesha ubabe wake kwa Simba kwa vile hafurahishwi kuona timu hiyo ikifungwa mara kwa mara na wapinzani wao hao wa jadi.
“Nilipokuwa Kaimu Rais wa Yanga mwaka 2003, tuliweza kuifunga Simba, hivyo uwezo wa kuwafunga tena watani wetu hao ninao, nichagueni ili turejeshe ubabe wetu kwa Simba,”alisema.
Igangula aliahidi kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam, ambao alisema alishaandaa ramani na kuikabidhi kwa uongozi unaomaliza muda wake, lakini ameshangaa kuona hakuna kilichofanyika.
Alisema aliandaa ramani hiyo baada ya kuombwa kufanya hivyo na Mweka Hazina wa zamani wa Yanga, Abeid Abeid kwa ahadi kwamba angesimamia ujenzi wa uwanja huo. Abeid ni mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo.
Aliitaja mikakati yake mingine ndani ya Yanga kuwa ni kuondoa makundi miongoni mwa wanachama na kuimarisha nidhamu kwa wachezaji.
Alisema chini ya uongozi wake, atahakikisha wachezaji wanalipwa kutokana na kujituma kwao na kusisitiza kuwa, hakutakuwa na tofauti kubwa ya mishahara kati ya wachezaji wazalendo na wa kigeni.
“Ninachowaomba wanachama wenzangu ni kunipa ushirikiano na kuepuka kuchagua viongozi waliowahi kuvurunda miaka ya nyuma kwa sababu hawatakuwa na kipya,”alisema.
Igangula pia aliahidi kuwa karibu zaidi na wazee wa klabu hiyo kwa vile ndio wanaoifahamu vyema Yanga na busara zao zinapaswa kutumika katika kuiendeleza.
Mgombea huyo aliahidi kuitisha mara kwa mara mikutano ya wanachama na kuwapa nafasi ya kutoa mchango wa mawazo yao kwa lengo la kuifikisha mbali zaidi klabu hiyo.
Alisema kamwe hatokuwa mwoga wa kuitisha mikutano ya wanachama kama ilivyokuwa kwa viongozi wengi waliopita kwa vile kufanya hivyo ni kuwanyima nafasi wanachama ya kuitumikia klabu yao.
Igangula ni mmoja wa wagombea watano waliopitishwa kuwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa Yanga, unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ukumbi wa PTA uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo ni rais wa zamani wa klabu hiyo, Francis Kifukwe, Abeid Abeid, Llyord Nchunga na Edgar Chibula
Igangula, aliwahi kuwa makamu wa rais wa Yanga mwaka 2001 hadi 2003. Pia alikuwa kaimu rais wa Yanga mwaka 2003 na mwenyekiti wa kamati ya muafaka.
K-SHYINA: Acheni kutukatisha tamaa wasanii chipukizi
KWA kawaida, safari ya wasanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini hutawaliwa na vikwazo vingi, vikiwemo kukatishwa tamaa na nyimbo zao kuibwa na wasanii wakongwe.
Lakini vikwazo vikubwa zaidi ni kukosa uwezo wa kurekodi nyimbo zao studio kutokana na kutokuwa na pesa ama watangazaji wa vipindi vya muziki kutopiga nyimbo zao hadi wapewe ‘kitu kidogo’.
Hayo ndiyo matatizo yanayomkuta msanii chipukizi wa muziki huo, Kelvin Stephano, ambaye ni maarufu kwa jina la K-Shyina, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Licha ya kutunga na kurekodi kibao kitamu na chenye mashairi yenye mvuto, kinachokwenda kwa jina la ‘Uzuri wa sura’, K-Shyina hajawahi kusikika hata siku moja kwenye vituo vya radio.
Kila anapopeleka CD za wimbo huo kwenye vituo mbalimbali vya radio, hupewa ahadi za ‘kitapigwa kesho’, lakini siku zinakwenda bila kibao hicho kusikika.
Adha hiyo ni ya pili kumkumba msanii huyo mwenye umri wa miaka 20. Adha ya kwanza ilikuwa ‘kuliwa’ pesa zake kila alipokwenda studio kulipia gharama za kurekodi wimbo huo.
“Nimeshawahi kuliwa pesa zangu mara nne katika studio tofauti, kubwa na ndogo. Nilikuwa napewa ahadi ya ‘njoo kurekodi kesho’ hadi nikakata tamaa na kuzisamehe pesa zangu,”alisema msanii hiyo alipozungumza na Burudani wiki hii mjini Dar es Salaam.
Mbali na kuliwa pesa zake, K-Shyina alisema amekuwa akikutana na kauli mbalimbali zenye lengo la kumkatisha tamaa katika safari yake hiyo ya kimuziki.
“Wasanii tunaochipukia tumekuwa tukikumbana na kauli nyingi za kutukatisha tamaa, hasa katika maeneo tunayoishi. Utakuta wengine wanakwambia, ‘kuimba anaimba, lakini kutoka hatoki’. Kauli hizi zinakatisha tamaa, lakini sikubali kushindwa,”alisema.
Msanii huyo aliitaja adha nyingine inayowakumba wasanii chipukizi kuwa ni pamoja na kuibwa kwa nyimbo zao, pale wanapowafuata wasanii wakongwe ili wawape msaada wa kiusanii.
“Ukimfuata msanii mkongwe kumuomba msaada, anaweza kukwambia ‘hebu niimbie wimbo wako’. Baada ya siku mbili tatu, utausikia wimbo huo redioni ukiwa umebadilishwa mashairi, lakini sauti ni ileile,”alisema. K-Shyina (18) alikiri kuwa, bila ya kuwa na mdhamini, ni vigumu kwa msanii chipukizi kuweza kupata mafanikio katika muziki huo kwa sababu gharama za kurekodi wimbo mmoja ni kubwa.
Amewataka wasanii nchini kupendana na kujenga tabia ya kusaidiana, badala ya kukatishana tamaa ama kujenga chuki baina yao.
“Nawaomba wasanii, ambao kwa sasa wapo juu, watusaidie sisi tuliopo chini badala ya kutuvunja nguvu ama kutuibia nyimbo zetu,” alisema msanii huyo mwenye elimu ya sanaa aliyoipata katika kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
“Nawaomba pia wasanii wenzangu, tuwe mfano wa kuigwa na jamii kwa kuielimisha juu ya mambo mbalimbali muhimu, lakini tunapofanya hivyo, isiwe tena sisi ndio watendaji wa hayo mambo,”aliongeza. Pia amewataka wasanii chipukizi wasikatishwe tamaa na vikwazo mbalimbali, ambavyo wamekuwa wakikutana navyo, badala yake waongeze bidii ya kuwasaka wadhamini ili waweze kutekeleza malengo yao.
Msanii huyo, anayevutiwa na wasanii Diamond, AY, Matonya na K-Sher alisema ameamua kujitosa kwenye fani hiyo baada ya kubaini kuwa, ana kipaji cha kutunga na kuimba nyimbo.
Akizungumzia kibao chake cha ‘Uzuri wa sura’, alichokirekodi kwa gharama zake katika studio za Waso Records, msanii huyo alisema ni kisa cha kweli alichosimuliwa na rafiki na kilimtokea mtu anayemfahamu.
Katika kibao hicho, K-Shyina anamlalamikia mwanadada mrembo kwa sura na anayependeza kwa mavazi, lakini tabia yake mbaya ilimsababishia kuambukizwa ugonjwa hatari wa ukimwi.
“Kwa kweli hiki ndicho kibao changu cha kwanza. Ndio kwanza naanza. Bado sijajulikana na wala kupata mafanikio. Nataka niwe mwanamuziki maarufu kama walivyo wasanii wengine,”alisema.
MAMBO YA SIKINDE
MPIGA gita la besi wa Mlimani Park Orchestra, Charles John Ngosha akifanya vitu vyake wakati wa onyesho hilo.
MHARIRI wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor akimkabidhi zawadi ya fulana shabiki wa Sikinde, Shabani Jiwe kutokana na kutokosekana kwenye maonyesho ya bendi hiyo yanayofanyika kila siku za Jumapili kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
MWIMBAJI nyota na mkongwe wa Mlimani Park Orchestra, Hassan Bitchuka akiimba moja ya vibao vya zamani vya bendi hiyo wakati wa onyesho hilo.
WAPULIZA trumphet wa bendi ya Mlimani Park, Mbaraka Othman (kushoto) na Hamisi Milambo wakifanya vitu vyao wakati wa onyesho la juzi.
WAPULIZA trumphet wa bendi ya Mlimani Park, Mbaraka Othman (kushoto) na Hamisi Milambo wakifanya vitu vyao wakati wa onyesho la juzi.
MHARIRI wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor (kulia) akizunguma na wanamuziki pamoja na
mashabiki wa bendi ya Mlimani Park Orchestra wakati wa onyesho lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Kushoto ni msemaji mkuu wa bendi hiyo, Jimmy Chika na katikati na mwanamuziki Hassan Kunyata. (Picha zote na Emmanuel Ndege).
mashabiki wa bendi ya Mlimani Park Orchestra wakati wa onyesho lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Kushoto ni msemaji mkuu wa bendi hiyo, Jimmy Chika na katikati na mwanamuziki Hassan Kunyata. (Picha zote na Emmanuel Ndege).
WAIMBAJI wa bendi ya Mlimani Park Orchestra wakiwajibika jukwaani wakati wa onyesho hilo. Kutoka kushoto ni Hassan Kunyata, Abdalla Hemba na Shaabani Dede.
MAMBO YA SIKINDE NA UHURU
MHARIRI wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor (kushoto) akikabidhi zawadi ya fulana yenye nembo ya magazeti ya Uhuru na Mzalendo kwa mwanadada, Kibibi Saidi aliyeibuka kuwa shabiki aliyecheza nyimbo nyingi za bendi ya Mlimani Park Orchestra wakati wa onyesho lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
MPULIZA saxaphone wa Sikinde, Shaabani Lendi akicheza muziki na mmoja wa mashabiki wa bendi hiyo.
Uhuru yaing'arisha Sikinde
MHARIRI wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor (kushoto) akikabidhi fulana yenye nembo za magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kwa kiongozi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, Habibu Abbas 'Jeff' (kulia) wakati wa onyesho la bendi hiyo lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni msemaji mkuu wa bendi hiyo, Jimmy Chika na wa pili kulia ni mwimbaji, Hassan Kunyata. (Picha na Emmanuel Ndege).
KAMPUNI ya Uhuru Publications Limited (UPL), wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, imetoa fulana 20 kwa wanamuziki wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra.
Fulana hizo zilikabidhiwa kwa kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ na Mhariri wa gazeti la Burudani, Rashid Zahor wakati wa onyesho lililofanyika juzi kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fulana hizo, Zahor alisema kampuni yake imefikia uamuzi huo ili kuonyesha jinsi ilivyo bega kwa bega na bendi za muziki wa dansi nchini katika masuala yanayohusu burudani.
Zahor, maarufu kwa jina la Ramoza alisema, kampuni hiyo kupitia magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, imejitolea kuchapisha mara kwa mara taarifa zinazohusu bendi hiyo ili mashabiki waweze kupata habari zake.
“Sikinde ni moja ya bendi kongwe na zinazoheshimika hapa nchini, ikiwa na wanamuziki wengi mahiri, hivyo kupitia magazeti yetu haya matatu, tutakuwa tukichapisha habari zake mara kwa mara,”alisema.
Kwa upande wake, Jeff aliishukuru UPL kwa kuonyesha mshikamano na bendi yake, ikiwa ni pamoja na kuwajali wanamuziki wake na kuripoti habari zake mara kwa mara.
“Msaada huu unaweza kuonekana ni mdogo, lakini kwetu sisi ni mkubwa kwa vile umeonyesha jinsi magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani yanavyoijali bendi yetu,”alisema.
Mbali na kuipatia Mlimani Park Orchestra fulana hizo, UPL pia iliwazawadia mashabiki wawili, fulana moja kila mmoja kutokana na kuonyesha mapenzi makubwa kwa bendi hiyo.
Mmoja wa mashabiki waliozawadiwa fulana hizo ni Shabani Jiwe, ambaye ni nadra kukosekana kwenye maonyesho ya bendi hiyo yanayofanyika kila Jumapili kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo.
Mwingine ni Kibibi Saidi, ambaye alitia fora katika onyesho la juzi kutokana na kujimwaga stejini kucheza vibao vyote vilivyopigwa na bendi hiyo. Stella alijitambulisha kuwa ni shabiki wa Sikinde tangu mwaka 1978.
Katika muda wote wa onyesho hilo, wanamuziki wa Mlimani Park Orchestra walikuwa wamevalia fulana zilizotolewa na UPL, zenye nembo ya magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Wakati huo huo, uongozi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra, umeahidi kutunga wimbo maalumu kwa ajili ya magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya viongozi wa Mlimani Park Orchestra, uongozi wa kundi la Sikinde Family na kamati ya habari ya bendi hiyo.
Mkuu wa mirindimo wa bendi hiyo, Hassan Bitchuka alisema wakati wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni kuwa, wameamua kutunga wimbo huo kwa lengo la kuuenzi mchango wa magazeti hayo kwa Mlimani Park Orchestra.
Sunday, July 11, 2010
HISPANIA BINGWA WA DUNIA
HISPANIA jana ilitwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Uholanzi bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Bao pekee na la ushindi la Hispania lilipachikwa wavuni na kiungo Andres Iniesta katika muda wa nyongeza wa dakika 30 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.
Iniesta alifunga bao hilo dakika ya 116 baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Cesc Fabregas na kufumua shuti lililompita kipa Maarten Stekelenburg wa Uholanzi.
Thursday, July 8, 2010
Papic kutangaza kikosi chake leo
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Kostadin Papic leo anatarajia kukutana na viongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuzungumzia usajili wa wachezaji wa kigeni na wa ndani.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema jana kuwa, kikao hicho kinatarajiwa kufanyika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Mwalusako alisema katika kikao hicho, Papic anatarajiwa kuwasilisha majina ya wachezaji watano wa kigeni watakaosajiliwa na Yanga msimu ujao na wengine 25 wa hapa nchini.
Kwa mujibu wa Mwalusako, kikao hicho ndicho kitakachohitimisha orodha ya usajili wa wachezaji wa Yanga kabla ya kuwasilishwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kikao hicho kinafanyika siku mbili baada ya Papic kurejea nchini juzi kutoka Serbia, alikokwenda kwa mapumziko mara baada ya ligi kuu ya msimu uliopita kumalizika.
Miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaotarajiwa kusajiliwa na Yanga msimu ujao ni beki wa kati, Isack Boakye, kiungo Ernest Boakye, mshambuliaji Keneth Asamoah kutoka Ghana na kipa Ivan Knezevic kutoka Serbia.
Pia kumezuka mvutano baina ya viongozi kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji wa kigeni, walioichezea timu hiyo msimu uliopita, ambapo baadhi wanataka waachwe wote wakati wengine wanataka wabaki wawili.
Kwa mujibu wa kanuni mpya za usajili za TFF, klabu zote za ligi kuu zinatakiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni. Mchezaji wa tano wa kigeni wa Yanga ni kipa Yaw Berko kutoka Ghana.
Mchezaji pekee wa kigeni mwenye mkataba na Yanga hadi sasa ni beki John Njoroge kutoka Kenya. Mkataba wa kipa Berko umeshamalizika, lakini uongozi umeamua kumuongezea mkataba mwingine.
Wachezaji wa kigeni waliotemwa na klabu hiyo ni Robert Jama Mba,Steven Bengo, Boniface Ambani, Moses Odhiambo, Obren Curkovic, Honore Kabongo, Wisdom Ndlovu na George Owino.
Michuano ya ligi kuu msimu ujao imepangwa kuanza Agosti 21 mwaka huu. Mazoezi ya Yanga kwa ajili ya ligi hiyo yamepangwa kuanza Julai 15.
Igangula, Kifukwe kazi ipo Yanga
TAKUKURU yawawekea mitego wagombea
WAKATI wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu ya Yanga wameanza kampeni, umezuka mchuano mkali kati ya wagombea wawili wa nafasi ya mwenyekiti, Mbaraka Igangula na Francis Kifukwe.
Kuzuka kwa mchuano huo kumekuja baada ya Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumrejesha Kifukwe kwenye uchaguzi huo baada ya awali kutemwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.
Kifukwe na mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Abeid Abeid waliondolewa kwenye uchaguzi huo baada ya kuwekewa pingamizi na baadhi ya wanachama wa Yanga.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Igangula na Kifukwe ndio pekee wanaoungwa mkono na wanachama wa Yanga kutokana na kuiongoza klabu hiyo kwa nyakati tofauti miaka ya nyuma.
Kutokana na wagombea hao kuwa na wafuasi wengi, wanachama wa Yanga kwa sasa wamewanyika makundi mawili, kila moja likiwafanyia kampeni wagombea hao wawili kwa ajili ya kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa, Igangula ndiye mwenye wafuasi wengi, ambao wamekuwa wakitembelea matawi mbalimbali ya klabu hiyo kwa ajili ya kumfanyia kampeni.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Igangula anakubalika katika matawi mengi ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam wakati Kifukwe anakubalika na wanachama wa makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani.
Igangula aliwahi kuwa makamu wa rais wa Yanga chini ya uongozi wa Tarimba Abbas kabla ya kuteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo na baadaye kupinduliwa na wanachama.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigoma jana, Igangula alisema amejipanga vyema kuhakikisha anaitwaa nafasi hiyo kwa vile ana uzoefu wa muda mrefu wa uongozi ndani ya Yanga.
“Mimi nipo Kigoma kikazi, lakini ninayo timu yangu inayoondesha kampeni kwa ajili yangu na mambo hadi sasa yanakwenda vizuri,”alisema mgombea huyo.
Wagombea wengine wanaowania nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi huo ni Lloyd Nchunga, Abeid Abeid na Edgar Chibura.
Mchuano mwingine mkali upo kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti, inayowaniwa na Ayoub Nyenzi, Constantine Maligo na Davis Mosha. Katika nafasi hiyo, wagombea wanaoonekana kuungwa mkono na wanachama wengi ni Nyenzi na Mosha.
Waliopitishwa kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji katika uchaguzi huo ni Yusuf Yasin, Robert Kasela, Shaaban Mohamed, Omary Ndula, Atufwigwegwe Mwakatumbula, Evance Matee, David Peter, Majid Simba, Mzee Yusuf, Ramadhan Kampira, Edgar Fongo, Jackson Maagi, Mwinyi Mangara, Hamis Ambari na Mohamed Bhinda.
Wengine ni Isaac Mazwile, Paul Malume, Sarah Ramadhan, Salim Rupia, Dk. David Ruhago, Titto Ossoro, Charles Mugondo, Ally Mayay, Pascal Kihanga, Ismail Idrissa, Lameck Nyambaya, John Mayala, Theonest Rutashoborwa na George Manyama.
Uchaguzi mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika Julai 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa PTA uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, John Mkwawa alitangaza juzi kuwa, kampeni kwa wagombea zilipaswa kuanza rasmi jana hadi Julai 17 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imesema, imeanza kuwafuatilia kwa karibu wagombea wa uongozi katika klabu ya Yanga kwa lengo la kuwashughulikia watoa rushwa.
Mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo alisema jana kwa njia ya simu kuwa, mgombea yeyote atakayekamatwa akitoa rushwa kwa wanachama, atachukuliwa hatua za kisheria.
WAKATI wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu ya Yanga wameanza kampeni, umezuka mchuano mkali kati ya wagombea wawili wa nafasi ya mwenyekiti, Mbaraka Igangula na Francis Kifukwe.
Kuzuka kwa mchuano huo kumekuja baada ya Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumrejesha Kifukwe kwenye uchaguzi huo baada ya awali kutemwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga.
Kifukwe na mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Abeid Abeid waliondolewa kwenye uchaguzi huo baada ya kuwekewa pingamizi na baadhi ya wanachama wa Yanga.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Igangula na Kifukwe ndio pekee wanaoungwa mkono na wanachama wa Yanga kutokana na kuiongoza klabu hiyo kwa nyakati tofauti miaka ya nyuma.
Kutokana na wagombea hao kuwa na wafuasi wengi, wanachama wa Yanga kwa sasa wamewanyika makundi mawili, kila moja likiwafanyia kampeni wagombea hao wawili kwa ajili ya kushika nafasi hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa, Igangula ndiye mwenye wafuasi wengi, ambao wamekuwa wakitembelea matawi mbalimbali ya klabu hiyo kwa ajili ya kumfanyia kampeni.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Igangula anakubalika katika matawi mengi ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam wakati Kifukwe anakubalika na wanachama wa makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani.
Igangula aliwahi kuwa makamu wa rais wa Yanga chini ya uongozi wa Tarimba Abbas kabla ya kuteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo na baadaye kupinduliwa na wanachama.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigoma jana, Igangula alisema amejipanga vyema kuhakikisha anaitwaa nafasi hiyo kwa vile ana uzoefu wa muda mrefu wa uongozi ndani ya Yanga.
“Mimi nipo Kigoma kikazi, lakini ninayo timu yangu inayoondesha kampeni kwa ajili yangu na mambo hadi sasa yanakwenda vizuri,”alisema mgombea huyo.
Wagombea wengine wanaowania nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi huo ni Lloyd Nchunga, Abeid Abeid na Edgar Chibura.
Mchuano mwingine mkali upo kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti, inayowaniwa na Ayoub Nyenzi, Constantine Maligo na Davis Mosha. Katika nafasi hiyo, wagombea wanaoonekana kuungwa mkono na wanachama wengi ni Nyenzi na Mosha.
Waliopitishwa kuwania nafasi za ujumbe wa kamati ya utendaji katika uchaguzi huo ni Yusuf Yasin, Robert Kasela, Shaaban Mohamed, Omary Ndula, Atufwigwegwe Mwakatumbula, Evance Matee, David Peter, Majid Simba, Mzee Yusuf, Ramadhan Kampira, Edgar Fongo, Jackson Maagi, Mwinyi Mangara, Hamis Ambari na Mohamed Bhinda.
Wengine ni Isaac Mazwile, Paul Malume, Sarah Ramadhan, Salim Rupia, Dk. David Ruhago, Titto Ossoro, Charles Mugondo, Ally Mayay, Pascal Kihanga, Ismail Idrissa, Lameck Nyambaya, John Mayala, Theonest Rutashoborwa na George Manyama.
Uchaguzi mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika Julai 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa PTA uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, John Mkwawa alitangaza juzi kuwa, kampeni kwa wagombea zilipaswa kuanza rasmi jana hadi Julai 17 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imesema, imeanza kuwafuatilia kwa karibu wagombea wa uongozi katika klabu ya Yanga kwa lengo la kuwashughulikia watoa rushwa.
Mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo alisema jana kwa njia ya simu kuwa, mgombea yeyote atakayekamatwa akitoa rushwa kwa wanachama, atachukuliwa hatua za kisheria.
Mrembo wa Temeke kusakwa kesho
WAREMBO 14 kesho wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji la mrembo wa Kanda ya Temeke 2010 katika shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya BMP Promotions, Benny Kisaka alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, warembo hao wanatoka katika vitongoji vya Kurasini na Chang’ombe.
Benny alisema ana hakika mshindi wa kanda hiyo ndiye atakayenyakua taji la mrembo wa Tanzania mwaka huu, baada ya kulikosa taji hilo kwa miaka miwili.
Kwa mujibu wa Benny, karibu washiriki wote wa shindano hilo wana sifa na vigezo vinavyotakiwa, hivyo alitabiri kuwa ushindani utakuwa mgumu.
Benny alisema kamati ya Miss Temeke ilikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa, wanapatikana warembo bomba kwa ajili ya kuwania taji hilo mwaka huu ili mshindi afanye vizuri katika shindano la Miss Tanzania.
Kabla ya kuanza kwa shindano hilo, Benny alisema washiriki watafanya onyesho maalumu la muziki walilofundishwa na Caroline Zayumba na Dickson Guntram kutoka kundi la THT.
Benny alisema shindano hilo litapambwa kwa burudani mbalimbali za muziki kutoka kwa wasanii Banana Zorro na baba yake, Zahir Ally Zorro pamoja na wacheza shoo wa bendi ya Twanga Pepeta International.
Taji la Miss Temeke kwa sasa linashikiliwa na Sia Ndaskoy.
K-SHER: Bongo Fleva ni sawa na ladha la Big G
MWIMBAJI machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khadija Shaaban ‘K-Sher’ amesema anapenda sana kuimba nyimbo zinazohusu mapenzi kwa lengo la kuisaidia jamii.
Akizungumza katika kipindi cha Friday Nite Live kilichorushwa hewani na luninga ya East Africa mwishoni mwa wiki iliyopita, K-Sher alisema nyimbo za aina hiyo zinagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya jamii.
K-Sher alisema kamwe hapendi kuimba nyimbo zinazozungumzia matukio yaliyowahi kumkuta katika maisha yake kama wanavyofanya wasanii wengine wa muziki huo.
Mbali na kupendelea zaidi kuimba nyimbo za mapenzi, msanii huyo alisema baadhi ya nyimbo zake hutungiwa na wasanii wengine. Alitoa mfano wa nyimbo hizo kuwa ni ‘Usinicheke’, uliotungwa na msanii Spider.
Msanii huyo aliyemaliza elimu ya kidato cha sita hivi karibuni alikiri kuwa, fani ya muziki imemuwezesha kupata manufaa mengi kimaisha ikiwa ni pamoja na uwezo kimapato.
“Namshukuru Mungu kuwa kwa sasa nina uwezo wa kununua nguo ya thamani yoyote, lakini kuna vitu ambavyo nimekuwa nikivipa kipaumbele,”alisema.
K-Sher alielezea masikitiko yake kuona kuwa, wapo baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ambao wamekuwa wakitunga na kuimba nyimbo za kuvutia, lakini hawapati mafanikio.
Alisema cha ajabu ni kuona kwamba, wale wasanii wanaotunga na kuimba nyimbo kwa mipigo ile ile ndio wanaopata mafanikio na kuvuma pembe zote za nchi.
“Sijui tuseme watanzania hawaujui muziki! Inashangaza kuona msanii anaimba nyimbo kwa melody ileile, lakini nyimbo zake zinavuma sana.
“Lakini wapo wanaoimba nyimbo zao kwa melody tofauti na kutoa ujumbe mzito kwa jamii, lakini nyimbo zao hazikubaliki,”alisema msanii huyo.
Alimmwagia sifa kemkem msanii mwenzake wa kike, Vumilia kwa kuimba nyimbo zenye mvuto na ambazo alisema si rahisi kuchujuka baada ya muda mfupi.
“Kwa kweli namzimia sana Vumilia. Tazama nyimbo zake za ‘Utanikumbuka’ na ‘Kama ni umaskini’. Ni nyimbo zenye mvuto, mashairi yake yanavutia na sauti yake ni tamu kuisikiliza,”alisema.
Alisema binafsi kila anapoamka asubuhi na kukerwa na jambo fulani, huwa anapenda kusikiliza nyimbo hizo kwa vile zinamfariji na kumpa liwazo murua.
Pamoja na mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwa wasanii nchini kutokana na muziki huo, K-Sher alisema si rahisi kwa muziki wao kudumu kwa muda mrefu.
Aliufananisha muziki wa kizazi kipya kuwa ni sawa na utamu wa Big G, ambayo baada ya kutafunwa kwa muda mfupi, humalizika na kuwa haina ladha tena.
“Hivi ndivyo muziki wetu ulivyo. Ni sawa na Big G. Ukishaitafuna na utamu kumalizika, haina ladha tena mdomoni,”alisema.
Kwa sasa, msanii huyu anatamba kwa kibao chake kipya kinachojulikana kwa jina la ‘Nastahili kupendwa’, ambacho ni miongoni mwa vibao vipya vitakavyokuwemo kwenye albamu ya kundi la Tip Top Connection.
Kundi hilo linajiandaa kufanya ziara katika mikoa kadhaa nchini kwa ajili ya kuitangaza albamu hiyo, itakayowajumuisha wasanii wengine kama vile Madee, Tundaman, Cassim Mganga na Dezo.
Mbali na kuitangaza albamu hiyo mikoani, K-Sher alisema kundi hilo pia linatarajia kufanya ziara katika nchi jirani za Kenya na Uganda.
K-Sher alisema japokuwa kundi lao lipo chini ya Meneja Babu Tale, wao ndio kama waajiri wake kwa sababu ndio wanaofanyakazi zinazomwezesha kupata kipato.
“Sisi ndio mameneja wa Babu Tale kwa sababu ndio tunaotoa kazi na kumlipa,”alisema.
REDONDO: Nitatisha zaidi nikiwa Azam FC
WAKATI usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara ukiendelea, mashabiki wengi wa soka wameanza kuitabiria makubwa Azam FC kutokana na kusajili wachezaji wengi nyota. Miongoni mwa wachezaji hao, ni kiungo mshambuliaji, Ramadhani Chombo ‘Redondo’. Katika makala hii iliyoandikwa na Mwandishi Wetu Athanas Kazige, mchezaji huyo kutoka Simba, anaelezea mambo mbalimbali kuhusu maisha yake kisoka.
SWALI:Nini kimekufanya uondoke ndani ya kikosi cha Simba wakati msimu ujao ungepata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya klabu bingwa Afrika?
JIBU: Nimeondoka Simba kwa ajili ya kutafuta maslahi mazuri zaidi, ambayo nimeahidiwa na uongozi wa Azam FC. Kama ni nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, naamini nitaipata nikiwa Azam kwa kushirikiana na wenzangu kutwaa ubingwa wa ligi msimu ujao.
SWALI: Inaelekea viongozi wa Azam wamekuahidi donge nono maana ulipata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa klabu ya Haras Al-Hadoud ya Misri, lakini umeitolea nje.
JIBU:Siwezi kukupa jibu la swali hilo kwa sababu linahusu masuala yangu binafsi na mwajiri wangu. Lakini safari ya kwenda Misri bado haijakufa. Bado naendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo hadi sasa.
SWALI: Umejifunza nini katika kipindi chote ulichoichezea klabu ya Simba, ambayo ni miongoni mwa klabu mbili kongwe hapa nchini?
JIBU: Yapo mambo mengi niliyojifunza ndani ya Simba. Lakini kikubwa ni changamoto ya kujituma ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Lakini pia nimeweza kuingia kwenye historia ya klabu hiyo kwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Simba kuweka historia ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu kabla haijamalizika.
Hakuna jambo, ambalo ninajivunia zaidi kama kuchangia ushindi wa Simba katika ligi kuu kwani tuliweka rekodi ya kutofungwa hata mechi moja. Hili kwangu ni jambo kubwa. Naamini mchango wangu ulisaidia mafanikio haya.
SWALI: Kwa nini klabu hizi kubwa zinapofungwa, huwa kunatokea tuhuma kwa baadhi ya wachezaji kwamba wamehujumu timu? Ulikuwa ukijisikiaje ulipohusishwa na tuhuma za aina hii?
JIBU:Namshukuru Mungu kwamba haijawahi kutokea hata siku moja mimi kuhusishwa na tuhuma za kuhujumu timu ama kupanga matokeo. Binafsi nafahamu vyema maana ya uaminifu na uadilifu katika kazi ndio sababu pia sijawahi kugombana hata siku moja na kiongozi, mchezaji ama mwanachama wa klabu hiyo.
SWALI: Umesema kuondoka kwako Simba kumekufanya uwe huru. Je, ni kipi kilichokuwa kinakupa wakati mgumu katika klabu hiyo?
JIBU: Hakuna kilichokuwa kikinipa wakati mgumu Simba, isipokuwa kulikuwa na watu wenye tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao. Ninachoweza tu kusema ni kwamba hivi sasa nipo huru na ninaamini nitaonyesha uwezo mkubwa zaidi katika ligi kuu ya msimu ujao.
SWALI: Kipi kilichowahi kukukera na kukunyima raha katika kipindi chote ulichokuwa ukiichezea Simba?
JIBU:Kwa kweli hakuna kitu kama hicho. Lakini kama wapo watu, ambao kwa namna moja ama nyingine nilitokea kuwaudhi, nawaomba wanisamehe kwa vile hakuna binadamu aliyekamilika. Inawezekana kabisa niliwafanyia maudhi bila kujitambua.
SWALI: Una matarajio gani katika timu yako mpya ya Azam, ukiwa na wachezaji wenzako wapya kama vile Mrisho Ngasa na Jabir Azizi?
JIBU: Nina hakika msimu ujao wa ligi nitacheza kwa kiwango cha juu zaidi ili niweze kupata ofa ya kujaribiwa nje ya nchi na pia kuipa ubingwa timu yangu mpya. Nina ndoto kubwa ya kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Kinachonifurahisha zaidi ni kuona kwamba ndani ya Azam wapo wachezaji wengine wazuri wengi kama vile Ngasa, Jabir, John Boko, Salum Swedi na wengineo. Naamini tukishirikiana vyema, hakuna kitakachoikosesha Azam ubingwa.
Kadhalika nina furaha kubwa ya kuona ndani ya kikosi cha Azam kuna wachezaji wengi wazuri wakiwemo Ngasa,Boko,Salum Sued na wengine ambao nina hakika tutaweza kuifikisha mbali kwenye ligi kuu.
SWALI:Una maoni gani kuhusu kumalizika kwa mkataba wa kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo?
JIBU: Binafsi nitamkumbuka sana kocha huyu kwani ameweza kutupa mafanikio makubwa wachezaji wa Tanzania na pia kutuelewesha vyema jinsi, ambavyo mchezo huu unavyoweza kuwa na manufaa kwetu kimaisha, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo wengi tuliichukulia soka kama burudani.
Chini ya Maximo, tuliweza kucheza na timu nyingi ngumu za Afrika kama vile Cameroon, Senegal na Ivory Coast na kufanya vizuri. Pia tuliweza kucheza na mabingwa wa zamani wa dunia, Brazil na japokuwa tulifungwa, tuliweza kujifunza mengi kutoka kwao.
Pia napenda kuwapongeza Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kufanikisha ujenzi wa uwanja mpya wa Taifa wa Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete kwa kuhamasisha kwa kiasi kikubwa mashabiki wa soka nchini kuipenda timu yao ya taifa. SWALI: Una maoni gani kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi ya waamuzi nchini kwamba wamekuwa wakipindisha kwa makusudi sheria za mchezo huo kwa sababu ya rushwa ama mapenzi kwa timu kubwa?
JIBU: Ni kweli baadhi ya waamuzi nchini wamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mchezo huo kutokana na kuvurunda katika uchezeshaji wao. Wengi wanashindwa kuheshimu sheria 17 za soka kwa sababu tu ya mapenzi ama kuhadaiwa na rushwa.
Nawashauri waamuzi wetu wabadilike kwa sababu wakiendelea hivyo, soka ya Tanzania itaendelea kudumaa badala ya kusonga mbele. Hatutaweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa kwa sababu timu zetu zimezoea kubebwa katika ligi za nyumbani.
Ni vizuri bingwa wa nchi apatikane kutokana na uwezo wake kisoka ili aweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa. Akipatikana bingwa kwa kubebwa, ni rahisi kuvurunda kwenye michuano ya kimataifa kwa sababu huko hakuna kubebwa.
Thursday, July 1, 2010
Ni Brazil vs Uholanzi, Ghana vs Uruguay
Mensah, Sarpei, Boateng hatarini kucheza
Dunga akiri pambano litakuwa gumu kwao
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MICHUANO ya soka ya fainali za Kombe la Dunia, inaingia katika hatua ya robo fainali leo wakati timu nne zitakapoteremka dimbani katika viwanja viwili tofauti.
Katika mechi hizo, Brazil itamenyana na Uholanzi kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Port Elizabeth wakati Ghana itavaana na Uruguay kwenye uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Brazil ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuichapa Chile mabao 3-0 katika raundi ya pili wakati Uholanzi ilitinga robo fainali baada ya kuishinda Slovakia mabao 2-1.
Nao wawakilishi pekee wa Afrika waliosalia katika fainali hizo, Ghana walifuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa Marekani mabao 2-1 wakati Uruguay iliitoa Korea Kusini kwa idadi hiyo ya mabao.
Pambano kati ya Brazil na Uholanzi ndilo linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka duniani, kufuatia timu hizo kuonyesha kandanda ya kuvutia tangu michuano hiyo ilipoanza Juni 11 mwaka huu.
Kocha Mkuu wa Brazil, Carlos Dunga alikiri juzi kuwa, pambano hilo litakuwa gumu kwao kutokana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na Uholanzi katika hatua za awali.
“Tunaelewa Uholanzi ni timu ngumu kuifunga na kucheza nayo,”alisema Dunga. “ Mchezo wao hauna tofauti na soka ya Amerika ya Kusini. Hawachezi soka ya kujihami na hutumia pasi ndefu. Wanacheza soka ya ufundi na tutalazimika kuwa tayari kukabiliana nao.”
Brazil haijakumbana na timu ngumu hadi sasa. Ilitwaa uongozi wa kundi G baada ya kuzifunga Korea Kaskazini mabao 2-1, ikaichapa Ivory Coast mabao 3-1 kabla ya kutoka suluhu na Ureno.
“Sasa ni mechi kati ya timu mbili zenye utamaduni tofauti wa kucheza soka na zenye wachezaji wa kiwango cha juu,” alisema nahodha wa Brazil, Lucio.
Beki huyo mkongwe kwenye kikosi cha Brazil alikiri kuwa, kadri michuano hiyo inavyosonga mbele, mechi zinakuwa ngumu zaidi.
Uholanzi haijawahi kutwaa Kombe la Dunia, lakini imefanya vizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Denmark, Japan, Cameroon na Slovakia.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Brazil kukutana na Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia, ambapo Brazil ilishinda mechi mbili na kufungwa moja.
Uholanzi iliishinda Brazil katika raundi ya pili ya michuano ya mwaka 1974 nchini Ujerumani kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 katika robo fainali mwaka 1994. Brazil pia iliishinda Uholanzi hatua ya nusu fainali katika michuano ya mwaka 1889 iliyofanyika Ufaransa.
Katika mechi hiyo, Brazil huenda ikawakosa viungo wake, Elano na Felipe Melo, ambao ni majeruhi. Elano alishindwa kufanya mazoezi Jumanne iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
Brazil pia itamkosa Ramires, aliyechukua nafasi ya Melo, kufuatia kuwa na kadi mbili za njano.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Uholanzi, Bert van Marwijk alisema ni vigumu kutabiri pambano hilo kwa vile timu hizo mbili zina historia ya kufungana kwa zamu.
Tegemeo kubwa la Uholanzi litakuwa kwa washambuliaji wake, Robin van Persie, Ryan Babel, Dirk Kuyt na Arjen Robben.
Wasiwasi wa Ghana kumkosa mshambuliaji wake nyota, Asamoah Gyan umepungua baada ya mchezaji huyo juzi kufanya mazoezi na wenzake.
Asamoah, nahodha John Mensah, kiungo Kevin Prince Boateng na beki Hans Sarpei walishindwa kufanya mazoezi mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
Kocha Milovan Rajevac wa Ghana alisema juzi kuwa, Mensah anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na hawezi kufanya mazoezi na amekuwa akisaidiwa na daktari maalumu kutoka Ufaransa.
Boateng aliumia mkono katika mechi dhidi ya Marekani na amekuwa akipatiwa tiba maalumu ili awemo kwenye kikosi kitakachocheza na Uruguay.
Uwezekano wa Sarpei kucheza mechi ya kesho ni mdogo kutokana na kuumia mguu na Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyanyakyi alithibitisha kuwa beki huyo hatacheza.
Milovan alisema pengo la Mensah litazibwa na beki Isaac Vorsah, lakini hana hakika kama Sulley Muntari anaweza kucheza nafasi ya Dede Ayew mwenye kadi mbili za njano.
Kocha Mkuu wa Uruguay, Oscar Tabarez alisema hawawezi kuidharau Ghana kwa vile imeonyesha soka ya kiwango cha juu katika mechi zake zilizopita na imepania kuweka historia mpya kwa bara la Afrika.
Tegemeo kubwa la Oscar katika mechi hiyo litakuwa kwa washambuliaji wake nyota, Diego Forlan, Luis Suarez na Jorge Martinez.
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MICHUANO ya soka ya fainali za Kombe la Dunia, inaingia katika hatua ya robo fainali leo wakati timu nne zitakapoteremka dimbani katika viwanja viwili tofauti.
Katika mechi hizo, Brazil itamenyana na Uholanzi kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Port Elizabeth wakati Ghana itavaana na Uruguay kwenye uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.
Brazil ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuichapa Chile mabao 3-0 katika raundi ya pili wakati Uholanzi ilitinga robo fainali baada ya kuishinda Slovakia mabao 2-1.
Nao wawakilishi pekee wa Afrika waliosalia katika fainali hizo, Ghana walifuzu kucheza robo fainali baada ya kuichapa Marekani mabao 2-1 wakati Uruguay iliitoa Korea Kusini kwa idadi hiyo ya mabao.
Pambano kati ya Brazil na Uholanzi ndilo linalovuta hisia za mashabiki wengi wa soka duniani, kufuatia timu hizo kuonyesha kandanda ya kuvutia tangu michuano hiyo ilipoanza Juni 11 mwaka huu.
Kocha Mkuu wa Brazil, Carlos Dunga alikiri juzi kuwa, pambano hilo litakuwa gumu kwao kutokana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na Uholanzi katika hatua za awali.
“Tunaelewa Uholanzi ni timu ngumu kuifunga na kucheza nayo,”alisema Dunga. “ Mchezo wao hauna tofauti na soka ya Amerika ya Kusini. Hawachezi soka ya kujihami na hutumia pasi ndefu. Wanacheza soka ya ufundi na tutalazimika kuwa tayari kukabiliana nao.”
Brazil haijakumbana na timu ngumu hadi sasa. Ilitwaa uongozi wa kundi G baada ya kuzifunga Korea Kaskazini mabao 2-1, ikaichapa Ivory Coast mabao 3-1 kabla ya kutoka suluhu na Ureno.
“Sasa ni mechi kati ya timu mbili zenye utamaduni tofauti wa kucheza soka na zenye wachezaji wa kiwango cha juu,” alisema nahodha wa Brazil, Lucio.
Beki huyo mkongwe kwenye kikosi cha Brazil alikiri kuwa, kadri michuano hiyo inavyosonga mbele, mechi zinakuwa ngumu zaidi.
Uholanzi haijawahi kutwaa Kombe la Dunia, lakini imefanya vizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Denmark, Japan, Cameroon na Slovakia.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Brazil kukutana na Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia, ambapo Brazil ilishinda mechi mbili na kufungwa moja.
Uholanzi iliishinda Brazil katika raundi ya pili ya michuano ya mwaka 1974 nchini Ujerumani kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 katika robo fainali mwaka 1994. Brazil pia iliishinda Uholanzi hatua ya nusu fainali katika michuano ya mwaka 1889 iliyofanyika Ufaransa.
Katika mechi hiyo, Brazil huenda ikawakosa viungo wake, Elano na Felipe Melo, ambao ni majeruhi. Elano alishindwa kufanya mazoezi Jumanne iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
Brazil pia itamkosa Ramires, aliyechukua nafasi ya Melo, kufuatia kuwa na kadi mbili za njano.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Uholanzi, Bert van Marwijk alisema ni vigumu kutabiri pambano hilo kwa vile timu hizo mbili zina historia ya kufungana kwa zamu.
Tegemeo kubwa la Uholanzi litakuwa kwa washambuliaji wake, Robin van Persie, Ryan Babel, Dirk Kuyt na Arjen Robben.
Wasiwasi wa Ghana kumkosa mshambuliaji wake nyota, Asamoah Gyan umepungua baada ya mchezaji huyo juzi kufanya mazoezi na wenzake.
Asamoah, nahodha John Mensah, kiungo Kevin Prince Boateng na beki Hans Sarpei walishindwa kufanya mazoezi mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
Kocha Milovan Rajevac wa Ghana alisema juzi kuwa, Mensah anasumbuliwa na maumivu ya mgongo na hawezi kufanya mazoezi na amekuwa akisaidiwa na daktari maalumu kutoka Ufaransa.
Boateng aliumia mkono katika mechi dhidi ya Marekani na amekuwa akipatiwa tiba maalumu ili awemo kwenye kikosi kitakachocheza na Uruguay.
Uwezekano wa Sarpei kucheza mechi ya kesho ni mdogo kutokana na kuumia mguu na Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyanyakyi alithibitisha kuwa beki huyo hatacheza.
Milovan alisema pengo la Mensah litazibwa na beki Isaac Vorsah, lakini hana hakika kama Sulley Muntari anaweza kucheza nafasi ya Dede Ayew mwenye kadi mbili za njano.
Kocha Mkuu wa Uruguay, Oscar Tabarez alisema hawawezi kuidharau Ghana kwa vile imeonyesha soka ya kiwango cha juu katika mechi zake zilizopita na imepania kuweka historia mpya kwa bara la Afrika.
Tegemeo kubwa la Oscar katika mechi hiyo litakuwa kwa washambuliaji wake nyota, Diego Forlan, Luis Suarez na Jorge Martinez.
LEILA: Sioni tatizo kufanyakazi kundi moja na mume wangu
L Ni mke wa Mzee Yusuf na mwimbaji wa Jahazi Modern Taarab
Na Mohammed Issa `
“NILIANZA kumfahamu Mzee Yusuf katika ukumbi wa Equator Grill uliopo Mtoni kwa Azizi Ally, Temeke, Dar es Salaam. Nilipenda sana jinsi alivyokuwa anapiga kinanda wakati huo, ” anasema mwimbaji nyota wa taarab wa kundi la Jahazi, Leila Rashid.
Anasema kipindi hicho alikuwa akihudhuria maonyesho mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na kikundi cha taarab cha Zanzibar Stars, ambacho Yusuf alikuwa mmoja wa wasanii wake, akiwa anapiga kinanda.
Leila, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji tangu akiwa mdogo anasema, alikuwa na kawaida ya kwenda kwenye ukumbi huo kila Zanzibar Stars ilipokuwa ikifanya onyesho.
“Nilikuwa na ndoto ya kuimba taarab tangu nilipokuwa mdogo na nilikuwa nikivutiwa sana na uimbaji wa Sabah Salum ‘Muchacho’ kutokana na uimbaji wake mzuri,” anasema.
Leila anasema alikuwa akitumia muda mwingi akiwa nyumbani kwao kuimba nyimbo mbalimbali za waimbaji nyota wa muziki huo kwa lengo la kupima uwezo wake kama anaiweza fani hiyo.
Mwimbaji huyo mwenye sura na umbo la kuvutia, ambaye wajihi wake unashabihiana na mwanamke wa kisomali, anasema siku ya kwanza kuanza kufahamiana na Yusuf, alijihisi mwenye furaha kubwa.
“Kwa kweli siku ya kwanza kufahamamiana na Yusuf nilijihisi mwenye furaha sana na niliamini ataweza kunisadia kukuza kipaji changu cha uimbaji nilichokuwa nacho,” anasema.
Baada ya kufahamiana na kuwa karibu na Yusuf, Leila anasema mwimbaji huyo gwiji wa taarab alimshawishi ajiunge na kikundi cha Zanzibar Stars, ambacho kilikuwa kikiwika wakati huo.
Leila, ambaye kwa sasa anasikika kila kona ya nchi kutokana na uimbaji wake mzuri, anasema ushauri aliopewa na Yusuf aliusikiliza na kuufanyia kazi.
Anasema alijiunga na Zanzibar Stars miaka tisa iliyopita na wimbo wake wa kwanza ndani ya kikundi hicho unajulikana kwa jina la ‘Riziki atoae Mola’.
Mwimbaji huyo mwenye bashasha anasema, baada ya kurekodi wimbo huo, hakufanikiwa kutoa wimbo mwingine kutokana na ubinafsi uliokuwepo katika kundi hilo.
Anasema mara yake ya kwanza kupanda kwenye steji alikuwa na hofu, lakini alifanikiwa kuimba vizuri na kushangiliwa na mashabiki wengi.
Leila, mwimbaji mwenye sauti nyororo na macho ya kuvutia anasema, aliamua kuondoka Zanzibar Stars kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ubinafsi na uchache wa maslahi.
Anasema licha ya kwamba kipindi hicho Zanzibar Stars ilikuwa inatamba kwa nyimbo za taarab, maslahi yalikuwa madogo, hali iliyosababisha waimbaji wengi mahiri kuhama.
Mwimbaji huyo anasema, mwaka 2006 alijiunga na kundi jipya la Jahazi Morden Taarab ‘Wana wa nakshinakshi’ chini ya Mkurugenzi wake Mzee Yusuf.
Anasema kuanzishwa kwa kundi hilo, ambalo linaongozwa na mume wake, Yusuf kulimfanya afahamike ndani na nje ya nchi hii.
“Jahazi ndiyo imenifanya nifahamike kila kona ya nchi hii, nadhani kama si kundi hili, hadi sasa ningekuwa sifahamiki,” anasema.
Leila anasema wimbo wa ‘Maneno ya mkosaji’, ambao ulikuwa wa kwanza kuimba katika kundi hilo, ulimpandisha chati na kumpa umaarufu mkubwa na kusisitiza kuwa, kwa sasa anajiona yupo kwenye chati ya juu.
“Sidhani kama kuna mwimbaji anayeweza kujaribu kusimama na mimi kwa sasa, niko juu na nimeiva kila idara,” anajigamba mwimbaji huyo.
Akizungumzia maendeleo ya muziki wa taarab nchini, Leila anasema upo juu na unazidi kukua kadri siku zinavyosonga mbele kutokana na kuwa na mashabiki wengi zaidi.
Mwimbaji huyo, ambaye ni mama wa watoto wawili anasema, haoni tatizo kufanyakazi katika kundi moja na mumewe kwa sababu ameshaizoea tabia ya mumewe.
Leila anasema ataendelea kuheshimiana na mume wake kwa kipindi chote watakachoendelea kuwa pamoja huku akisisitiza kuwa, hakuna anayeweza kuwatenganisha kwa vile anampenda kuliko kitu kingine chochote.
“Nampenda sana mume wangu ndio maana hata anapotaka kuoa mke mwengine, huwa nampa ruksa kwani najua kufanya hivyo ni sheria kwa mujibu wa dini yetu,” anasema.
Hata hivyo, mwimbaji huyo anayependa kutabasamu muda wote anasema, hafurahishwi kuona Yusuf na mdogo wake Khadija, ambaye ni mwimbaji wa kundi la Five Stars Modern Taarab wametofautiana.
Anasema ni vyema wanandugu hao wawili waishi kama awali na waendelee kufanyakazi katika kundi moja kwa vile kugombana kwao hakutoi sura nzuri mbele ya jamii.
Leilah, ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Ubinadamu kazi’, anasema kupitia fani hiyo, ameweza kusafiri katika mikoa mingi nchini na pia nje ya nchi. Alizitaja baadhi ya nchi alizowahi kutembelea kuwa ni Uingereza, Oman, Dubai, Nairobi na Burundi.
Mwimbaji huyo amekitaja kibao cha ‘Kwa hilo hujanikomoa’ kuwa ndicho kilichomfanya apendwe zaidi na mashabiki kutokana na kukiimba kwa umahiri mkubwa.
Ametoa mwito kwa serikali kuwasaidia waimbaji wachanga ili waweze kuonyesha vipaji vyao. Pia amewataka wasanii wenzake wa muziki huo, kuwa na upendo na kuacha majungu miongoni mwao.
Huyu ndiye kocha mpya wa Zanzibar Heroes
Subscribe to:
Posts (Atom)