KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, August 22, 2015

YANGA YALIPA KISASI KWA AZAM


Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm akimpongeza kipa Ally Mustafa 'Barthez' baada ya mechi jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MLINDA mlango Ally Mustafa ‘Barthez’ amepangua penalti mbili na kuiwezesha Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam FC kwa penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Barthez alipangua penalti za beki raia wa Ivory Coast, Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Ame Ali ‘Zungu’, wakati kipa wa Azam FC, Aishi Manula naye alicheza penalti ya Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ ikapanguliwa.
Penalti za Yanga SC zilifungwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na Kelvin Yondan aliyepiga ya mwisho.

Penalti za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Nahodha John Raphael Bocco, Himid Mao Mkami, Aggrey Morris, Jean Baptiste Mugiraneza, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe.
Ushindi huo ni sawa na kisasi baada ya Yanga SC kufungwa kwa penalti 5-3 katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, baada ya sare ya 0-0.
Katika dakika 90 za mchezo wa leo, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kosakosa zilikuwa za pande zote mbili, lakini dakika za mwishoni, Yanga SC walikuwa wakali zaidi.
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alionekana kabisa akijiangusha kupoteza muda ili kupunguza kasi ya Yanga SC dakika za mwishoni.
Kevin Yondan alicheza kwa kiwango kikubwa leo na dakika ya 37 aliitokea vizuri pasi ndefu ya Mzimbabwe Thabani Kamusoko na kumchambua vizuri kipa Aishi Manula, lakini beki Shomary Kapombe akabinuka ‘tik tak’ kuuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.

Almanusra Bocco aifungie Azam FC dakika ya 86 baada ya pasi nzuri ya Mugiraneza, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Barthez aliyekuwa katika ubora wake siku ya leo.
Hii inakuwa mara ya tano Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii ikiwa ni rekodi, baada ya kuifunga Simba SC mara mbili, mwaka 2001 mabao 2-1 na 2010 kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90, kabla ya kuifunga Azam FC miaka mitatu mfululizo, 2013 bao 1-0 na 2014 mabao 3-0.
Inafuatia Simba SC iliyotwaa Ngao mara mbili, mwaka 2011 wakiifunga Yanga SC 2-0 na 2012 wakiifunga Azam FC 3-2, wakati Mtibwa Sugar ni timu nyingine iliyowahi kutwaa Ngao mwaka 2009 ikiifunga 1-0 Yanga SC.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondani, Nadir Haroub, Said Juma/Haruna Miyonzima dk57, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Deus Kaseke dk85, Amisi Tambwe na Godfrey Mwashiuya.
Azam FC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Agrey Morris, Paschal Wawa, Mudathir Yahya/Jean Mugiraneza dk68, Himid Mao, Frank Domayo/Ame Ally dk82, Farid Mussa, John Bocco na Kipre Tchetche.

No comments:

Post a Comment