Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amemshukuru Rais wa CECAFA, Leodgar Tenga kwa kuipa Tanzania uenyeji wa mashindano ya Vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) iliyomalizika jana kwa klabu ya Azam FC kutawazwa Mabingwa wapya wa michuano hiyo.
Aidha Malinzi ameishukuru Kamati ya Ndani ya Uendeshaji ya Michuano hiyo (LOC) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa na kuhakikisha michuano hiyo inafanyika na kumalizika katika hali ya usalama na amani.
Malinzi pia amewapongeza wapenzi, washabiki na wadau wa soka nchini waliojitokeza kushuhudia michezo ya michuano hiyo na kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ndani nan je ya uwanja kipindi chote cha michuano.
Rais Malinzi ameipongeza klabu ya Azam FC kwa kutwaa Ubingwa Kagame, kwa kutwaa ubingwa huo imeweza kuweka historia ya kutwaa Ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake na pia kuwa klabu iliyocheza michuano hiyo na kuwa Bingwa bila kuruhusu nyavu zake kutikisika.
Pia Malinzi amewashukuru waandishi wa habari/vyombo vya habari kwa sapoti yao wakati wa michuano hiyo. Shukrani hizo pia zimepelekwa kwa klabu za Yanga SC, KMKM kwa kushiriki mashindano hayo.
U-15 YAREJEA KUTOKA ZANZIBAR
Kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15), kimerejea leo asubuhi kutokea kisiwani Zanzibar kilipokwenda kucheza michezo ya kujipima nguvu na kombani ya U-15 ya kisiwani humo.
Katika michezo miwili iliyocheza kisiwani humo, iliweza kushinda michezo yote miwili, (4-0 ), (1-0), huku kocha Bakari Shime akiwapongeza vijana wake na kusema wanaendelea kuimarika kuelekea kujiandaa na kuwania kufuzu kwa fianali za Mataifa Afrika chini ya miaka 17 mwakani.
Baada ya kurejea jijini Dar es salaam leo, kambi ya timu hiyo imevunjwa na vijana hao watakutana tena mwisho wa mwezi wa Agosti kama ilivyo katika program yao ya kukutana kila mwisho wa mwezi na kucheza michezo ya kirafiki.
Mwishoni mwa mwezi Agosti timu hiyo ya vijana inatarajiwa kuelekea mkoani Tanga kucheza michezo ya kirafiki na kombani ya mkoani humo, ambapo kocha wake Shime pia anatumia nafasi hiyo kutazama wachezaji wengine wenye uwezo mzuri katika timu za kombaini za mikoa kwa ajli ya kuwaongeza katika kikosi chake.
Mpaka sasa timu hiyo ya vijana chini ya miaka 15 (U15) imeshafanya ziara na kucheza michezo katika miji ya Mbeya na kisiwani Zanzibar.
No comments:
Post a Comment