KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, August 2, 2015

TAARIFA YA KAMATI YA UTENDAJI TFF


Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichokutana leo kimepitia na kutoa maamuzi yafuatayo:

(i)           Kila mkoa utakua na kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto (Regional Sports Centre). Mapato ya mchezo wa Ngao ya Hisani msimu huu yatatumika kuagiza kontena la vifaa (mipira size 3, 4, bips na cones) ambavyo vitasambazwa katika vituo vyote vya michezo vya mikoa.

(ii)         Ubovu wa viwanja – Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretariat kuwaandikia barua wamiliki wa viwanja vyenye mapungufu, kufanyia kazi marekebisho hayo haraka kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi nchini. Kiwanja ambacho hakitafanyiwa marekebisho hakitatumika kwa michezo ya ligi msimu huu.

(iii)       Twiga Stars – Timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu nchini Tanzania (Twiga Stars) inatarajiwa kuingia kambini tarehe 04 Agosti kisiwani Zanzibar kwa gharama za TFF kujiandaa na Fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofanyika nchini Congo Brazaville mwezi Septemba mwaka huu. Aidha Kamati ya Utendaji imeiagiza sekretariet kuwasiliana na Kamati ya Olympic nchini (TOC) kuweza kujua mchango wao katika maandilizi hayo ya michezo ya Afrika.

(iv)        Kamati ya Utendaji imeipongeza Kamati ya ndani ya Uendeshaji wa Michuano ya Kombe la Kagame (LOC) kwa kuandaa michuano hiyo vizuri kuanzia mwanzo mpaka sasa inapoelekea mwishoni kesho kwa mchezo wa Fainali.  Aidha Kamati inaipongeza klabu ya Azam FC kwa kufika hatua ya fainali ya michuano hiyo na kuitakia kila la kheri katika mchezo wa kesho ili iweze kulibakisha kombe hilo nyumbani. Kamati hiyo pia imeipongeza klabu ya Yanga kwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

(v)          Aidha Kamati ya utendaji imeiagiza sekretariat kuandika barua kwenda kwa uongozi wa CECAFA juu ya masikitiko na mapungufu yaliyoenekana katika michuano hiyo. Timu ya Gor Mahia pamoja na washabiki wake wamekuwa wakifanya vitendo vya utovu wa nidhamu huku CECAFA ikiwatazama pasipo kuwapa adhabu yoyote.

(vi)        Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji pia kimepitia na kupitisha mapendekezo ya rasimu ya kanuni za uendeshaji wa Bodi ya ligi nchini (TPLB), yaliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji Wakili, Idd Mandi.

DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA AGOSTI 6
Dirisha la Usajili kwa Vilabu vya Ligi Kuu (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (RCL) linatarajiwa kufungwa tarehe 06 Agosti, 2015.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) linavikumbusha vilabu vyote kufanya usajili wa wachezaji wao mapema kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo, ili kuondokana na usumbufu wa kufanya usajili dakika za mwisho.

Pindi dirisha hilo litakapofungwa Agosti 06, hakuna klabu au timu yoyote itakayoweza kufanya tena usajili wake, hivyo ni vyema vilabu vitahakikisha vinamaliza mausala ya usajili mapema kabla ya siku ya mwisho.

U15 KUJIPIMA LEO ZANZIBAR
Kikosi cha timu ya Taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) leo kinatarajiwa kushuka dimbani kisiwani Zanzibar kucheza michezo wa kirafiki na kombani ya kisiwani humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.

Timu ya vijana ya Taifa wenye umri chini ya miaka 15 (U15) imekua ikiingia kambini kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kucheza michezo ya kirafiki ya kujipima nguvu, na kocha kupata nafasi ya kuona maendeleo ya vijana na kuongeza wachezaji wengine wanaonekana katika kuboresha kikosi hicho.

Kikosi hicho cha Vijana cha U-15 kilichopo chini ya kocha mzawa Bakari Shime, kinajumuisha wachezaji 22 waliopo kambini, na kinatarajiwa kucheza michezo miwili kisiwani Zanzibari leo jumamosi na jumapili, kabla ya kurejea jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment